|
|
|
Mwandishi: Maalim Ali Bassaleh WAPINZANI wanaposema kuwa Uislamu ulienezwa kwa upanga; Waislamu huja juu na kuwarudi hao wnaoeneza uongo huo, kwa hoja zilizo nzito. Kwa kweli dhana hiyo ni potofu. Kuna dalili na ushahidi wa kutosha kuthitibisha kuwa Uislamu ni dini ya amani na siyo dini ya vita. Amani hiyo ni baina ya binadamu na Muumba wake, na pia, baina ya binadamu na binadamu wenzake. Lakini kwa kuwa, siku zote, lengo la maadui limekuwa nikutaka kuifanya dini hii ichukize machoni kwa watu, ndiyo wakauchora Uislamu katika sura ya ukatili, vita na ugaidi. Ikiwa dini ya Uislamu ni dini ya amani kama Waislamu wanavyodai, na hivyo ndivyo ilivyo hasa, mbona basi matendo ya Waislamu yanaashiria katika shari shari na siyo katika amani? Jina la dini ni amani, lakini matendo ya wafuasi wake ni moto! Wakati wa uhai wa katuni ya vichekesho vya Chakubanga na Polo, safari moja alionyeshwa Chakubanga akiwaambia wenziwe aliokuwa amekaa nao pamoja, "Hebu na tuondoke haraka hapa. Wanausalama wale wanakuja; wakifika hapa tutakosa usalama!" Msanii aliyechora katuni hiyo alikusudia kutoa burudani kwa wasomaji wake, lakini hapo hapo alilenga kutoa ujumbe maalumu kwa jamii, juu ya ile tabia ya baadhi ya askari wachache wa Jeshi la Polisi, wenye tabia ya kuwasumbua raia wasio na hatia. Jeshi la Polisi lipo kwa ajili ya kulinda usalama wa raia, lakini kuna baadhi ya askari polisi, wanaotumia madaraka yao vibaya kusumbua raia wema bure, kwa ajili tu ya kutaka kuwatoa upepo. Chombo kilichokusudiwa kulinda usalama wa wananchi, watu wachache, wasio waaminifu wanakigeuza kuwa ni chombo cha kuwatisha na kuwasumbua raia. Je! Kwa vitendo hivyo viovu vya askari wachache, ndiyo tusema jeshi zima la polisi ni baya na halifai? Hivyo sivyo! Ubaya ni wa wale wakorofi wachache walioacha kufuata maadili ya kazi zao, na siyo jeshi lote la polisi. Kwa mantiki hiyo hiyo si sawa kuulaumu Uislamu kwa sababu ya vitendo vya watu wachache wasiofuata maadili sahihi ya Uislamu, na wanaofuata matamanio ya nafsi zao, lakini kwa vile tu wana majina ya Kiislamu ikaonekana labda ni Uislamu ndio uliowasababisha kutenda hivyo. Na hiyo nayo ni dhana potofu! Juzi nilipokuwa nikitazama televisheni, kipindi kiitwacho INSIGHT, kinachopeperushwa hewani na kituo cha CNN, mtayarishaji wa kipindi hicho, Bwana Jonathan Mann alikuwa akimhoji mwanadiplomasia mmoja wa Iran, juu ya mgogoro uliopambana moto hivi sasa baina ya Iran na Afghanistan. Bwana Mann alimwuliza afisa huyo, "Huwaje Iran na Afghanistan, ambazo zote mbili ni Jamhuri za Kiislamu zijengeane uhasama mkubwa kama huu?" Yule ofisa wa Iran alijibu kuwa ni kwa sababu Afghanistan hawafuati sawasawa vile Uislamu ulivyoagiza. Nina hakika kama na ofisa kutoka Afghanistan angalipatikana na kuulizwa, naye angalijibu kuwa Iran ndiyo isiyofuata mafunzo ya Uislamu! Lakini inaonekana mwulizaji kwa mujibu wa swali lake alikuwa akiwashangaa Waislamu, vipi waseme kuwa dini yao ni ya amani, halafu wao wenyewe wawe ni wenye kupenda ugomvi na vita tena baina yao wenyewe kwa wenyewe, wala siyo baina yao na maadui zao! Hivi sasa hali katika mpaka wa Afghanistan na Iran ni mbaya sana. Kumekuwa na wasiwasi wa kutokea vita baina ya nchi mbili hizo za Kiislamu wakati wowote ule. Iran imepeleka nguvu kubwa za kijeshi kwenye mpaka huo. Na imekuwa ikifanya mazoezi ya kivita tayari kuishambulia Afghanistan dakika yoyote. Afghanistan nayo imesema imejiweka tayari kujibu mashambulizi yoyote yatakayofanywa dhidi yake. Hali hiyo imetokana na kuuawa kwa wanadiplomasia saba wa Iran huko Afghanistan, katika mji wa Bamiyani, ambao ni makao makuu ya kikundi cha upinzani cha Kishia. Iran imedai kuwa watu hao wameuawa na kikundi cha Sunni Muslim Taleban, ambacho ndicho kinachoongoza serikali huko Afghanistan. Serikali ya Afghanistan nayo imetoa taarifa ya kukataa Taleban kuhusika na mauaji hayo. Na ikaishutumu Iran kwa kuwasaidia wapinzani wa Kishia waliopo katika mji huo wa Bamiyan. Kwa vyovyote vile mauaji hayo lazima yashutumiwe. Lakini mbona mauaji hayo yametokea katika hali ya utatanishi? Yasemekana wanadiplomasia hao waliuawa wakati wa harakati za kuuteka mji wa Mazar-I –Shariff, mji wa mwisho mkubwa uliokuwa mikononi mwa wapinzani. Inadaiwa kuwa maofisa hao walikuwa wakiwasaidia wapinzani wa Kishia katika jimbo hilo. Hata hivyo, kama walitambulikana kuwa ni maofisa wa ubalozi wa Iran, hapakuwa na uhalali wowote wa kuwaua. Zingalitumika njia za kidiplomasia kuwashughulikia kama kweli walikuwa wakiwasadia wapinzani. Mradi kwa kuwa kosa limekwishatendeka na wale waliokufa ndiyo hamekwisha kufa, hawatarudi tena, na nchi mbili hizo ni za Kiislamu na zimekubali kutekeleza sharia za Kiislamu, basi ni lazima watumie sharia hiyo kutatulia mgogoro huo. Kwanza wale wanaotuhumiwa kusababisha mauaji hayo wafikishwe katika vyombo vya sharia. Wakionekana kuwa wametenda hilo kwa makusudi wapewe adabu kwa mujibu wa sharia na kama itabainika kuwa mauaji hayo yalitokea kwa bahati mbaya na hayakupangwa, basi wafiwa wapewe fidia kwa vifo hivyo. Hakuna sababu ya kutaka kuupalilia uhasama unaoweza kupelekea kuvunjika kwa amani na kukosekana utulivu katika nchi hizo. Habari zisizothibitishwa zinasema eti Iran ina nia ya kuishambulia kijeshi Afghanistan. Lakini inasita kufanya hivyo mpaka inahakikishiwe na Marekani kuwa haitaingilia kati kukisaidia Afghanistan. Ndiyo maana Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo anakusudia kukutana na Waziri mwenziwe wa Marekani kupata uhakikisho huo. Kama habari hizo zina ukweli wowote inafaa Iran ichukue hadhari kubwa kabla ya kufanya uamuzi wa namna hiyo. Isisahau ule usemi maarufu wa Marekani wanaoupenda kuukariri mara kwa mara, kwamba Marekani haina rafiki wala adui wa kudumu bali ina maslahi ya kudumu. Inasemekana kuwa Iraq kabla ya kuivamia Kuwait, kwanza iliomba ridhaa ya Marekani, na ilipozipata ndiyo ikajiingiza Kuwait. Baadaye Marekani ikaigeuka Iraq na kuunda umoja wa kijeshi wa nchi mbalimbali na kuipiga Iraq na kuziharibu silaha za nchi hiyo. Marekani ilikuwa ikitafuta kisingizio cha kuziharibu nguvu za kijeshi za Iraq kwa vile zilikuwa ni tishio kwa Israel. Kabla ya hapo Israel ilikwishaishambulia Iraq kwa kisingizio kuwa Iraq ilikuwa ikitengeneza silaha za nyuklia. Na kumbe hata Israel yenyewe ilikuwa ina silaha za aina hizo. Na wala Marekani haikuona haja ya kuunda jeshi la kuipiga Israel kwa kitendo chake hicho. Kama ni uhalifu kwa nchi za Mashariki ya Kati kuwa na silaha za nyuklia, basi Israel inazo silaha hizo? Huko nyuma Marekani ilikuwa na ushirikiano mkubwa na Iran ilipokuwa chini ya utawala wa Shah. Lakini tokea kufaulu kwa mapinduzi ya nchi hiyo na kutangaza kufuata mfumo wa serikali ya Kiislamu, Iran ikageuka ni adui mkubwa wa Marekani. Uhasama huo umekuwa ukiendelea hadi hivi leo. Marekani imekuwa mara kwa mara ikidai kuwa Iran inasaidia ugaidi wa kimataifa na kwamba inataka kumiliki silaha za nyuklia. Je! Iran haioni kuwa kutafuta ridhaa ya Marekani kuishambulia Afghanistan kuwa huenda ukawa ni mtego wa kutaka kuzivunja nguvu za kijeshi za nchi hiyo, kwa vile, machoni kwa Marekani ni tishio kwa usalama wa Israel? Kiongozi wa juu kuliko wote nchini Iran Bwana Ali Khamenei amekaririwa akisema kuwa nchi yake haitaishambulia Afghanistan. Na sisi hatuna sababu ya kuyatilia mashaka maneno yake hayo, hasa kwa vile kiongozi wa nchi tu, bali pia ni kiongozi wa kidini na tena ni mwanachuoni mwenye kutegemewa. Ikiwa Allah (sw) anasema: " na suluhu ni kitu bora", (An Nisaa 4:128). Kwa nini hatutafuti suluhu, tukafuata kile kilicho bora? Muislamu wa kweli ni yule anayeifuata Qur’an Tukufu kwa vitendo na siyo kuisoma tu kama nyimbo! Qur’an inasema: " Na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake wala msizozane, msije mkaharibikiwa, na zikapotea nguvu zenu. Na subirini. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanaosubiri". (Al Anfaal 8:46). Waislamu tuzinduke! Tusiziangamize nguvu zetu kwa mikono yetu wenyewe. |
YALIYOMO
|