NASAHA
Na. 053 Jumatano Juni 21 - 27, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Lishe 

Kuhifadhi matunda kwenye jokofu

CHAMOS, H.J 

SI matunda yote yanayopatikana majira yote.Kuhifadhi matunda kwenye jokofu kunaweza kutunza ladha halisi ya matunda ya masika mpaka kiangazi iwapo kanuni muhimu zitazingatiwa. Halikadhalika matunda katika msimu wake hupatikana kwa bei rahisi na kwa urahisi zaidi.

Kuhifadhi matunda katika jokofu (freezing) ni njia nzuri ya kutunza ubora wa matunda kwa muda mrefu. Matunda (mengi) karibu ya aina zote huweza kuhifadhika vizuri kuliko utakavyofikiri.Yaani yatabaki katika ladha yake asilia. Badala ya njia hii ya kuweka kwenye jokofu, njia nyingine ni ile ya kuhifadhi kwenye makopo, ambayo hailiachi tunda katika ladha na umbo asilia. Kwa hiyo ni njia ya jokofu pekee ndio inayoweza kutunza uasilia. 

Kama ilivyo kwa vyakula vingine vyo vyote , matunda yatatoka kwenye jokofu kama vile ulivyoyaweka katika ubora na ukubwa. Kwa sababu hii ni vyema kuwa mwangalifu katika aina za matunda na jinsi ya kuhifadhi ili kupata matokeo mazuri. 

Matunda kwa ajili ya kuhifadhi kwenye jokofu ni lazima yawe yameiva kiasi cha kuweza kuliwa.Yaani yasiive sana wala yasiwe mabichi sana. Usitegemee jokofu kuivisha matunda yako iwapo utayaweka mabichi. Iwapo matunda yatakuwa yameiva sana yashikwe kwa utaratibu ili yasichubuke hata kidogo. Na yale ambayo yameiva sana yanaweza kuhifadhiwa kwa njia nyingine, mathalani kutengeneza maji ya matunda, jam au juice nzito ya kupondaponda. 

Wakati unapanga matunda yako zingatia kuweka kila matunda peke yake. Kuchanganya matunda kunaweza kusababisha uharibifu mapema zaidi kuliko inavyoweza kuwa. Usihifadhi matunda kwa wingi kuliko uwezo wa jokofu lako. 

Kuna aina mbalimbali za kuhifadhi matunda. Njia kavu ya wazi hufaa zaidi kwa matunda laini na yaliyoiva na kukatwakatwa. Mfano nanasi ililoiva limenywa na kukatwakatwa, vipande kisha viwekwe kwenye sinia (tray) mpaka vitakapokuwa vigumu yaani tayari vina barafu. Vitakapokuwa tayari unaweza kuvitoa na kuviweka kwenye vikopo au vibakuli vya plastiki vyenye mfuniko. Baada ya hapo ndipo unaweka vibakuli au vikopo hivyo kwenye jokofu. Usihifadhi vipande au matunda yaliyomenywa bila kuwa na barafu (ice) hayatadumu muda mrefu. 

Kuhifadhi matunda kama yalivyo,inawezekana kwa matunda ambayo yana ngozi ngumu kiasi kama vile mapera, embe, machungwa n.k.Iwapo utatumia njia hii itakubidi uchague matunda yasiyo na tundu hata dogo. Vilevile njia hii si ya muda mrefu zaidi kama ile ya kumenya, kugandisha na kuhifadhi. Matunda mazima huweza kudumu kwa miezi minne hadi sita. 

Matunda yatakapohifadhiwa mazima yasitolewe vikonyo kwani iwapo vikitolewa vitaleta uwazi (tundu). Lakini kama uangalifu utakuwepo kuzuia kutokea matundu waweza kuvitoa. Kausha baada ya kuyaosha matunda kwa kitambaa safi. Panga matunda vizuri kwenye chombo (tray) mojamoja ukiacha nafasi kati ya tunda na tunda. Weka kwenye jokofu sehemu inayogandisha haraka. Yakisha kuwa magumu toa weka kwenye vifuko au vibakuli vya plastiki funga mfuko vizuri au funika bakuli sawasawa kuzuia hewa isiingie. Bandika lebo kuonesha siku uliyoweka na aina gani ya matunda. Weka mifuko yako kwenye sehemu ya baridi ya kati kwenye jokofu tayari kwa matumizi ya baadaye. Kumbuka kuwa ndizi mbivu hazifai kuhifadhiwa kwa muda mrefu unaozidi mwezi mmoja. 

Njia nyingine ni ya kuhifadhi matunda katika hali ya majimaji(juisi). Katika njia hii utatakiwa kwanza utengeneze "sirap". Sirap ni maji ni yaliyochanganywa na sukari. Ukiwa na sirap, unaandaa matunda yako vizuri kwa kumenya, kukatakata katika ukubwa unaotaka. Panga vipande vizuri kwenye kibakuli kipana cha pembe nne au duara kubwa cha plastiki. Halafu mwagia sirap juu yake hadi vipande vyote vimezama. Hakikisha umeacha nafasi kidogo kwenye bakuli kwani maji huvimba yanapoganda. Na sirap utayoweka iwe imepoa kiasi cha kuwa na ubaridi ndipo vimwagie. Funika na weka kwenye jokofu. Kwa njia hii matunda yaweza kudumu zaidi ya miezi 4. Wakati wa kutumia vipande hivyo vya matunda yeyusha kwanza. Ukipenda unaweza kutumia sirap tena. 

Jinsi ya kutengeneza "sirap". Chemsha maji katika moto mdogo na yeyusha sukari ndani yake. Ikisha yeyuka,ongeza moto na acha ichemke sana. Iopoe acha ipoe. Sirap ipo tayari kwa matumizi. Kwa kumwagia kwenye matunda, iweke kwenye jokofu ipoe zaidi ndipo umwagie. 

Hayo ndio maelezo kwa ufupi kuhusu uhifadhi wa matunda kwenye jokofu. 

Juu
 

YALIYOMO
 
 

Tahariri
Uhuru wa kuabudu utiwe katika matendo bila ya ubaguzi

Kauli ya Sumaye yawakera wananchi

Licha ya Katiba ya nchi kutambua uhuru na haki ya kuabudu: Qur’an kizimbani

CCM yapata kiwewe

Wapinzani Waishutumu sheria mpya ya uchaguzi

Mtoto wa Afrika yutaabani

CCM wanatumia pesa za serikali kwa kampeni - Chenyenge

USHAURI NASAHA
Dhuluma haiondoki bila kubadili mfumo

Habari za Mikoani

Kalamu ya Mwandishi
Kweli CUF ni ngangari!

MAKALA
Manabii wa kale na mageuzi

MAKALA
CCM na sera za maendeleo

MAKALA
Wajibu wa wananchi kwenye uchaguzi mkuu

Habari za Kimataifa

Lishe
Kuhifadhi matunda kwenye jokofu

RIWAYA
Dunia ndivyo ilivyo - 3

MASHAIRI

MICHEZO

  • Uingereza, Ujerumani nje
  • Washabiki wamshangaa Mkapa, wambeza Sumaye
  • BMT waipiga ngwara FAT

  • -

       Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita