|
|
| Waislamu
Moro watakiwa kutoyumba
Na Rajab Rajab, Morogoro WAISLAMU nchini wametakiwa wasikubali kuyumbishwa na sera za kimagharibi zenye malengo ya kusambaratisha Uislamu na badala yake wawe imara katika kufuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu na kupinga yale yote yanayokwenda kinyume nao. Wito huo ulitolewa Ijumaa iliyopita na Ustaadh Abadallah Kombo wakati wa hotuba ya Ijumaa katika Msikiti wa Uwanja wa Ndege mjini hapa. Kauli hiyo inakuja siku chache baada ya wanafunzi wa shule za msingi mjini hapa kuanza kufundishwa elimu ya ngono na kugaiwa kondom. "Waislamu tuwe na msimamo kutokomeza hali hii ya vijana wetu wadogo kufundishwa elimu ya ngono na kupewa mipira ya kufanyia zinaa (kondom) kinyume cha hivyo, vijana wetu wataharibikiwa mapema na wazazi watawajibika kujibu uharibifu wowote utakaotokea mbele ya Mwenyezi Mungu", alisema Ustaadh Kombo. Akinukuu vifungu mbalimbali vya Qur’an na Sunnah, Ustaadh Kombo amesema kuwa siku zote makafiri hawataufurahia Uislamu na Waislamu mpaka wahakikishe mila zao zinafuatwa, hivyo wameamua kuwaopa watoto wadogo kondom kwa lengo la kubomoa maadili ya Uislamu na kuendeleza zinaa na magonjwa ya kuambukiza. "Wazazi wa Kiislamu msije mkashangaa watoto wenu wakiwaletea mimba na vitoto vichanga huku wakiwa bado shuleni, kuweni tayari watoto wenu wameshaidhinishiwa kufanya hivyo kwa kupitia elimu ya ngono", aliendelea kuwaasa Waislamu Ustaadh Kombo. Wakati huo huo, wazazi kadhaa mjini hapa wameendelea kushtushwa na mpango ulioanzishwa na serikali wa kufundisha watoto wadogo elimu ya ngono na wanajiandaa kutoa malalamiko yao rasmi kwa serikali kufuatia kuanza kuyaona mabadiliko ya kitabia kwa vijana wao. "Nilimsikia mtoto wangu akiongelea mipira ya kiume (kondom) na mwenzie, hali ambayo ilinishtua na kunifanya nimuulize ndipo alinifahamisha kuwa siku hiyo walikuwa wamefundishwa habari hizo, hivyo wamekuwa wanakumbushiana", alisema mzee mmoja wa Uwanja wa Taifa ambaye hakupenda jina lake liwemo gazetini. Katika kuonyesha kukasirishwa zaidi na jambo hili, wazazi kadhaa mjini hapa wamedhamiria kwenda kwa walimu wakuu mashuleni na kupinga watoto wao kufundishwa mambo ya ngono. Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hzi umebaini kuwepo kwa zoezi la kufundishwa watoto wa shule za msingi somo hilo ambapo wanatolewa shuleni na kwenda kufundishwa katika kituo kimoja kinachojihusisha na masuala ya ugonjwa wa ukimwi. Wasema kutofuata sheria za Kiislamu ndio chanzo cha matatizo yote Na Muhibu
Saidi, Masasi
JUMUIYA ya Wanawake Waislamu Masasi (O.M.W.) imewataka viongozi wa Kiislamu nchini kutominya ndimi zao kubainisha sheria za Allah (sw) na kumfumbia macho adui wa Allah, anayepinga kutekeleza sheria zake katika jamii. Aidha akina mama hao wamepinga vikali kiongozi wa Kiislamu kutumia fursa yoyote kutoa msisitizo wa kumtii kiumbe wakati anaiacha jamii ya Kiislamu inateketea kwa kukosa nafasi katika nyanja muhimu. Akina mama hao waliyasema hayo hivi karibuni kupitia risala yao waliyoiwasilisha katika hafla maalum ya kuwaaga wahitimu waliomaliza masomo ya awali ya Kiislamu katika taasisi ya Al-Azizu Islamic Centre yenye makao makuu mjini hapa, na kukabidhiwa vyerehani kwa jumuiya yao. Vyerehani hivyo vilitolewa na kampuni ya Cats Michro Systems yenye makao makuu yake makuu Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wake Bwana Akbar Hameer. Hafla hiyo ilifanyika hivi karibuni mwaka huu katika uwanja wa taasisi hiyo karibu na Msikiti wa Al-Azizu uliopo maeneo ya Jeddah mjini hapa, na kuhudhuriwa na maelfu ya Waislamu kutoka sehemu mbalimbali za mjini na vijiji vyake hapa kanda ya kusini. Mapema akisoma risala hiyo kwa niaba ya jumuiya hiyo ya akina mama, Bi. Zaituni Shabani alisema kuwa kiongozi wa Kiislamu anatakiwa auweke Uislamu mbele ya kitu kingine chochote na asijiweke kifua mbele kuwa kigingi cha kuzuia kusimama kwa Uislamu. "Afahamu yeye ni binadamu, mauti yapo mlangoni kumpeleka akhera. Huku hakuna zaidi ila pepo na moto. Hakuna yeyote atakayenufaika na cheo au wadhifa wake, ila ucha Mungu wake. Hivyo ni bora kuweka historia imkumbuke kama mtetezi wa Uislamu kuliko historia kumkumbuka kama kikwazo cha maendeleo ya Uislamu", alisema Bi. Zaituni. Bi. Zaituni alisema kuwa tatizo la msingi linalowafanya viongozi wengi kushindwa kuifanya diin ya Allah (sw) kuwa juu ya taratibu nyingine zote ni kutokuwa na ujuzi sahihi juu ya Uislamu. Hivyo kiongozi yeyote wa Kiislamu hana budi kuufahamu vyema Uislamu kwa upande wake. Alisema ni kwa njia hiyo ndipo atakapoweza kuwapa Waislamu ujuzi sahihi wa Uislamu ambao ni mfumo wa maisha yetu hapa duniani. Aidha, alisema viongozi lazima wahakikishe kuwa jitihada zote zinazolenga kuinua hadhi na nafasi ya mwanamke katika jamii lazima zitokane na mafundisho ya Qur’an na Sunnah, na kuiga mfano wa Mtume (saw) jinsi alivyowatendea wanawake. "Hadhi na heshma ya mwanamke isitafutwe kwa kuyakataa mafundisho ya Allah (sw) na kuwaiga wengine kibubusa kama zinavyoenezwa propaganda kufuatia mkutano wa Beijing kuhusu usawa na haki za wanawake", alisema Bi. Zaituni na kuongeza kuwa "heshima, hadhi na wajibu wa mwanamke vimehifadhiwa katika Qur’an na Sunnah, kama mafundisho hayo yataeleweka vizuri hapatakuwa na matatizo". Bi. Zaituni alisisitiza kwa kusema matatizo yanayowapata wanawake kamwe hayatokani na sheria za Kiislamu bali yanatokana na kuacha kuifuata kikamilifu sheria hiyo, na kuongeza kuwa hayo ni matatizo ya watu na sio Uislamu. Kwa hali hiyo, alimtaka kiongozi wa Kiislamu awe na yakini kuwa njia sahihi ya maisha ni ile tu iliyofundishwa na Mtume (saw) na kwamba chochote kisichokuwa katika mafundisho ya Mtume (saw) ni batili, hakifai kukifundisha. Aidha, alimtaka kiongozi wa Kiislamu kufahamu kuwa kipimo pekee kupimia usahihi wa maoni na jambo jipya lililowakilishwa na yeyote yule ni kitabu cha Allah (sw) na Sunnah ya Mtume wake (saw). Alisema chochote kisichokubaliana na kipimo hiki siyo sahihi na hakifai kukifuata. Bi. Zaituni pia alimtaka kiongozi kufanya juhudi ya kufundisha Uislamu kupitia misingi yake halisi –Qur’an na Sunnah, aufundishe Uislamu kama ulivyo, yaani asijaribu kuupindisha ili ulingane na anavyotaka yeye au kinavyotaka chama fulani, au wanavyotaka watu wa mila fulani. Pia alimtaka kiongozi aufuate Uislamu bila kuuonea haya, asijaribu kuonyesha kuwa Uislamu unakubaliana na kila jambo linalozushwa na vyama vya siasa au serikali, hasa kama Uislamu unalikemea jambo hilo kama; ugawaji wa kondom katika kuimarisha uzinzi salama, uzazi wa mpango na kufunga kizazi katika njia zisizowafiki sheria, matangazo ya pombe, sigara, riba na mashindano ya urembo. "Kwa sababu leo imekuwa ni kitu cha kawaida kuwakuta viongozi wa vyombo vya kidini hapa nchini ambao hutafsiri aya za Qur’an kuhalalisha matendo ya chama na serikali, kama amri na utii kwa viongozi hao bila kuhoji", alisema Bi. Zaituni. Akitilia mkazo nukta ya kushikamana na Uislamu kikamilifu, Bi. Zaituni alisema ni wajibu wa kiongozi wa Kiislamu kusimamia sheria zote za Kiislamu zitekelezwe bila kuchagua, kwani alisema kutekeleza sheria moja na kusita kutekeleza nyingine siyo katika Uislamu. Akifafanua alisema Qur’an iliyoamrisha kusali ndiyo hiyo hiyo iliyokataza riba na kuamrisha wanawake kuvaa hijabu. Qur’an iliyoharamisha kula nguruwe ndiyo hiyo hiyo iliyoharamisha zinaa, Qur’an iliyoamrisha kufunga Ramadhani ndiyo hiyo hiyo iliyoamrisha wazinifu kupigwa bakora na wezi kukata mikono. "Zote ni sheria za Allah (sw) na lazima zitekelezwe", alisema Bi. Zaituni huku akinukuu aya ya Qur’an tukufu inayowaonya Waislamu tabia ya kuamini sehemu ya kitabu (Qur’an) na kukataa sehemu nyingine, isemayo: "Je, mnaamini baadhi ya kitabu na kukataa baadhi (yake)? Basi hakuna malipo kwa wenye kufanya haya katika nyinyi ila fedheha katika maisha ya dunia, na siku ya kiama watapelekwa katika adhabu kali. Na Allah si mwenye kughafilika na yale mnayoyatenda". (2:85). Mwisho, Bi. Zaituni alitoa wito kwa viongozi wa Kiislamu kuwa na mashikamano na ushirikiano katika kazi yao muhimu ya kuongoza ummah wa Kiislamu na kuwaomba waondoe tofauti zao ili waweze kusimamia kikamilifu majukumu yao. Alisema kwa kufanya hivyo watawapa akina mama nguvu na msimamo imara. Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa ni Sheikh wa BAKWATA Mkoa wa Mtwara, Sheikh Ally Said. Naye Imamu wa Msikiti uliopo maeneo ya Wapiwapi, karibu na kituo kikuu cha mabasi mjini hapa Sheikh Yusufu Akiba alionekana wazi kupinga madai ya risala ya kina mama hao. Sheikh Akiba alisema kwa kuwa Uislamu nchini umekaliwa na dola isiyokuwa ya Kiislamu hakuna Sheikh atakayeweza kusimamia na kutekeleza sheria za Kiiislamu. Hata hivyo kauli hiyo ya Sheikh ilipingwa na Amiri wa Darul Furqani Islamic Foundation yenye makao yake makuu mjini Newala Sheikh Ahmad Yusufu Bakari. Sheikh Ahmad ambaye pia ni Imamu wa Masjid Hidaya mjini Newala alisema ndani ya Qur’an hakukufundishwa utawala wa sheria peke yake, bali mna ibada pia. Hivyo alisema pamoja na Waislamu kuzuiwa kutekeleza sheria za Kiislamu, lakini bado hawajazuiwa kuabudu kama katiba ya nchi inavyoagiza. Ugaidi na Uislamu siyo kitu kimoja – Sheikh Jongo Na Bakari Musa IMAM wa Ijumaa wa Msikiti wa Manyema jijini, Sheikh Hamid Jongo amewataka wale wote wanaojifanya vinara wa kutetea haki za binadamu duniani kuuacha Uislamu na sura yake halisi badala ya kubuni mbinu ya kuuhujumu. Sheikh Jongo aliyasema hayo alipokuwa akitoa khutba ya Ijumaa ya Septemba 24, 1998 katika msikiti wa Manyema. "Katu hawataweza kuiua dini ya Allah (sw) labda watakachoweza ni kuwayumbisha wale Waislamu wasio madhubuti katika mipango yao", alionya Sheikh Jongo. Sheikh Jongo aliwataka wanaojiita watetezi wa haki za binadamu na wapinga ugaidi kuachana na tabia ya kufumbia macho aina fulani ya ugaidi na kuukemea ule wasioutaka wao tu. "Hivi sasa wananchi wa Cosovo wanauliwa mchana hadharani, wake kwa waume, lakini si Umoja wa Mataifa wala jumuiya zake waliotoa tamko la utekelezaji kupinga mauaji hayo, badala yake wanaumauma meno tu", alieleza Sheikh Jongo na kuongeza kuwa "Wapalestina wanatolewa katika ardhi yao na kunyang’anywa Misikiti na wanauliwa, lakini waporaji na wauaji hao hawaitwi magaidi wala wauaji". Kufuatia milipuko ya balozi za Marekani jijini Dar es Salaam na kule Nairobi kuwekuwa na tuhuma za kuhusisha milipuko hiyo na Usama bin Ladin na nchi au makundi ya Waislamu. Huko Kenya taasisi kadhaa za Kiislamu zinazotoa misaada kwa wananchi wasiojiweza zimefutiwa usajili wake na serikali ya nchi hiyo kwa kuhusishwa na milipuko hiyo, jambo ambalo Wabunge Waislamu nchini humo wameionya serikali yao kubadili hatua yake hiyo vinginevyo wametishia kujiuzulu nyadhifa zao za kisiasa, kutokana na kile walichokitafsiri ni uonevu kwa wanyonge. Nayo Sudan nchi ambayo ina Waislamu wengi na inayojitahidi kutaka kuwa nchi ya Kiislamu imerushiwa makombora na Marekani na kuteketeza kiwanda cha madawa kwa madai kuwa kiwanda hicho kinatengeneza silaha za sumu. Sudan imepinga vikali hujuma hiyo na kuahidi kulipiza kisasi kwa Marekani endapo itaendelea na uchokozi wake. Na Abu Zubair, Dodoma IMAM wa Masjid Rahman na Sheikh wa Wilaya ya Dodoma, Sheikh Abbas amewatahadharisha wananchi juu ya mwenendo unaoelekea kuota mizizi wa kupoteza muda wao mwingi wa kuangalia mambo ya Laghwi katika video. Sheikh Abbas amesema kwamba watu wanapoteza muda mwingi wenye thamani kuangalia picha (programu za TV) zisizo na mafunzo yoyote ila huwa ni pumbazo tu. Aliwahimiza Waislamu wautumie muda wao vyema hasa baada ya kazi kwa kusoma Qur’an kuliko kupoteza kwa laghwi za sinema na mpira. Sheikh Abbas alizitoa nasaha hizo katika ujumbe wake wa Ijumaa ya Septemba 25, mwaka huu mjini Dodoma. Wakati huo huo, Sheikh Ahmed Said wa Msikiti wa Manyema mjini Dodoma amewahimiza Waislamu kuimarisha umoja na mshikamano wao ili kuipa nguvu dini yao na kuleta maendeleo. Sheikh Ahmed akiongea Msikitini hapo Ijumaa iliyopita, aliwataka Waislamu warejee katika historia wamejenga mshikamano na Ansaar na Muhajiriin ulivyowapa Waislamu nguvu Madina. Na Badru Kimwaga VIJANA wengi nchini wamedaiwa kudanganywa na kupotoshwa kimaadili kutokana na magenge wakaayo ambapo hupeana elimu mbovu inayowapotosha na kuharibika kitabia, ikiwemo kujiingiza katika vitendo vya kihalifu. Hayo yalisemwa na Sheikh Juma Ally Dumwe wa Bunju nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam aliyekuwa jijini hivi karibuni wakati akiongea na na mwandishi wa habari hizi. Sheikh Dumwe ambaye pia anafundisha Madrasat el Kadria iliyoko huko huko Bunju, alisema kuwa vijana wengi kutokana na magenge wanayokaa ambayo huwa na mchanganyiko wa vijana wenye tabia tofauti, hufundishana mambo mengi maovu yakiwemo uvutaji bangi na madawa ya kulevya na kujiingiza katika ufuska na kushiriki vitendo vya wizi na uporaji. Alisema kuwa kutokana na vijana wengi kutokuwa na kazi za kufanya hasa mijini, wamejikuta wakilazimika kupoteza muda katika magenge hayo na hivyo kujifunza maovu kutoka kwa wenzao waliobobea ambao kwao imekuwa desturi. Alifafanua kwa kusema kuwa, "Wazazi hutoa elimu yao kwa vijana na sisi walimu halikadhalika, lakini jitihada zetu za elimu zetu ambazo msingi mkuu ni kuwaadabisha vijana na watoto, zimekuwa zikigonga ukuta kwa sababu ya elimu "kijiweni’. Aliongeza kuwa ili kuweza kudhibiti wimbi hili la kuharibika kwa vijana, hapana budi wazazi kuwatafutia vijana shughuli za kufanya kusudi wasishinde bila kazi na kuwazoesha kujifunza elimu ya dini ambayo humfanya kijana kumuogopa Mungu na kutojihusisha na maovu. Aliongeza kuwa serikali nayo inachangia sana katika kuharibika kwa vijana kutokana na wengi kukosa nafasi za kuendelea kusoma au kukosa ajira na kuongeza kuwa serikali ikiwa inadhamiria kutokomeza uhalifu nchini, basi haina budi kuwaanzishia vijana miradi mbalimbali. Alimalizia kwa kuwaasa vijana hasa wa Kiislamu kuepuka kufuata mkumbo
wa msemo wa ‘kwenda na wakati’ ambapo hupotea na kukiuka maadili ya Mwenyezi
Mungu na mafundisho ya Mtume Muhammad (saw) na kutoa picha mbaya.
|
YALIYOMO
TAHARIRI Majeshi ya nje kupelekwa Lesotho: Je, ni sera za Nguvumali? Nyumba ya Wakfu yageuzwa Baa
Dar
‘VAT’ yaingia Bakwata Same
Mchungaji asema hakuna mihadhara ya
kashfa
Maoni yetu: Masheikh tupeni Fatwa Safari yangu Ufini
Unyanyasaji wa kidini mashuleni, vyuoni
ukomeshwe
Wanaume toeni haki za wanawake
MAONI: Yesu ni yule yule Isa
Hatuna uwezo wa kuwapinga manabii
Ukoloni mwingine unaingizwa
nchini?
Khatamy ni ‘Gorbacheiv’ mwingine?
Tufuate Uislamu kwa vitendo na siyo
kwa maneno
AN-NUUR lina chuki na
Wakristo
Msiiparamie ovyo Biblia
Yaliyosemwa na viongozi wa dini juu
ya idadi ya watu 1989
Uislamu ulivyoingia Zanzibar -2 Waislamu Moro watakiwa kutoyumba
Wanawake Masasi wawataka Masheikh
kutangaza sheria za Allah
Ugaidi na Uislamu siyo kitu
kimoja – Sheikh Jongo
Sheikh Abbas awataka wananchi
Dodoma waepuke upuuzi
Vijana watakiwa kujiepusha
na ‘vijiwe’
Mafundisho ya Quran
Chakula na Lishe
|