AN-NUUR 
Na.184 Ramadhan 1419, Januari 15 - 21, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Ole wenu Marekani 

Kwa wote wapenda haki, ilaniwe Marekani, 
Kushambulia Iraki, unyama uso kifani, 
Wanaona kwao haki, ndo wababe duniani, 
Ole wenu Marekani, hamtaona Sirati. 
 
Mabomu na mafataki, kuua waso hatiani, 
Jambo hilo siyo haki, Kapilima nabaini, 
Kwa wote wapenda haki, muilani Marekani, 
Ole wenu Marekani, hamtaona Sirati. 
 
Mabomu ya Atomiki, yamejaa Marekani, 
Yaloua Nagasaki, Mashariki ya Japani, 
Wao hawakaguliki, ndo polidi duniani, 
Ole wenu Marekani, hamtaona Sirati. 
 
Saddam msitahiki, apongezwe duniani, 
Mkwara hababaiki, wa hao Wamarekani, 
Kaishikilia haki, kukagua 'asilani', 
Ole wenu Marekani, hamtaona Sirati. 
 
Dunia kimya yabaki, yatetea Marekani, 
Kushambulia Iraki, kwa waso hatiani, 
Kosa kudhirisha, Uislamu duniani, 
Ole wenu Marekani, hamtaona Sirati. 
 
Sasa kweli nahakiki, makafiri Marekani, 
Kushambulia Iraki, mfungo wa Ramadhani, 
Kateremsha Maliki, ndani yake Furi-qani, 
Ole wenu Marekani, hamtaona Sirati. 
 
Ya Allahu ya Maliki, ziweke pema peponi, 
Roho za walofariki, kwa hao masheitwani, 
Hakuna kitakachobaki, chochote ulimwenguni, 
Ole wenu Marekani, hamtaona Sirati. 
 
Juma Said Kapilima (Super), 
P.O. Box 237, 
Moshi. 



Iddi Mubaraka! 

Bismillahi naanza, kutoa yangu maoni, 
Kaeni mkisikiza, enyi ndugu waumini, 
Kwa baraka za Muweza, tushamuaga mgeni. 
Sherehe iwe ya kheri, leo Iddi Mubaraka. 
 
Kilelele cha hii Iddi, ni kuenda uwanjani, 
Kuswali swala ya Iddi, kwa manukato mwilini, 
Kuvaa nguo jadidi, na kuzidisha imani, 
Sherehe iwe ya kheri, leo Iddi Mubaraka. 
 
Iddi ya mfungo mosi, Fitri tuzitoweni, 
Na Dhulhaji halisi, tuwezao tuchinjeni, 
Tutumie chetu sisi, na kuwapa maskini, 
Sherehe iwe ya kheri, leo Iddi Mubaraka. 
 
Tuandae vinywaji, na vyakula majumbani, 
Vile tunavyohitaji, tuvipendavyo nyoyoni, 
Haramu tusihitaji, ulevi tusithamini, 
Sherehe iwe ya kheri, leo Iddi Mubaraka. 
 
Tupeaneni zawadi, kwa ndugu na majirani, 
Ili watu wafaidi, yatima na maskini, 
Leo ni siku ya Iddi, tumshukuru Manani, 
Sherehe iwe ya kheri, leo Iddi Mubaraka. 
 
Tuzidisheni Ibada, kwa ndugu na majirani, 
Tufanye yenye faida, huu ndio uumini, 
Takbira kila muda, zisitoke midomoni, 
Sherehe iwe ya kheri, leo Iddi Mubaraka. 
 
Mtume ameshasema, kutwambia waumini, 
Yale Mungu alosema, asiye siku ini, 
Kama siku ya Kiyama, ndio yuko maasini, 
Sherehe iwe ya kheri, leo Iddi Mubaraka. 
 
Tamati hapa yatosha, naomba yafuateni, 
Shawwali imehodisha, siku sita tufungeni, 
Kila kheri kuzidisha, shari kuweka pembeni, 
Sherehe iwe ya kheri, leo Iddi Mubaraka. 
 
Juma M. Bwanakheri, 
(Ustaadh), 
S.L.P. 45245, 
Dar es Salaam. 



Waitwao siasa kali 

Ni khofu imewafunga, la maana hawanalo, 
Kudhani siye wajinga, kusema walizualo, 
Wasemwao wanapinga, kila ovu litendwalo, 
Wetwao siasa kali, ni maovu wapingao. 
 
Ulaya na Amerika, limetoka jina hilo, 
Ni mpango waliweka, wakamba liwe liwalo, 
Hii dini kuifyeka, ndo lengo walitakalo, 
Wetwao siasa kali, ni maovu wapingao. 
 
Batili imeenea, hakuna likemewalo, 
Watu wanachekelea, kila ovu lifanywalo, 
Madhalimu wamepea, halipo waogopalo, 
Wetwao siasa kali, ni maovu wapingao. 
 
Kuiondoa dhuluma, wao lengo lao ndilo, 
Lilo haki kulisema, japo ndo liumizalo, 
Hawaketi wako wima, kutetea lifaalo, 
Wetwao siasa kali, ni maovu wapingao. 
 
Hili jina la "ukali", ndilo neno litishalo, 
Muislamu wa kweli, kufanywa jema hanalo, 
Akaundiwa kauli, kupotosha afanyalo, 
Wetwao siasa kali, ni maovu wapingao. 
 
Wima wanafanya sa'i, lipo watumainilo, 
Dini ipate uhai, ndilo wakusudialo, 
Dhuluma ja Mwembechai, ni jambo wachukialo, 
Wetwao siasa kali, ni maovu wapingao. 
 
Daima watapambana, hawana wakhofialo, 
Na ushindi watavuna, Inshaallahu kwa hilo, 
Japo wanawatukana, tusi halitimu kilo, 
Wetwao siasa kali, ni maovu wapingao. 
 
Ole wataka "rahisi", kufanya walitakalo, 
Wapendao uwepesi, na lile watamanilo, 
Wamejaa wasiwasi, lenye raha hawanalo, 
Wetwao siasa kali, ni maovu wapingao. 
 
Nakhitimisha witiri, wasikie nisemalo, 
Waache kujikhasiri, lenye kheri hawanalo, 
"Siasa kali" jasiri, wafanye waliwezalo, 
Wetwao siasa kali, ni maovu wapingao. 



Dimbwi la maji machafu 

Tupo kwenye dimbwi refu, lilofurika uchafu, 
Masheikh na Masharifu, twayanywa maji machafu, 
Katika kina kirefu, tumezama kwa marefu, 
Mwenzenu nimejawa khofu, kwenye hili dimbwi chafu. 
 
Zote zetu nyumba ndefu, zindani ya dimbwi chafu, 
Zote mejaa uchafu, wenye kutoa harufu, 
Zachukiza kwa harufu, kwenye pua na mapafu, 
Mwenzenu nimejawa khofu, kwenye hili dimbwi chafu. 
 
Hatokuwa mwenye khofu, yule aliye kipofu, 
Haitomshika khofu, asosikia harufu, 
Hali haiwi hafifu, nakereka na uchafu, 
Mwenzenu nimejawa khofu, kwenye hili dimbwi chafu. 
 
Waweza ukajisifu, kuwa u-mtwaharifu, 
Wapendezwa na harufu, kukataa usahafu, 
Moyoni wajiarifu, kupata Pepo tukufu, 
Mwenzenu nimejawa khofu, kwenye hili dimbwi chafu. 
 
Hatupati uongofu kwa kutupa msahafu, 
Hata kama u-dhaifu, kumbuka bado mchafu, 
Hukutana kwenye safu, twanuka mbaya harufu, 
Mwenzenu nimejawa khofu, kwenye hili dimbwi chafu. 
 
Huu mwezi maarufu, Ramadhani mtukufu, 
Hizi sikuze tukufu, twafunga kwenye uchafu, 
Hili dimbwi lilochafu, twafutari bila khofu? 
Mwenzenu nimejawa khofu, kwenye hili dimbwi chafu. 
 
Zetu swala zipungufu, kwenye kina cha uchafu, 
Zetu dua hazirifu, kufika mbingu tukufu, 
Zetu nguo si nadhifu, kweli ninawaarifu, 
Mwenzenu nimejawa khofu, kwenye hili dimbwi chafu. 
 
Mwenzenu naawarifu, nataka mnipe "tafu", 
Tukamate kamba ndefu, toka kwa Mola Latifu, 
Tutoke kwenye uchafu, kwa kufata msahafu, 
Mwenzenu nimejawa khofu, kwenye hili dimbwi chafu. 
 
Zama zile kamilifu, na mbinu ziso dhaifu, 
Tupangane safusafu, tusiwe watu dhaifu, 
Tusijali usumbufu, tumwitikie Latifu, 
Mwenzenu nimejawa khofu, kwenye hili dimbwi chafu. 
  
Tusifanye ulegefu, nje tutoe uchafu, 
Tujue kazi ni ndefu, yataka wachangamfu, 
Tuyatoe masurufu, kwa mapana na marefu, 
Mwenzenu nimejawa khofu, kwenye hili dimbwi chafu. 
 
Wale watu waso khofu, tutoe wao upofu, 
Waone maji machafu, wachukizwe na harufu, 
Wajizinge kwenye safu, tuukomeshe uchafu, 
Mwenzenu nimejawa khofu, kwenye hili dimbwi chafu. 
 
Kaditamati si refu, shairi lenye kukhofu, 
Kaditama nalisifu, gazeti letu tukufu, 
Kaditama maarufu, kwa kukemea machafu, 
Mwenzenu nimejawa khofu, natoweka kwenye safu. 
 
Idd S. Kikong'ona. 
 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 

Tahariri 
Baada ya futari nzuri: Tuwatupie macho wenye njaa 

Rais Mkapa kuwa mgeni rasmi Baraza la Idd 

Ubungo yakumbwa na ukame 

Waumini, Masheikh Arusha wasutana kwa futari ya Mrema 

Dondoo za saikolojia 
Na. Abu Halima Sa Changwa 

Waislamu turejee kwa Allah 

MSADAT yazidi kutia moyo Tanga 

Mjue Usama bin Ladin 

MAFUNZO KUHUSU FUNGA YA RAMADHANI 

Michezo isiyoruhusiwa katika Uislamu 

Ustadh Farid: Kijana aliyejitolea kuwapa Da'awa watalii 

Hakuna Magharibi wala Mashariki: Uislamu ni ubinaadamu 
Na Abubakari S. Marwillo 

Ijue madrasati Mar-wa ya Dodoma mjini 
Na Abu Zuberi, Dodoma 

Ijue Madrasat Jadidul Fiqhyyat - Tabata Kimanga 
Na B. Mwakangwale 

Madrasat Hidayatul Muumini Mwadui 

Washindi wa mashindano ya Hadithi za Mtume (s.a.w.) wapatikana 

Madrasa Shafii Ujiji Kigoma yaonyesha umahiri wake 

Waanzisha mifuko kusaidia wagonjwa Dodoma 

Waislamu Kondoa waomba msaada kumalizia Msikiti 

Mnyororo wa imani-2 
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa 

Kutoka magazeti ya zamani: 
Wanaoshitakiwa kwa uhaini kortini leo 

Jengo la Waislamu Moshi lageuzwa Kanisa la Walokole 
Na Mwandishi Wetu, Moshi 

Masjid Nurania yaswaliwa Ijumaa 
Na Rajab Rajab, Morogoro 

Jabal Hira kutoa mafunzo ya Kompyuta Morogoro 
Rajab Rajab na Mussa Ally, Morogoro 

Sayansi na Teknolojia 
[Internet ni nini?] 

Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Thamani ya mlo wa Uyoga] 
  


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita