|
|
|
Wanaume toeni haki za wanawake kuepusha ufisadi Na Zabibu Iddi Ng’onda Box 78, Mwadui AWALI ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu (sw) kuwapa moyo Bi. Zuhra Tajiri na Halima Issa kwa makala zao katika gazeti hili kuchangia mada hii na kutupa ari wengine kuipapasa kwa kuguswa na ukweli uliopo. Mwenyezi Mungu awajazie kheri duniani na akhera. AMIN. Mimi katika mchango wangu pamoja na kukubaliana na yote waliyosema wenzangu naendelea kuwalaumu Masheikh, Wazazi na wenzetu wanaume kwa kuwaacha mabinti wanaadhirika hadi kuzaa nje ya ndoa na wenyewe wapo, mwisho kupatikana kizazi kisicho cha Kiislamu, kwa maana ya watoto wasio na msimamo wa dini kisha kudhoofisha Uislamu. Eee ndugu zangu Waislamu! Tuamke kuuendea Uislamu kikamilifu. Upande wa Masheikh kila siku wanahimiza swala, swala, swala tano. Al-hamdulilahi kwa jambo hili naweza kuwapa 90%. Lakini wameghafilika kabisa katika suala la ndoa. Wameshindwa kuwaelimisha vijana wetu na kuwakemea kwa bidii kama wanavyoamrisha swala. Vijana wanapotea na wao wapo. Kosa la kukaa na vimada na kuoa ndoa za serikali ndiyo limeshamiri na kuchanua kama maua. Hata wale wanaojaaliwa kuwa hawachagui mchumba kwa hadithi za Mtume (saw). Huenda Masheikh wetu wangelivalia njuga jambo hili la ndoa, hali isingekuwa kama ilivyo sasa ambapo kila mmoja anayo macho ya kushuhudia na masikio ya kusikia. Vijana au wanaume kwa ujumla wanachagua wachumba kwa kipengele kimoja tu kati ya vipengele vikuu vinne alivyoamrisha Mtume (saw) katika kuchagua mchumba, yaani uzuri basi! Ana nywele nyingi, ana macho mazuri, ana shingo ndefu akigeuka utapenda n.k. kuliko binti mcha Mungu. Matokeo yake ni hatari inayokuja baadaye kwa wengi ya kutokuelewana kwa kila hali kama mume huyo ni mcha Mungu, hivyo kushuhudia ndoa zikivunjika kila siku au mifarakano na watoto kubaki hawana maadili kwa kukosa malezi ya baba na mama katika Uislamu. Na hao watoto ndiyo tunaowategemea kuwa Masheikh wa kesho. Lau kama mume atavumilia na kubaki kuumia tu basi bado watoto hawatapata malezi ya Kiislamu kwa sababu mama ndiye mlezi mkuu anayekuwa karibu na watoto kila wakati. Kama yeye anatia dawa kichwani na bintiye atamruhusu na kumpamba kwa kila pambo akishapendeza ndiyo kwanza anamtuma mbali ili aonekane. Matokeo yake ni ufisadi na malezi ya mama huyo na kusababisha ummah wa Kiislamu kupotea, Lakini hayo yamesababishwa na wale wasiotaka kuoa wacha Mungu. Shime ndugu zangu Waislamu! Oeni wacha Mungu ambao ni wengi sana hasa katika miji ya Dar es Salaam na Mwanza kama alivyosema Bi. Halima Issa. Na wengine ni wale wanaosilimu kutoka kwenye ukafiri na kuijia njia ya haki (din ya Mwenyezi Mungu) Uislamu. Je, hamuwaoni? Mnataka waolewe na nani? Hamjui kwamba mtaulizwa kesho mbele ya haki? Mtamjibu nini Mwenyezi Mungu enyi wanaume wa Kiislamu! Oeni hao mpate utulivu. Hamuwezi kupata utulivu bila kuoa wacha Mungu. Usipokuwa na utulivu katika ndoa yako hata hizo swala zako tano wanazozikazania Masheikh kwa bidii wakasahau utulivu. Na kama ni hivyo unategemea malipo gani kwa swala hizo mbele ya Mwenyezi Mungu? Hivyo viongozi wetu waamrishe swala ambazo ndiyo ufunguo wa peponi sambamba na mambo mengine kwani yote ni amri ya Allah (sw) na yanategemeana. Wazazi nao wamechangia kuathiri sanandoa za mabinti zao kwa kuwalazimisha kuolewa na wasiowataka ili hali binti ana haki ya kuchagua mchumba amtakaye. Hupelekewa tu bila kuchunguza mienendo ya hao waoaji na matokeo yake ni kama nilivyokwishasema. Enyi wazazi zindukeni! Waulizeni Masheikh na someni vitabu mpate mafundisho ya Mtume (saw) na mwenendo wa masahaba zake. Acheni kuona haya kufuata sunnah za Mtume (saw) hadi mnafikia kuwatokomeza mabinti zenu katika maasi. Hamjui hayo siku ya malipo? Kumuomba kijana amuoe binti yako ni suna wala si aibu hata kidogo kama mnavyodhani kuliko kusubiri tu ajaye ndiye huyo huyo bora mwanangu ameolewa au binti anakaa hadi anapata mtoto wa nje ya ndoa. Matokeo yake ni kama nilivyokwishasema. Angalia mafunzo haya ya Maswahaba. Sayidna Omar (ra) alimwendea Sayidna Abubakar (ra) kutaka amuoe mwanawe Bi. Hafsa, lakini hakumjibu kitu. Akamwendea Sayidna Uthman (ra) akakataa. Hapo Sayidna Omar moyo wake ukaharibika na kwenda kumshitakia Mtume (saw), Mtume akamtoa huzuni kwa kumwambia, "Hafsa ataolewa na mume bora kuliko Uthman, na Uthman ataoa mke bora kuliko Hafsa". Kipindi hicho Sayidna Uthman alikuwa katoka kufiwa na mkewe Bi Ruqaya mtoto wa Mtume (saw). Hivyo Mtume akamuoa Bi. Hafsa na Uthman akamuoa Bi. Umukulthum mwana mwingine wa Mtume (saw). Hapo ndipo Omar akafurahika kweli kweli. Baada ya hapo Sayidna Abubakar alimuomba raadhi Sayidna Omar na kumwambia aliwahi kumsikia Mtume (saw) kutaka kumposa Bi. Hafsa. Ila alishindwa kulisema hilo kwani alikuwa hajaruhusiwa. Naye Sayidna Uthman (ra) akamuomba radhi Sayidna Omar (ra) na kumweleza kuwa alikuwa na tamaa ya kuozeshwa binti wa pili wa Mtume (saw). Basi Sayidna Omar akawasamehe na kuishi salama katika kuuendeleza Uislamu hadi umetufikia sisi leo. Je, kati yetu ndugu zangu Waislamu kuna mbora kuliko Sayidna Omar (ra) aliyemtafutia bintiye mume? Na ambaye amebashiriwa pepo na Mtume (saw)? Hivyo wazazi na wanaume wa Kiislamu hasa vijana wetu yale makosa mliyokwishayafanya msiyarudie kamwe! Tufuate mafunzo ya Uislamu. Amesema Mtume (saw) "Mwanamke huolewa kwa mambo manne, dini yake (ucha Mungu), mali yake, uzuri wake na nasaba yake. Basi wewe jitwalie pato kwa mwenye dini. Usipofanya hivyo, fahamu mikono yako itapata mchanga (yaani utakorofika)". Mwisho nawahimiza mabinti kupitia gazeti letu tukufu la AN-NUUR kuanzisha
kamati ya NUSRA, jitokezeni kwa wingi bila aibu kutafuta wenzi wenu mnaowapenda
na watakaowafaa kisha kuwaelimisha wazazi wenu kwa upole ili tupate nusra
na tuepuke lawama mbele ya Mwenyezi Mungu siku ya Qiyama kwa kufuata nyayo
za Bi. Khadija (ra) vile alivyofanya kwa Mtume (saw). Haya wenzangu uwanja
uko wazi!
|
YALIYOMO
TAHARIRI Majeshi ya nje kupelekwa Lesotho: Je, ni sera za Nguvumali? Nyumba ya Wakfu yageuzwa Baa
Dar
‘VAT’ yaingia Bakwata Same
Mchungaji asema hakuna mihadhara ya
kashfa
Maoni yetu: Masheikh tupeni Fatwa Safari yangu Ufini
Unyanyasaji wa kidini mashuleni, vyuoni
ukomeshwe
Wanaume toeni haki za wanawake
MAONI: Yesu ni yule yule Isa
Hatuna uwezo wa kuwapinga manabii
Ukoloni mwingine unaingizwa
nchini?
Khatamy ni ‘Gorbacheiv’ mwingine?
Tufuate Uislamu kwa vitendo na siyo
kwa maneno
AN-NUUR lina chuki na
Wakristo
Msiiparamie ovyo Biblia
Yaliyosemwa na viongozi wa dini juu
ya idadi ya watu 1989
Uislamu ulivyoingia Zanzibar -2 Waislamu Moro watakiwa kutoyumba
Wanawake Masasi wawataka Masheikh
kutangaza sheria za Allah
Ugaidi na Uislamu siyo kitu
kimoja – Sheikh Jongo
Sheikh Abbas awataka wananchi
Dodoma waepuke upuuzi
Vijana watakiwa kujiepusha
na ‘vijiwe’
Mafundisho ya Quran
Chakula na Lishe
|