|
|
|
Na Nandenga wa Mkomidachi SUALA jengine la msingi ni mahusiano kati ya mja na Muumba (Allah). Qur’an inatufahamisha kwamba tofauti za kijamii (mbari) ni suala la kimaumbile. Mwanaadamu amepandikizwa elimu ya kumjua Allah na hisia za kiroho, lakini hisia hizi za kiroho huweza kuwa dhidi yake iwapo hazitaelekezwa katika ulekeo sahihi. Kwa hivyo kutegemea matashi, maoni au mitazamo ya kibinadamu kama mwongozo ni hatari. Baadhi ya makundi na madhehebu fulani fulani hudai kuongozwa na Mwenyezi Mungu, roho au ufunuo, lakini bado makundi hayo yametofautiana au hata kupingana kiimani. Kila dhehebu au kundi hudai kutekeleza maamrisho ya Mungu. Mara nyingi tumewasikia au kukutana na wale wanaodai kujisikia kuokoka na kuongozwa na roho.Tutakuwa wenye busara zaidi iwapo tutaachana na madai hayo yasiyo na mashiko. Kuweka mkazo wa kuwa na vyanzo sahihi vya ufunuo ni muhimu. Ndio maana Allah (s.w.) katika historia yote ya mwanaadamu amewatuma watu maalum tu kufikisha ujumbe wake kwa wengine, kupokea ufunuo na kuufasiri kimatendo kwa wanaadamu. Baadhi ya Mitume hawa walipewa vitabu au maandiko matakatifu yenye hukumu na mwongozo wa Allah. Kimsingi Mitume wote walifikisha ujumbe wa aina moja: "Na hatukumtuma kabla yako Mtume yoyote ila tulimfunulia ya kwamba hakuna abudiwaye ila Mimi, basi Niabuduni." (21:25). Hata hivyo, sehemu inayogusa zaidi ambayo imepelekea malumbano yanayoendelea na labda inaweza kufanya kutofikiwa muafaka ni lile dai la Qur’an kwamba Mitume - Nuhu, Ibraham, Ishmael, Yesu, Isaka, Jakob, Musa, Daudi, Suleiman, Yohana (mbatizaji), Yesu na Mtume wa mwisho Muhammad, kwamba wote hawa ni Waislamu, kwa sababu Muislamu ni yule aliyejisalimisha kwa kufuata maamrisho ya Allah (s.w.). Wafuasi wa Mitume hao wote pia ni Waislamu. Kuwaamini Mitume wote ni katika nguzo za imani ya Muislamu. Kwa hakika Waislamu wanaonywa kwamba yoyote yule atakaewakubali baadhi ya Mitume na kuwabagua (kuwakana) wengine ni kama amewakana wote. Kwa hiyo, kwa Muislamu, kumuamini Musa wakati huo huo akamkana Yesu na Muhammad ni kinyume na mafundisho ya Musa. Hali kadhalika kumuamini Yesu na kuwakana Musa na Muhammad ni kuvuruga kile ambacho Musa na Muhammad walikisimamisha. Na kwa Muislamu kumuamini Muhammad na kuwakana Musa na Yesu ni kuyakana mafundisho ya kitabu chake kitakatifu. Msimamo huu umesisitizwa katika Qur’an kama ifuatavyo:- "Hakika wale wanaomkanusha Mwenyezi Mungu na Mitume yake, na wanataka kutenga baina ya Mwenyezi Mungu na Mitume yake, kwa kusema: "wengine tunawaamini na wengine tunawakataa", na wanataka kushika njia iliyo katikati ya haya.. Hao ndio makafiri kweli. Na tumewaandalia makafiri adhabu idhalilishayo. (4:150-151). Kuwatambua Mitume wote ni nguzo ya imani ya Muislamu si Diplomasia wala kuwastahi au kuwafurahisha wengine. Ni msingi wa maelewano sio mgogoro. Vile vile ni msingi wa majadiliano sio mabishano. Kwa nini Muhammad? Kwa nini Wasilamu wanapotoa shahada wanasema, "Nashuhudia kwamba hakuna Mola apasaye kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu na Muhammad ni mjumbe wake? Hivi kwa kusema hivi anawakana Mitume wengine? Hili haliwezi kuwa kiini kingine cha migogoro? Kwa kauli ya wazi kabisa, jukumu alilopewa Muhammad kama hatima (mwisho) ya wajumbe wa Allah (s.w.) limewaweka Waislamu wa Ummah huu katika nafasi ambayo kumsifu na kumheshimu kwao Muhammad kunatafsiri kuwaheshimu Mitume wote waliokuja kabla yake. Waislamu wanaonywa, na hili lazima lifahamike vema na wasio Waislamu, kwamba wasitafautishe, kubagua au kuleta ushabiki baina ya Mitume. Qur’an inatufahamisha:- "Mtume ameamini yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Mola wake na Waislamu wote wamemwamini Mwenyezi Mungu na malaika wake, na vitabu vyake, na Mitume yake", "Hatutafautishi baina ya yoyote katika Mitume yake (wote tunawaamini). Na tuseme: "Tumesikia na tumetii". (Tunakuomba) Msamaha, Mola wetu! Na marejeo ni kwako. (2:285). Wakati huo huo, hata hivyo, Qur’an inatufahamisha kwamba Allah (s.w.) amewafadhilisha baadhi ya Mitume kwa kuwapa vipaji, majukumu na kazi makhususi kuliko wengine: "Na Mola wako anawajua sana wote waliomo katika mbingu na ardhi. Na kwa hakika tuliwafadhilisha baadhi ya manabii kuliko wengine; na Daudi tulimpa Zaburi: (17:55). Hata hivyo, Mitume wote hao ni ndugu, ingawa ni Muhammad pekee aliyepewa ujumbe kwa ajili ya walimwengu wote. Kwa hiyo Waislamu wanaamini kwamba Muhammad ni ndugu kwa Yesu, Musa, Ibrahim na Mitume wote. Qur’an inaeleza waziwazi kwamba kuja kwa Muhamamad kulitangulia kuelezwa na Mitume waliomtangulia ikiwa ni pamoja na Musa na Yesu, amani ya Allah iwe juu yao: "Ambao wanamfuata Mtume, Nabii aliye Ummy (asiyejua kusoma wala kuandika), ambaye wanamuona ameandikwa kwao katika Taurati na Injili ambaye anawaamrisha mema na anawakataza yaliyo mabaya na kuwahalalishia vizuri na kuwaharamishia vibaya na kuwaondolea mizigo yao na minyororo iliyo juu yao. Basi wale waliomuamini yeye na kumuheshimu na kumsaidia na kuifuata Nuru iliyoteremshwa pamoja naye hao ndio wenye kufaulu.(7:157). "Nawakumbusha aliposema Isa bin Mariamu: Mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, nisadikaye yaliyokuwa kabla yangu katika Taurati, na kutoa habari njema ya Mtume atakayewajia nyuma yangu ambaye jina lake litakuwa Ahmad. Lakini alipowajia kwa hoja zilizo wazi, walisema: "Huu ni udanganyifu uliodhahiri. (61:6). Kuja kwa Muhammad vile vile kumetajwa katika Biblia: "Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako..... (Mwanzo 21:13). Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe, nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru. (Kumbukumbu 18:18). Vifungu hivi vinamzungumzia Mtume Muhammad (s.a.w.). Qur’an ina maneno ya moja kwa moja ya Allah na pia nukuu, yote yakiwa yamefunuliwa kwa Mtume Muhammad (s.a.w.). Wengi wa wasio Waislamu wanachanganya Qur’an na Hadith au kauli za Mtume. Ifahamike hapa kwamba Hadith ni tofuati (mbali) kabisa na Qur’an. Qur’an ilifunuliwa kwa Muhammad neno kwa neno kupitia Malaika na kuhifadhiwa vifuani kisha kuwekwa katika maandishi. Ni muhimu kubainisha kwamba Qur’an haikuandikwa na Muhammad (s.a.w.). Kuipinga kauli hii ni kukhitalifu Qur’an vile inavyosema kuhusu yenyewe na juu ya Muhammad (s.a.w.); kwamba Mtume hakutamka kwa matashi yake bali kila alichosema kilifunuliwa kwake kupitia Malaika Jibrili (a.s.). Yapo madai mengi kuhusu Qur’an, baadhi ya madai hayo kwa kweli ni ya ajabu hasa yale yatolewayo na wasio Waislamu. Dai moja linasema kwamba Qur’an imetegemea vitabu vilivyotangulia. Kusema kwamba Qur’an imeazima au kunakili maelezo ya vitabu vilivyotangulia, kama vile Biblia ni sawa na kuitakidi kwamba kwa kuwa kitabu cha Nandenga Mkomidachi kimefanana na kitabu cha Kalyalya Mveji na Mkomidachi ndiye aliyeandika mwanzo kitabu chake basi lazima Mveji awe amenakili kwa Mkomidachi. Mantiki hii inafumbia macho ukweli kwamba inawezekana wote hao wamenakili kutoka mahali fulani. Hii ina maana kwamba ikiwa Taurat na Injili zimetoka kwa Mwenyezi Mungu na Qur’an nayo imetoka kwa Mwenyezi Mungu basi vitabu vyote hivyo vitakuwa vimetokana na chanzo kimoja. Kuna kuwiana kiasi fulani kati ya Qur’an na vitabu vilivyopita, hili ni jepesi kuelezeka. Yule aliyewapa ufunuo Mitume waliopita ndiye huyo huyo aliyeiteremsha Qur’an kwa Muhammad ambaye, ni Mungu mmoja wa kweli Allah (s.w.). Hivi kuna aliyetegemea Qur’an kuwa vinginevyo? Qur’an ni ufunuo wa mwisho. Kwa maana hiyo, inavizidi vitabu vyote vitakatifu vya kabla yake, na ni kitabu pekee ambacho kipo katika neno na lugha yake asilia iliyofunuliwa kwa Muhammad (s.a.w.). Muhasaba, Uokovu: Muhasaba (accountability) na uokovu ni maeneo mengine yenye kuhitajia kueleweka vyema ili kupunguza migogoro na misuguano baina ya wanadini, na kwa hivyo kutengeneza daraja kuyaelekea majadiliano. Ni namna gani Mwanaadamu atakavyoweza kuepukana na dhambi kwa mtazamo wa Kiislamu? Haitoshi kwa Muislamu kuamini tu juu ya malipo mema, adhabu, na maisha baada ya barzakh; na kwamba malipo mema au adhabu huanza mara mtu anapozikwa, bali imani hii inaimarishwa kwa kufufuliwa na kuhesabiwa kisha kuhukumiwa. Qur’an inaeleza wazi juu ya hili:- "Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni; ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi. Naye ni mwenye nguvu (na) Mwenye Msamaha. (67:2). Hii ina maana kwamba uhai ni mtihani na kwamba maisha haya ya dunia ni ya muda mfupi. Maisha ya mwanaadamu yamewekewa lengo la kumuabudu Allah (s.w), kuishi kinyume na lengo hilo ni kumuasi Allah (Muumba). Kwa Muislamu kutaraji utakatifu ili kuupata uokovu ni kinyume na mafundisho. Ni kama kwamba kutaraji kitu kisichowezekana ambao ni uovu. Hili linatiliwa mkazo hapa kwa sababu Waislamu wanafahamu yapo baadhi ya madhehebu ya wasio Waislamu ambayo hudai kupata uokovu hapa hapa duniani. Ni muhimu vile vile kusisitiza hilo kwa sababu ni kweli Uislamu umefundisha mtu kuwa Mnyenyekevu kwa kiwango cha juu kwa Muumba wake, lakini pia matendo mema (unyenyekevu) wa mja si ishara ya kuufikia uokovu. Dhana ya ulokole haina nafasi katika Uislamu. Upatanisho baina ya Mungu (Allah) na Mwanaadamu mkosefu unategemea vigezo vitatu: Kigezo cha kwanza ambacho ni muhimu sana ni Rehma, neema na ukarimu au ufadhili wa Allah (s.w.). Kigezo cha pili ni matendo mema. Na kigezo cha tatu ni imani sahihi. Imani sahihi na matendo mema ni sharti katika kupata rehma na msamaha wa Allah (s.w.) na kuushinda udhaifu wetu. Namna gani ya kujitakasa na dhambi? Hili ni suala muhimu kwa namna mbili. Kwa upande mmoja, baadhi ya wasio Waislamu hufikia kudhania kwamba ulazima wa Muislamu kupata udhu kabla ya swala unamaanisha kujitakasa kutokana na dhambi. Mawazo haya si makosa tu bali ni upotoshaji mbaya wa ukweli. Kwa upande wa pili, yapo baadhi ya madhehebu ya wasio Waislamu ambayo wafuasi wake huoshwa dhambi zao na wanaadamu wenzao kwa kuungama mbele yao. Hili ni eneo jingine lenye mgogoro ambalo pia lahitaji majadiliano. Qur’an ina maelezo yafuatayo kuhusu kujitakasa na dhambi. "Na mwenye kutenda uovu au akajidhulumu nafsi yake; kisha akaomba maghufira kwa Mwenyezi Mungu, atamkuta Mwenyezi Mungu ni mwenye kughufiria, Mwenye kurehemu. (3:110). Aya nyingine inaelekeza ifuatavyo: "Na simamisha sala katika ncha mbili za mchana na nyakati za usiku zilizo karibu na mchana. Hakika mema huondoa maovu. (11:114). Hii ina maana kwamba Uislamu unafundisha toba, kuacha maovu, kujuta mtu kwa maovu aliyoyafanya na kuazimia kufuata njia ya Allah kwa kadri kiwango cha ubinadamu kitakachowezekana. Hii ni tofauti kabisa na kutaka uokovu na kuokolewa hapa hapa duniani au kuoshwa dhambi kupitia sala za wanaadamu wengine. Waislamu, pamoja na mambo mengine, hawaamini "ulazima wa kafara ya damu", mbaya zaidi ya mtu asiye na makosa, kwa ajili ya kuoshwa dhambi wengine. Waislamu wanaamini kwamba Allah (s.w.) hana haja ya damu au muhanga fulani bali anachokitaka ni toba ya kweli (Taubatan Nasuuha). Kuhusiana na suala hili Qur’an ina maelezo ya wazi kabisa: "Na utuandikie mema katika dunia hii na akhera.Sisi tunarejea kwako....Nitawaandikia
wale wanaojikinga na yale niliyowakataza, na wanaotoa Zaka na wanaoziamini
Aya zetu. (7:156)..
|
YALIYOMO
TAHARIRI Tuacheni na njaa yetu msituongezee silaha Serikali
yakumbushwa kujiunga OIC
Polisi walizingira nyumba yangu usiku wa manane - Sheikh Mbukuzi Wafungwa waomba Futari na Vikoi Macho
ya shutuma
Hoja
pofu
Ubaguzi katika mfumo wa elimu nchini: Chuo Kikuu chasikia kilio cha wanawake 'Vichupi'
vya nini Kimiti?
Mjadala
wa Katiba na haki za Waislamu
Mdahalo
kati ya Waislamu na Wakristo- 3
Waliochukuliwa
utumwa Uarabuni
Teknologia:
Jifunze Kuunganisha Kompyuta (4)
Kuweni wabunifu muinue taaluma - Wito TVZ na kipindi cha 'Wasemavyo' Kesi ya Waislamu Mwembechai: Mashahidi washindwa Wanyimwa fursa ya kuswali Ijumaa Mwanza Shule ya Bakwata yafungiwa Tanga Mafunzo
ya Qur'an
|