|
|
| MAONI
Yesu ni yule yule Isa SEHEMU ya kwanza ya makala hii iliyoandikwa Saleh Ngoi ilichapishwa katika matoleo yetu ya nyuma na tuliahidi kuendelea matoleo yaliyofuatia. Kwa sababu za kiutendaji tulilazimika kuisitisha kwa muda, sasa endelea… KUUMBWA Mwinuke ameandika hivi: Qur’an inasema Isa (as) aliumbwa na Mwenyezi Mungu sawa na alivyoumbwa Nabii Adamu (Al Imran 59) hii ina maana kuwa Isa aliumbwa kutoka katika udongo. Biblia inasema Yesu alikuwako tangu milele yote kama Nafsi ya Mungu (Yohana 17:5 na I Petro 1:20) vile vile Biblia inasema alishuka toka mbinguni na kutwaa umbo la mwanadamu (Yohana 11:14). Yesu mwenyewe anasema yeye si wa ulimwenguni bali ametoka kwa Baba (Yohana 8:23 na 16:28) hii huoni kuwa ni tofauti? Mwinuke ndani ya Qur’an umesoma kwamba Mungu amemfananisha Bwana Issa (Yesu) na Nabii Adam kwa kuumbwa, je, kuna tofauti gani: Yohana 1:14: "Naye neno alifanyika mwili, akakaa kwetu nasi tukaona utukufu wake, utukufu kama mwana pekee atokaye kwa Baba amejaa nema na kweli". Qur’an 3:59: "Bila shaka hali ya Issa kwa Mwenyezi Mungu ni kama hali ya Adam, alimwumba kwa udongo, kisha akamwambia "kuwa" basi akawa. Hii ni haki inayotoka kwa Mola wako Basi usiwe miongoni mwa wanaofanya shaka". Mwenyezi Mungu yuko juu anasema: "Kuwa mimba" katika tumbo la Mariamu na saa ile ile mimba, hapa Mungu katumia NENO ndio maana ndani ya Biblia Bwana Yesu ameitwa kwa jina la NENO tena bila ya aibu mnajaribu kuumba Mungu kwa herufi yaani Neno ikiwa na herufi ndogo hiyo ni kauli lakini NENO ikiwa na herufi kubwa huyo ni Yesu. Qur’an 4:171: "Enyi watu wa kitabu! Msipindukie mipaka katika dini yenu, wala msiseme juu ya Mwenyezi Mungu ila yaliyo kweli. Masihi Isa bin Mariamu ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na ni kiumbe aliyeumbwa kwa TAMKO LAKE (NENO) tu, Mwenyezi Mungu alilompelekea Mariyamu. Na ni roho iliyotoka kwake Mwenyezi Mungu kama roho nyingine. Basi mwaminini Mwenyezi Mungu na Mitume yake wala msiseme WATATU, jizuieni na itikadi hiyo itakuwa bora kwenu. Bila shaka Mwenyezi Mungu ni Mungu mmoja tu. Ni mbali na Utakatifu wake kuwa ana mwana. Ni vyake vyote vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini na Mwenyezi Mungu ni Mlinzi wa kutosha. Kwa maelezo haya ya Bw. Mwinuka mimi nina imani kwamba huyu Bwana ameandika haya kwa kunakili kutoka kwa mtu mwingine kwa sababu Mwinuke amekubali kwamba Yesu wake wa Biblia amezaliwa na Mariamu ambaye ni mtu, mara anakataa kwamba Yesu hakuumbwa bali alishuka toka Mbinguni na kutwaa umbo la mwanadamu. Ili nijibu na kumfundisha vizuri bora nizitaje aya zake na nizijibu vema. Yohana 17:5 : "Na sasa Baba, unitukuze mimi pamoja nawe, kwa utukufu ule niliotoka nao pamoja nawe kabla ulimwengu kuwako". Hapa Bwana Yesu anaomba kwa Mungu ili atukuzwe pamoja na yeye (Mungu). Aya hii ni kweli kabisa kwa kila mwandamu kuonyesha unyenyekevu mbele ya Mola wake kama vile Mungu alivyosema katika Qur’an 66:12 "Tukampulizia humo roho yetu inayotokana na sisi akayashika maneno ya Mola wake na vitabu vyake na alikuwa miongoni mwa wanyenyekevu. Mpuliziaji roho alikuwa Mungu na Mungu anakaa juu mbinguni. Isaya 66:1 "Bwana asema hivi Mbinguni ni kiti chpangu cha enzi na duniani mahali pa kuweka miguu yangu mtanijengea nyumba ya namna gani? Na mahala angu pa kupumzika ni mahali gani? Mama Mariamu alikuwa duniani na Mungu yupo Mbinguni anakusudia kupulizia roho ya Yesu kwa Mariamu aliye duniani, hivyo ni lazima itoke juu na roho hiyo ni ya Yesu. Mwanzo 2:7: "Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi akampulizia puani pumzi ya uhai, mtu akawa nafsi hai". Baada ya kufanya haya, Mungu hana kati tena uzao unajiendesha wenyewe mpaka hii leo. Hivi unadhania Mungu aliumba akiwa ardhini! Hapana, aliumba akiwa mbinguni, hivyo roho za wanadamu kabla ya kutiwa ndani ya mimba za mama zetu kwanza zinakaa mbinguni, fahamu Mungu haumbi kila siku kama unavyofikiria. Qur’an 3:59: "Bila shaka hali ya Isa kwa Mwenyezi Mungu ni kama hali ya Adam; Aliumbwa kwa udongo kisha akamwambia "KUWA" basi akawa". Qur’an 4:1 "Enyi watu mcheni Mola wenu ambaye amekuumbeni katika nafsi (Asili moja) Na akamuumba mkewe (Hawa) katika nafsi ile ile (ya Adam) Na akaeneza wanaume wengi na wanawake wengi katika wawili hao (Adam na Hawa)". Mwanzo 2:18 "Bwana Mungu akasema, si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye". Mwanzo 2:21 "Bwana Mungu akamfanyia usingizi mzito, naye akalala, kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake. Na ubavu ule alioutwaa katika Adam Bwana Mungu akamfanya mwanamke. Akamleta kwa Adam. Aya zote hizi za Qur’an na Biblia zinatufahamisha jinsi wanadamu tunavyotoka katika nafsi moja ya Uumbaji. Hapa katika aya hii kuna mambo mawili, la kwanza Hawa hakuihitaji kupuliziwa pumzi puani kama Adam kwa sababu Hawa ni nyama ya Adam ambaye tayari alikuwa na pumzi ya Mungu. Pili, inatufahamisha kwamba, jinsi mwanaume anavyohusika moja kwa moja na upatikanaji wa mimba kwani bila ya mwanaume, mwanamke hapati mimba, lakini upatikanaji wa Nabii Isa (as) ambaye ni mwanaume aliyelala ndani ya mwili wenye asili ya udongo kama Adam, Mungu anaongeza kwa kutia roho na dongo la Isa tumboni mwa Mariam ambaye Isa huyo ndiye Yesu wa Biblia. Yohana 8:23 "Akawaambia, Ninyi ni wa chini, mimi ni wa juu, ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu". Maneno yako ni sawa kabisa kwamba Bwana Yesu si wa chini ni wa juu, na kama ni wa juu kweli si wa ulimwengu huu kwa sababu, Waislamu tunaamini kwamba Isa (as) ambaye ndiye Yesu amepaa mbinguni. Qur’an 4:158 "Bali Mwenyezi Mungu alimnyanyua kwake na Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu na mwenye hekima". Matendo 1:11 "Wakasema Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu, mbinguni, atakuja jinsi hiyo hiyo mlivyomuona akienda zake mbinguni". Bwana Mwinuka huyo ndiye Isa (as) ambaye wewe unamwita Yesu. Je, bado tu haujaamini kwamba sote tuko pamoja mpaka hapa si pamoja ya hapa tu nakuomba tuwe sote kwa imani, ibada na maamuzi ili tuiname kwa pamoja (sujuda) na tuinuke kwa pamoja tuwe chini ya uongozi wa Mtume Muhammad (saw). Kuzaliwa Qur’an inasema Isa alizaliwa chini ya Mtende tena wakati wa mchana (Mariamu 25) Qur’an haitaji mji aliozaliwa Isa, Biblia inasema Yesu alizaliwa katika mji wa Bethelehemu wakati wa usiku katika zizi la ng’ombe (Luka 2:7) Je, huoni kuwa hiyo ni tofauti? Kabla sijajibu hili ningependa kusahihisha mahala panaposema Isa (as) amezaliwa kwenye shina la mtende ni 19:23 "Kisha uchungu ukampeleka katika shina la Mtende (akawa anazaa na huku) anasema laiti ningekufa kabla ya haya, na ningekuwa niliyesahaulika kabisa". Unataka kujua mama Mariamu alimzaa Nabii Isa (as) katika mji gani. Qur’an 19:16-17 "Na mtaje Mariamu (humu) Alipojitenga na jamaa zake (akaenda) mahali upande wa mashariki wa Msikiti. Na akaweka pazia kujikinga nao tukampeleka Muhuisha sharia yetu JIBRILI akajimithilisha kwake kwa sura ya binadamu aliyekamili. Fahamu mama Mariamu alikuwa analelewa na Nabii Zakaria baba yake Nabii Yahya (Yohana Mbatizaji) kama nilivyokufahamisha kwenye mada ya Ukoo nilipokwambia Imrani wa Mwanzo (Kutoka 15:16) si huyu Imran baba yake Mariamu, huyu Imran aliye baba wa Mariamu alikuwa anaitwa Imran bin Yoshhim au Yoshim, lakini Imran baba yake Musa na Haruni alikuwa anaitwa Imran bin Kohath. (Kutoka 6:18-20). Hivyo Mzee Zakaria alikuwa anaishi Bethelehemu. Qur’an inatuambia katika mji huo mama Mariamu alikwenda mashariki ya Msikiti. Pamoja na Biblia inafahamisha kwamba mama Mariamu alizaa katika zizi la ng’ombe sisi hapo tuna mashaka mashaka napo kwa sababu nyingi sana, kwanza mama Mariamu alikuwa kwao hivyo isingewezekana kwenda zaa ndani ya zizi la ng’ombe. Pili kutokana na utukufu wa Bwana Yesu ni vigumu mama yule kwenda ndani ya zizi la ng’ombe kwenye uchafu wa kinyesi cha ng’ombe na mikojo, kwa kuamini hivyo ni kudhalilisha mazazi ya Bwana Yesu. Qur’an 19:30-31 "Yule mtoto akasema. Hakika mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu, Amenipa kitabu na Amenifanya Nabii. Na amenifanya mbarikiwa popote nilipo, Na ameniusia Sala na Zaka maadamu ni hai". Kwa aya hizi mbili, Mwenyezi Mungu anaonyesha kwamba Yesu ni kiumbe
mtakatifu wa Mungu hivyo Mungu hawezi akajaalia mazazi yake yawe mahala
pachafu. Pia Bwana Yesu anasema mimi nimebarikiwa popote nilipo! Au ni
nani miongoni mwetu anaweza akampeleka mke au ndugu yake kwenye zizi la
ng’ombe kuzaa?
|
YALIYOMO
TAHARIRI Majeshi ya nje kupelekwa Lesotho: Je, ni sera za Nguvumali? Nyumba ya Wakfu yageuzwa Baa
Dar
‘VAT’ yaingia Bakwata Same
Mchungaji asema hakuna mihadhara ya
kashfa
Maoni yetu: Masheikh tupeni Fatwa Safari yangu Ufini
Unyanyasaji wa kidini mashuleni, vyuoni
ukomeshwe
Wanaume toeni haki za wanawake
MAONI: Yesu ni yule yule Isa
Hatuna uwezo wa kuwapinga manabii
Ukoloni mwingine unaingizwa
nchini?
Khatamy ni ‘Gorbacheiv’ mwingine?
Tufuate Uislamu kwa vitendo na siyo
kwa maneno
AN-NUUR lina chuki na
Wakristo
Msiiparamie ovyo Biblia
Yaliyosemwa na viongozi wa dini juu
ya idadi ya watu 1989
Uislamu ulivyoingia Zanzibar -2 Waislamu Moro watakiwa kutoyumba
Wanawake Masasi wawataka Masheikh
kutangaza sheria za Allah
Ugaidi na Uislamu siyo kitu
kimoja – Sheikh Jongo
Sheikh Abbas awataka wananchi
Dodoma waepuke upuuzi
Vijana watakiwa kujiepusha
na ‘vijiwe’
Mafundisho ya Quran
Chakula na Lishe
|