|
|
| Mwinyimkuu
kufanya sensa ya waumini Magomeni
Na Jamillah Nassoro MSIKITI wa Mwinyimkuu uliopo Mtaa wa Mwinyimkuu Magomeni Mapipa Jijini Dar es Salaam upo katika mikakati ya kuendeleza mshikamano miongoni mwa waumini wa Msikiti huo. Hii ni kutokana na kauli ya Qur’an isemayo: "Na shikamaneni kwa kamba ya Mwenyezi Mungu nyote, wala msiachane, na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu, mlikuwa maadui, naye akaziunganisha nyoyo zenu, hivyo kwa neema yake mkawa ndugu, na mlikuwa ukingoni mwa shimo la jahanamu, naye akakuokoeni nalo. Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni aya zake ili mpate kuongoka", Suuratul-al-Imraan aya ya 103. Katika utekelezaji wa aya hiyo, uongozi wa Msikiti wa Mwinyimkuu chini ya Imam wake Sheikh Manzi Saidi Manzi uliazimia kulifanyia kazi tamko hilo adhimu. Uongozi wa Msikiti huo umeamua kwamba, ifanywe sensa ya waumini wote wanaoangukia chini ya kimvuli cha Msikiti huo. Pia uliona umuhimu wa kuwa na majina kamili ya waumini, jinsia zao, makazi yao na shughuli zao kwa ujumla ili kuleta mafanikio katika kila jamii ya Kiislamu. Imeelezwa kwamba taarifa hizo zitasaidia kwa kiwango kikubwa kuimarisha mshikamano unaokusudiwa kwani waumini watakuwa wanafahamiana zaidi pale mmoja wao atapopatwa na masahibu kutakuwa na wepesi wa kumfikishia msaada unaohitajika. Msikiti wa Mwinyimkuu upo katika mpango wa muda mrefu wa kujenga Msikiti unaokidhi mahitaji muhimu ya waumini wake na katika kipindi kifupi kijacho, eneo la nyuma la Msikiti linakusudiwa kuvunjwa ili kutoa nafasi ya jengo la ghorofa moja litakalokuwa na sehemu ya ibada kwa wanawake, madrasa, sehemu ya kuoshea maiti, sehemu ya kutawadha na vyoo na bafu tofauti kwa jinsia zote. Yote haya yatafanyika kwa nguvu za waumini wenyewe na ni miongoni mwa sababu zilizopelekea kuwa na orodha ya waumini wote na kufahamu makazi yao pamoja na shughuli zao. Uongozi wa Msikiti una malengo ya kuwahamasisha waumini wake kufanya shughuli zote za kijamii ndani ya Msikiti wao kwani itarahisisha kupata ushirikiano wa waumini wengine bila kumpa mzigo muhusika halisi, mathalani mazishi, kufunga ndoa na dua zinazowahusu waumini ziwe zinafanyiwa Msikitini, na hilo kwa uhakika litajenga mshikamano wa hali ya juu. Hivi sasa Msikiti huo kuna darasa wanafundishwa watu wakubwa miongoni mwa akina baba na wanawake. Masomo ni pamoja na lugha, Qur’an na tafsiri yake, Tawheed, Sira, Fiqh na mengi mengineyo ambayo yanahusiana na dini yenyewe. Aidha, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu uongozi wa Msikiti wa Mwinyimkuu
unao malengo ya kuchukua majukumu mengi ya kijamii yanayowasibu waumini
wake kwa kutumia mfuko utakaoanzishwa kwa wakati muafaka, ili kuwaondolea
kero zinazokuwa juu ya uwezo wao. Hivyo, wito umetolewa kwa Waislamu wote
kushikamana.
Same tusilimu upya NIMESOMA kwa masikitiko makubwa habari iliyotokea ukurasa wa mbele wa gazeti hili juu ya fitna ya viongozi wa Bakwata Same. Nikiwa mwenyeji wa Same nimeguswa sana na matukio ya kufukuzwa kwa waalimu ambao pengine wangedumu, leo Same tusingekuwa ujingani na kuonekana kiroja mbele ya waumini wa dini nyingine. Tukio la kufukuzwa Ustaadh Thabit Athman kwa vile kajiepusha na zinaa kama Uislamu unavyotaka; si pekee katika matukio ya kuonyesha ujahili wetu. Kwa lengo la kutanabahisha na kuwazindua wenzangu, napenda nitoe mifano ya matukio mengine mawili; hasaa ikiwa ni kichocheo cha kufungua ukurasa mpya wa kutafuta elimu na kuepukana na ufuasi wa kibubusa. Tukio la mwanzo ni lile la miaka ya awali ya themanini (1980s) ambapo ‘Sheikh’ mheshimiwa sana mpaka leo alifanya uganga wake ndani ya madrasa huku akiwashirikisha watoto wetu wa madrasa. Zama hizo ‘Sheikh’ alikuwa ndio pia mwalimu wa madrasa, na watoto wengi wakija madrasa kusoma. Siku moja ‘Sheikh’ alikuja na mteja wake ndani ya madrasa akafanya aliyofanya akamchukua kuku akamchinja juu ya kichwa cha mteja na kumwachia apaparike. Watoto wa madrasa waliamriwa watawadhe na kuswali rakaa mbili kuelekea ‘mzoga’ wa kuku. Kisha kuku akanyonyolewa na kuchemshwa na kila mtoto kupewa kipande cha nyama. Wazazi walikuja juu. Baada ya kukosekana maelezo kutoka kwa viongozi, wazazi wakazuia watoto wao, madrasa ikafa. Lakini ‘Sheikh’ wetu tunae mpaka leo na ni katika Maulamaa wa mkoa ! Tatizo la pili ni lile la mwaka 1986. Ilivyo kawaida kwa washirikina ni kwamba ratiba ya mvua inapobadilika kiangazi kikawa kirefu hufanya matambiko yao ili kuita mvua. Katika matambiko hayo huchinjwa ng’ombe mweusi na kondoo wa rangi hiyo hiyo kwa ajili ya mizimu. Kwa vile aliyekuwa kiongozi wa tambiko hili alikuja akasilimu, baada ya kifo chake tambiko moja lilifanywa kwa ushirikiano wa viongozi wa Msikiti na washirikina. Kama ilivyo ada tambiko lilifanyiwa katika korongo la maji kwa ajili ya mizimu. Hapo akachinjwa kondoo mweusi na ng’ombe mweusi akapelekwa Msikitini. Ilikuwa siku ya Ijumaa ya Septemba 19, 1986. Wakati Imam akiendelea na khutba ya Ijumaa watu wengine nje walikuwa wakishughulika na kupikicha na kunywa damu mbichi ya ng’ombe huyo huku wengine wakikata kata nyama na kuzipika. Baada ya kunywa damu huku khutba ikiendelea walichukua nyama za tambiko ambazo ni ulimi, sehemu ya ini na kidari wakazipeleka Mtoni walipo wazee watambikaji. Baada ya tambiko, nyama hizo zikarudishwa na kuchanganywa na zile nyingine zilizokuwa zinaendelea kupikwa. Baada ya swala Imam aliwatangazia waumini wakae mkao wa kula na asitoke yeyote kwenda nyumbani ila awe ameshakula nyama ya tambiko ambayo yeye aliita sadaka. Awali, katika Ijumaa iliyotangulia ya Septemba 12, 1986 Waislamu walitangaziwa na Mwenyekiti Mtendaji wa Bakwata wa Wilaya kwamba angeletwa ng’ombe wa tambiko la mvua na atachinjwa na kuliwa hapo Msitikini. Kwanini ng’ombe wa tambiko aletwe Msikitini, ilielezwa kwamba hilo lilikuwa
agizo la mganga wa mvua Chifu Kibacha kabla hajafa kwamba ng’ombe mweusi
wa tambiko la mizimu kwa ajili ya mvua achinjwe na kuliwa Msikitini.
Wazazi Mwanza wahimizwa kuwashonea watoto wao Hijab Na Idd Katimba, Mwanza WITO umetolewa kwa wazazi wa Kiislamu kuwashonea watoto wao wa kike hijab. Wito huo umetolewa na Amiri wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu wilaya ya Mwanza, Ustaadh Omar Said Mbalamwezi kwenye mahafali ya wanafunzi wa Kiislamu waliomaliza darasa la saba mwaka 1998 yaliyofanyika kwenye ukumbi wa shule ya Sekondari ya Thaqafa mjini Mwanza hivi karibuni. Mahafali hayo yaliyohudhuriwa na viongozi wa taasisi mbalimbali za Kiislamu mjini Mwanza, wazazi na wanafunzi wenyewe, yaliandaliwa na Jumuiya ya Walimu wa dini ya Kiislamu shule za msingi inayojulikana kwa kifupi JUVIKKU. Ustaadhi Mbalamwezi alisema kuwa kwa sasa hakuna haja ya kuendelea kuilalamikia serikali wakati tayari ruhusa ipo. "Kilichobakia kwetu sasa hivi ni kutilia mkazo kwa watoto kuvaa mavazi haya ya heshima ambayo ni chaguo la Allah (s.w.) kwa wanawake wacha Mungu", alisema Ustaadh Mbalamwezi. Aliendelea kusema kuwa kwa kuwavalisha watoto wetu mavazi stara iwe ndio mwanzo wa kuwepo mafunzo bora. Alisema mavazi yawe ni changamoto ya wao kujitahidi kuanzia masomo, tabia nzuri, adabu na moyo wa kupenda kujielimisha zaidi. Alisema kuwa kwa siku za nyuma kabla ya vijana hawa chini ya Amiri wao Ustaadh Shaib Ambali kuanza kujitoa na kwenda mashule mbalimbali katika manispaa ya Mwanza ilikuwanusuru watoto wengi ambao wakati wa vipindi vya dini wao walikuwa wanacheza tu bila ya kuwa na la kufanya, hali hiyo imebadilika kidogo mwaka huu wa 1998 wanafunzi waliokadiriwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi yaani Maarifa ya Uislamu shule za msingi ni wanafunzi mia sita, lakini kutokana na matatizo mbalimbali hasa uwezo mdogo wa kuandaa na kuchapisha mitihani wanafunzi 244 tu walioweza kukaa na kufanya mitihani hiyo. Akirejea kutilia mkazo juu ya vazi la Hijab, Ustaadh Mbalamwezi alisema kuwa akinamama kwa ujumla wasijipambe kwa hijaab wakati maalum tu, bali vazi hilo ndilo liwe pambo la kawaida kwa wanawake wote wa Kiislamu. "Vaeni hijab majumbani, makazini kwenu, madukani, kuanzia shule za msingi hadi vyuo vya elimu ya juu na popote mtakapokuwa", alisema Ustaadh Mbalamwezi. Akichangia hotuba ya ufunguzi, mmoja wa walimu wa JUVIKKU na mjumbe wa kamati ya utendaji, Ustaadh Mshumba alisema kuwa ni muhimu kwa wazazi wote wa Kiislamu kushirikiana na walimu wa dini ya Kiislamu ili kuwadhibiti vizuri watoto wenye tabia isiyo ridhisha na kuwarekebisha haraka.. Katika mahafali hayo, vijana walifanya maonyesho mbalimbali kuonyesha aina ya nguo ambazo wazazi wanatakiwa wawashonee watoto kama sare za shule. Pia walifanya michezo kama vile kucheza mpira wa pete, kuruka kamba, kukimbia na michezo mbalimbali, michezo yote ilifanywa na wanafunzi wa kike ili kuonyesha nguzo za hijab si tatizo kama walimu wengi wanavyodai kuwa zinawafanya waonekane wazee na zinawazuia masikio na hawasikii vizuri wawapo darasani, na kutoweza kucheza michezo mbalimbali. Vile vile watoto katika ngonjera walisema kuwa walimu wanawakejeli kuwa wanaonekana wazee, wanavaa maguo ya watu wa jangwani, na kuwa wao wanaleta sura mbaya kati ya wanafunzi na zinachochea udini. Watoto hao waliwaomba wazazi kuwapa moyo watoto wao ili waendelee kuvaa hijab na kuwahimiza kufanya juhudi ya masomo yote. Katika risala ya JUVIKKU waliwaomba wazazi wenye wanafunzi shule za msingi, shule za sekondari na vyuo kuwashonea hijab zenye rangi inayofanana na sare sehemu husika. Pia wale wanaotegemewa kuanza darasa la kwanza mwaka ujao. Walitoa wito kwa walimu Waislamu kutoa msaada wa kuwalinda watoto waliokubali kuvaa hijab ili wasiendelee kubughudhiwa. Walisema kuwa lengo la taasisi yao sio kujionyesha bali lengo ni kunusuru mila za Kiislamu na taaluma kwa vijana na malipo ni kwa Allah (s.w.) wao hawatozi chochote, JUVIKKU walisema kuwa idadi ya shule za msingi za manispaa ya Mwanza ni shule 54, wameweza kuhudumia shule 16 tu. |
YALIYOMO
TAHARIRI
Wasomi watetea haki ya wananchi kumiliki ardhi Serikali izungumze na wananchi–Mzee Gonga Akina mama watakiwa kushikamana na dini yao Maoni
Dondoo
za Saikolojia: Hoja kengeza
Makala ya mtangazaji
Makala
Tanzania
tuna sera gani kuhusu kanda
Mdahalo
kati ya Waislamu na Wakristo- 2
Teknologia
Makala na habari
Mwinyimkuu
kufanya sensa ya waumini Magomeni
Wazazi
Mwanza wahimizwa kuwashonea watoto wao Hijab
Tuwaige
Wangazija, 'tutafanikiwa'
Serikali
imeweka rekodi ya kutisha – Sheikh Salim
Muhadhara
waunguruma Geita
Fuateni
Sharia ya Allah - Sheikh
Wanawake wa Kiislamu Mburahati wahimizwa kutafuta elimu Mafunzo
ya Qur'an
Chakula na lishe
|