|
Na. 053 Jumatano Juni 21 - 27, 2000 |
|
|
|
|
|
Hivi karibuni Chama Cha Wananchi (CUF) kilifanya mkutano Mkuu mkoani Mwanza na baadaye kiongozi wa chama hicho Prof. Lipumba alifanya ziara katika maeneo mbalimbali mkoani humo na mkoa wa jirani wa Musoma. Mwandishi wetu Rajab Nkawa ambaye alikuwepo kwenye msafara anaripoti baadhi ya matukio aliyokutana nayo. Wasukuma waazimia kuifuta CCM Mwanza
Hayo yamedhihirika wakatiwa ziara ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Prof. Ibrahim Lipumba aliyoifanya katika mikoa ya Mwanza na Mara. Katika baadhi ya vijiji mwandishi wa habari aliweza kushuhudia jinsi CCM ilivyofutika katika maeneo hayo ambapo watu wote katika maeneo hayo ni ama wanachama wa CUF au UDP. Baadhi ya vijiji hivyo ni pamoja na Isabilo na Jojiro vilivyo katika kata ya Mwandu, tarafa ya Isabilo, wilayani Kwimba na Busongo, Ngobo, Kasadi na Busekwe vilivyo katika wilaya ya Misungwi. Vingine ni Shigala kilicho katika wilaya ya Magu na Karuma kilicho katika tarafa ya Msalala wilayani Geita. Katika vijiji hivyo vyote Profesa Lipumba alifanyiwa sherehe kubwa alipowasili na ujumbe wake ambapo vikundi mbalimbali vya utamaduni viliimba. Aidha wananchi hao walichinja ng'ombe na mbuzi katika kufanikisha sherehe hizo. Prof. Lipumba hakuwa na la kuwaambia wananchi hao zaidi ya kutoa salamu na kufafanua sera za chama chake, baada ya wananchi hao kupitia nyimbo za vikundi vya utamaduni kuelezea kwa upana na marefu hali halisi inayoikabili nchi yetu hivi sasa ya matatizo ya kiuchumi na kisiasa. Katika kijiji cha Isabilo vikundi 40 vilishiriki na Shigala vikundi 28. Kikundi cha akina mama katika kijiji cha Isabilo kilielezea CCM kuwa ni papasi aliyewaganda kwa kuwanyonya bila ya huruma kutokana na michango mingi na kodi za kila aina wanazotozwa huko vijijini. "Lekagi alile-e CCM lekagi alile kumanila....", ulikuwa ni mmoja wa wimbo ulioimbwa na akina mama wa Busongo, ikiwa na maana ya iache ilie CCM itazoea tu. Aidha ujumbe mwingine ulimtaja Lipumba kuwa ni mkombozi wa wanyonge aliyekuja kuwakomboa wamnanchi kutoka utumwa wa CCM wa miaka 40. Akiwa Bunda Prof. Lipumba alikabidhiwa mkuki na wazee wa hapo ikiwa ni ishara ya kumtakia uongozi mzuri na usiogeuka. "Chombo hiki hakija wahi kubadlika jina toka kuumbwa dunia...tunakukabidhi kijana wetu ili uwe imara, usigeuke geuke", alisema mwakilishi wa wazee hao. Mwandishi wa habari hizi aligundua ushirikiano mkubwa miongoni mwa vyama vya UDP na CUF,ambapo wanachama wa vyama hivyo walishirikiana kuandaa kwa pamoja sherehe hizo. Akizungumza na wananchi Prof. Lipumba aliwakumbusha kuwa miaka 40 ya uhuru ni mingi sana kwa chama cha siasa kushika serikali. Aliwaambia kuwa wakati TANU ambayo sasa ndio CCM walipakabidhiwa nchi waliwasuta wakoloni kuwa walihitaji miaka 10 tu ili kuyafanya makubwa zaidi ya yale yaliyofanywa na wakoloni katika miaka 76 ya utawala wao. "Sasa ni miaka arobaini, sio kumi tena. Waulizeni CCM nini wamefanya, na wasituambie nini watafanya miaka mitano ijayo", alisema mtaalamu huyo wa uchumi. Naye mkurugenzi wa wanawake wa chama hicho Bi. Rozaria Mugisa aliwaambia akina mama katika mikutano hiyo kuwa wao ndio waathirika zaidi wa matatizo ya kiuchumi yaliyopo, hivyo wahakikishe wanayaondoa madhila hayo kwa mikono yao ifikapo Oktoba mwaka huu. Aliwataka wanawake kuachana na kasumba ya kusema 'CCM ndio baba yetu' na kuwauliza, "lini CCM ilipeleka posa ya kuwachumbia mama zetu mpaka ikawa baba?" Mwenyekiti wa CUF Prof. Ibrahim Lipumba amemaliza
ziara katika mikoa ya Mwanza na Mara na sasa yuko Pemba katika mfululizo
wa ziara za kuhamasisha wananchi.
MSAFARA wa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba uliokuwa katika ziara ya Kanda ya Ziwa ulifanyiwa fujo na watu wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa CCM ulipokuwa mjini Ngudu katika wilaya ya Kwimba June 13, mwaka huu. Ilikuwa majira ya saa 3 usiku msafara huo ulipowasili kwenye nyumba ya kulala wageni ya 'Safari Lodge', ambapo wanaume wawili waliokuwa wamevaa nguo za kijani zenye kuashiria kuwa ni wapenzi wa CCM walikuwa wakinywa pombe kwenye baa iliyo mbele ya nyumba hiyo. Wakati msafara ulipokuwa ukiendelea na chakula cha usiku palikuwa na kelele kubwa nje zilizojaa kejeli dhidi ya chama cha CUF na Mwenyekiti wake ambaye pia ni mgombea wa Urais wa chama hicho Prof. Ibrahim Lipumba. "Mtoeni huyo Lipumba humo ndani... Watoeni CUF hao... Sisi tunamjua Rais mmoja tu sio huyo Profesa Uchwara", yalisikika baadhi ya maneno kutokea nje sehemu ya Baa. Katika sehemu hiyo ya Baa palikuwa na kundi kubwa la watu 28 wakiwemo wale watatu wa mwanzo wakiwa wameshika chupa za bia wakinywa huku wakiendelea na vijembe vya hapa na pale dhidi CUF ni Prof. Lipumba. Wakati hali hiyo ikiendelea alifika polisi mmoja na kwenda kwa muhusika wa Baa ambapo alimuamuru afunge Baa hiyo ili kuzuia mtafaruku ambao ungeweza kutokea endapo wanachama wa CUF waliokuwa nje ya nyumba hiyo wangeamua kujibu mapigo. Baada ya amri hiyo kutekelezwa wapambe wa CCM walishutumu uongozi wa Baa kwa kuwakumbatia wageni, yaani msafara wa CUF, badala ya wao wenyeji. Utulivu uliporejea kwenye eneo la tukio mwandishi wa habari hizi alitaka kujua nini maoni ya CUF kuhusiana na tukio hilo na hatua zipi wanategemea kuchukua. Afisa mmoja anayembatana na msafara huo Bw. Haji Abdallah alisema walikusudia kwenda polisi kutoa ripoti ili waweze kurejesha amani katika eneo hilo. "Kwa kuwa polisi huyu kafanikiwa kurejesha hali ya amani, hatuoni sababu ya kwenda kutoa ripoti", alisema. Bwana Haji alisema kuwa haiwezekani kwa usiku ule pawepo na watu wenye mavazi ya ushabiki wa CCM katika eneo la Baa, wakati hapakuwa na shughuli yoyote ya kichama ya CCM katika eneo la Ngudu. Akaongeza kusema kuwa anavyojua yeye hii ni katika hujuma za CCM dhidi ya chama hicho hasa baada ya kuiweka sehemu kubwa ya wilaya hiyo ya Kwimba katika milki ya CUF. Katika maeneo mengi ya vijijini ya wilaya za mkoa wa Mwanza, ama CCM imefutwa kabisa au wako wanachama wachache sana hasa katika wilaya ya Kwimba. Msafara wa Prof. Lipumba ambao upo katika ziara
ya kuhamasisha wananchi kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba uliondoka hapa
kuelekea wilaya ya Magu.
POLISI mjini hapa walivamia nyumba ya kulala wageni iitwayo New Binza Guest House iliyopo barabara ya uhuru ambapo msafara wa CUF ulilala, usiku wa Junu huku wakikataa kutoa sababu za uvamizi huo. Kundi hilo la polisi wasiopungua nane na wengine kuwa na SMG wakiongozwa na mkuu wa kituo ambaye hakutaja anatoka kituo gani wala jina lake waliivamia nyumba hiyo saa 8:30 usiku na kufanya upekuzi chumba hadi chumba. Dalili za kuwepo kwa hali ya dharula katika gesti hiyo zilianza mapema kiasi cha saa 5 usiku baada ya milango ya kutokea nje kufungwa na hivyo wateja kushindwa kuingia wala kutoka nje. Katika upekuzi wao walidai kuoneshwa vitambulisho, mahali unapokaa, upo Mwanza kwa ajili gani na kupekua nyaraka na mizigo. Aidha walimuuliza mwandishi wa habari hizi aliyekuwa kwenye gesti hiyo usahihi wa habari alizoziandika baada ya kuona nakala ya habari iliyohusu mkutano mkuu wa chama cha CUF uliofanyika Mwanza hivi karibuni. Baada ya kila mteja wa gesti hiyo kujitambulisha na kuamuliwa watoke nje tayari kwa safari ya kwenda kituo cha polisi, ghafla maamuzi yalibadilika na kuwaruhusu kurejea ndani kwa awamu. Kundi la mwanzo likiwa lile la msafara wa CUF ambao ulikuwa ukitokea Musoma kuelekea Dar es Salaam. Mmoja wa wateja waliokuwamo kwenye gesti hiyo ambaye ni mwanamke alipigwa makofi na kutolewa maneno ya kejeli na mmoja wa polisi hao ambao walikuwa wamevaa kiraia kwa madai ya kutukanwa na kuchelewa kufungua mlango. Kitendo hicho kilionesha wazi ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Mwanamke huyo alirudi katika gesti hiyo nusu saa baada ya kuchukuliwa na polisi. Hata hivyo hakuwa tayari kusema lolote zaidi ya kudai kuwa alichelewa kufungua mlango kwa kuwa alikuwa anavaa. Kisheria mwanamke anatakiwa kupekuliwa na polisi wa kike tu, na pale ambapo polisi wa kike hayupo mwanamke yeyote raia ataombwa kufanya hivyo kwa maelekezo ya polisi. Mwandishi wa habari hizi alipozungumza na wahudumu wa gesti hiyo mara baada ya polisi kuondoka walikiri kuwepo kwa taarifa ya ujio wa polisi na kwamba waliamuriwa wasifungue milango baada ya saa 5 usiku mpaka polisi watakapofanya upekuzi. Kiongozi wa wahudumu hao aliyejitambulisha kwa jina la Hadija Ayubu alisema kuwa ni mara ya kwanza kwa nyumba hiyo kupekuliwa na polisi, lakini akasema polisi hao hawakumpa maelezo ya upekuzi zaidi ya kusema wanatafuta vitu vilivyoibiwa. |
YALIYOMO
Tahariri
Kauli ya Sumaye yawakera wananchi Licha ya Katiba ya nchi kutambua uhuru na haki ya kuabudu: Qur’an kizimbani Wapinzani Waishutumu sheria mpya ya uchaguzi CCM wanatumia pesa za serikali kwa kampeni - Chenyenge USHAURI NASAHA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
MAKALA
MAKALA
Lishe
RIWAYA
- |
|
|
|
|