|
|
| Wasomi
watetea haki ya wananchi kumiliki ardhi
Wasomi na Wataalamu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wameelezea haja ya kuangalia upya suala la umiliki wa ardhi kuwa mikononi mwa Mamlaka Kuu pekee (Executive) na wananchi wengine kuwa kama kwamba hawana haki yoyote katika ardhi zao za asili. Wamesema mwananchi leo anayemiliki ardhi kwa taratibu za mila hana haki na anaweza kuhamishwa wakati wowote na akihurumiwa sana alipwe fidia ya mazao na sio ardhi Hayo yalisemwa na wasomi hao kufuatia tukio la wananchi wa Nzasa kuhamishwa kwenye makazi na mashamba yao bila hata ya fidia. Akiongea katika semina ambayo ilijadili suala la wananchi kuchomewa nyumba zao, Profesa Seitty Chachage alieleza masuala kadhaa muhimu kuhusiana na kadhia hii. Kwanza ni kwamba wananchi wa Nzasa walikuwa nje kabisa ya mipaka ya msitu. Pili mipaka ya msitu imepanuliwa kinyume na ile ya awali. Tatu zilizochomwa ni nyumba na makazi ya watu na wala sio Madungu na kwamba kilichofanyika ni uvunjaji mkubwa wa haki za binaadamu. Prof. Seitty Chachage ambaye kabla hata ya tukio alishafanya utafiti juu ya eneo hilo na kutembelea baada ya nyumba kuchomwa moto alisema kwamba hata kama ilibidi wahamishwe, basi wangestahili kupewa makazi mapya na fidia. Naye Dk. Ringo Tenga akiongea katika semina hiyo ambayo ilifurika wanafunzi, waalimu na wafanyakazi wengine wa Chuo Kikuu alisisitiza kwamba matatizo kama ya Nzasa yanatokana na mgogoro wa Mamlaka ya Kumiliki Ardhi. Amesema suala la ardhi leo linachukua sura ya kitabaka.Wakati wananchi wa Nzasa wamechomewa moto nyumba zao; Majumba makubwa makubwa yaliyojengwa ufukweni na maeneo mengine kinyume cha sheria hayaguswi, halikadhalika wawekezaji. Dk. Ringo Tenga ambaye ni Mtaalamu wa Sheria za Ardhi (Land Law Specialist) katika Kitivo cha Sheria, alihitimisha mazungumzo yake kwa kutoa hoja kwamba ardhi isibaki kuwa mali ya watawala. Taarifa ya DARUSO ambayo ilisomwa na Rais wake Bw. Kitila Mkumbo ilibainisha kwamba mipaka ya msitu wa Kazimzumbwi ilihamishwa kwa zaidi ya k.m. 9 toka mipaka ya asili kuelekea kijiji cha Nzasa. Kazi ya kuhamisha mipaka hiyo ilifanyika baada ya nyumba za wananchi kuchomwa. Wanachama wawakilishi wa DARUSO walikwenda Nzasa Oktoba 17 kuangalia hali ilivyo na walipeleka machango wao wa shilingi 50,000. Chama cha Waalimu wa Chuo Kikuu UDASA nacho kilipeleka 30,000/-. Semina hiyo iliyofanyika Oktoba 21 katika Ukumbi wa Nkrumah iliandaliwa na UDASA ikishirikiana na DARUSO, "HAKI ARDHI", JET, TLHRC na TGNP. Wazungumzaji wengine katika semina hiyo walikuwa wawe Bw. Richard Mabala (TGNP), James Mpinga (JET) na Zainabu Muruke (TLHRC). Chini ya Mwenyekiti wake Dk. Rugatiri Mekacha, semina hiyo ilitizama
suala la Nzasa katika mtizamo wa Hifadhi ya Mazingira ikilinganishwa na
kuheshimu haki za kibinaadamu za wananchi masikini ("Nzasa: Conserving
the Environment versus Respecting the Human Rights of Poor Alleged Squatters.").
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Wasomi watetea haki ya wananchi kumiliki ardhi Serikali izungumze na wananchi–Mzee Gonga Akina mama watakiwa kushikamana na dini yao Maoni
Dondoo
za Saikolojia: Hoja kengeza
Makala ya mtangazaji
Makala
Tanzania
tuna sera gani kuhusu kanda
Mdahalo
kati ya Waislamu na Wakristo- 2
Teknologia
Makala na habari
Mwinyimkuu
kufanya sensa ya waumini Magomeni
Wazazi
Mwanza wahimizwa kuwashonea watoto wao Hijab
Tuwaige
Wangazija, 'tutafanikiwa'
Serikali
imeweka rekodi ya kutisha – Sheikh Salim
Muhadhara
waunguruma Geita
Fuateni
Sharia ya Allah - Sheikh
Wanawake wa Kiislamu Mburahati wahimizwa kutafuta elimu Mafunzo
ya Qur'an
Chakula na lishe
|