AN-NUUR  Na.174 Rajab 1419, Novemba 6 - 12, 1998 
 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Mashairi 
 

Maovu nitakemea - 1 
 

Bismillahir Rahmani, illah Mola jalia, 
Kalamu I mkononi, Luanda nimerejea, 
Nilikuwa likizoni, leo nawasalimia, 
Sitaacha asilani, maovu kuyakemea. 

Tukisoma Qur’an, Allah kasisitiza, 
Ni amri ya Manani, maovu kuyakemea, 
Kesho tutasema nini, lengo lisipotimia, 
Kw uwezo wa Manani, maovu nitakemea. 

Katuumba Rahmani, tupate mhimidia, 
Siyo kuvaa vimini, na kurithishwa mabia, 
Au kusema pigeni, na nyumba kutuchomea, 
Hii ni sheria gani, nasema naikemea. 

Tumeingia mkengeni, huyu tulomchagua, 
Atuua hadharani, na mateso kidedea, 
Sisi tumekosa nini, wadhifa kumpatia, 
Sitaacha asilani, maovu kuyakemea. 

Hata kule vijijini, wengi wamuulizia, 
Aibu gani nchini, Raisi atuletea, 
Au hayupo nchini, mbona mambo amezea? 
Nimerejea Jijini, maovu nayakemea. 

Ikiguswa Marekani, hapo utamsikia, 
Na atakuwa makini, mambo kufuatilia, 
Tulomuweka enzini, kongoni atulipua, 
Sitaacha asilani, maovu kuyakemea. 

Kero kuzidi nchini, sera anopalilia, 
Rushwa na umasikini, maji anavinyweshea, 
Choma moto majumbani, au bomoabomoa, 
Huyu ni Raisi gani, maovu asokemea. 

Kila mara safarini, kodi zetu atumia, 
Mara leo Marekani, Ureno Hispania, 
Uchofuata nini, haukai Tanzania ? 
Tunakutaka nchini, mauaji kukemea ! 

Maraisi duniani, wewe tunajivunia, 
Mpendwa nambari wani, kwa nyumbani kutokaa, 
Safari nyingi ng’amboni, dunia watembelea, 
Tunafaidika nini, walala hoi Songea ? 

Mkarimu kwa wageni, kila wakitembelea, 
Anachosema mgeni, mwepesi mkubalia, 
Kesho silaha dukani, kama pipi tanunua, 
Twende wapi masikini, haifai Tanzania !!! 

Haupendi tafrani, yakutambua dunia, 
Utayalipa madeni, wani hukuyazoea, 
VAT nyingi kampeni, wanyonge tunaumia !! 
Leo hii madukani, nashindwa kuhadisia. 

Wangapi serikalini, ngazi wameziachia, 
Makosa yalo bayana, nini kinaendelea, 
Kweli na uwazi gani, Rais anatumia, 
Ninaumia moyoni, na wazi nayakemea. 

Kero ni nyingi nchini, nashindwa kuendelea, 
Nimetoka safarini, uchovu najisikia, 
Malenga bara na pwani, salaam nawatumia, 
Sitaacha asilani, maovu kuyakemea. 

K.S. Luanda (Nolo) 
Dar es Salaam. 


Nawapenda Twalaban
 

Wapo binadamu hawa, walohiari pumbao, 
Maisha walewale, fisadi kila uchao, 
Wapenda vya kutungua, kushona ni dhiki kwao, 
Mimi siwapendi hao, nawapenda Twalaban. 

Wapo wapendao nyimbo, muziki wapigiwao, 
Wakawasifu “warembo”, jukwaa walipambao, 
Wao wana lao jambo, lasibu dhamira zao, 
Mimi siwapendi hao, nawapenda Twalaban. 

Wapo wachezao ngoma, wasio na haya zao, 
Waume na kina mama, kuwa wachanganyikao, 
Wakidhani huo wema, wakawa waupendao, 
Mimi siwapendi hao, nawapenda Twalaban. 

Wapo wapishi wa shari, waume na ndevu zao, 
Huwapanga msitari, mabinti washindanao, 
Eti “shoo” ya uzuri, waonwe unyama wao, 
Mimi siwapendi hao, nawapenda Twalaban. 

Wapo wakwea jukwaa, kuhubiri sera zao, 
Matumbo yamewajaa, mebana mavazi yao, 
Mapenzi yamewatwaa, uongo ndo jambo lao, 
Mimi siwapendi hao, nawapenda Twalaban. 

Wapi pia “wapinzani”, walounda vyama vyao, 
Wenye kupenda kudhani, Ikulu mahala pao, 
Wawapo majukwaani, huhubiri ndoto zao, 
Mimi siwapendi hao, nawapenda Twalaban. 

Wengine tunao humu, hatuna salama  nao, 
Wamejaa madhalimu, wanyonge watunyongao, 
Lengo ni kutuhujumu, wafaidi peke yao, 
Mimi siwapendi hao, nawapenda Twalaban. 

Wale wapora uhai, shabaha watulengao, 
Mfano wa Mwembechai, rungu na risasi zao, 
Damu yetu tutadai, hadi kwa Mungu tunao, 
Mimi siwapendi hao, nawapenda Twalaban. 

Sipendi mshikamano, ulobeba lengo lao, 
Kupangusana mikono, na huku twacheka nao, 
Ndani wana chuki mno, ungeona myoyo yao, 
Mimi siwapendi hao, nawapenda Twalaban. 

Mapenzi yangu ya kweli, kwa hao niwapendao, 
Mazito wanahimili, tamaa kwa Mola wao, 
Ikhiwan ni wa pili, Hamas na wenzao, 
Kwa zile juhudi zao, nawapenda Twalaban. 

Dua yangu naitaja, Allah aniunge nao, 
Awashushie faraja, wafeli wawapingao, 
Na kila shari ya kuja, ikute wanayo ngao, 
Hasa kwa malengo yao, nawapenda Twalaban. 

Washindi wa ukaidi, madhalimu walo nao, 
Wao nyuma hawarudi, mbele ni wasogeao, 
Na kuitwa MAGAIDI, hawawi watishikao, 
Ndo mana kila uchao, nawapenda Twalaban. 

Witiri wape kuweza, Mola wa uhai wao, 
Witiri washinde kiza, isimame dini yao, 
Witiri kwako muweza, naomba nusura kwao, 
Witiri ninamaliza, nawapenda Twalaban. 

Jihad R. Saballah, 
Box 347, 
Shinyanga. 
 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
TAHARIRI  
Tuacheni na njaa yetu msituongezee silaha 

Serikali yakumbushwa kujiunga OIC 
Na Mwandishi wetu 

Polisi walizingira nyumba yangu usiku wa manane - Sheikh Mbukuzi 

Wafungwa waomba Futari na Vikoi 

Macho ya shutuma 
Na Abu Halima Sa Changwa 

Hoja pofu 
Na Abu Halima Sa Changwa 

Tafuteni ufalme wa kisiasa 

Ubaguzi katika mfumo wa elimu nchini: Chuo Kikuu chasikia kilio cha wanawake 

'Vichupi' vya nini Kimiti? 
Na. Said Rajab 

Mjadala wa Katiba na haki za Waislamu 
Na Masoud Mohammed Mbogo 

Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo- 3 
Na Nandenga wa Mkomidachi 

Waliochukuliwa utumwa Uarabuni 
Na Hassan Omar 

Madrasatul Maamury Islamiya 

Teknologia: Jifunze Kuunganisha Kompyuta (4) 
Na Hassan Omar 

Kuweni wabunifu muinue taaluma - Wito 

TVZ na kipindi cha 'Wasemavyo' 

Kesi ya Waislamu Mwembechai: Mashahidi washindwa  

Wanyimwa fursa ya kuswali Ijumaa Mwanza 

Shule ya Bakwata yafungiwa Tanga 

Mafunzo ya Qur'an  
Shetani anawaogopesha wenye mali kutoa 

Barua za wasomaji  

Masomo ya dini ya Kiislam  

Chakula na lishe 

Mashairi 

Matangazo 
 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita