|
Na. 053 Jumatano Juni 21 - 27, 2000 |
|
|
|
|
|
Manabii wa kale na mageuzi Na Mwinjilisti Kamara Kusupa MSAMIATI wa neno mageuzi, umeanza kutumika
miaka ya 1990 wakati mfumo wa Kikomunisti ulipoanza kuanguka na kusambaratika.
Katika lugha ya Kiingereza neno "reform" lenye maana ya kuunda upya
ama kufanya upya ndilo lililotumika kuyaelezea mabadiliko ya kisiasa, na
kiuchumi yaliyozikumba nchi za kijamaa. Mabadiliko hayo yalizikumba nchi
mithili ya kimbunga chenye nguvu kinavyoweza kuipiga nyumba iliyojengwa
juu ya msingi mbovu wa mchanga. Katika historia ya Kanisa, neno "reform"
linatafsiriwa kuwa ni matengenezo, na kwa ajili hiyo mabadiliko yote yaliyotokea
ama yaliyolikumba Kanisa kama taasisi kati ya karne ya 14 na ya 16 yalipewa
ama yaliitwa kwa jina la "wakati wa matengenezo". Hata enzi za Manabii
kama akina Isaya, Yeremia, Amosi, Zakaria na Yohana mbatizaji zilikuwa
ni nyakati za matengenezo. Kumbe neno halisi lililostahili kutumika ni
matengenezo badala ya mageuzi.
KATIKA Tanzania, zamani za miaka ya 1989, hadi 1990 dola ya Urusi (USSR) ilipokuwa kwenye kilele cha mtikisiko, magazeti yaliyokuweko hapa nchini, na yaliyotolewa katika lugha ya Kiswahili ni UHURU na MZALENDO hatimaye likaja Mfanyakazi. Kwa makusudi kabisa magazeti hayo yakaamua kuushupalia msamiati wa mageuzi ili tu kuwaonyesha wananchi kwamba hao wanaotaka mabadiliko, wanataka kugeuza mambo na kwamba wako kinyume na mapinduzi yao. Walifanya hivyo kwa makusudi kabisa huku wakijua kwamba kutokana na nguvu ya habari (power of the press) waliyonayo katika jamii yetu ambayo zamani hizo ilitawaliwa na ukiritimba wa chama kimoja uliopelekea kuweka ukiritimba wa habari, basi nguvu hiyo itawafaa katika kupotosha umma usiunge mkono harakati za mabadiliko ambayo walidhani wana uwezo wa kuyazuia yasiingie nchini na kuutikisa mfumo wao wa siasa na utawala. Kwa ajili hiyo neno Reform likapata tafsiri potofu ya kuitwa mageuzi hadi wote tuliokuwa tunajihusisha kwa bidii na harakati za mabadiliko tukaitwa wanamageuzi. Hata hivyo reform inabaki na maana ile ile ya matengenezo na kwa mantiki hiyo mageuzi yaeleweke kwamba ni matengenezo. Kipindi cha matengenezo huja baada ya watu hasa kuharibu sana mambo yanayohusu maisha ya watu hadi kusababisha uwepo uhitaji wa kutengeneza sawa na uhitaji wa kutibu binaadamu inapotokezea kwamba mtu huyo ameugua ugonjwa hatari. Watawala au viongozi kuharibu maisha ya watu ni kitu rahisi sana, hii ni kutokana na ukweli kwamba madaraka ni ulevi, inapotokea watu wa aina moja au wenye mawazo yanayofanana wakadumu madarakani kwa muda mrefu basi hulewa madaraka yao na kupoteza lengo. Tukichukulia mfano wa viongozi wa dini ya Kiyahudi na viongozi wa taifa la Israeli waliofuatia baada ya Mussa, ingawaje walikuwa wanatawala kwa kutumia sheria ile ile ya Mussa ambayo haina kasoro, bado kutokana na kasoro zao binafsi sheria iliharibika na kugeuka kuwa mwiba na mzigo mzito klatika maisha ya watu. Hapo ilipotokea uharibifu wa sheria yaani viongozi kupotoka na kufanya kinyume na mapenzi ya Mungu na pia kinyume cha makusudi ya awali ya sheria, huku wao wenyewe wakidhani kwamba wanatekeleza maagizo ya Mungu yaliyo katika sheria ya Mussa, ndipo walipoinuka Manabii kutabiri, yaani kuonya, kukemea, kukaripia na kufundisha ili wahusika waenende vizuri na Mungu wao (to be upright with God). Mfumo wowote japokuwa utakuwa sahihi lakini kama utakuwa na viongozi wabaya, ni lazima utatoa matunda mabaya. Mbaya zaidi ni hapo inapotokezea kwamba watu wawe wanatawaliwa na mfumo mbaya wenye viongozi wabaya hapo ni sawa na ubaya kupita kiasi. Hivyo ndivyo ilivyokuwa nyakati za Nabii Yeremia. Huyu Nabii, Mungu alimwita huku akingali na umri mdogo tu wa miaka 15. Yeremia alipoitwa alitoa udhuru wa kusema sitoiweza kazi unayonipa ewe Mungu kwa kuwa mimi ni mdogo. Lakini Mungu akamwambia usiseme kwamba mimi ni mdogo maana utakwenda pale nitakapokutuma na kwa yule nitakayekutuma, hutaenda kusema maneno yako bali utasema yale nitakayoweka kinywani mwako. Kisha Yeremia akatoa udhuru mwingine kwamba yeye si mtu mtakatifu na kwahiyo hawezi kuchukuliana na Mungu ambaye kwa asili ni Mungu mtakatifu, lakini pia hoja hiyo Mungu akaizima kwa kusema kabla hujazaliwa nalikujua na kabla ungali (mimba) tumboni mwa mama yako nalikutakasa. Kisha Mungu akaendelea kumfunulia Nabii Yeremia majukumu kwa kusema "Tazama, nimekuweka kuwa nabii wa mataifa ili:- (a) Kung'oa, (b) Kubomoa, (c) Kuharibu na (d) Kuangamiza, Ili kupanda na kujenga". Kinachozungumziwa hapa ni mifumo miovu na uongozi uliyooza kwani haiwezekani mtu akajenga chochote kilicho chema juu ya mfumo mbaya, wala haiwezekani mtu akapanda mbegu njema katika mfumo mwovu kisha akavuna mavuno mema yanayofanana na mbegu aliyoipanda bali ni lazima uovu utaiharibu mbegu njema hadi ikatoa matunda yasiyofaa ama isitoe matunda kabisa. Kwahiyo ni lazima uongozi uliooza, ung'olewe, na mfumo mbaya ubomolewe, uharibiwe na taasisi zake za kidhalimu ziangamizwe kabisa hapo ndipo mtu anaweza akaanzisha kitu kipya katika jamii na kikastawi hata kutoa matunda ya kuonekana. Ndiyo maana baadaye Mungu anaendelea kumwambia Yeremia "Nao watapigana nawe lakini hawatakuweza, watashindana nawe lakini hawatakushinda, usiongope maana mimi niko pamoja nawe ili nikuokoe". Je ni nani hao wa kushindana na Yeremia? Ni nani? Jibu liko wazi nalo ni kwamba hao siyo mashetani wasiokuwa na miili bali ni wanadamu wenzake, nao ni wale watawala dhalimu ambao siku zote huwa hawana jicho la kuuona udhalimu wao badala yake wanakuwa tayari kutumia nguvu za dola na kupambana kwa nguvu zao zote na mtu yeyote yule anayewaeleza ukweli. Udhalimu una kawaida moja nayo ni kwamba unapozidi kiwango huwa unampofusha mtu (mhusika) na kumfanya aone mabaya ndiyo yanayofaa, na mema ndiyo yasiyofaa. Kwa mfano, biashara ya IMF na World Bank ya kuuza na kununua sarafu ni biashara ya udhalimu sawa na maana hiyo inastahili ikomeshwe kama ilivyokomeshwa biashara ya utumwa. Biashara ya kuuza dola moja ya Marekani kwa TShs. Mia nane ama pauni moja ya Uingereza kwa TShs. Elfu moja, ni biashara haramu ambayo inaongeza umaskini kwa nchi maskini na kuziongezea utajiri nchi zilizokwisha tajirika. Ni biashara inayoyafanya mataifa mengine kugeuka kuwa mtumwa wa kudumu wa mataifa tajiri. Lakini wahusika IMF na Benki ya Dunia na viongozi wa nchi maskini kama Tanzania wamepofushwa na dhambi hii hadi kuuona udhalimu huu kama kitu cha kawaida na kinachofaa maishani wakati ambapo kulingana na maneno ya Mungu aliyoyasema kwa kinywa cha Nabii Yeremia hii ni biashara ya kuangamizwa. Mfumo wa sasa wa uchumi duniani, na mfumo wa biashara unastahili kubomolewa na kuharibiwa kabisa ili kuupisha mfumo mpya. Katika uhalisi wa mambo mfumo unaoendelea kutumika sasa katika uchumi, na biashara za kimataifa, ni mfumo mwovu kuliko hata ukomunisti uliokwisha anguka isipokuwa kwa kuwa tu unazinufaisha nchi za magharibi zilizoendana katika mfumo wa ubepari, kwa muda mrefu ndio maana unalindwa lakini kuna kila dalili za kuonyesha kwamba tayari ni mfumo uliokwisha anguka kwasababu nao ni mfumo wa kishetani kama ulivyokuwa ukomunisti. Siku utakapoanguka rasmi utaangusha na serikali nyingi za mataifa makubwa. Mataifa madogo na yenye uchumi dhaifu kama Tanzania yanashiriki katika mfumo huu kama mtekelezaji tu wa kile kinachotakiwa. Kwa mfano kama kinachotakiwa ni faida basi taifa lenye uchumi dhaifu litaambiwa nini cha kufanya ili faida ipatikane pasipo kujali kwamba faida hiyo kubwa kwa IMF na Benki ya Dunia kunaitia hasara kiasi gani nchi husika. Lakini siku zote Mungu amekuwa ndiye muuaji, muangamizaji, na mkomeshaji wa mifumo dhalimu akitumia wanadamu aliowaita kwa kusudi lake. Katika Afrika iliwahi kuinuka kwa biashara ya utumwa ikashamiri kwa miaka zaidi ya mia mbili lakini hatimaye mfumo huo wa utumwa ukakomeshwa. Baadaye ukaja mfumo wa ukoloni ambao ulidumu karibu miaka mia, nao ukakomeshwa. Lakini katika mifumo yote hiyo yaani utumwa, na ukoloni haikukosa wapiga debe waliotumia maandiko matakatifu kujaribu kuhalalisha udhalimu wa mifumo hiyo na papo hapo kuhami isibomolewe, isiharibiwe wala isiangamizwe. Mifumo yote hiyo ilikuwa ni siasa. Utumwa ilikuwa ni siasa isipokuwa ilikuwa ni siasa ya kishetani, ukoloni pia ilikuwa ni siasa, isipokuwa ilikuwa ni siasa ya kishetani, na kama ilivyo kawaida ya siasa yoyote ile, ni lazima liwepo kundi linalonufaika na mfumo huo, na kundi linaloathirika kwa hasara aidha ya kuumizwa ama kukandamizwa. Kwa ajili hiyo wale wote waliojitoa mhanga kupambana kwa nguvu zao zote na utumwa au na ukoloni, walikuwa na wito wa Kimungu mioyoni mwao na kwahiyo walifanya kazi kama manabii wa Mungu, kazi ya kung'oa, kuharibu kubomoa, na kuangamiza, kutokana na ukweli kwamba siku zote Mungu ndiye chanzo cha matengenezo. Hakuna matengenezo (au mageuzi) yoyote yaliyofanywa kwa nguvu za wanadamu peke yake wala matengenezo ambayo yalipata ridhaa ya shetani, kutokana na ukweli kwamba waharibifu wote, au waanzilishi wa mfumo dhalimu na waendelezaji wake huwa wanafanya yote chini ya uvuli wa baba yao ibilisi (Satanic influence). Hivyo tusitegemee yeyote yule anayenufaika na mfumo wa kishetani atapenda mfumo huo ung'olewe au ubomolewe, au uharibiwe, ama uangamizwe badala yake atapigana kwa njia zote kuanzia vita vya maneno hadi vita vya silaha za kudhuru mwili ili kuuhami. Kwa ajili hiyo, wale wote wanaokazana na propaganda hii ya kutaka dini itenganishwe na siasa inabidi wachunguzwe. Kama watatazamwa kwa makini itagundulika kwamba wananufaika na mfumo dhalimu na kwahiyo wasichotaka wao ni mabadiliko yanayoweza kuathiri maslahi yao,wala hawana nia ya kuitetea dini ama jamii inayoumizwa. Chukulia mfano wa mtu mwenye wadhifa serikalini asiyekuwa Mwislamu anasimama kumshambulia Sheikh kwa maneno kwamba asichanganye dini na siasa, ama yule asiye Mkristo anasimama kumshambulia Askofu kwamba asichanganye siasa na dini badala yake "vya Mungu ampe Mungu na vya Kaisari ampe Kaisari". Je huyu anachokitetea hasa nini nini? Ukweli ni kwamba hana uchungu wowote na dini iwe Uislamu, au Ukristo, badala yake ana uchungu na siasa yake ambayo anahisi kwa nguvu za dini ama kwa kutumia nuru na mwanga wa dini watu wengi wenye kuifuata dini hiyo iwe Ukristo au Uislamu wasije wakaona kisha wakaiasi siasa mbaya inayowatawala. Mtu wa namna hii angeona dini inachanganywa na ushirikina wala hangesema, ama angeona siasa inachanganywa na dini ya ushirikiana asingesema kitu kwa kuwa anajua ushirikiana hauna nuru ya ukombozi. Kwahiyo nasema viongozi wa dini wote waliojitokeza kupinga udhalimu iliyo kwenye eneo la siasa wafanye kwa nguvu zao zote wana thawabu kubwa kwa Mungu maana wanachukua nafasi ya Yeremia, kung'oa, kubomoa, kuharibu na kuangamiza. |
YALIYOMO
Tahariri
Kauli ya Sumaye yawakera wananchi Licha ya Katiba ya nchi kutambua uhuru na haki ya kuabudu: Qur’an kizimbani Wapinzani Waishutumu sheria mpya ya uchaguzi CCM wanatumia pesa za serikali kwa kampeni - Chenyenge USHAURI NASAHA
Kalamu ya Mwandishi
MAKALA
MAKALA
MAKALA
Lishe
RIWAYA
- |
|
|
|
|