AN-NUUR 
Na.169 Jamadul Akhir 1419, Oktoba 2 - 8, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
 
Safari yangu Ufini 

Ustaadh Ka-Batembo 

Matata Uwanja wa Ndege 

BAADA ya urasimu mkubwa ulionuka rushwa katika kufuatilia upatikanaji wa pasi hatimaye nilikuwa uwanja wa ndege Dar es Salaam kwa safari kuelekea Helsinki Mji Mkuu wa nchi ya Ufini (Finland) iliyopo juu kaskazini mwa dunia. 

Ilikuwa ni saa kumi na mbili na nusu jioni, uwanja wa ndege ulizingirwa na maaskari wa kila aina tangu wale wa kuzuia fujo na hata maakachero wa FBI. Haikuwa rahisi hata kuagana vizuri na wasindikizaji nahaswa kama wataonekana wana ndevu nyingi au shungi na mabaibui. 

Hii ni kwa kuwa siku tano tu zilizopita, ofisi za ubalozi wa Marekani nchini Tanzania na Kenya zililipuliwa na waliodaiwa kuwa ni Waislamu wenye siasa kali. Kama ni kweli wewe na mimi natujui. 

Baada ya kukurukakara, saa moja kamili nilishakuwa kwenye ndege ya Shirika la Uingereza. Nilivua viatu na kufunga mkanda mara baada ya kukaa. Alhamdulillah nilikumbuka mtu mmoja aliyepatishwa tabu na afisa wa uhamiaji nusura achelewe ndege. Kisa alikuwa na pasi kubwa yenye kurasa nyingi mithiri ya kitabu cha hekaya za Abunuwasi. 

Punde hivi ndege ilianza safari. Nilileta dua ya ‘Subhanalladhi Sakharalana’ nikainamia kuswali magharibi pamoja na isha. Baada ya safari ya usiku mzima kupitia Entebe, Uganda tuliwasili London Gatwick saa kumi na moja alfajiri kwa saa za Uingereza, Baada ya mapumziko ya masaa manne hivi niliingia katika ndege nyingine ndogo kuelekea Helsinki. Nilifika Helsinki saa tano asubuhi kwa masaa ya Finland na huku Afrika ya Mashariki. 

Kupitwa na Alfajiri 

Baada ya kupokelewa na wenyeji wangu, nilipelekwa hadi Tikkuvilla-Vantaa ambako nilipangiwa katika Hoteli. 

Siku iliyofuata ilikuwa ni Alhamisi. Nilishaitega saa yangu ili niamke mapema kwa swala ya Alfajiri. Lahaullah wa Laquatta! Saa ilipogonga saa kumi na moja jua lilishatoka zamani. Nje kulikuwa kweupe na hata taa za barabarani zilishazimwa nikabakia kupiga astaghafirullah. Nilitawadha na kuswali nikijua labda saa yangu imepoteza majira. 

Baadaye nilikumbuka kuwa wenyeji wangu walipata kunieleza kuwa kuna msimu ambapo Finland huwa kuna mchana mrefu kuliko usiku. Hivyo kwa wakati huo jua lilikuwa likitoka saa kumi na robo usiku na kuzama saa 4.30 usiku. 

Pia ifikapo mwezi wa Oktoba hadi Januari Finland huwa giza kabisa na miezi ya Mei – Julai ni kinyume chake. 

 

Viitakivi mpaka Ilslalmi 

Majuma mawili ya kwanza yalikuwa ni yenye ratiba ngumu. Tulisafiri kwenda mji mdogo wa Viitari ambapo tulikuwa na warsha ya siku tatu iliyoitwa ‘Morogoro semina’ warsha hii iliandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Finland liitwalo UHUSIANO. Nilitoa mada juu ya matumizi ya michoro ya katuni katika mawasiliano. 

Jumatatu Agosti 17, tulirejea Helsinki ambapo nilitoa mada tena katika mkutano na waandishi wa habari ukumbi wa KEPA. Siku ya Jumanne nilifanya maandalizi ya safari kwenda Ilsalmi kwa treni. 

Hii ni mara ya kwanza kusafiri peke yangu katika nchi hii kondakta wa treni alipogundua kuwa mimi ni mgeni aliniahidi kunigongea chumbani kwangu ili kuniamsha mara treni ifikapo Ilslami. Alizungumza huku akitoa ishara kwani hakukua hata neno la Kiingereza. 

Jambo moja nililojifunza ni kuwa japo Wafini ni watu wanaopenda kujali mambo yao binafsi tu lakini hawasiti kutoa msaada pale anapojua kuwa unahitaji msaada wake. Kwani treni ilipokaribia kituo cha Ilsalmi kiasi kama saa 10.58 yule kondakta tayari alifika mlangoni kwangu tayari kunigongea. 

Hata niliposhuka bado alikuwa akinielekeza wapi naweza kupata taxi. 

Baada ya kutembelea maeneo mbalimbali na kuona shughuli za shirika la Ilsalmen Kenypaja Ijumaa Agosti 21, 1998 nilihadhiri katika chuo cha Ilsalmi Polytechnic na kuwa katika safari kurejea Helsinki. 

Vaasa 23 – 26/8/1998 

Jumapili ya Agosti 23, 1998 nilikuwa safarini tena kuelekea mji mwingine wa Vaasa ambako nilialikwa na shirika la Vaasa Association. 

Baada ya kutoa mhadhara juu ya matumizi ya michoro katika mawasiliano chuo cha International Baralbrate na kufundisha katika shule kadhaa kwa muda wa siku tatu nilirejea tena mji mkuu wa Helsinki. 

Katika safari zangu zote nilijifunza mambo makubwa mawili. Kwanza ambapo wanafunzi hugawanywa katika makundi kutokana na mfumo wa elimu toka chekechea hadi vyuo vikuu ni tofauti kabisa na hapa kwetu. 

Pili, Wafini ni watu wenye bidii ya kazi kwa maana ni wenye kujituma. Muhimu zaidi ni kwamba chochote wanachofanya huangalia zaidi kitafaa vipi kesho. Mfano mzuri unaoekana katika ufundi selemala hasa walivyo stadi. Hata kigoda kidogo cha jikoni hutengenezwa ili kutumike hata kwa zaidi ya miaka mia. 

Kukutana na Waislamu 

Kwa muda wote wa majuma mawili ya kwanza sikuweza kupata nafasi ya kuswali swala ya jamaa na kukutana na Waislamu. 

Alhamisi ya Agosti 28, nilifanya mawasiliano kwa simu na kijana mmoja wa Kisomali ambaye nilisafiri naye katika treni toka Vaasa kwenda Helsinki. Alinifahamisha kuwa alikuwa ni mhitimu katika chuo cha Helsinki University of Science and Technology lakini akiwa bado si mwajiriwa. 

Baada ya mawasiliano hayo nilipatiwa anuani ya Msikiti Mkuu wa Helsinki Masjid Hudaa ulioko 27 Annankatu. Siku ya Ijumaa Agosti 29, nilifika Msikitini. 

Msikiti haukuwa kama tulivyozoea. Ni jumba tu la ghorofa lisilokuwa na minara wala spika za nje kwa ajili ya adhana. Msikiti uligawanyika katika kumbi tatu tofauti na walikuwepo Waislamu takriban mia mbili. 

Baada ya swala ya Ijumaa nilikutana na baadhi yaWaislamu na kuzungumza nao kwa muda mfupi. 

Kwa kuwa wengi walikuwa wakikimbilia katika shughuli zao mmoja wa viongozi Ustaadh Mohammed Djaloh aliniahidi kuja kunichukua hotelini nilipofikia katika mji mdogo wa Vaasa ili nihudhurie mkutano wao ambao hufanyika kila siku ya Jumapili baada ya adhuhuri. 

Baada ya kuswali adhuhuri Msikiti wa Itakeskes tulienda ukumbi wa mikutano ulio jirani na Msikiti huo ambao hutumiwa na wanaharakati hao wa Finnish Malticultural Da’awa Association. Nilitambulishwa na Ustaadh Mohammed Djaloh na kupewa nafasi kuelezea hali halisi ya Uislamu Tanzania. 

Ni mambo mengi yanayotokea huku ambayo hawakuyafahamu kuhusu Uislamu na hivyo nilisisitiza kuwepo na ubadilishanaji wa habari baina ya mashirika yao ya Kiislamu kati ya Tanzania na Finland. Hii itaweza kujenga uhusiano wa karibu zaidi na kushikamana kwa dini ya Mwenyezi Mungu. 

Kisha Ustaadh Abdoul Majid aliendesha darasa kwa kutoa mada juu ya familia ya Kiislamu. Washiriki wengi walionekana kuchangia. Washiriki wa darasa hili la kila Jumapili hufikia hadi arobaini. 

Hali ya Uislamu Finland 

Kwa mujibu wa Bwana Mohammed Djaloh Uislamu unatambuliwa na serikali ya Finland tangu mwaka 1925. Lakini tangu wakati huo Waislamu bado ni wachache. 

Awali walikuwepo Waislamu toka Uturuki na nchi kama Iran, Yugoslavia ya zamani na nchi jirani yake. Katika mwanzo mwa miaka ya tisini Waislamu wamekuwa wakiongezeka. 

Waislamu wote wanasali pamoja katika Misikiti yote mitano iliyopo Helsinki na miji mingine ya jirani ya Espoo na Vantaa. Lakini katika maswala ya kijamii na harakati wamegawanyika katika makundi matatu. 

Kwanza kuna Wasomali ambao ni kundi kubwa na walio wengi huishi kama wakimbizi! Kwa kiasi fulani wamejitenga na kujiona kama jamii tofauti kama ilivyo huku. Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwapo na Wasomali kati ya elfu tano na elfu sita nchini Finland. 

Pili, kuna Waarabu ambao kwa kiasi fulani hushirikiana na Waislamu weusi toka Afrika katika harakati za kuendeleza Uislamu. 

Hata hivyo, kuna matatizo katika masuala ya uongozi. Hivi karibuni tu aliletwa Imam wa Kiarabu katika Masjid Huda ambaye hajui lugha nyingine isipokuwa Kiarabu tu badala ya Ustaadh Mohammed Issac Sherif ambaye ni Mgambia. 

Kwa sasa Ustaadh Mohammed Sherif husafiri kati ya Helsinki na Stockholm Sweden kwa ajili ya harakati za Uislamu na kutoa hotuba katika Msikit Mkuu wa Stockholm. 

Ama kuhusu Wafini wenyewe wengi ambao wamefikishiwa ujumbe wa Kiislamu wameanza kusilimu. Kwa ujumla Wafini walio wengi si wenye kufuata mambo ya dini japo Kanisa kubwa huko ni Walutheri liitwalo Orthodox lakini likiwa na waumini wachache sana. 

Mpaka sasa kuna umoja wa wanawake wa Kiislamu wa Kifini (Suomen Islamilainen Yndyskunta) ambao una wanachama karibu hamsini. 

Moja ya shughuli zao katika kuendeleza Uislamu Finland ni kuchapisha gazeti ANNUUR Valo ambalo huchapishwa kwa lugha ya Kifini na kutolewa kila mwezi. 

Tatizo kubwa ambao Waislamu wa Finland wanakabiliwa nalo ni kwamba mpaka sasa hawajaruhusiwa kujenga majengo yao ya Misikiti. Kwa hiyo Misikiti yote ni ya kupanga. 

Sababu kubwa inayozuia ujenzi wa Misikiti ni minara yenye spika za kutolea adhana ambazo wanahofia "zitawabughudhi" baadhi ya watu. Ni mji mmoja tu wa Malmo ulioko Sweden ambao mpaka sasa wana Msikiti mkubwa wenye minara. 

Helsinki – Stockholm 

Agosti 30, 1998 tulikuwa safarini kwenda Stockholm Sweden kufungua maonyesho ya Katuni za Afrika Mashariki. 

Tulikaa Stockholm kwa muda wa juma moja na nikakutana na Waislamu wa huko kwa muda mfupi tu. Shughuli zilikuwa nyingi na mara kwa mara nililazimika kuswali katika chumba maalum ndani ya Maktaba ya Comics Serieteket. 

Siku tatu kabla ya kurudi Tanzania nikiwa na rafiki yangu ambaye ni Mfini mwenye asili ya Kiswid tulikuwa ndani ya meli kubwa ya Viking Line yenye ghorofa saba hivi tukirejea Helsinki. 

Alinieleza kuvutiwa kwake na jinsi nilivyotekeleza ibada ya swala hata tukiwa tangu melini hadi katika maktaba japokuwa yeye alisema hana dini yoyote anayofuata. Anaupenda sana Uislamu na amekaa na Waislamu huko Sudan kwa miaka kadhaa. Hata hivyo bado ana wasiwasi kuhusu sura ya Uislamu kama inavyoonekana kutoka mataifa ya Magharibi. 

Alionekana kusita kidogo na kisha akanitupia swali; "Unamuonaje Usama bin Ladin?" 

Jibu lilinitoka kama mshale ‘Nani anajua?’ huenda Usama ni Che mwingine. 

‘Mnnh’ aliitikia na kutoa tabasamu kisha alianza kunihadithia alivyotembelea Cuba miezi mitatu iliyopita na kuona mwanamapinduzi wa Cuba Che Guevara aliyeuawa miaka 31 iliyopita. 

 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
TAHARIRI 
Majeshi ya nje kupelekwa Lesotho: Je, ni sera za Nguvumali? 

Nyumba ya Wakfu yageuzwa  Baa Dar 
Na Mwandishi Wetu 

‘VAT’ yaingia Bakwata Same 
 Na Mwandishi Wetu 

Mchungaji asema hakuna mihadhara ya kashfa 
 Na Muhibu Saidi 

Maoni yetu: Masheikh tupeni Fatwa 

Safari yangu Ufini 
Ustaadh Ka-Batembo 

Unyanyasaji wa kidini mashuleni, vyuoni ukomeshwe 
Na Abuu Afahah 

Wanaume toeni haki za wanawake 
Na Zabibu Iddi Ng’onda Box 78, Mwadui 

MAONI: Yesu ni yule yule Isa 
Na Saleh Ngoi 

Hatuna uwezo wa kuwapinga manabii 
Na Elia Batendi, S.L.P. 538, DSM 

Ukoloni mwingine unaingizwa nchini? 
Sheikh Thabit H. Mbago,S.L.P. 21486,DSM 

Khatamy ni ‘Gorbacheiv’ mwingine? 
Na Athman Rajab 

Tufuate Uislamu kwa vitendo na siyo kwa maneno 
Mwandishi: Maalim Ali Bassaleh 

AN-NUUR  lina chuki na Wakristo 
Na Charles Kamuhabwa, DSA Mtwara 

Msiiparamie ovyo Biblia 
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa 

Yaliyosemwa na viongozi wa dini juu ya idadi ya watu 1989 
Na Rajab Rajab 

Uislamu ulivyoingia Zanzibar -2 

Waislamu Moro watakiwa kutoyumba 
Na Rajab Rajab, Morogoro 

Wanawake Masasi wawataka Masheikh kutangaza sheria za Allah 
Na Muhibu Saidi, Masasi 

Ugaidi na Uislamu siyo kitu kimoja – Sheikh Jongo 
Na Bakari Musa 

Sheikh Abbas awataka wananchi Dodoma waepuke upuuzi 
Na Abu Zubair, Dodoma 

Vijana watakiwa kujiepusha na ‘vijiwe’ 
Na Badru Kimwaga 

Mafundisho ya Quran 
Kutoa katika njia ya Allah: Al-Baqarah aya   261-263 

Barua za wasomaji 

Mashairi 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na Lishe 
Magonjwa yanayoathiri lishe 
   

 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita