AN-NUUR 
Na.173 Rajab 1419, Oktoba 30 - Novemba 6, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
 
Jifunze Kuunganisha Kompyuta (3) 
  

Na Hassan Omar 

Kwenye sehemu mbili za mwanzo za makala hii inayohusiana na kuunganisha kompyuta, tumejadili kwa kina njia ya kuunganisha kompyuta mbili kwa kutumia programu ya Direct Cable Connection (DCC) iliyomo kwenye Windows 95. Tumeona kwamba ili kuweza kuitumia programu hiyo utahitaji kuwa na waya maalum - ama parallel cable Male/Male au null-modem serial cable Female/Female. Inaweza kutokezea ukawa huna au huwezi kupata kwa urahisi nyaya za namna hiyo. Sehemu hii ya tatu ya mazungumzo yetu juu ya kuunganisha kompyuta yatakita kwenye namna nyengine ya kuunganisha kompyuta isiyohitaji kutumia nyaya za namna hiyo. 

Tuseme, kompyuta yako ni ya mezani, yaani ya aina ya desktop, na ungependa kuingiza kwenye kompyuta hiyo programu mpya kutoka kwenye CD iliyo kwenye CD-ROM drive ya kompyuta nyengine. Na tuseme huwezi kutumia DCC kwa sababu yoyote ile. Kwa namna hiyo itabidi ufuate utaratibu ufuatao: 

1. Wakati kompyuta yako imezimwa, kwa uangalifu, ifungue kompyuta yako iliyokuwa haina CD-ROM drive na uifunue ili uweze kuona ndani ya kompyuta hiyo. Uangalie waya bapa ("flat cable" unaojuilikana kama "IDE cable" - IDE ni ufupisho wa Integrated Drive Electronics), mara nyingi waya huo huwa wa rangi ya kijivujivu, unaotoka kwenye motherboard, (yaani bao kubwa zaidi ndani ya kompyuta yako), na kuingia kwenye hard disk

Waya huo mara nyingi huwa na plagi tatu - moja kila ncha na nyengine katikati. Kama moja kati ya plagi hizo hazikuchomekwa mahali popote pale, basi mambo mazuri, endelea na hatua ya 2. Kama waya huo una plagi mbili tu, yaani hauna plagi ya katikati, unaweza kuazima waya wenye plagi tatu kutoka kwenye kompyuta yenye CD-ROM drive. Lakini kabla hujauchomoa kutoka kwenye kompyuta hiyo angalia vizuri jinsi ulivyochomekwa. 

Ukiiangalia vizuri IDE cable ya kuchomekwa kwenye hard disk (au CD-ROM drive) ya aina ya IDE utaona kuwa upande mmoja una ufito (mstari) wa rangi nyekundu. Hiyo ni alama ya kuonesha kuwa upande huo ndio unatakiwa uchomekwe kwenye pini nambari 1 ya soketi iliyo kwenye hard disk au CD-ROM drive. Soketi ya hard disk ya aina ya IDE ina pini 40. Mara nyingi utaona nambari "1" imeandikwa juu ya pini nambari 1 ya soketi hiyo. Kwa hivyo, kabla ya kuuchomoa waya, angalia ufito mwekundu unawekwa upande gani ili iwe rahisi kuurudisha ukishamaliza kazi zako. 

2. Wakati ikiwa imezimwa, kwa uangalifu ifungue kompyuta ya pili, yenye CD-ROM drive, na uifunue ili uweze kuona ndani yake. Kwa kutumia waya wa IDE wenye plagi tatu, hakikisha kuwa waya huo umechomekwa kama ifuatavyo: 

ncha moja imechomekwa kwenye motherboard ya kompyuta isiyo na CD-ROM drive

plagi ya katikati ya waya huo ichomeke kwenye hard disk ya kompyuta isiyo na CD-ROM drive

plagi iliyo kwenye ncha iliyobakia ichomeke kwenye CD-ROM drive iliyo kwenye kompyuta yenye CD-ROM drive. Kama waya huo ni mfupi na hauwezi kufika kwenye CD-ROM drive iliyo ndani ya kompyuta ya pili, basi itabidi uifungue CD-ROM drive hiyo na uitoe kabisa nje na uiweke mahali ambapo utaweza kuiunga kirahisi. Huna haja ya kuifunga ndani ya kompyuta isiyo na CD-ROM drive - unaweza hata kuiweka juu yake tu. 

Uungaji wa namna hiyo unaifanya hard disk yako kuwa "Master" na CD-ROM drive kuwa "Slave". Hakikisha kuwa vipini (jumpers) vilivyo kwenye hard disk na CD-ROM drive vimechomekwa kuwezesha kuifanya hard disk kuwa "Master" na CD-ROM drive kuwa "Slave". Maelezo ya namna ya kuvichomeka vipini hivyo mara nyingi huwekwa juu ya hard disk na CD-ROM drive zenyewe. Pia unaweza kusoma maelezo hayo kutoka kwenye "manual", yaani vitabu vya maelekezo vilivyokuja na vifaa hivyo. 

3. Ukiiangalia nyuma ya hard disk, sehemu moja utaona kuna plagi yenye nyaya nyekundu na za njano. Hiyo ni plagi ya umeme ambayo mara nyingi ni ya rangi nyeupe. Kwenye kompyuta isiyo na CD-ROM drive, angalia kama ipo plagi ya namna hiyo iliyokuwa haikuchomekwa mahali popote. Kama ipo, ichomeke kwenye soketi inayolingana kwenye CD-ROM drive. Kama kwenye soketi hiyo tayari umechomekwa waya wa namna hiyo, itabidi kwanza uuchomoe ili uweze kuuchomeka waya wa umeme kama huo unaotoka kwenye kompyuta isiyo na CD-ROM drive

4. Weka tayari diskette yenye mafaili maalum (drivers) ya kutumika pamoja na CD-ROM drive. Diskette hiyo unapewa kila unaponunua CD-ROM drive mpya. Ukishakuwa na diskette hiyo, washa kompyuta yako uliyoichomekea CD-ROM drive, na iruhusu Windows 95 kuitafuta na kuiona CD-ROM drive. Ukihitajika kuweka drivers za CD-ROM drive hiyo, chomeka diskette yenye drivers kwenye kompyuta, na kisha ielekeze kompyuta kwenye drive A: ili iweze kuyanakili mafaili yanayohitajika. Kama huna diskette ya namna hiyo unaweza kuiachia Windows 95 ikakutafutia driver kwa ajili ya CD-ROM drive yako. 

Kama kila kitu kitakwenda vizuri, baada ya hapo CD-ROM drive itakuwa tayari kutumika kuingizia programu kwenye kompyuta yako. Ukimaliza shughuli zako, izime kompyuta yako na uichomoe CD-ROM drive na kurudisha kila kitu kama kilivyokuwa mwanzo. Mara nyengine wakati wa kuweka driver ya CD-ROM drive mafaili C:\AUTOEXEC.BAT na C:\CONFIG.SYS huongezwa mistari michache lakini nakala za zamani za mafaili hayo hutunzwa kwenye mafaili mengine ya akiba (backup) yenye majina kama hayo isipokuwa yanayomalizikia .OLD (kwa mfano AUTOEXEC.OLD) au .BAK (kwa mfano CONFIG.BAK) au kitu kama hicho. Yabadilishe majina mafaili hayo kuwa mafaili yenyewe halisi yaani AUTOEXEC.BAT na CONFIG.SYS lakini kabla ya kufanya hivyo hakikisha kuwa mafaili hayo ya akiba yana tarehe sawa na tarehe uliyoingiza CD-ROM drive kwenye kompyuta yako. Isije ikawa yalitengenezwa zamani. 

Kama hukutanabahi mpaka kufikia hapa, maelezo tuliyoyatoa hapo juu ni sawa na namna ya kuiweka CD-ROM drive kwenye kompyuta yako katika hali ya kawaida. Tumeyatumia maelezo hayo katika muktadha huu wa kuunganisha kompyuta kwa vile unaweza, kwa kutumia maelezo tuliyoyatoa hapo juu, kuitumia CD-ROM drive iliyo kwenye kompyuta ya pili bila ya kuichomoa kutoka kwenye kompyuta hiyo kiasi cha kuonekana kama kwamba umeziunganisha kompyuta hizo mbili. 

Utaratibu kama huo unaweza kuutumia kuunganisha kompyuta moja na hard disk iliyo kwenye kompyuta ya pili bila ya kuhitaji kuichomoa kutoka kwenye kompyuta hiyo. Waya wa IDE na ule wa umeme ni lazima utoke kwenye kompyuta ile itakayotumika. Kompyuta ya pili yenye hard disk iliyoazimwa wala haihitaji kuwashwa. 

Lakini kabla ya kuweza kuitumia hard disk ya kompyuta ya pili, itabidi kompyuta ya kwanza ielezwe kuwa imewekewa hard disk nyengine. Mara tu ukiiwasha kompyuta, bonyeza mara kadhaa ama kifungo cha Delete au kifungo chochote kile (mara nyingi F1) cha kukuwezesha kuanzisha programu ya kubadilisha kumbukumbu zilizomo kwenye CMOS (Complementary Metal Oxide Semiconductor). 

Programu nyingi za kubadilisha kumbukumbu za CMOS, zina sehemu ya kubonyeza kuweza zenyewe (automatically) kuitafuta hard disk mpya na kuitambua sifa zake. Hard disk mpya ikishaonekana toka (Exit) kwenye programu ya kubadilishia kumbukumbu za CMOS lakini chagua "Save" ili uzihifadhi taarifa mpya zilizowekwa humo. Baada ya hapo utaweza kuyaona mafaili yote yaliyo kwenye hard disk iliyo kwenye kompyuta ya pili. 

Kitu cha muhimu ni kuelewa namna ulivyoiunga hard disk hiyo: yaani umeiunga kama "Slave" au "Master". Kama umeiunga kwenye plagi ya ncha ya waya wa IDE wakati plagi ya katikati ya waya huo imeungwa kwenye hard disk au CD-ROM drive nyengine, basi hard disk hiyo itakuwa "Slave" na ni lazima uzichomeke "jumpers" kwenye hard disk hiyo kwenye sehemu ya "Slave". Kama umeichomeka kwenye plagi ya ncha lakini kwenye plagi ya katikati hapakuchomekwa kitu, au umeichomeka kwenye plagi ya katikati lakini plagi ya ncha haina kitu, au umeichomekea waya wa IDE usio na plagi ya katikati, basi hard disk hiyo itakuwa "Master" na itabidi uzichomeke "jumpers" zilizo kwenye hard disk hiyo kwenye sehemu ya "Master". Hard disk nyingi (na hata CD-ROM drive) kufanyakazi kama "Master" wala hazihitaji kuchomekewa "jumpers" zozote. Itabidi uhakikishe hilo kwa kutumia maelezo yaliyo juu ya hard disk yako au kwenye "manual" ya hard disk hiyo. 

Kompyuta zenye motherboard zinazoweza kuchomekewa vifaa vya IDE (IDE devices - yaani hard disk au CD-ROM drive) nne, zinakuwa na soketi (connectors) mbili za kuchomekewa nyaya za IDE. Soketi ya kwanza inaitwa "Primary IDE connector", na ya pili inaitwa "Secondary IDE connector". Hard disk au CD-ROM drive itakayoungwa kama "Master" kwenye "Primary IDE connector", hiyo hujuilikana kama "Primary Master", na ile iliyoungwa kama "Slave" kwenye soketi hiyo hujuilikana kama "Primary Slave". Hard disk au CD-ROM drive zinazoungwa kwenye "Secondary IDE connector" hujuilikana kama "Secondary Master" na "Secondary Slave" kwa mfuatilio kama huo. Taarifa hiyo ni muhimu kuielewa wakati unaporekebisha kumbukumbu za CMOS kwani mara nyengine unaweza kuhitaji kuziingiza data za hard disk kwa mitulinga (manually) kwa kupitia taarifa za "Cylinders", "Heads" na "Sectors" za hard disk hiyo kama zilivyoandikwa juu ya hard disk hiyo. 

Tunamalizia kwa kutahadharisha kuwa maelezo yaliyotolewa kwenye makala hii yanahitaji uangalifu kuyafuatilia. Kama mtu hakuwa muangalifu anaweza kusababisha uharibifu kwenye kompyuta yake. Ni vyema, kama huna ujuzi wa kutosha wa masuala ya kompyuta, kutafuta msaada wa mtu mwenye ujuzi kidogo wa masuala hayo ili akusaidie zaidi kujifunza kwa vitendo - kwani la kuambiwa si la kuona! 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 

TAHARIRI 
Wakipewa fursa watainusuru nchi

Wasomi watetea haki ya wananchi kumiliki ardhi

Serikali izungumze na wananchi–Mzee Gonga

Akina mama watakiwa kushikamana na dini yao

Maoni
Serikali inaWhite Paper:  Wananchi mna nini?

Dondoo za Saikolojia: Hoja kengeza
Na Abu Halima Sa Changwa

Makala ya mtangazaji
Khatamy sio Gorbacheiv!!!

Makala
Malipo ya fadhila
Na Mohamed Saleh

Tanzania tuna sera gani kuhusu kanda
Na Abu Abdullah, Tanga

Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo- 2
Na Nandenga wa Mkomidachi

Teknologia
Jifunze Kuunganisha Kompyuta (3)
Na Hassan Omar

Makala na habari
'Usiiparamie ovyo Theolojia'
Na Charles Kamuhabwa, DSA Mtwara

Mwinyimkuu kufanya sensa ya waumini Magomeni
Na Jamillah Nassoro

Same tusilimu upya

Wazazi Mwanza wahimizwa kuwashonea watoto wao Hijab
Na Idd Katimba, Mwanza

Tuwaige Wangazija, 'tutafanikiwa'
Mwandishi: Maalim Bassalah

Serikali imeweka rekodi ya kutisha – Sheikh Salim
Na Mwandishi Wetu

Muhadhara waunguruma Geita
Na Hussein Abdallah, Geita

Fuateni Sharia ya Allah - Sheikh
Na Badru Kimwaga

Wanawake wa Kiislamu Mburahati wahimizwa kutafuta elimu

Mafunzo ya Qur'an
Vijana wa pangoni

Barua za wasomaji 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na lishe
Chakula ni silaha ya kukabiliana na changamoto ya kansa
Na Mujahid Mwinyimvua
 
 

 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita