AN-NUUR  Na.174 Rajab 1419, Novemba 6 - 7, 1998 
 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Serikali yakumbushwa kujiunga OIC
  • Yaambiwa itoe maelezo kuhusu ‘Memorandum of understanding’
  • Waislamu watakiwa kurejesha hadhi yao
Na. Mwandishi wetu

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekumbushwa kutekeleza ahadi iliyoitoa huko nyuma ya kujiunga na Shirika la OIC.

Akiwasilisha taarifa ya Baraza Kuu katika kongamano la Waislamu lililofanyika Jumapili Novemba 1, 1998, Katibu Mkuu wa Baraza hilo Sheikh Abas Kilima alisema kwamba ni muda mrefu sasa tangu Serikali iahidi kujiunga na OIC kwa hiyo kwa niaba ya Baraza lake angeikumbusha Serikali kutekeleza ahadi hiyo.

Sheikh Kilima alisema haoni sababu ya Serikali kuendelea kusita kujiunga na shirika hilo kwani tofauti na ilivyokuwa ikiripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari, malengo ya shirika hilo yako bayana kwa Serikali hivi sasa.

Akikumbusha yaliyopelekea Zanzibar kutojiunga na shirika hilo, Sheikh Kilima alisema kwamba hapakuwa na sababu za kidini kwa Zanzibar kuzuiwa kujiunga na jumuiya hiyo.

"Lakini Bunge, Serikali na hasa Mwalimu Nyerere, waliipinga kweli kweli, Mwalimu Nyerere kwa mikutano ya hadhara na ya waandishi wa habari alipinga hatua ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano kujiunga na Shirika la O.I.C.", alieleza Sheikh Kilima.

Mwaka 1992 Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar ilitaka kuwa mwanachama wa O.I.C.ili ijikwamue kiuchumi kutokana na misaada na mikopo isiyo na riba inayotolewa na jumuiya hiyo ya Waislamu.

Hatua hiyo ya Serikali ya Mapinduzi ilizua mtafaruku ndani ya Bunge, CCM, Serikali na katika vyombo vya habari, kwamba ililenga kuiingiza Zanzibar katika Sharia za Kiislamu na hatimaye kuisilimisha Jamhuri ya Muungano.

Sheikh Kilima alilieleza kongamano hilo kwamba O.I.C. haina malengo ya kusilimisha bali kusaidia nchi wanachama wake kuboresha hali za kijamii.

"Ni kweli hili ni shirika la dini lakini malengo yake ni kuwajengea huduma za maendeleo, elimu na afya nchi wanachama wake wenye raia Waislamu", alisema katibu huyo wa Baraza Kuu.

Wakati huo huo, Waislamu nchini wametakiwa kuwa waangalifu katika chaguzi mbali mbali ili kujiepusha na wale wote wenye mawazo ya kuwafanya ngazi ya kufikia malengo yao kisha kuwapuuzilia mbali mara baada ya uchaguzi.

Akizungumza katika kongamano hilo katibu wa jumuiya ya wazazi nchini Bwana Shaaban Kakinga aliwataka Waislamu waanzishe utaratibu wa kupiga kura ya maslahi badala ya kujitumbukiza kwenye chaguzi bila ya malengo ambako kumechangia kuwafanya Waislamu wasiwe na sauti katika sera za nchi.

"Kura inayozingatia maslahi yetu kama Waislamu hapa nchini ndiyo liwe azimio letu", aliongea kwa msisitizo katibu huyo wa Wazazi.

Waislamu nchini mara kwa mara wamekuwa wakiishutumu Serikali kwamba haiwatendei haki, hata hivyo malalamiko yao yamekuwa yakipuuzwa na vyombo mbali mbali.

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
TAHARIRI  
Tuacheni na njaa yetu msituongezee silaha 

Serikali yakumbushwa kujiunga OIC 
Na Mwandishi wetu 

Polisi walizingira nyumba yangu usiku wa manane - Sheikh Mbukuzi 

Wafungwa waomba Futari na Vikoi 

Macho ya shutuma 
Na Abu Halima Sa Changwa 

Hoja pofu 
Na Abu Halima Sa Changwa 

Tafuteni ufalme wa kisiasa 

Ubaguzi katika mfumo wa elimu nchini: Chuo Kikuu chasikia kilio cha wanawake 

'Vichupi' vya nini Kimiti? 
Na. Said Rajab 

Mjadala wa Katiba na haki za Waislamu 
Na Masoud Mohammed Mbogo 

Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo- 3 
Na Nandenga wa Mkomidachi 

Waliochukuliwa utumwa Uarabuni 
Na Hassan Omar 

Madrasatul Maamury Islamiya 

Teknologia: Jifunze Kuunganisha Kompyuta (4) 
Na Hassan Omar 

Kuweni wabunifu muinue taaluma - Wito 

TVZ na kipindi cha 'Wasemavyo' 

Kesi ya Waislamu Mwembechai: Mashahidi washindwa  

Wanyimwa fursa ya kuswali Ijumaa Mwanza 

Shule ya Bakwata yafungiwa Tanga 

Mafunzo ya Qur'an  
Shetani anawaogopesha wenye mali kutoa 

Barua za wasomaji  

Masomo ya dini ya Kiislam  

Chakula na lishe 

Mashairi 

Matangazo 
 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita