AN-NUUR 
Na.169 Jamadul Akhir 1419, Oktoba 2 - 8, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
MASHAIRI

Kumbukumbu 

Salamu alaykum, jamani Isilamia, 
Namshukuru Karimu, Allahu Mola, Jalia, 
Nimeishika kalamu, ya moyoni kuyatoa, 
Matendo ni kumbukumbu, ya mtu kukumbukiwa. 

Matendo yakiwa mema, kumbu twaitarajia, 
Hata mabaya nasema, kumbukumbu hutujia, 
Na umfanyie mnyama, watu watasimulia, 
Matendo ni kumbukumbu, ya mtu kukumbukiwa. 

Nakiri mema matendo, yana faraja sikia, 
Unajihisi upendo, unapoyakumbukia, 
Mabaya yana uvundo, mawazoni kukujia, 
Matendo ni kumbukumbu, ya mtu kukumbukiwa. 

Hata ukishafariki, watu watakumbukia, 
Nguvu zako na mikiki, matendo kuwafanyia, 
Kwa wema au kwa dhiki, jinalo kulitambua, 
Matendo ni kumbukumbu, ya mtu kukumbukiwa. 

Beti hii ni khamsa, lengo linawafikia, 
Viongozi nawaasa, matendo kuyapimia, 
Wanapofanya mikasa, kuwatendea raia, 
Matendo ni kumbukumbu, ya mtu kukumbukiwa. 

Kadhia ya Mwembechai, kumbukumbu imekaa, 
Ni vurugu walidai, Salehe wakamuua, 
Walimuona hafai, kauliwa kama paa, 
Matendo ni kumbukumbu, ya mtu kukumbukiwa. 

Kukumbukumbu askari, make mkitambua, 
Mmeshaitaka shari, ya akhera na dunia, 
Chuki wetu hana heri, risasi kumfyatulia, 
Matendo ni kumbukumbu, ya mtu kukumbukiwa. 

Na kwa wale viongozi, uongo wanaotoa, 
Walioota mizizi, ya ukubwa Tanzania, 
Kumbukumbu waziwazi, vichwani mwatujengea, 
Matendo ni kumbukumbu, ya mtu kukumbikiwa. 

Askari Magereza, madaraka walitwaa, 
Mateso wakayakuza, kinamama kuumia, 
Walikuwa kama Pweza, kuwaweka kwenye jua, 
Matendo ni kumbukumbu, ya mtu kukumbukiwa. 

Kumbukumbu kwa Kitwana, Bungeni kufuatilia, 
Ukweli umeunena, Mola atakulipia, 
Umesaidia sana, viongozi wameloa, 
Matendo ni kumbukumbu, ya mtu kukumbukiwa. 

Hata Ponda na Magezi, wakitajwa twajua, 
Omar Juma yu wazi, Yusufu Makamba pia, 
Twajua walotuenzi, kwa Mwembechai kadhia, 
Matendo ni kumbukumbu, ya mtu kukumbukiwa. 

Kumbukumbu historia, vizazi kufuatilia, 
Nawe Waziri Amiri, watoto watakujua, 
Na tena wawe tayari, sheria kushikilia, 
Matendo ni kumbukumbu, ya mtu kukumbukiwa. 

Uongozi wa Mkapa, awamu hii twalia, 
Sheria wamezikwepa, maovu kutufanyia, 
Wengine tumeshaapa, CCM kutochagua, 
Matendo ni kumbukumbu, ya mtu kukumbukiwa. 

Msione tunasema, muda mrefu sikia, 
Kwa kweli limetuuma, Islamu kujifia, 
Uuaji kama nyama, iwe mwisho Tanzania, 
Matendo ni kumbukumbu, ya mtu kukumbukiwa. 

Mwl. Zazibu Iddi Ng’onda, 
S.L.P. 78, Shinyanga. 

Waislamu tumche Mungu  

Bisimillahi Rabbuka, Ubariki ummatia, 
Pia nijaze fanaka, nipate kusimulia, 
Tuhimizane hakika, Mola kukusujudia, 
Tumche Mungu dawamu, Janna tupate tulia. 

Mhariri msifika, litawanye shairia, 
Wapate soma hakika, yalo ndani ummatia, 
Tukimtii hakika, Mtume wetu Nabia, 
Tumche Mungu dawamu, janna tupate tulia. 

Islam kwa hakika, tubu kwa Mola Jalia, 
Na e atupe baraka, kiumbe kutujalia, 
Kheri nyingi na fanaka, zitufike ummatia, 
Tumche Mungu dawamu, Janna tupate tulia. 

Ramadhani ikifika, tubu pia kujutia, 
Madhambi kuyafunika, mema kujifanyia, 
Dawamu kutowa zaka, fitiri kujitolea, 
Tumche Mungu dawamu, Janna tupate tulia. 

Kipindi kinapofika, shughuli zote achia, 
Daima fika haraka, Sunna kujifanyizia, 
Kama zako nne raka, salama kutumizia, 
Tumche Mungu dawamu, Janna tupate tulia. 

Waheshimiwa wahusika, wazazi wetu na pia, 
Mola pia katamka, katika Qur’an pia, 
Nalo pia lahusika, ibada yako sikia, 
Tumche Mungu dawamu, Janna tupate tulia. 

Jamii inapasika, kusoma na kusikia, 
Elimu isiyo shaka, moyoni ije tulia, 
Kisha pasipo mashaka, muifundishe jamia, 
Tumche Mungu dawamu, Janna tupate tulia. 

Nane beti nimefikia, kalamu naachilia, 
Misikitini kufika. Kumuabudu Jalia, 
Peponi nipate tulia, Mola akiniridhia, 
Tumche Mungu dawamu, Janna tupate tulia. 

Wabillahi Taufiqi 

Ustaadh Muhammed Ibn Hakika Machellah, 
Almasjid Answary – Makonga, 
P.O. Box 298, 
Newala – Mtwara – TZ. 

Mkwezi (jibu) 

Kalamu ninaishika, kuandika gazetini, 
Salamu kwa wahusika, wote wa ulimwenguni, 
Bwanakheri msifika, jibu weka akilini, 
Bwanakheri omba Mungu, mkwezi tasalimika. 

Kwanza ninakupongeza, kwa kuhamia shambani, 
Maisha unayaweza, bila ya purukushani, 
Mungu atakuongeza, kwa mema ya duniani, 
Bwanakheri omba Mungu, mkwezi tasalimika. 

Mimi nilijiuliza, yametokana mageni, 
Ya mkwezi kujikwaza, katikati mnazini, 
Na nimepeleleza, jibu nimelibaini, 
Bwanakheri omba Mungu, mkwezi tasalimika. 

Tusibaki jiuliza, huyo ni mkwezi gani, 
Tena wacha jiumiza, huo ni mnazi gani, 
Hayo mambo ya Muweza, Muumba ulimwenguni, 
Bwanakheri omba Mungu, mkwezi tasalimika. 

Ni kweli na uhakika, mkwezi kwama mtini, 
Anaweza salimika, na kushuka mnazini, 
Kama ulivyotamka, lakufanya hulioni, 
Bwanakheri omba Mungu, mkwezi tasalimika. 

Usiende kwa waganga, wala hospitalini, 
Bora nenda kwa Maganga, muulize kwa makini, 
Mlingotini na Tanga, hayatokea kwa nini, 
Bwanakheri omba Mungu, mkwezi tasalimika. 

Bwanakheri tulizana, umuombe Bwana Mola, 
Ndio jambo la maana, nahimiza hala hala, 
Mkwezi mjuzi sana, kukwama jua ni hila, 
Bwanakheri omba Mungu, mkwezi tasalimika. 

Tamati nakamilisha, jibu hili lipokea, 
Kama halijakutosha, usisite kunambia, 
Zuberi sijachemsha, swali lako kutegua, 
Bwanakheri omba Mungu, mkwezi tasalimika. 

Zuberi Mohammed (Amiri) 
Box 61428, Dar es Salaam. 
 
Juu 
 
YALIYOMO 
 
 TAHARIRI 
Majeshi ya nje kupelekwa Lesotho: Je, ni sera za Nguvumali? 

Nyumba ya Wakfu yageuzwa  Baa Dar 
Na Mwandishi Wetu 

‘VAT’ yaingia Bakwata Same 
 Na Mwandishi Wetu 

Mchungaji asema hakuna mihadhara ya kashfa 
 Na Muhibu Saidi 

Maoni yetu: Masheikh tupeni Fatwa 

Safari yangu Ufini 
Ustaadh Ka-Batembo 

Unyanyasaji wa kidini mashuleni, vyuoni ukomeshwe 
Na Abuu Afahah 

Wanaume toeni haki za wanawake 
Na Zabibu Iddi Ng’onda Box 78, Mwadui 

MAONI: Yesu ni yule yule Isa 
Na Saleh Ngoi 

Hatuna uwezo wa kuwapinga manabii 
Na Elia Batendi, S.L.P. 538, DSM 

Ukoloni mwingine unaingizwa nchini? 
Sheikh Thabit H. Mbago,S.L.P. 21486,DSM 

Khatamy ni ‘Gorbacheiv’ mwingine? 
Na Athman Rajab 

Tufuate Uislamu kwa vitendo na siyo kwa maneno 
Mwandishi: Maalim Ali Bassaleh 

AN-NUUR  lina chuki na Wakristo 
Na Charles Kamuhabwa, DSA Mtwara 

Msiiparamie ovyo Biblia 
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa 

Yaliyosemwa na viongozi wa dini juu ya idadi ya watu 1989 
Na Rajab Rajab 

Uislamu ulivyoingia Zanzibar -2 

Waislamu Moro watakiwa kutoyumba 
Na Rajab Rajab, Morogoro 

Wanawake Masasi wawataka Masheikh kutangaza sheria za Allah 
Na Muhibu Saidi, Masasi 

Ugaidi na Uislamu siyo kitu kimoja – Sheikh Jongo 
Na Bakari Musa 

Sheikh Abbas awataka wananchi Dodoma waepuke upuuzi 
Na Abu Zubair, Dodoma 

Vijana watakiwa kujiepusha na ‘vijiwe’ 
Na Badru Kimwaga 

Mafundisho ya Quran 
Kutoa katika njia ya Allah: Al-Baqarah aya   261-263 

Barua za wasomaji 

Mashairi 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na Lishe 
Magonjwa yanayoathiri lishe 
  
   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita