AN-NUUR 
Na.173 Rajab 1419, Oktoba 30 - Novemba 6, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
 
Vijana wa pangoni As-haabil Kahfi ni jina lililotumika katika Qur’an (Sura ya 18) kumaanisha vijana waliokimbilia pangoni kukwepa mateso ambayo wangeyapata kutokana na kumuamini kwao Mwenyezi Mungu. 

AS-HAABIL KAHFI KATIKA QUR’AN 

Kuja kwa kisa hiki ndani ya Qur’an kumetokana na maswali aliyokuwa akiulizwa Mtume Muhamamad (s.a.w.). Wapagani walichochewa na Wayahudi wamuulize Mtume (s.a.w.) maswali matatu, kwanza kuhusu roho (17:85). Pili kuhusu Dhul Karnain (18:83) na tatu kuhusu hawa As-haabil Kahf. Mtume (s.a.w.) alikuwa hana ujuzi wa masuala kama haya, ambayo yalikuwa yanahitaji elimu ya kina, (kama vile kuhusu roho) na mengine yalitokea karne za nyuma kabla hajazaliwa. Mtume (s.a.w.) alikuwa akiwaomba wampe muda ili apate majibu kutoka kwa Mola wake Allah (s.w.), na ndio maana tunasoma katika aya ya 23 ya Sura yenye kisa hiki (Al-Kahf, Mtume anaambiwa: 

"Wala usiseme kamwe kwa lolote lile kuwa: "Nitalifanya kesho",idipokuwa (uongeze kusema) "Inshaallah (Mwenyezi Mungu akipenda)..." 

Hii ilitokea baada ya Mtumekuwaahidi waliomuuliza maswali kwamba angewajibu siku iliyofuatia, lakini Allah (s.w.) alilichelewesha jibu, na wenye maswali yao wakamsumbua sana Mtume, hadi pale Allah (s.w.) alipoamua kumletea majawabu. 

MAFUNZO: 

Kisa hiki kinatupa mafunzo mbali mbali. Mafunzo haya tunayapata kwa kufuatilia aya moja hadi nyingine zinazogusia kisa chenyewe. 

Kisa hasa kinaanza katika aya ya 9. Aya hii inauliza. 

Je, unafikiri kwamba wale watu wa pangoni na raqiim walikuwa ni miongoni mwa dalili zetu za ajabu? 

Mwenyezi Mungu ameleta baadhi ya aya zikiwa katika hali ya maswali yasiyohitaji majibu, kwani utakuta aya nyingi zinazofuatia maswali haya huwa ni majibu yake. Maswali haya yanafanya kazi ya kutuweka tayari kupokea maelezo yanayoyahusu. 

Aya inawataja watu wa pangoni na raqiim. Neno raqiim limepewa tafsiri tofauti na wafasiri mbalimbali. Wengine wamesema lina maana ya maandiko (inscription). Inasemekana kuwa raqim ni upapi wa madini ya risasi ambao umeandikwa majina ya vijana wa pangoni wajulikano kama Walalaji Saba (the Seven Sleepers), pamoja na habari yao nzima. Wafasiri wengine wanasema raqiim ni jina la mbwa ambaye alikuwa pamoja na wale vijana. Hata hivyo, Qur’an si kitabu cha hadithi, hivyo mkazo haukutiwa katika kusimulia hadithi nzima, ila katika vipengele ambavyo vina mafunzo. 

Aya ya 10 inaanza kutoa maelezo. 

Vijana hao walipokimbilia katika pango na wakasema: "Mola wetu, tupe rehema zinazotoka kwako na tutengenezee uongofu katika mambo yetu." 

Funzo la kwanza tunalolipata hapa ni kwamba watu wale wa pangoni walikuwa ni vijana, na wao walikuwa wanakimbia kujisalimisha na uovu wa jamii yao, kwa ajili ya kutaka radhi za Allah (s.w.), na wakamuomba Allah ndiye awanyooshee mambo yao. 

Hawa vijana walikuwa wanaikimbia jamii iliyotaka kuwalazimisha waabudu kinyume na imani ya kweli. Vijana wa leo wanayo mengi ya kuyakimbia kwa ajili ya kutaka radhi za Allah (s.w.), tena kwa uamuzi wao tu, bila ya kutenzwa nguvu. 

Aya ya 11 inatupeleka moja kwa moja pangoni na kutueleza kubwa lililotokea pale. 

Tukaziba masikio yao katika pango lile kwa idadi ya miaka mingi. 

Hii ina maana kwamba vijana wale kihisia wakaondolewa kabisa katika mazingira ya ulimwengu waliokuwemo - ndipo tunapoambiwa walilala usingizi wakiwa hawajui kilichokuwa kinaendelea. 

Aya ya 12 inatueleza yaliyotokea baada ya hiyo miaka mingi: 

Kisha tukawaamsha ili tujulishe ni lipi katika makundi mawili lililohisabu sawasawa muda waliokaa pangoni

Makundi mawili hapa ni vijana wenyewe wa pangoni na wale watu waliokuwa wakiishi wakati huo baada ya kuamka kwao. Hapa ilibidi wapambanishwe ili kujaribiwa ni nani angekuwa sahihi katika kuhesabu muda. Somo kubwa hapa ni kwamba watu wanaweza kubishana sana katika masuala fulani (kama ambavyo kumekuwa na mawazo mbali mbali kuhusu muda waliolala vijana wale pangoni) na wasipate jibu,zaidi ya kupoteza muda katika mabishano yasiyosawasaidia wao wala jamii yao. La maana hapa ni kusema: "Mwenyezi Mungu ndiye mjuzi." (18:19). 

Aya ya 13 zinazidi kutupanulia wasifu wa vijana wale, kwa kuturudisha nyuma kidogo (flash back) kutupasha yaliyotokea kabla vijana wale hawajakimbia. 

Sisi tunakusimulia habari zao kwa ukweli. Hakika hao walikuwa ni vijana waliomuamini mola wao. Nasi tukawazidishia uongofu. 

Mwenyezi Mungu hapa anasisitizia ukweli wa hadithi ya vijana wale kwamba hiki sio kisa cha kubuni (fiction). Kisha msisitizo unawekwa hapa kwamba wale vijana wakikuwa ni waumini kweli kweli, sio wababaishaji, na kutokana na hilo Mungu akawazidishia uongofu (yaani akawaongoza katika mafanikio). 

Aya ya 14 inatupa jaza ya mtu mwenye imani thabiti anayoipata kutoka kwa Mwenyezi Mungu. 

Na tukazitia nguvu nyoyo zao waliposimama (kidete) wakasema (wazi): "Mola wetu ni Mola wa mbingu na ardhi. Hatutamwabudu kabisa Mungu mwingine badala yake, kwani hapo tutakuwa tumesema uovu uliopita kiasi. 

Imani zao zilikuwa thabiti, na Mwenyezi Mungu akazitia nguvu nyoyo zao, na hawakuogopa kuitangaza imani yao na kuziweka wazi sera zao. Kwa uthabiti mkubwa wakaisimamisha kalima ya Laa ilaahba illallah. Usipomuogopa Allah lazima utawaogopa wengine, lakini imani yako ikiwa thabiti, hutishwi na mfalme wala zimwi. Na Allah ndiye anakupa ulinzi. 

Aya ya 15 inatueleza sababu za wao kukataa imani ya watu wa jamii yao. Wanatoa hoja. 

Hawa watu wetu wamefanya miungu wengine badala yake (Mungu wa kweli). Kwa nini hawaleti juu yao vigezo (dalili/hoja) za wazi. Basi ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule anayemzulia Mungu uongo? 

Hivyo tunaona kuwa hawa vijana hawakukubali kuamini mambo kibubusa, ila walitaka vigezo au hoja za imani ya watu katika wakati ule, hapo ndipo wakawa wametangaza vita na utawala. 

Aya ya 16 inatueleza kuhusu wazo lililowafikia: 

"Na mnapojitenga nao na vile wanavyoviabudu badala ya Mwenyezi Mungu, basi kimbilieni pangoni; huko Mola wenu atawafungulia neema zake na kuwafanyia wepesi katika mambo yenu." 

Aya ya 17 inaturudisha pangoni, wakati vijana wale wakiwa katika usingizi wao. 

Unaliona jua linapochomoza linapita mbali na pango lao kwa upande wa kulia. Na linapokuwa linakuchwa linawapitia upande wa kushoto (haliwapati), na hali wao wako katika uwazi ndani yake humo. Hizo ni katika ishara za uwezo wa Mwenyezi Mungu. Anayeongozwa na Mwenyezi Mungu, basi huyo ndiye kaongoka, na anayepotea, huwezi kumpatia mlinzi wala mwongozi. 

Hapa tunapewa picha ya mwongozo walioupata. Walijiwa na wazo kukimbilia pangoni bila ya kujua hali ya pango lile kwa usalama wao. Lakini kwa vile walimtegemea Allah kwa uongofu, walifika mahala ambapo palikuwa salama katika hali zote, hata jua likawa haliwapati. Anayefuata mwongozo wa Allah amesalimika duniani na akhera, na anayemuomba Allah kwa dhati, basi Allah humuongoza katika njia za salama tupu. 

Aya ya 18 inaendelea kutupa picha ya vijana wale wakiwa mle pangoni.: 

Na unawadhani wako macho na hali wamelala. Na tunawageuza upande wa kulia na upande wa kushoto. Na mbwa wao akiwa amenyoosha miguu yake ya mbele kizingitini. Kama ungewaona hakika ungegeuka upesi kuwakimbia, na hakika ungejawa na hofu juu yao. 

Hapa tunapata picha pia kwamba vijana wale walionekana kama walikuwa macho japo walikuwa wamelala. Tunaweza kusema vijana wenye imani thabiti ndivyo wanavyoonekana, hata kama hawajafanya lolote, basi wengine huona wanafanya mambo (hasa wale wasiopenda wanachokifanya), hivyo ule mjumuiko wao tu ni tabu kwa wengine, na unatia moyo kwa wanaowatakia mema.Vijana waliendelea kupata huduma ya rehema za Allah kwa kugeuzwa miili yao mara kwa mara kama mtu ageukavyo usingizini kupata kupumzisha upande uliolaliwa muda mrefu. Pamoja nao alikuwa ni bwa wao, ambaye alikuwa kizingitini kama mlinzi vile, (japo naye alilala). Tunaambiwa kuwa kama mtu anagebahatika kuwaona, angegeuka na kutimua mbio kwa hofu, na angebakia hivyo akiwa amejawa na hofu kubwa. Funzo la hapa ni kwamba, wale vijana walikuwa wamelala fofofo, lakini wanatia hofu. Kuonekana kwao kama wako macho na hali walikuwa wamelelala, na kutisha kwao, ni ulinzi aliowawekea Mwenyezi Mungu (defense mechanism) bila wao wenyewe kujua. Ndivyo hivyo ambavyo vijana wenye msimamo walivyo. Huwa wanatisha. Mahala walipo wanaogopewa. Huu ndio mpango wa Mwenyezi Mungu, kwamba vijana wa kazi huogopewa kabla hawajaanza kazi. Je, vijana wa leo tunatisha? Na kutisha huku sio kwa sura mbaya, bali watu wa Mungu, hasa vijana, huogopewa, kwa imani zao na matendo yao, na hivyo wanapokuwepo mahala, wengine, hasa waovu na madhalimu, hushika adabu zao. 

Aya ya 19 inaanza kusimulia yaliyotokea baada ya kuamka kwao. 

Basi namna hii tuliwaamsha ili waulizane kati yao, akasema msemaji katika wao: "Mmekaa muda gani (humu)?" Wakasema: "Tumekaa siku moja au sehemu ya siku." (Wengine) wakasema: "Mola wenu anajua zaidi muda mliokaa. Basi mtumeni mmoja wenu pamoja na fedha yenu hii mjini na akatazame chakula bora (kizuri) awaletee riziki kutokana nacho. Na (tena) afanye mambo haya kwa busara, wala asiwataje kabisa kwa yeyote." 

Kwanza baada ya kuamka, walianza kuulizana kuhusu muda waliokuwepo pale. Funzo tunalolipata ni kwamba kwa vijana wale suala la muda lilikuwa ni la kwanza (time consciousness). Walipojaribu kujadiliana au kutofautina kuhusu muda, wakaacha majadiliano wakasema Allah (s.w.) ndiye aliyejua zaidi suala la muda waliokaa pale. 

Uamuzi wa la kufanya ukafuatia, wakaamua kumtuma mmoja wao aende kununua chakula. Tahadhari walizozitoa ni:- 

1. Akatazame chakula kizuri. Neno kizuri hapa limetiliwa mkazo kwa sababu vijana wale hawakufikiria tu suala la kununua chakula, bali chakula kizuri. Uzuri unaosisitizwa hapa ni uzuri wa kiafya, kwamba ni lazima wapate chakula bora kitakachowapa afya nzuri katika kukaa kwao kule, na vile vile kizuri kwa mujibu wa imani yao, kisije kikawa cha haramu. 

2. Afanya mambo kwa busara na tahadhari kubwa. 

3. Asiwataje wenzake (yaani ikitokea bahati mbaya ya kukamatwa, afiche siri kabisa). 

Aya ya 20 inatupa dhana waliokuwa nayo wakati wakichukua tahadhari, wakidhani wale watu wao bado wamo kwenye ukafiri. 

"Kwani wao wakiwatokeeni watawarujumu, au watawarudisha kwenye mila zao, na hapo hamtafaulu abadan." 

Neno kurujumu hutumika na wafasiri wengi kama "kupiga kwa mawe". lakini leo hii tusitegemee kuwa madhalimu watatumia mawe. Mawe ya sasa hivi ni risasi na mabomu. Hivyo tahadhari ya rujuma hapa iwe ni ya juu zaidi kuendana na wakati wetu. Leo hii risasi na mabomu ndio zinazotumika na madhalimu kote duniani dhidi ya Waislamu, hasa vijana. Hivyo, kama vijana hawa walivyochukua tahadhari ya kutojulikana walipo, vijana walio katika jamii yenye udhalimu wachukue tahadhari ya kutojulikana katika harakati zao. Endapo itatokea mmoja wao akakutana na madhalimu, basi ni mwiko kuwataja wenzake kwa yeyote. 

Aya ya 21 inatupasha kwamba yule aliyetumwa alipoitoa ile sarafu yao, watu wakaishangaa, na wakagundua siri iliyokuwepo. 

Na namna hii tuliwatambulisha (kwa watu) ili watu wapate kujua ya kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu (ya ufufuo) ni kweli, na kwamba siku ya mwisho haina shaka. Na (watu) walipobishana juu ya suala lao (vijana wa pangoni) wakasema. "Jengeni jengo juu yao. Mola wao anawajua vyema." Wale waliokuwa na sauti juu ya suala lao wakasema: "Tutajenga msikiti juu yao." 

Hivyo vijana wale waliamshwa ili wakutane na watu, ili watu hao wapate kupata mafunzo kuhusu kufufuliwa, pamoja na uhakika wa siku ya mwisho. 

Aya ya 22 inatuelezea mabishano ya watu kuhusu idadi ya vijana wale. 

Wengine wanasema: Walikuwa watatu na wa nne mbwa wao", na wengine wanasema "Walikuwa watano, wa sita mbwa wao"; wakibahatisha wasioyajua. Na wengine wanasema: "Walikuwa saba, na wa nane wao mbwa wao." Basi usibishane juu yao ila kwa masuala yaliyo wazi. Wala usiulize habari zao kwa yeyote yule. 

Funzo tunalolipata hapa ni kwamba, suala la idadi ya watu sio la msingi mbele ya Allah. Mnapokuwa pamoja na Allah kwa dhati mjue mna nguvu tu hata kama mko wachache. 

Hivyo, suala la vijana wale walikuwa wangapi si la msingi. La msingi walikuwaje na walifanya nini. 

Mwisho tunarushwa hadi aya ya 25, ambapo tunatajiwa muda waliokaa vijana wale pangoni. 

Na walikaa katika pango lao miaka mia tatu,na wakazidisha tisa. 

Hivyo tunajifunza hapa kuwa vijana hawa walikaa pangoni katika hali yao ya usingizi kwa muda wa karne tatu na miaka tisa takriban. 

Inasemekana kuwa kwa hesabu ya miaka ya jua 300 ni sawa na miaka ya mwezi 306. Hata hivyo, hii ni hesabu kwa akili ya kibinadamu, Mwenyezi Mungu pekee ndiye anayejua hesabu kamili ya muda waliokaa kama inavyoeleze aya iliyofuatia hii (aya ya 26). 

La msingi katika kisa hiki ni uimara wa vijana wale, ambao ulimridhisha Allah hadi wao wakawa ni fano kwa vijana wa Kiislamu wa leo. Tukiwa na imani thabiti, tutapata ulinzi na mwongozo wa Allah (s.w.), na mwenye ulinzi na mwongozo wa Allah (s.w.) ni mwenye kufanikiwa tu. 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 

TAHARIRI 
Wakipewa fursa watainusuru nchi

Wasomi watetea haki ya wananchi kumiliki ardhi

Serikali izungumze na wananchi–Mzee Gonga

Akina mama watakiwa kushikamana na dini yao

Maoni
Serikali inaWhite Paper:  Wananchi mna nini?

Dondoo za Saikolojia: Hoja kengeza
Na Abu Halima Sa Changwa

Makala ya mtangazaji
Khatamy sio Gorbacheiv!!!

Makala
Malipo ya fadhila
Na Mohamed Saleh

Tanzania tuna sera gani kuhusu kanda
Na Abu Abdullah, Tanga

Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo- 2
Na Nandenga wa Mkomidachi

Teknologia
Jifunze Kuunganisha Kompyuta (3)
Na Hassan Omar

Makala na habari
'Usiiparamie ovyo Theolojia'
Na Charles Kamuhabwa, DSA Mtwara

Mwinyimkuu kufanya sensa ya waumini Magomeni
Na Jamillah Nassoro

Same tusilimu upya

Wazazi Mwanza wahimizwa kuwashonea watoto wao Hijab
Na Idd Katimba, Mwanza

Tuwaige Wangazija, 'tutafanikiwa'
Mwandishi: Maalim Bassalah

Serikali imeweka rekodi ya kutisha – Sheikh Salim
Na Mwandishi Wetu

Muhadhara waunguruma Geita
Na Hussein Abdallah, Geita

Fuateni Sharia ya Allah - Sheikh
Na Badru Kimwaga

Wanawake wa Kiislamu Mburahati wahimizwa kutafuta elimu

Mafunzo ya Qur'an
Vijana wa pangoni

Barua za wasomaji 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na lishe
Chakula ni silaha ya kukabiliana na changamoto ya kansa
Na Mujahid Mwinyimvua
 
 

 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita