|
|
| Mafundisho
ya Qur’an
Kutoa katika njia ya Allah Al-Baqarah aya 261-263 "MFANO wa wale wanaotoa mali zao katika njia ya Allah ni kama mfano wa punje moja iliyotoa mashuke saba, ikawa katika kila shuke pana punje mia. Na Allah humzidishia amtakaye. Na Allah ni Mwenye wasaa mkubwa na mwenye kujua". Katika matoleo ya nyuma wakati tulipokuwa tunaelezea aya 243 ya sura hii tulionyesha msisitizo wa Allah kuhusu suala la kutoa mali katika njia ya Allah. Hapa sasa aya zinarudia tena katika somo hilo la kutoa katika njia ya Allah kwa namna nyingine. Katika msururu wa aya hizi, aidha pana nyongeza ya baadhi ya masharti ya kutoa katika njia ya Allah. Pamoja na hilo tunafahamishwa malipo au fadhila anazopata mtu kwa kufanya matendo hayo ya utoaji. Aya hii mashuhuri kwa Waislamu inatoa mfano wa malipo ambayo Allah anamuhakikishia mtoaji wa mali. Kwa jambo moja Allah anaweza kulipa hadi mara mia saba au zaidi. Malipo ya kawaida ya kufanya mema yanaelezewa katika sura nyingine kama ifuatavyo: "Afanyae kitendo kizuri, atalipwa mfano wake mara kumi. Na afanyae kitendo kibaya hatalipwa ila sawa na ubaya huo (alioutenda) nao hawatadhulumiwa". (6:60) Kwa mujibu wa aya hii malipo ya kawaida ni moja kwa kumi. Ama kwa upande wa utoaji katika njia ya Allah malipo yana mfumo tofauti. Jambo hili linaonyesha umuhimu wa kutoa. Kwa wanadamu wengi wenye imani inayotingatinga suala la kutoa mali bila ya kuhakikishiwa kuwa na wao watapata kitu kingine limekuwa gumu. Watu hawa mara nyingi hupiga mahesabu ya kupata zaidi kwa kila senti unayoitoa, jambo ambalo halionekani kwa macho katika utoaji katika njia ya Allah. Pamoja na kuonyesha umuhimu wa kutoa aya hizi vile vile zimelengwa kuwahamasisha Waislamu kutumia mali zao katika njia ya Allah. Aya ya 262 "Wale wanaotoa mali zao kwa nia ya Allah, kisha hawafuatishi waliyoyatoa masimbulizi wala udhia, wao wana ujira wao kwa Mola wao, wala haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika". Katika aya hii linatajwa sharti au msingi mmoja wa kutoa katika njia ya Allah. Uchunguzi wa aya hii unaweza kutuonyesha kuwa wengi wa wale wanaojigamba kuwa wanatoa katika njia ya Allah huwa hawapati kitu kwa sababu ya kukosa agizo hilo. Si kwamba tu si ubinadamu bali ni jambo lenye kuchukiza sana kutokea mtu akamsaidia binadamu mwenzie lakini baada ya hapo akaanza kumsimbulia au kumsababishia maudhi mbalimbali. Masimbulizi yako ya viwango tofauti kuanzia mtu binafsi hadi kufikia upeo wa mataifa. Wako wale ambao huwasaidia wenzao kwa vitu fulani fulani na baada ya hapo huanza kupita wakimtangazia kuwa fulani hivi, fulani hivi. Wakati mwingine hufika kujisahau wakadai kuwa "kama si mimi asingeishi"! Au angetembea uchi na mararu yake!" Kwa upande wa mataifa ni jambo la fedheha na la udhalilishaji wa hali ya juu wakati wawakilishi wa nchi masikini wanapokabiliana na wale wa nchi matajiri kwenye vikao vya Paris Club. Kama si suala la nchi kwa kweli mtu binafsi asingeweza kustahamili masimango na kashfa anayoipata wakati wa kuomba katika vikao hivyo. Marais na Mawaziri wa nchi masikini wanafahamu vema udhalili wanaokuwa nao mbele ya nchi tajiri. Aya ya 263 "Kauli njema na kumsamehe (aliyekukosea) ni bora kuliko sadaka inayofuatishwa na udhia. Na Allah ndiye Mkwasi na Mpole". Allah katika aya hii anatumia njia ya ulinganisho wa mambo mawili – kauli njema na kusamehe kwa upande mmoja na sadaka inayofuatishwa na maudhi kwa upande mwingine – kuweka muongozo wa kutoa katika njia yake. Kauli hii ya Allah isichukuliwe kuwa sadaka inayofuatishwa na udhia nayo ni bora lakini kauli njema na kusamehe mtu aliyekukosea ni bora zaidi, la hasha. Aya inayofuatia chini inathibitisha hilo kwani inaeleza kuwa sadaka za aina hiyo huwa zinabatilika na hivyo hapana ubora. Kwa lugha nyingine, Muislamu wa kweli kama alivyosema Mtume (saw) ni yule ambaye anatoa sadaka yake kwa mkono wa kulia (kuume) bila ya mkono wake wa kushoto kujua. Utoaji mzuri ni ule unaofanywa kwa siri ingawaje uko wakati ambapo kutoa kwa jahara ni vizuri zaidi. Hata hivyo hakuna wakati ambapo masimango na maudhi yanaruhusiwa.
Aya ya 264 "Enyi mlioamini! Msiharibu sadaka zenu kwa masimbulizi na udhia, kama yule anayetoa mali yake kwa kuwaonyesha watu, wala hamuamini Allah wala siku ya mwisho. Basi hali yake ni kama hali ya jabali ambalo juu yake pana udongo, kisha ikalifikia mvua kubwa na ikaliacha tupu. Basi hawatakuwa na uweza (wa kupata) chochote katika walivyovichuma; na Allah hawaongozi watu makafiri". Hapa Allah analinganisha masimbulizi na udhia katika kutoa mali kuwa ni sawa na riya ile kutoa kwa ajili ya kujionyesha kwa wanadamu wengine na siyo kwa kutaka radhi za Allah. Hii ni picha halisi ya unafiki na utendaji wa wanafiki kwani sifa yao kuu ni kushindwa kuoanisha kati ya nia (yale yaliyo moyoni) na yale yanayotokea nje ya moyo wake na hivyo kuthibitisha kauli ya Allah kuwa hawa si watu wenye kuamini. Tendo la kutoa kinafiki siku zote ni la hatari na lisilo na manufaa yoyote kwa mtoaji wala kwa yule anayepewa. Ni kwa sababu hiyo, Allah akatoa mfano wa utoaji huo kulingana na mvua inayonyesha juu ya jabali lililofunikwa na mchanga kidogo juu yake ambao kwa kawaida hapana kitu kinachoweza kuota juu yake. Kutoa katika njia ya Allah kumelinganishwa au kupigiwa mfano wa mvua katika aya hii wakati jabali limefananishwa na ile nia mbaya ya kutoa kwa nia au kutoa na baadaye kufuatisha masimango. Mchanga kidogo ulio juu ya jabali ni sawa na ile picha wanayoipata wanadamu wengine ambao hawajui nia ya mtoaji kwani imefichika moyoni. Kikawaida mvua inaponyesha hutegemewa kuleta manufaa kwenye ardhi na hatimaye kwa wanadamu ambao wanaitumia ardhi hiyo kwa shughuli mbalimbali zikiwemo zile za kilimo. Hata hivyo, jambo hilo halitokei wakati mvua inapoanguka kwenye jabali lenye mchanga na kuliwacha jabali tupu ambalo halioteshi mmea wowote. Kitendo cha utoaji kinategemewa kiongeze hisia za wema au ucha Mungu kwa mtoaji lakini inapokosekana nia nzuri huwa hakina manufaa sawa na mvua inyeshayo juu ya jabali tu. Kwa lugha nyingine mali itolewayo kinyume na maagizo ya Allah haitofautiani na mali inayofisidiwa kwa mtoaji zaidi ya kuiharibu hiyo mali yenyewe. Aya inamalizia kuwataja watu hao wanaotoa kwa malengo mengine yasiyo ya kupata fadhila za Allah kama makafiri. Kafiri kwa hapa ni mtu asiye na shukrani au kukubali utoaji kwa lengo la radhi za Allah. Mtu huyu hastahili kuongozwa na Allah kwani hana anachokifanya kwa kutaraji
chochote kutoka kwake hivyo ameachiwa aende atakako.
|
YALIYOMO
TAHARIRI Majeshi ya nje kupelekwa Lesotho: Je, ni sera za Nguvumali? Nyumba ya Wakfu yageuzwa Baa
Dar
‘VAT’ yaingia Bakwata Same
Mchungaji asema hakuna mihadhara ya
kashfa
Maoni yetu: Masheikh tupeni Fatwa Safari yangu Ufini
Unyanyasaji wa kidini mashuleni, vyuoni
ukomeshwe
Wanaume toeni haki za wanawake
MAONI: Yesu ni yule yule Isa
Hatuna uwezo wa kuwapinga manabii
Ukoloni mwingine unaingizwa
nchini?
Khatamy ni ‘Gorbacheiv’ mwingine?
Tufuate Uislamu kwa vitendo na siyo
kwa maneno
AN-NUUR lina chuki na
Wakristo
Msiiparamie ovyo Biblia
Yaliyosemwa na viongozi wa dini juu
ya idadi ya watu 1989
Uislamu ulivyoingia Zanzibar -2 Waislamu Moro watakiwa kutoyumba
Wanawake Masasi wawataka Masheikh
kutangaza sheria za Allah
Ugaidi na Uislamu siyo kitu
kimoja – Sheikh Jongo
Sheikh Abbas awataka wananchi
Dodoma waepuke upuuzi
Vijana watakiwa kujiepusha
na ‘vijiwe’
Mafundisho ya Quran
Chakula na Lishe
|