NASAHA
Na. 053 Jumatano Juni 21 - 27, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
MASHAIRI

Mwana kafikisha mwaka

Bismillah nanena, kwa kuanza tungo yangu,
Tumfurahie mwana, mimi na ninyi wenzangu,
Kamjalia Rabana, mwaka pasipo machungu,
Mwana kafikisha mwaka, Malenga tufurahie.

Mwana huyu si mgeni, Shemdoe wamjua,
Mwenetu si limbukeni, kusema asiyojua,
Mtoto hana utani, utovu kuufichua,
Mwana kafikisha mwaka, Malenga tufurahie.

Mwana huyu wa ajabu, wala hataki mchezo,
Katia watu adabu, bila kuleta mizozo,
Katoa watu ububu, kukumbatia kuozo,
Mwana kafikisha mwaka, Malenga tufurahie.

Mtoto huyu hodari, Mtauni humkani,
SIHABA Mama jasiri, Mtagalukwa Mtani,
Hakuna kutafakari, mwanenu siyo muhuni,
Mwana kafikisha mwaka, Malenga tufurahie.

Sihaba hebu wambie, mwana huyu mwana gani,
Archiduka Pasulie, mwanetu wambaini,
Katanga wapekulie, fumbo fumbua tungoni,
Mwana kafikisha mwaka, Malenga tufurahie.

Kaditama naishia, ninaenda shereheni,
Mwana namfagilia, ngangari ije iwini,
Debe ninampigia, atimke uwanjani,
Mwana kafikisha mwaka, Malenga tufurahie.

       Y. Kijukuu,
      Mapumzikoni Mkuranga



Uchaguzi ukingoni

Nashika kalamu yangu, naingia uwanjani,
Kuwaeleza wenzangu, yalonisibu moyoni,
Tasaidiwa naMungu, kuwaeleza mwandani,
Elfu mbili ni hii,shime kura tupigeni.

Wananchi amkeni, Oktoba imefika,
Na tujiandikisheni, tusijengia mashaka,
Kura nayo tupigeni, tusije kufedheheka,
Elfu mbili ni hii, shime kura tupigeni.

Mwaka huu kwa hakika, dhulma tuondoeni,
Wasije wakamuweka,  yule tusombaini,
Tusije kuhangaika, kutwa kucha majiani,
Elfumbili ni hii, shime kura tupigeni.

Misuli na suruali, hivyo vya muda sikia,
Tutajakukosa wali,  na mchuzi wa bamia,
Kwa kumkosa jabali, tulokwisha dhamiria,
Elfu mbili ni hii, shime kura tupigeni.

Lazima muwe makini, siku ya kura tambuwa,
Msiingie mitini, kura zikaja -ibiwa,
Mubaki hadi jioni, mshindi kumtambuwa,
Elfu mbili ni hii, shime kura tupigeni.

Chama nitachochagua, lazima kiwe cha haki,
Kisije kuwaumbua,  mkaja kutaharuki,
Na wengine kuugua, hali ugumu ikibaki,
Elfu mbili ni hii, shime kura tupigeni.

Chama kisicho na dira, wala mwema usukani,
Hicho hakina busara, tatutia mashakani,
Tutaja kula hasara, tutapofika mwakani,
Elfu mbili ni hii, shime kura tupigeni.

Nani wa kumchagua, bila shaka tamuona,
Ni wewe unomjua, hakika yuko bayana,
Haki ataitetea, bila ya kubaguana,
Elfu mbili ni hii,shime kura tupigeni.

Nimesema kwa mapana, hapa ninaishilia,
Ninamuomba rabana, mwanga kutuangazia,
Nawakumbusha vijana, haki yenu kutumia,
Elfu mbili ni hii, shime kura tupigeni.

Ummul Jamilah, 
Safarini Dodoma.



Wakulaumiwa nani? (Swali)

Nashika kalamu yangu, naingia uwanjani,
Kuwaeleza wenzangu, haya niliyobaini,
Yanitia uchungu, sijui nifanye nini,
Zanzibar imekwisha, hadhi yake siioni?

Suali nawauliza, Malenga lisikieni,
Msije mkalibeza, kufanya  hamlioni,
Kwa hakika ninawaza, alosababisha nani,
Zanzibar imekwisha, hadhi yake siioni?

Mimi ninajiuliza, sipati jibu jamani,
Tena ninawahimiza, mnijibu kwa makini,
Ili nipate eleza, akili yangu mwandani,
Zanzibar imekwisha, hadhi yake haioni?

Mnieleze nataka, sababu hasa ni nani?
Kwa huyo anayetaka, kuitia mashakani,
Asije akaiteka, kwa kudhani hatuoni,
Zanzibar imekwisha, hadhi yake siioni?

Hapo ilipofikia, aloiweka ni nani?
Katika hii dunia, lengo lake hasa nini,
Au anatuchuria, nielezeni jamani,
Zanzibar imekwisha, hadhi yake siioni?

Visiwa vya Zanzibari, huruma vinatutia,
Wanajifanya hodari, wale wano shikilia,
Pia huwa na jeuri, pale unapowambia,
Zanzibar imekwisha, hadhi yake siioni?

Hivi sasa kwa hakika, dhulma imekithiri,
Wananchi wateseka, na hutolewa jeuri,
Wabaki kuhangaika, hawana hata hiyari,
Zanzibar imekwisha, hadhi yake siioni?

Kijukuu nauliza, suali liko bayana,
Jushaka nawe waweza, kulijibu kwa mapana,
Msije mkalibeza, wala kulibanabana,
Zanzibar imekwisha, hadhi yake siioni?

Tunda la matumaini, nieleze nielewe,
Nakuombea amani, usijepata kiwewe,
Usijeleta utani, nataraji kwako wewe,
Zanzibar imekwisha, hadhi yake siiooni?

Na mtoto Mtauni, mashaka ungenitoa,
Nieleze kwa makini, yale unayoyajua,
Wakulaumiwa nani, katika hii dunia,
Zanzibar imekwisha, hadhi yake siioni?

Niambie Achiduke, mwenzio nnaumia,
Wala usichekecheke,wahka ungenitoa,
Eleza ueleweke, nami nipate sikia,
Zanzibar imekwisha, hadhi yake siioni?

Baby Fumo na Jabiri, amkeni nawambia,
Lazima muwe tayari, haki kuipigania,
Tena muifanye ari, muovu kumfichua,
Zanzibar imekwisha, hadhiyake siioni?

Wote mliobakia, naomba mawazo yenu,
Na Wanzanzibari pia, kwani hii haki yenu,
Ndio mnaoumia, hiyo ndiyo nchi yenu,
Zanzibar imekwisha, hadhi yake siioni?

Hadhi yake kwa hakika, haipo tena nchini,
Hadhi imepukutika, imeingia mitini,
Wanatutia mashaka, jamani tufanye nini?
Zanzibar imekwisha, hadhi yake siioni.

H.S.B. 
Ummul Jamilah,
Safarini Makunduchi Zanzibar.



Lipumba tunakuita

Mhariri nakuita, nipisheni gazetini,
Sitaki pika ufuta, nataka toa maoni,
Sitatumia mafuta, kalamu 1 mkononi,
Lipumba tunakuita, Bara hata Visiwani.

Uteuzi umepita, mashina na matawini,
Watani walishatota, hili walipobaini,
Kisu hiki kitapita,nyama hata mufupani,
Lipumbatunakuita, twasema tupo ngangari.

Tabora na tena pita, Isevya na Kiloleni,
Tanga hakuna matata,na uje tena Handeni,
Na ukifika Tabata, sisahau Kinondoni,
Lipumbatunakuita, wananchi tumechoka.

Hata tukinywa ya kata, tasubiri majiani,
Furaha tutaipata, tapokutia machoni,
Kura zetu katakata, tutompa hayawani,
Lipumba tunakuita; wanafunzi na walimu.

Sisi hii kwetu vita, kura nyenzo namba wani,
Hayawani ukitwita, hatuji mikutanoni,
Kalamu ninaikita, nimefika kituoni,
Lipumbatunakuita, njoo uje na ngangari.

Na Abu Maryama, 
Dar es Salaam.



Wazimu kukurudia

CCM namba moja, kwa kila lenye ubaya,
Miaka arubaini, ulichofanya ubaya,
Elfu mbili ni mwisho, au wataka umbeya?
Kimuuzi mchinja mbwa, wazimu kukurudia.

Mhariri samahani, sikuanza kukuomba,
Sababu ya magazabu, kichwa kina yumba yumba,
CCM huna sera, imebaki ni ghiliba,
Kimuuzi mchinja mbwa, wazimu kukurudia.

Mwembe Chai umeua,halafu ukajisifu,
Kwa maneno ya kiburi, yasiyo na usanifu,
Uchaguzi umefika, kura kwetu ni turufu,
Kimuuzi mchinja mbwa, wazimu kukurudia.

CCM nakwambia ,tutakupeleka kapa,
Turufu zote kwa CUF, ninganda tutazokupa,
Dume tunae Lipumba na seti yupo Kasupa,
Kimuuzi mchinjambwa, wazimu kukurudia.

Zungu la nne ni Seif, la tatu yupo Mloo,
Turufu hazina shaka, sim zapigwa haloo,
Zungu la pili ni Tambwe, siku hiyo halo haloo,
Kimuuzi mchinja mbwa, wazimu kukurudia.

Matusi ulotukana, bado yako akilini,
Na sisi hatushangai, Mwalimu alibaini,
Kwamba hii CCM ,inaongozwa kihuni,
Kimuuzi mchainja mbwa, wazimu kukurudia.

CCM elfu mbili lazima upigwe bao,
Kwa siasa wewe tobwe, sera zako za uongo,
Ukweli ukisha fika, uongo salam zao,
Kimuuzi mchinja mbwa, wazimu kukurudia.

Beti nane zinatosha, maneno sijamaliza,
Hali yangu sitwaibu, mguu ninauguza,
Hima wananchi hima, Lipumba awe wakwanza’
Kimuuzi mchinja mbwa wazimu kukurudia.

Mwela Bondo (Kipupwe),
Makumbusho, Dar es Salaam.

Juu
 

YALIYOMO
 
 

Tahariri
Uhuru wa kuabudu utiwe katika matendo bila ya ubaguzi

Kauli ya Sumaye yawakera wananchi

Licha ya Katiba ya nchi kutambua uhuru na haki ya kuabudu: Qur’an kizimbani

CCM yapata kiwewe

Wapinzani Waishutumu sheria mpya ya uchaguzi

Mtoto wa Afrika yutaabani

CCM wanatumia pesa za serikali kwa kampeni - Chenyenge

USHAURI NASAHA
Dhuluma haiondoki bila kubadili mfumo

Habari za Mikoani

Kalamu ya Mwandishi
Kweli CUF ni ngangari!

MAKALA
Manabii wa kale na mageuzi

MAKALA
CCM na sera za maendeleo

MAKALA
Wajibu wa wananchi kwenye uchaguzi mkuu

Habari za Kimataifa

Lishe
Kuhifadhi matunda kwenye jokofu

RIWAYA
Dunia ndivyo ilivyo - 3

MASHAIRI

MICHEZO

  • Uingereza, Ujerumani nje
  • Washabiki wamshangaa Mkapa, wambeza Sumaye
  • BMT waipiga ngwara FAT

  • -

       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita