|
|
| Tanzania
tuna sera gani kuhusu kanda
Na Abu Abdullah, Tanga WIKI iliyopita nilifanya safari mbili za kwenda na kurudi Dar es Salaam. Kila mara nilijaribu kupanda gari ambayo haina historia ya mikosi ya njiani. Pengine matajiri wao ni miongoni mwa wenye kutoa katika njia ya Allah (s.w.). Kanda ya video tuliyoanza nayo safari siku ya mwanzo ilionyesha vita kati ya Waarabu waliovaa vilemba na Wamarekani kwenye miji ya viunga vya Algeria, kufuatia kutekwa nyara kwa ndege ya Kimarekani na magaidi hao wa kubuni. Pamoja na kutumia magari ya deraya na kuwa wengi lakini magaidi walishindwa vibaya na Wamarekani waliokuwa na silaha chache na pikipiki ya kurushia makombora, moja tu. Madhumuni ya igizo hilo ililenga kuwadhalilisha Waislamu (wenye siasa kali) wanaoitwa magaidi kwa upande mwingine kuitukuza Marekani. Kanda hii haikunikera sana kwa vile niliamini ni uongo uliokuwepo usingeweza kuleta ushawishi ulio kusudiwa. Zaidi nilihisi kujenga dhana ya mapambano kati ya miamba miwili ya kifikra ya ulimwengu wa leo, yaani Uislamu na Marekani. Kana kwamba gari haiwezi kuendelea bila kanda ya aina yoyote, baada ya kumalizika kwa video hiyo "kondakta" aliyumba yumba mpaka akafika kuweka kanda nyingine ya radio. Makelele yake yasiyoeleweka yalitukera wengi. Ndo-mboloo. Ndo-mbo-loo. Mama yee. Maa ooo! Makelele ya namna hiyo kwa wengi tulihiyari ukimya, lakini hatukuwa na uchaguzi. Safari ya pili: Gari ya pili na ya tatu, kurudi na kwenda tena, nilipanda gari za shirika hilo hilo na mambo yalikuwa yale yale ya vita vita na vita vya mara hizi ni vya kikatili kweli kweli, vile vinavyoigizwa na watu wenye asili ya Kichina, akina Bruce Lee. Watu hawa hupenda sana kutumia vifaa vya ncha kali vyenye kuwaka na makucha yao kama ya wanyama mwitu kutoa damu na kuuana kiholela. Teknolojia za kisasa za kutengeneza picha na kuhifadhi sauti zinafanya iwe vigumu kutokuamini unayoyaona na kuyasikia. Wasafiri ambao ni wagonjwa huwa na muda mgumu sana mpaka wafike waendako. Mzee mmoja ambaye alionekana kutokea moja ya vijiji vya ndani ndani Tanga, hakuweza kufaidi vyema safari yake, kwani alitazamana na video hiyo na spika moja ilikuwa juu tu ya kichwa chake. Nilimuona akiuma vidole vyake kwa masikitiko karibu muda wote wa kanda hiyo, ambayo ukatili wake hautoi muda wa mtangazaji kupumua. Msafiri mwingine alidumu na kusikitika kwa kubana ulimi wake na ufizi wake wa juu na kutoa sauti za"T-ch, t-ch, t-ch " huyu mambo yalivyozidi aliamua kujificha kabisa nyuma ya kiti cha mbele yake. Nikaendelea kusoma haiba ya wasafiri wengine wenzangu, niliwaona wasafiri wengine wawili ambao yaelekea walikuwa ni mtu na mkewe, kwenye viti vya wawili wawili. Wao walionekana kupendelea kufaidi safari yao kwa kuangalia mandhari nzuri ya nchi, na kujulishana majina ya vijiji gari lilimopita. Hata hivyo walipata matatizo ya kusikizana vyema na utulivu wa kumbukumbu. Binafsi niliamua mara ya nne kupanda gari isiyokuwa na video wala redio. Nilibahatika isiyokuwa na video lakini isiyokuwa na sauti ya kanda haikuwezekana. Sauti za nyimbo hizo nilidhani ndizo za wale vibwengo niliokuwa nikisimuliwa utotoni, ambao pamoja na kuona maganda ya samaki aina ya kamba waliokuwa wakiwala kwenye mito ya bahari, lakini sikuwahi kuwasikia. Sauti zenyewe ni "Kwech –kwech – kwech yoo !!" na mifano yake, zenye kutia wazimu kichwani. Katika kuzidi kutafakari nikawakumbuka Twaleban wa Afghanistan ambao ili kuhifadhi dini yao ya Kiislamu, wamepiga marufuku vituo vyote vya televisheni mpaka vitakaporekebisha aina ya matangazo na picha zao. Sambamba na hilo wanaendesha msako wa kuzinasa kanda zote zisizokubaliana na Uislamu. Na sisi Watanzania hata kama sera za wa Afghanistan hatunazo,
lakini tuna sera za kudumisha na kuleta amani. Sera hii nina uhakika haitakuwa
na matunda yoyote kwa kuangalia kanda za waigizaji wauaji na ni lazima
tutafute sera maalum inayokubaliana na sera ya amani.
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Wasomi watetea haki ya wananchi kumiliki ardhi Serikali izungumze na wananchi–Mzee Gonga Akina mama watakiwa kushikamana na dini yao Maoni
Dondoo
za Saikolojia: Hoja kengeza
Makala ya mtangazaji
Makala
Tanzania
tuna sera gani kuhusu kanda
Mdahalo
kati ya Waislamu na Wakristo- 2
Teknologia
Makala na habari
Mwinyimkuu
kufanya sensa ya waumini Magomeni
Wazazi
Mwanza wahimizwa kuwashonea watoto wao Hijab
Tuwaige
Wangazija, 'tutafanikiwa'
Serikali
imeweka rekodi ya kutisha – Sheikh Salim
Muhadhara
waunguruma Geita
Fuateni
Sharia ya Allah - Sheikh
Wanawake wa Kiislamu Mburahati wahimizwa kutafuta elimu Mafunzo
ya Qur'an
Chakula na lishe
|