|
Na. 053 Jumatano Juni 21 - 27, 2000 |
|
|
|
|
|
Wapinzani Waishutumu sheria mpya ya uchaguzi Na Mwandishi Wetu VIONGOZI wa vyama vya upinzani nchini wameishutumu vikali sheria iliyopitishwa na Bunge hivi karibuni ambayo imewapa mamlaka wasimamizi wa uchaguzi kuamua kuhamisha sehemu ya kuhesabia kura tofauti na sehemu zilipopigwa. Shutuma hizo zilitolewa mbele ya maelfu wa wananchi wa mkoa wa Dares Salaam na mikoa ya jirani kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na chama cha CUF wa kuwatambulisha wagombea Urais kupitia chama hicho Profesa Ibrahim Lipumba aliyepitishwa kugombea urais wa Muungano na Maalim Seif Sharif Hamad kwa urais wa Zanzibar. Mkutano huo ulifanyika katika viwanja vya Kidongo Chekundu jijini Dar es Salaam Jumamosi iliyopita. Mwenyekiti wa CHADEMA Bwana Bob Makani ambaye alikuwa mgeni mwalikwa kwenye mkutano huo, alisema kuwa mswada huo umepitishwa ili kuandaa mazingira ya kuiba kura. Akiongeza kuwa endapo 'dharura' itatokea na msimamizi wa uchaguzi akaamua kuondoka na maboksi ya kura itakuwa vigumu kwa mawakala wa vyama kuwafuata kwani wao hawana vyombo vya usafiri. Bob Makani ndie anayeongoza Kamati ya Vyama vya CUF,UDP na CHADEMA vinavyotaka kushirikiana katika uchaguzi mkuu. Naye Mwenyekiti wa CUF Profesa Lipumba aliwataka wapiga kura kuwa 'ngangari' kuhakikisha kuwa hakuna boksi ambalo litatoka kwenda sehemu nyingine yeyote tofauti na pale kura zilipopigwa. "Sheria ya uchaguzi inawaruhusu wapiga kura kukaa mita kadhaa toka sehemu ya kupigia kura. Hivyo mtakapopiga kura zenu hakikisheni mnakaa umbali huo na msiondoke mpaka kura zihesabiwa hapo hapo kituoni. Na wala wasimamizi wasiondoke mpaka wametia saini fomu zinazohusika. Alisema Profesa Lipumba, na kuongeza kuwa "miaka arobaini sasa tumekuwa tukipiga kura mbona hayo wanayoyasema ni 'dharura' hatukuyasikia. Hizi ni njama za kutaka kuiba kura. Dharura ambazo zilitolewa kwenye mswada huo wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge ni kama mvua, moto au kutokea kwa nyoka na wanyama mkali wakati wa kuhesabu kura. Kipengele kingine katika mswada huo ni kile kinachowaruhusu wagombea kufanya kampeni ya nyumba kwa nyumba. Akizungumzia kipengele cha kampeni ya nyumba kwa nyumba Profesa Lipumba alisema kipengele hicho kimewekwa ili kuhalalisha rushwa. Aliwataka wale wote watakaofuatwa na viongozi wa CCM ili kupewa vipande vya kanga au fedha wazipokee kwani hizo ni haki zao lakini kura wasiwape. Awali wakati muswada huo ulipokuwa ukijadiliwa
Bungeni, kipengele cha kuhamisha sehemu ya kupigia kura kilionyesha kuwatia
wasiwasi hata Wabunge wa CCM akiwemo Hawa Ngulume (wanawake) na Corona
Busongo (Kukene). Aidha wabunge wote wa upinzani waliupinga mswada huo.
Na Hussein Bashir, Morogoro IMEFAHAMIKA kuwa watoto wengi barani Afrika wapo katika hali mbaya kimalezi, kutokana na wazazi wao kuwa na hali ngumu ya kiuchumi. Hayo yamesemwa na Ndugu Mussa Mlasi katika hafla ya mtoto wa Afrika iliyofanyika katika viwanja vya shule ya Msingi Magole, taarafa ya Magole, wilayani Kilosa mwishoni mwa wiki. Ndugu Mlasi ambaye ni Afisa Mipango katika wilaya hiyo amesema kuwa hali ya watoto imekuwa duni kwa kuwa hawapati haki zao za msingi ambazo alizitaja kuwa ni kulindwa, kuendelezwa, kutokubaguliwa pamoja na kupata huduma bora za jamii. Akitoa takwimu mbali mbali zilizoonesha uchovu waliokuwa nao watoto wataarafa mbalimbali katika wilaya hiyo alisema kuwa mwaka 1999 malengo ya uandikishaji watoto wa shule katika kijiji cha Magole yalikuwa ni 759 watoto walioandikishwa ni 303 na watoto 456 hawakuandikishwa. Mwaka huu malengo ni 913, walioandikishwa 374, wasioandikishwa 539. Takwimu hiyo inakifanya kijiji hicho kuwa ni cha 34 katika kata 36 za wilaya hiyo,hali ambayo imetokana na wazazi wao kuwa na hali mbaya kiuchumi kwa vile wengi wao hutegemea sana kilimo cha kutumia zana duni za mkono. Aidha Afisa huyo alitembelea zahanati ambayo iko katika ukarabati kutokana na michango ya wanakijiji hao, akielezea huduma katika zahanati hiyo daktari Ramadhani Mkawa alisema "katika zahanati hii pia tunawapumzisha wagonjwa ,hali zao zikiwa mbaya zaidi tunawapeleka mbele zaidi ya hapa",alisema hayo huku akionyesha moja ya vyumba ambavyo vimefanyiwa ukarabati ambapo mwandishi wetu alifanikiwa kuingia na kuona kitanda kimoja tu cha kamba. Takwimu za lishe katika kijiji hicho zinaonesha kuwa katika Kata 36 kimekuwa cha 14, na Chanjo kimekuwa cha 18,Surua ni cha 26. Siku ya mtoto wa Afrika ilizinduliwa na Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) mwaka 1991,ili kuazimisha,siku walioteswa watoto wa Afrika ya Kusini, maazimisho hayo hufanyika kila mwaka ,Juni 16.
Na Mwandishi Wetu IMEDAIWA kura kuna kampeni zinazoendelea kufanywa hivi sasa na chama tawala cha CCM kabla ya wakati, tena kwa kutumia vyombo vya umma na kwamba lengo lake ni kuwakomoa wapinzani. Akiongea na gazeti hili hivi karibuni katika hoteli ya Iko mjini hapa, Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP) mkoani Mwanza Mhe. Cosmos Ikombe Chenyenge alisema kuwa CCM wanajua kuwa vyama vya upinzani havina fedha hivyo havitaweza kufungua kesi za madai ya kukiukwa kwa taratibu za uchaguzi. Kwani kiwango cha shilingi milioni tano zilizopangwa kuwekwa dhamana mahakamani ili mdai afungue kesi ni nyingi kwa kambi ya upinzani kuweza kumudu. "Kampeni hizi zinazoendelea sasa ni za makusudi kwani wanajua hatutaweza kufanya lolote, wakati wao watatumia pesa za serikali", alisema Mhe. Chenyenge na kuongeza kuwa kutumia vyombo hivyo vya habari na vya usafiri vya umma ni kuwachezea faulo wapinzani na kwamba fedha za serikali zinatumika kwa manufaa ya wachache waliopo madarakani. Mhe. Chenyenge alisema kuwa si viongozi wa kitaifa tu wanaofanya kampeni hivi sasa kwa kutumia vyombo vya serikali bali hata wabunge wa CCM nao wanafanya hayo hayo. "Mbunge wa Buzega, kwa mfano, anatumia gari la serikali kufanya kampeni zake huko Buzega", alisema. Hivi karibuni palikuwepo na malalamiko toka kambi ya upinzani kuwa Mwenyekiti wa CCM Rais Benjamin Mkapa anatumia vyombo vya habari vya serikali kama vile televisheni ya Taifa (TVT) na RTD kufanya kampeni kabla ya wakati. Aidha, Chenyenge alisema kuwa kama pangekuwepo na tume huru ya uchaguzi ingeingilia kati na hatimaye kuizuia CCM isifanye hayo inayoyafanya sasa. Hata hivyo akaiombatume hiyo ijitahidi kufanya uadilifu kwa kuutendea haki upande wa upinzani. |
YALIYOMO
Tahariri
Kauli ya Sumaye yawakera wananchi Licha ya Katiba ya nchi kutambua uhuru na haki ya kuabudu: Qur’an kizimbani Wapinzani Waishutumu sheria mpya ya uchaguzi CCM wanatumia pesa za serikali kwa kampeni - Chenyenge USHAURI NASAHA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
MAKALA
MAKALA
Lishe
RIWAYA
- |
|
|
|
|