AN-NUUR 
Na.173 Rajab 1419, Oktoba 30 - Novemba 6, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
 
‘Usiiparamie ovyo Theolojia’ 

Na Charles Kamuhabwa, DSA Mtwara 

MAKALA iliyoandikwa na msomaji wako mmoja kwenye AN-NUUR toleo Na. 169 la Oktoba 1998 ajulikanaye kama Sheikh Bernard P. Nyangasa haiwezi kupita bila kupingwa. Sheikh Bernard ametuonyesha kuwa Wakristo wengi wanaojaribu kuthibitisha au kukanusha madai mbalimbali kuhusu Ukristo hawana elimu ya Theolojia na hasa masomo ya Bible Knowledge na Church History, hilo ni kweli kabisa Sheikh Bernard na wala halina ubishi na ninadhani hata Waislamu wengi wanaoandika kuhusu Ukristo hawana elimu hiyo ya Theolojia. 

Ninachotaka kukufahamisha Sheikh Bernard ni kwamba Theolojia sio msingi wa imani ya Ukristo. Theolojia ni tawi tu la elimu kama ilivyo sheria, unajimu, falsafa, fizikia, lugha na kadhalika. Si jambo la lazima au muhimu kwa muumini Mkristo kuwa Mtheolojia ili aweze kuwaeleza wengine kuhusu habari za Imani yake. 

Msingi mkuu wa Ukristo ni Upendo, haimlazimu Mkristo kuwa Mwanatheolojia ndipo ajue "mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa akili zako zote, mpende jirani yako kama nafsi yako na wala haihitajiki Theolojia kujua kuwa Yesu Kristo ni mwana wa Mungu. 

Pia Mkristo haihitaji Theolojia kuzijua na kuzishika amri kumi za Mungu. Ukisoma vyema Biblia hiyo unayotuambia tusiiparamie ovyo utaona katika kuchagua watumishi wake kama waamuzi, Manabii na Masihi. Alitazama zaidi uaminifu na uchaji wa mtu. 

Daudi alikuwa mchungaji kondoo tu hatuambiwi kuwa alikuwa mtaalamu au msomi wa Torati. Alilolijua yeye ni kupiga kinanda, kinubi na kuimba Zaburi. Lakini Mungu alimchagua yeye kuwa Mfalme wa Israel akawaacha kaka zake waliokuwa wakiishi mjini Bethelehem. 

Tena Mungu alimchagua kijana mdogo Yoshua awe Nabii wake, Makuhani, wakuu wa watu na wazee wakamkataa maana hakuwa msomi wala hakuwa miongoni mwao, lakini Mungu alimchagua yeye akawaacha wao na Theolojia yao. 

Hata Yesu Kristo alipozaliwa Bethelehem ni wachungaji makondeni waliopashwa habari hizo kwanza ndio waliopewa Heri ya Krismasi ya kwanza kabisa na maarufu duniani kote "Utukufu wa Mungu juu mbinguni na duniani amani kwa watu wote wenye mapenzi mema". Walikuwepo wasomi wengi sana wa sheria na historia (Torati) enzi hizo lakini Mungu hakuwapa wao habari hizi na hata walipozipata kupitia kwa mamajusi (wanajimu) pamoja na kudhibitisha kuwa kweli Kristo alizaliwa Bethelehem kwa sababu wanazozijua wenyewe walimkataa. 

Hao ndio wasomi (watheolojia) wataalamu wa dini wa Kiyahudi. Kristo mwenyewe alipowachagua wale thanashara aliwachukua watu wasio na elimu yeyote ya dini mradi tu wawe waaminifu wacha Mungu na wavumilivu. Petro na wana wa Zebadayo walikuwa wavuvi wa samaki. Wengi wa wale thenashara walikuwa watu wa kawaida wasio na elimu yeyote ya dini. 

Twaambiwa hata Nabii wa Uislamu Muhammad (s.a.w.) hakujua hata kuandika wala kusoma. Kristo mwenyewe alimshukuru Mungu kwa jambo hilo". Saa ile ile alimshangilia kwa Roho Mtakatifu akasema nashukuru Baba, Bwana wa mbinguna nchikwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili umewafunulia watoto wachanga. (Luka 10:21). 

Kristo mara nyingi alipambana sana na wasomi wa dini wa enzi zake ( wanasheria, waandishi na Mafarisayo) ambao walijidai kuzifuata sheria na kuzijua sana kumbe walikuwa wanafiki tu. Luka 11:39-44 Kristo anaendelea kuwaonya watu hao katika msitari wa 46 wa sura hiyo hiyo ya 11. Nanyi wanasheria ole wenu kwa sababu mwawatwika watu mizigo isiyochukulika wala ninyi wenyewe hamuigusi mizigo hiyo hata kwa ncha za vidole vyenu. Hiyo ndiyo tabia mojawapo mbaya miongoni mwa wasomi (watheolojia) wa dini mbalimbali huchambua mambo madogo madogo na kusababisha mifarakano miongoni mwa waumini. Watheolojia ndio chanzo kikubwa cha kugawanyika kwa Kanisa la Mungu, madhehebu mengi yametokea baada ya migongano ya kutoelewana miongoni mwa wasomi wa dini. 

Hivi leo hata Theolojia yenyewe imegawanyika kuna Theolojia ya Kanisa Katoliki, Theolojia ya Waanglikana, Theolojia ya Walutheri n.k. Sasa sijui wewe Sheikh Bernard umesomea Theolojia ipi hiyo unayotamba nayo. Hata kwa upande wa Waislamu magomvi mengi na kutokuelewana miongoni mwa waumini huletwa na hao wanaojifanya wasomi sana wa Theolojia mara ukifunga sala usifungie tumboni mara usivae kanzu ndefu; mambo madogo madogo kama hayo yasiyo na msingi yanasababisha watu watiane bakora Misikitini (TOT na Chimumunya – Lindi) lakini yote hayo ukiangalia yanaletwa na hao wanaojidai kuwa ndio wenye elimu ya dini zaidi ya wengine na ndio wenye kujua wengine hawajui kitu. 

Tabia hii ya kujiona ujuaji, kujisifu na kuwadharau wengine kama ilivyoonyeshwa na Sheikh Bernard katika makala yake namnukuu: "Mimi siwezi kulumbana na watu kama akina Batendi kwani siwezi kuelewana nao. Ndio maana nawataka wanatheolojia (wasomi) wapinge makala zangu kama wana ubavu".Akina Batendi siwezi hata kuwa reffer kwenye vitabu vinavyotumika katika vyuo vya Theolojia kwani hawajui sasa tutaelewana vipi ?" mwisho wa kunukuu. 

Hii ni tabia iliyoonyeshwa hata na wasomi wa Kiyahudi kuwadharau watu wengine mradi tu si wasomi kama wao. "Basi Mafarisayo wakawajibu. Je, ninyi nanyi mmedanganyika? Ni nani katika wakuu amwaminiye au katika Mafarisayo ? Lakini makutano hawa (umati wa watu) wasioifahamu Torati wamelaaniwa". Hivyo Sheikh wetu Bernard anapowadharau akina Batendi ambao ndio tulio wengi maana kati ya Wakristo elfu moja (1000) unaweza kuwapata wanatheolojia wawili tu nadhani hali ni kama hiyo hata kwa Waislamu. 

Kwa hiyo, sisi ndio hao makutano tusiojua kitu "tumelaaniwa". Tabia hii ya kujiona na kujisifu iliwafanya wasomi hao wa Kiyahudi kumkataa Bwana Yesu na wakawafanya na wengine wamkatae matokeo yake hadi leo wanangojea Masiha. 

Ukiangalia hata mfano alioutoa Sheikh Bernard wa Utabiri wa kuzaliwa Emmanuel na Bikira utaona kuwa theolojia haithitibitishi mambo mara nyingi na hutoa dhana au mtazamo na mawazo binafsi ya mtaalamu mhusika. Theolojia mara nyingi hutujia na mambo kama "yawezekana", "yaonekana", "inaweza kuwa", "pengine", n.k. 

Maana Sheikh Bernard na huyo mtalaamu mwenzie Norman J. Bull (MA.) wanataka kutusadikisha kuwa habari iliyotabiriwa na Isaya haikumhusu Kristo lakini hawatuambii kwa uhakika utabiri huu ulimhusu nani mara "yawezekana" ni mtoto wa Isaya mwenyewe au mfalme Ahaz, tuchukue lipi hapo. Maana kama ni mtoto wa Isaya au Ahaz si alizaliwa enzi hizo za Isaya na Ahaz je, aliitwa Emmanuel ? Pengine "kuwa huyo mwanamke hakuwa bikira (aliyetabiriwa) na tayari alikuwa na mtoto", huyo mtoto aliyekwisha kuwa naye aliitwa nani ? Na "wala sio Maria bali mke wa Isaya au Ahaz Sheikh Bernard hao wake wa Nabii Isaya na mfalme Ahaz hawakuwa na majina mpaka Nabii amtaje bikira tu ? Je huyo mtoto wa huyo mwanamke aliitwa nani ? Je Nabii Isaya alikuwa anamsema mtoto wake au Ahaz aliposema "ataitwa Mshauri wa ajabu, mfalme wa amani Mungu mwenye nguvu je mtoto wa Ahaz au/ na Nabii Isaya kuna aliyeitwa hivyo ? 

Haihitaji theolojia au elimu ya juu ya dini kulinganisha utabiri wa Isaya na ujumbe wa Gabriel (Jibril) kwa Mariam "Huyo atakuwa mkuu ataitwa Mwana wa aliye juu na Bwana Mungu atampa kiti cha Daudi babaye. Sheikh Bernard anataka kutuaminisha kuwa hayo mawazo au dhana binafsi ya Norman J. Bull na wataalam wengine ndio bora na ya kufuatwa kuliko neno la Mungu lenyewe yaani Biblia na hata kama Mapadre, Maaskofu na Makadinali (ambao wengi ni watheolojia) wanafundishwa hayo si lazima kuyakubali kwani wao si wajinga, "Mjinga huamini kila neno bali mwenye busara huangalia sana aendavyo (Mithali 14:15). 

Sifa za Mchungaji, Shemasi na Askofu ni hizi "Basi imempasa Askofu awe mtu asiyelaumika, mume na mke mmoja mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji ajuaye kufundisha". Hizo ndizo sifa za Askofu, Mchungaji na Shemasi. Tazama 1 Timotheo 3:3-13 utaona sifa za kiongozi wa Kanisa la Mungu hakuna hata sehemu moja kwenye Biblia inayotaja theolojia (elimu ya dini) kama kigezo cha kupata viongozi wa Kanisa. 

Sisi Wakristo tunamshukuru Mungu kwani tulikwishaonywa juu ya watu kama Sheikh Bernard miaka karibu mia sita (600) kabla kuzaliwa Nabii wa Uislamu Muhammad (s.a.w.): "Kuwa watu wabaya na wadanganyi wataendelea na kuzidi kuwa waovu wakidanganya na kudanganyika". ( 2 Timetheo 2:13-14). "Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia walimu makundi makundi kwa kuwa wana masikio ya utafiti nao watajiepusha wasisikie yaliyo ya kweli na kuzigeukia hadithi za uongo (za akina Norman Bull) (2 Timotheo 4:3-5). 

Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu wala si kwa jinsi ya Kristo. (Wakolosai 2:8). 

Ewe Timotheo ilinde hiyo amana ujiepushe na maneno yasiyo na dini yasiyo na maana na mashindano ya elimu iitwayo elimu ya uongo ambayo wengine wakiikiri hiyo wameikosa imani (Sheikh Bernard badala ya kuifuata Biblia yeye ameifuata theolojia). 

Sheikh Bernard yaonekana ni mtu wa kujisifu na kujitweza mara "Oh naweza kuandika kuhusu Roho Mtakatifu kurasa tatu (3) zisitoshe, mara oh nikitaka kueleza Yesu alimaanisha nini nitajaza si chini ya kurasa nne (4). Hayo yote ni ya nini ? Sheikh Bernard unataka tukuone kuwa unajua sana au ? Tunao Madaktari na Maprofesa wa Theolojia hatuwaoni Makanisani au popote wakijisifu ingawaje wengi wao wameandika vitabu mbalimbali vya theolojia achia wewe unayenukuu kutoka kwa akina Norman Bull. 

Sisi wasomaji wa AN-NUUR Wakristo kwa Waislamu wengi wetu si wanatheolojia tutafaidika nini na hiyo theolojia yako ? 

Sheikh Bernard amewaalika wanatheolojia Wakristo kama wana ubavu walumbane naye ! Hilo Sheikh Bernard haliwezekani. Wanatheolojia Wakristo wanaisoma sana Biblia na kuifuata. Biblia inazuia Wakristo kushiriki katika malumbano na ubishi wa kidini kama ni kushauriana na kuelimishana sawa ila kulumbana NO ! 

Mtu awaye yeyote akifundisha elimu nyingine wala hayakubali maneno yenye uzima ya Bwana wetu Yesu Kristo wala mafundisho yapatikanayo na utawa, amejivuna, wala hafahamu lolote bali ana wazimu wa kuwazia habari za maswali na mashindano ya maneno ambayo katika hayo hutoka husuda na ugomvi na shauku mbaya na majadilano ya watu walioharibika akili zao walioikosa kweli huku wakidhani ya kuwa utawa ni njia ya kujipatia faida (1 Timotheo 6:3-5). 

Muwe tayari kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu lakini kwa upole na kwa hofu. ( 1 Petro 3:15) Pia hata Kristo mwenyewe amezuia ubishi. "Usishindane na mtu muovu" tena neno lenu liwe ndio, siyo mana yale mengine yatoka kwa yule muovu. Hivyo hakuna Mtheolojia hata mmoja Mkristo atakayeingia katika malumbano na wewe au yeyote mwenye kiu ya malumbano ! Malumbano Sheikh Bernard sio sifa njema wala hayajengi bali ujenga chuki, kejeli, shutuma, matusi, kashfa, n.k. 

Napenda kumkumbusha Sheikh Bernard kuwa lililo muhimu ni Biblia yenyewe si Theolojia ya Kanisa. Sheikh wetu uliiparamia theolojia matokeo yake ukaanguka anguko kuu. Ukaiacha Nuru na kweli ukarudi gizani. Nakuombea kwa Mwenyezi Mungu si wewe tu bali na wale wote ambao kama wewe waliangukia kwenye tanzi la shetani waione tena ile kweli na nuru. 

Mwisho kabisa napenda kumshukuru sana Mhariri na Wachapishaji wa gazeti la AN-NUUR kwa sadaqa yao waliotupatia sisi wasomaji wa Mtwara. Mtu mwingine aweza kuona kama ni jambo dogo tu ila kwetu sisi wasomaji na wapenzi wa gazeti hili tunashukuru sana. Tunachoangalia zaidi si ile shilingi 100 tuliyopunguziwa, bali ni ule moyo wa kutukumbuka na kutupunguzia hiyo thamani yake haipimiki kwa kipimo chochote ila imezidi hata shilingi (1,000,000) milioni. Tunatumai mtatukumbuka hata kwa mengine mtakayokuwa na uwezo nayo. Inshaalah. 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 

TAHARIRI 
Wakipewa fursa watainusuru nchi

Wasomi watetea haki ya wananchi kumiliki ardhi

Serikali izungumze na wananchi–Mzee Gonga

Akina mama watakiwa kushikamana na dini yao

Maoni
Serikali inaWhite Paper:  Wananchi mna nini?

Dondoo za Saikolojia: Hoja kengeza
Na Abu Halima Sa Changwa

Makala ya mtangazaji
Khatamy sio Gorbacheiv!!!

Makala
Malipo ya fadhila
Na Mohamed Saleh

Tanzania tuna sera gani kuhusu kanda
Na Abu Abdullah, Tanga

Mdahalo kati ya Waislamu na Wakristo- 2
Na Nandenga wa Mkomidachi

Teknologia
Jifunze Kuunganisha Kompyuta (3)
Na Hassan Omar

Makala na habari
'Usiiparamie ovyo Theolojia'
Na Charles Kamuhabwa, DSA Mtwara

Mwinyimkuu kufanya sensa ya waumini Magomeni
Na Jamillah Nassoro

Same tusilimu upya

Wazazi Mwanza wahimizwa kuwashonea watoto wao Hijab
Na Idd Katimba, Mwanza

Tuwaige Wangazija, 'tutafanikiwa'
Mwandishi: Maalim Bassalah

Serikali imeweka rekodi ya kutisha – Sheikh Salim
Na Mwandishi Wetu

Muhadhara waunguruma Geita
Na Hussein Abdallah, Geita

Fuateni Sharia ya Allah - Sheikh
Na Badru Kimwaga

Wanawake wa Kiislamu Mburahati wahimizwa kutafuta elimu

Mafunzo ya Qur'an
Vijana wa pangoni

Barua za wasomaji 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na lishe
Chakula ni silaha ya kukabiliana na changamoto ya kansa
Na Mujahid Mwinyimvua

 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita