AN-NUUR 
Na.173 Rajab 1419, Oktoba 30 - Novemba 6, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
 
Tuwaige Wangazija, ‘tutafanikiwa’ 

Mwandishi: Maalim Bassalah 

JAMII ya Kingazija hapa Dar es Salaam, na hata nchini kote, ina watu wachache sana. Lakini juu ya uchache wao, wana umoja na bidii ya mchwa ya kupanda udongo wa kukandikia nyumba yake, siyo kwa maji bali kwa mate na kinywa chake. Wiki iliyopita jamii iliandaa hafla iliyofana sana kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa Msikiti Ngazija uliopo katikati ya Jiji. 

Kwa kweli Wangazija wametuonyesha kuwa penye umoja na nia, pana njia. Ingawa wao ni wachache kwa idadi, na kwa kipato hawana hali nzuri, lakini inaonekana rasilimali kubwa wanayoitegemea maishani mwao ni ule mshikamano wao. 

Walijijua kwa unyonge wao wasingalimudu peke yao gharama za kuujenga upya Msikiti huo, zinazokadiriwa kufikia milioni mia mbili na hamsini. Kwa hivyo walikutana wakashauriana na kuandaa mkakati wa kutafuta jinsi ya kupata fedha za ujenzi huo. 

Walitafuta ushauri na msaada wa kila yule waliyemdhania kuwa anaweza kufanikisha lengo lao. Hawakujali rangi, kabila au madhehebu ya mtu. Kama walimwona mtu huyo anafaa kwa jambo fulani; basi hawakusita kumwendea kumwomba msaada wake. 

Inaonekana hawakumdharau hata yule aliye fundi wa kuonja chumvi, au sambusa na kababu ili kuona kama zimekolea viungo au hapana; kwani Mashaalalh, hata dhifa waliyoiandaa maridhawa na hakusikika yeyote akitoa kasoro. Ukumbi uliofanyiwa shughuli hiyo nao ulipambika vizuri sana ukidhihirisha ustadi wa waliopamba namna hivyo. Kila kilichopangwa kifanywe kilifanywa kwa umahiri mkubwa. Mradi ratiba ilikwenda kama ilivyokusudiwa. 

Hawakusema madamu huo ni Msikiti Ngazija, basi hafla hiyo iongozwe na Wangazija peke yao. Walielewa kuwa wakijitenga nao watatengwa. Na wana sababu gani ya kujitenga ? Na hali Msikiti huo unatumiwa na Waislamu wote, wawe ni Wangazija au wengineo. Wao wamebaki ni wadhamini tu ila kuona kuwa nyumba hiyo ya ibada inatumika kama inavyotakikana. Huu ni mfano mzuri wa ushirikiano walioweza kutuonyesha. Inafaa na sisi wengine tuuige. 

Msikiti Ngazija ulianzishwa katika miaka ya arobaini, kama ni msala kwa wafanyakazi wa eneo hilo. Lakini kidogo kidogo ukajengwa jengwa mpaka ukapata jengo la kudumu ambalo ndilo hilo linaloonekana hivi sasa. Kutokana na kukua kwa Jiji la Dar es Salaam, na kuongezeka idadi ya wakaazi wake, imebidi Msikiti huo uwe mdogo, haukidhi tena mahitaji ya wakati tulionao. 

Waumini wanaosali hapo wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa wakati wa kusali sala za jamaa. Inawabidi wasali jamaa mbili au tatu kwa zamu. Na sehemu ulipo Msikiti huo hakuna Msikiti mwingine karibu. Waislamu wote wanautegemea Msikiti huo lakini ndiyo una tatizo la uhaba wa nafasi. Kuona hivyo, wadhamini wakashauriana na waumini wakaona ipo haja ya kuupanua Msikiti huo. Lakini kwa vile kiwanja chake ni finyu sana waliona heri wauvunje Msikiti wote na wajenge jengo la ghorofa. 

Wakaamua wachangishane kwa ajili ya kupata gharama za ujenzi. Walianzisha mchango hapo hapo Msikitini; kila wakikutana walikuwa wakichangishana, kidogo kidogo, kila mmoja kwa kadiri ya uwezo wake. Michango hiyo iliweza kukusanya shilingi milioni tisa na ushee. 

Ilikuwa kama wasemavyo Waswahili, "Haba na haba hujaza kibaba". Naam na si uwongo kibaba kilijaa ! Ingawa walikuwa wakichangia shilingi shilingi na shilingi tano na kumi na hamsini na mfano wa hizo, lakini zilihifadhiwa katika mikono yenye uaminifu na nyoyo zilizojaa kinaa. Laiti hizo shilingi mbili tatu zilizokuwa zikichangwa na kudundulizwa zingaliangukia mikono inayovuja; nyoyo zilizotawaliwa na tamaa zingalivuja zote, kisipatikane kitu. 

Milioni tisa ni fedha ndogo sana kwa ujenzi wa Msikiti kama huo. Lakini ndizo waumini wa Msikiti Ngazija wanaosali hapo na wale wanaokutana hapo kila Alhamisi kusoma uradi wa Al-Attas walizomudu kuzikusanya; mradi zipo na zimehifadhiwa vyema. Misikiti mingapi na vikundi vingapi vya Kiislamu vinavyosanyasanya shilingi shilingi nahata zaidi ya hizo lakini maisha hazifikii milioni; na hata zikifika hivyo tunahamaki kuyeyuka kama barafu. Na afadhali barafu maana inayeyuka unaweza ukapata maji lakini hizo fedha huambulii chochote. Tunazidharau na kuzifuja shilingi shilingi mwishowe zinatukosesha mamilioni. 

Baada ya kuona kuwa fedha zinazohitajika kwa ujenzi ni nyingi sana, na zile zilizochangwa ni kidogo sana, jamii ya Kingazija ilikutana kuzungumzia vipi watapata fedha. Waliamua waandae chakula cha hisani kwa ajili ya kutafuta michango. Kazi ya kuandaa hafla hiyo walipewa vijana waifanikishe. 

Vijana katika jamii yoyote ni hazina bora ya kutumainiwa. Wakishirikishwa katika mambo yanayohudu jamii wanaweza kufanya maajabu makubwa katika kuiletea jamii hiyo maendeleo. Jambo hilo wengi wetu hatulioni. Kila wanapotokea vijana katika Misikiti yetu, wenye moyo na ari ya kutaka kuleta maendeleo, hupigwa vita na vingunge wanaohofia kupokonywa nyadhifa zao. Matokeo yake Misikiti mingi imedorora na imeshindwa kujiletea maendeleo. Ili kubadili hiyo inabidi wazee wabaki kama wadhamini na washauri tu; na utendaji wote wawaachie vijana wanaoweza kupiga mbio huku na kule kutafuta maendeleo. 

Basi wadhamini wa Msikiti Ngazija walibaki kama ni washauri tu na jukumu lote wakakabidhiwa vijana. Naam, vijana hao wakaiandaa hafla hiyo na ikafana sana. Waislamu wakaitikia kwa moyo mkunjufu. Kwa muda mfupi usiofikia masaa matano tayari ziliweza kupatikana jumla ya shilingi milioni sabini, mbali ya ahadi mbalimbali zilizotolewa na wafadhili. Kuna walioahidi kutoa vifaa vya ujenzi, kama saruji na nondo, na wapo waliochukua ahadi ya kuweka umeme katika jengo lote na wengine wamesema watajitolea kuleta vifaa vyote vya kupazia sauti. Na tunaamini kuwa ujenzi utakapoanza wengi watajitokeza kutoa michango yao ya hali na mali. 

Jambo hilo limeonyesha kuwa Waislamu wana moyo na uwezo wa kuchangia kwa ajili ya maendeleo yao. Na wakati wa kufanya hivyo hawajali tofauti zao. Wanachokihitaji ni mshikamano, uongozi mzuri, uaminifu na uhamasishaji. Vitu hivyo ndivyo vilivyokuwa siri kubwa ya mafanikio ya hafla hiyo. Msikiti Ngazija haukuchangiwa na Wangazija peke yao, bali kwa ukweli ni Waislamu wote, nao ndio waliotoa sehemu kubwa ya mchango huo. Waafrika, Waarabu na Wahindi, weupe na weusi wote walichangia. Huo ndio mshikamano wa Kiislamu. Basi na uendelezwe. 

Tukitaka tusitake Waislamu tuko nyuma sana kimaendeleo katika nchi hii. Shule zinazoweza kunasibishwa kuwa ni za Kiislamu ni chache sana na hatuna hata hospitali moja ya kujivunia. Zipo zahanati, lakini nazo ni haba na hazipo katika hali ya kuridhisha. Wakati wenzetu wanamiliki vyombo vya habari, kama redio na magazeti na pengine televisheni, sisi tuna gazeti moja tu la AN-NUUR, nalo halina nyenzo zinazohitajika kulipa ufanisi gazeti hilo. 

Wala halipati msaada wa uhakika. Lipo lipo tu kwa rehema ya Allah (s.w.) na juhudi za wale waliojitolea nafsi zao na wakati wao kuliendeleza. Waislamu tutabaki katika hali kama hii mpaka lini ? Ni wajibu wetu tuanze kujitafutia maendeleo. 

Tuige vile walivyofanya Wangazija. Tuwashirikishe Waislamu wote wachangie kwa ajili ya maendeleo yao. Uweko mfuko wa maendeleo ya Waislamu kwa nchi nzima. Waislamu walipochangia ujenzi wa Msikiti Ngazija hawakuwa na shaka na wale waliokuwa wakichangisha. Waliwaona ni waaminifu na kwa hiyo hawakuwa na wasiwasi nao. Ndiyo maana wakachangia kwa ukarimu mkubwa. Bila ya shaka wakichaguliwa watu wakweli, waaminifu, waadilifu, wanaokubalika na jamii, Waislamu watakuwa na moyo wa kuchangia. Lakini tukichagua matapeli, tutaondokea patupu ! Inawezekana tujaribu ! 



Serikali imeweka rekodi ya kutisha – Sheikh Salim 

Na Mwandishi Wetu 

KITENDO cha serikali kuchoma moto mashamba na vyakula vya wananchi wa Nzasa kimemuhuzunisha kila mtu aliye japo na chembe ya ubinadamu katika nafsi yake.  

Hayo yameelezwa katika khotuba ya Ijumaa katika Msikiti wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Oktoba 23, 1998. 

Katika khotuba yake, Khatibu Sheikh Salim Khotour alisema kwamba serikali imeweka rekodi ya kutisha na ya kipekee kwa kufanya vitendo ambavyo dunia nzima huvinasibisha na ama wahuni au magaidi. 

Akinukuu aya ya Qur’an, Sheikh Salim alisema kwamba Mwenyezi Mungu hapendi uharibifu ikiwa ni pamoja na kuangamiza mimea na roho za watu. 

Alitoa wito kwa Waislamu popote walipo, kuwasaidia wakazi wa Nzasa bial kujali dini zao kama Qur’an inavyoagiza kuwatetea wanyonge wanaonyanyaswa kwa sababu tu ya unyonge wao. 

Aliuliza ikiwa serikali inayotarajiwa kuwalinda raia hao, ndio inayowachomea moto nyumba zao huku mawaziri na wakuu wa mikoa wakizikejeli nyumba hizo, ni nani atakayewasaidia watu hao kama si raia wenzi wao ? 

Alinukuu Hadith ya Mtume (s.a.w.) isemayo kwamba mtu asiyetaka kushughulika na matatizo ya wengine si katika sisi. 

Akiongelea hoja ya mazingira, Sheikh Salim alisema kwamba Mwenyezi Mungu ameumba vitu vyote kwa ajili ya manufaa ya binadamu. Vipi leo mazingira yawe bora kuliko binadamu ? alihoji. 

Kuhusu suala la kuvamia hifadhi, alisema kwamba hili lipo sehemu nyingine. Akasema huko Kilimanjaro watu hukata miti na mara kwa mara huchoma misitu, lakini huelimishwa, hawachomewi nyumba moto. 

Kwa hatua hii ya kuchoma nyumba moto, alisema kwamba nchi yetu yaweza kujikuta katika maafa makubwa pindi raia wanyonge watakapoelewa darsa hili. 



Muhadhara waunguruma Geita 
 
  • Kumi na moja wasilimu 
  • OCD aamuru vipaza sauti ving’olewe
Na Hussein Abdallah, Geita 

WATU kumi na moja kutoka madhehebu mbalimbali za Kikristo wamesilimu huko Geita kufuatia muhadhara uliodumu wilayani hapo kwa siku tisa. 

Watu hao walirejea katika dini ya Uislamu baada ya mada mbalimbali kutoka vitabu vinne vya dini kuchambuliwa na Wakristo kuuliza maswali mengi juu ya dhana ya Mungu Mmoja. 

Muhadhara huo ambao uliendeshwa na Vijana wa ALMALLID tawi la Mwanza ulihudhuriwa na ummati mkubwa wa watu na mara ya kwanza ulifanyika katika uwanja wa mpira Kalangalala Oktoba 11. 

Katika siku zilizosalia Muhadhara ulihamia katika viwanja vya Msikiti Mkuu wa Ijumaa Geita baada ya polisi kuzuia kibali kwa madai kwamba muhadhara ni wa kashfa dhidi ya dini nyingine. 

Katika kudhibiti athari ya muhadhara huo ambao uliwavuta Wakristo wengi waliokuwa wakiuliza maswali mbalimbali O.C.D. aliamuru vipaza sauti ving’olewe. Hata hivyo waumini waligoma kwani vilikuwa vimefungwa kwenye msikiti. 

Wakati huo huo, Masheikh wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa mjini hapa wamedaiwa kususia kufungisha ndoa ya Muislamu mmoja ambaye anasemekana kuandaa ulevi katika sherehe hiyo kitendo ambacho kimeelezwa kuwa ni ukiukaji wa maadili ya Uislamu. 

Imeelezwa kuwa kufuatia susio hilo la Masheikh, Mkuu wa Wilaya ya Geita Bi. Halima alifika nyumbani kwa mmoja wa Masheikh hao anayeishi karibu na msikiti kumwomba afungishe ndoa hiyo. 

Hata hivyo imeripotiwa Sheikh huyo naye alikataa kwa hoja kwamba uamuzi wa kususia ulikuwa wa Shura (Masheikh) hivyo asingeweza kwenda kinyume nao. 

Haikufahamika mara moja kama mkuu huyo wa wilaya ni muhusika wa hafla hiyo au la, lakini baadhi ya watu wamesikika wakisema kwamba mama mzazi wa kijana aliyetaka kuoa ni mfanyakazi katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya. 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 

TAHARIRI 
Wakipewa fursa watainusuru nchi

Wasomi watetea haki ya wananchi kumiliki ardhi

Serikali izungumze na wananchi–Mzee Gonga

Akina mama watakiwa kushikamana na dini yao

Maoni
Serikali inaWhite Paper:  Wananchi mna nini?

Dondoo za Saikolojia: Hoja kengeza
Na Abu Halima Sa Changwa

Makala ya mtangazaji
Khatamy sio Gorbacheiv!!!

Makala
Malipo ya fadhila
Na Mohamed Saleh

Tanzania tuna sera gani kuhusu kanda
Na Abu Abdullah, Tanga

Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo- 2
Na Nandenga wa Mkomidachi

Teknologia
Jifunze Kuunganisha Kompyuta (3)
Na Hassan Omar

Makala na habari
'Usiiparamie ovyo Theolojia'
Na Charles Kamuhabwa, DSA Mtwara

Mwinyimkuu kufanya sensa ya waumini Magomeni
Na Jamillah Nassoro

Same tusilimu upya

Wazazi Mwanza wahimizwa kuwashonea watoto wao Hijab
Na Idd Katimba, Mwanza

Tuwaige Wangazija, 'tutafanikiwa'
Mwandishi: Maalim Bassalah

Serikali imeweka rekodi ya kutisha – Sheikh Salim
Na Mwandishi Wetu

Muhadhara waunguruma Geita
Na Hussein Abdallah, Geita

Fuateni Sharia ya Allah - Sheikh
Na Badru Kimwaga

Wanawake wa Kiislamu Mburahati wahimizwa kutafuta elimu

Mafunzo ya Qur'an
Vijana wa pangoni

Barua za wasomaji 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na lishe
Chakula ni silaha ya kukabiliana na changamoto ya kansa
Na Mujahid Mwinyimvua
 
 

 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita