|
|
| Ijue
madrasati Mar-wa ya Dodoma mjini
MADRASATI Mar-wa ni madrasa ya akina mama iliyopo Area "A" mjini Dodoma. Madrasa hii ilianzishwa Aprili 10, 1998 ikiwa na wanafunzi watano, hadi sasa idadi ya wanafunzi imefikia 46, chini ya uongozi wa Maalim Hamudu Mohammed ambaye ni muasisi. Ustadh Hamudu katika kuendesha shughuli hizi za taaluma anasaidiana na walimu wenzake ambao ni Mama Rukaya, Mama Shan, Mama Jauzan na Asha Abdurlahmani. Aidha, kwa upande wa uongozi wa madrasa hii, wamo Mama Habiba ambaye ni Mwenyekiti na Mama Yusufu akiwa Katibu. Dhumuni la kuanzishwa madrasa hii ni kuelimisha akina mama wa Kiislamu wa mkoa wa Dodoma ili wawe na msimamo wa maadili ya dini ya Kiislamu. Masomo yafundishwayo ni Qur’an tukufu, Fiqh, Sira, Nahau, Tafsiri ya Qur’an, Hadith na Tasawufi. Madrasa hii inaendeshwa kwa jitihada za mwanafunzi mwenyewe na imo katika
nyumba ya mtu binafsi. Wanafunzi hawa wanaomba msaada kwa Waislamu wote
wanaosoma gazeti hili wasaidiwe kwa hali na mali ili waweze kupata jengo
lao.
Ijue Madrasat Jadidul Fiqhyyat - Tabata Kimanga Na B. Mwakangwale MADRASAT Jadidul Fiqhyyat ni madrasa pekee iliyoinuka na kuchukua umaarufu katika jihadi ya kuelimisha vijana iliyopo Tabata Kimanga Jijini Dar es Salaam chini ya Bi. Mtumwa Rashid Tussaka. Madrasa Fiqhyyat ilianzishwa mnamo mwaka 1992 na muasisi (muhisani) Bi. Mtumwa Rashid Tussaka akishirikiana kwa pamoja na Maustadh wawili, Juma Saddiq Kigwinya na Masoud Said Kigage. Madrasa hiyo ilianza na wanafunzi watatu tu wakiwa ni watoto wa muasisi Bi. Mtumwa na baada ya muda waliongezeka na kufikia sita, hawakuishia hapo tu kutokana na juhudi kubwa na ufanisi mzuri wa madrasa kwa wale waliokuwa nao, wazazi waliona umuhimu mkubwa wa kuwapeleka watoto wao katika madrasa hiyo pekee na kufikia wanafunzi mia mbili. Mwaka 1994 madrasa ilifanya onyesho kwa malengo ya kuvutia zaidi wazazi wa vitongoji vya jirani. Mwaka 1995 madrasa ilipata pengo baada ya Ustadh Juma Sadiq Kigwinya alipata mitihani migumu (kifamilia) hivyo alirudi kwao Kigoma na madrasa kubaki na mlezi Bi. Mtumwa. Madrasa hiyo iliweza kupata mafanikio kwani imetoa wanafunzi kadhaa katika Chuo cha Kiislamu Chang’ombe Markazi kupata elimu zaidi ambao ni waanzilishi wa madrasa na wana uwezo mkubwa wa kufundisha wenzao wakisaidiana na Ustadh Mubaraka Kambangwa. Pia imejiunga na Baraza la JUWAQUTA la Kiislamu Tanzania na nchi nyingine vile vile imefungua masomo ya chekechea kuanzia umri wa miaka mitatu hadi saba pamoja na masomo ya ziada ya shule za msingi kuanzia darasa la kwanza hadi la saba chini ya uongozi wa Bi. Mtumwa na mwalimu kiongozi msimamizi Ustadh Ally Mwinchande. Madrasa hiyo inatoa mafunzo ya Fiqh, Tawheed, Sira, Qur’an (kuhifadhi na tafsiri) pamoja na Lugha ya Kiarabu. Kama kawaida ya tatizo sugu la madrasa nyingi za nchini, nayo inakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na vifaa vya kufundishia, ubao, majengo (kwani madrasa ipo nyumbani kwa Bi. Mtumwa), fedha, ugumu wa michango kutoka kwa wazazi. Wito wa Bi. Mtumwa Rashidi Tassaka kwa Waislamu, anawaomba Waislamu
kote nchini na nje kusaidia madrasa kwa anuani: S.L.P. 12752, Dar es Salaam.
Madrasat Hidayatul Muumini Mwadui
Kwa jitihada za Waislamu wa Mwadui, vijana na akina mama wakishirikiana na kamati ya Msikiti, mnamo mwaka 1996 walifanikiwa kujenga madrasa hiyo ambayo ina vyumba viwili pamoja na ofisi mbili. Awali madrasa hiyo wakati huo ikiitwa madrasati Husnayni ilianza kuwepo Msikitini takriban kama miaka 25 iliyopita. Mnamo Agosti 8, 1998 madrasa hiyo ilifunguliwa na Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga Alhaj Issa Shaaban. Muasisi wa madrasa hii akiwa ni Ustadh Maaliki Yaasini na ikaitwa jina Hidayatul-Muumini. Tangu ilipofunguliwa madrasa hii kumekuwa na ufanisi mzuri wa wanafunzi kusoma Qur’an kwa ufasaha zaidi tofauti na kipindi kiichopita. Vile vile madrasa hii inafundisha Fiqh na Kiarabu na Sira. Miongoni mwa wazee ambao wametoa ushirikiano wa hali ya juu wakishirikiana vijana wanaokaa katika mtaa wa Mwadui ni mzee Ally Kasanura, Mzee Ahmed Mshwezi, Mzee Mrisho Kapambwe, Mzee Yassin Jumaa, Mzee Abdallah Dello, Mzee Mussa Salumu, Mzee Abdallah Mwasoni, Mzee Muhammed Byabusha, Mzee Diwani Mrutu. Madrasa hii inawanafunzi wapatao 50. Wasichana 29 na wavulana 21, japokuwa kila baada ya mwaka mmoja au miwili Waislamu hupunguzwa kazi na wengine kustaafu. |
YALIYOMO
Tahariri Baada ya futari nzuri: Tuwatupie macho wenye njaa Rais Mkapa kuwa mgeni rasmi Baraza la Idd Waumini, Masheikh Arusha wasutana kwa futari ya Mrema Dondoo za saikolojia
MSADAT yazidi kutia moyo Tanga MAFUNZO KUHUSU FUNGA YA RAMADHANI Michezo isiyoruhusiwa katika Uislamu Ustadh Farid: Kijana aliyejitolea kuwapa Da'awa watalii Hakuna Magharibi wala Mashariki:
Uislamu ni ubinaadamu
Ijue madrasati Mar-wa ya Dodoma
mjini
Ijue Madrasat Jadidul Fiqhyyat
- Tabata Kimanga
Madrasat Hidayatul Muumini Mwadui Washindi wa mashindano ya Hadithi za Mtume (s.a.w.) wapatikana Madrasa Shafii Ujiji Kigoma yaonyesha umahiri wake Waanzisha mifuko kusaidia wagonjwa Dodoma Waislamu Kondoa waomba msaada kumalizia Msikiti Mnyororo wa imani-2
Kutoka magazeti ya zamani:
Jengo la Waislamu Moshi lageuzwa
Kanisa la Walokole
Masjid Nurania yaswaliwa
Ijumaa
Jabal Hira kutoa mafunzo
ya Kompyuta Morogoro
Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|