AN-NUUR 
Na.184 Ramadhan 1419, Januari 15 - 21, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
MAFUNZO KUHUSU FUNGA YA RAMADHANI
 

Sifa njema anazistahiki Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe vyote, na rehema na amani zimfikie Mtume wetu Muhammad, Jamaa na Sahaba wake wote. 
  

ZAKAATUL-FITRI: 

Zakaatul-fitri ni pishi moja ya chakula (Takriban kilo mbili na nusu =2500gm), mchele au ngano au tende au chakula kingine ambacho watu wanakula. 

Haitoshelezi Zakaatul-fitri kutoa pesa na nguo isipokuwa chakula tu. 

Zakaatul-fitri hutolewa asubuhi ya siku ya Idd kabla ya kusali sala ya Idd, na inatosha kuitoa kabla ya siku ya Idd kwa siku moja au siku mbili. 

Haifai kuahirisha na kuitoa Zakaatul-fitri baada ya sala ya Idd isipokuwa kwa udhuru tu. 

Zakaatul-fitri hutolewa kumtolea mtoto mdogo, mtu mzima, mwanamume na mwanamke katika Waislamu. 

SALA YA IDD: 

HUKUMU YAKE 

Sala ya Idd ni sunna iliyosisitizwa. Baadhi ya wanazuoni wamesema kuwa sala ya Idd ni wajibu kwa sababu zifuatazo: 

1. Mwenyezi Mungu ameamrisha kuisali sala ya Idd. "Basi sali kwa ajili ya Mola wako na chinja (kwa ajili ya Mola wako)" - Sura Al-Kauthar(108), aya 2. 

2. Mtume (S.A.W.) daima alikuwa akisali sala ya Idd. 

WAKATI WAKE 

Wakati wake unaanza tangu kuchomoza jua na kupanda kiasi cha mkuki (kama mita 3) mpaka kabla ya jua kupinduka (kutoka usawa wa katikati ya dunia kuelekea magharibi). 

Kusali mapema ni bora zaidi hasa katika sala ya Idd Al- Adh’haa (Idd El- Hajj) ili kuwe na wakati wa kutosha kwa anayetaka kuchinja. 

MAHALI PAKE 

Jambo lililo bora zaidi ni kuwa sala ya Idd isaliwe katika uwanja ikiwezekana, kwa kuwa Mtume (S.A.W.) alifanya hivyo na pia Sahaba wake waongofu walifanya hivyo. 

HAKUNA ADHANA WALA IQAMA 

Imepokewa kutoka kwa Ibn-Abbaas kwamba Mtume (S.A.W.) alisali sala za Idd mbili (Idd El-Fitri na Idd El-Hajj) bila ya Adhana wala Iqama. 

NAMNA YAKE 

Sala ya Idd ni rakaa mbili. Amesema Omar, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, kwamba: "Sala ya Idd ni rakaa mbili, ikiwa ni sala kamili isiyopunguzwa (yakiwa ni mafunzo yaliyotoka) juu ya ulimi wa Mtume wenu na hakika amehasirika aliyeleta uzushi". 

Katika rakaa ya kwanza ataleta Takbira saba ukitoa Takbira ya kuanzia sala, na katika rakaa ya pili ataleta Takbira tano. 

Imepokewa kutoka kwa Aisha (mke wa Mtume S.A.W.), Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.) katika sala ya Idd El-Fitri na Idd El-Hajj alileta Takbira saba na tano ukitoa Takbira ya kuanzia sala ya Idd. Katika rakaa mbili hizo atasoma sura Al-Aalaa (87) na sura Al- Ghaashiyah (88) kama ilivyo katika Hadithi ya Nuuman bin Bashiir aliyoipokea Imam Muslim au atasoma sura Qaaf (50) na sura Al-Qamar (54) kama ilivyo katika hadithi ya Abi -Waaqid Al-Laythiy ambayo pia ameipokea Imam Muslim. 

HOTUBA 

Hotuba inakuwa baada ya sala. Amesema Ibn-Abbas, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, kwamba: "Nilishuhudia (nilihudhuria) Idd pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.), Abu-Bakari, Omar na Othman, Mwenyezi Mungu awawiye radhi, na wote walikuwa wakisali kabla ya hotuba". Ameipokea Hadithi hii Imam Bukhary na Muslim. 

MAMBO YALIYO SUNNA SIKU YA IDD 

Kuoga. Imepokewa kutoka kwa Aliy bin Abi-Twalib, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, kwamba aliulizwa kuhusu kuoga akasema kuwa: Ni siku ya Ijumaa, siku ya Arafah, siku ya Idd El-Fitri na siku ya Idd El-adh’haa" 

2. Kuvaa nguo nzuri sana. Amesema Ibn Abbass kuwa: Mtume (S.A.W.) alikuwa akivaa kashida (shali) nyekundu siku ya Idd. 

3. Kula siku ya Idd El-Fitri kabla ya kutoka kwenda kusali. Imepokelewa kutoka kwa Anas, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, akisema kwamba: Mtume (S.A.W.) Alikuwa hatoki (kwenda kusali) siku ya Idd El-Fitri mpaka ale tende. 

4. Kuchelewesha kula siku ya Idd El-Adh’haa mpaka ale katika 

Udh-hiyah (mnyama) wake (atakayemchinja). Hiyo ni kwa mujibu wa Hadithi ya Abu-Dharr isemayo kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.) alikuwa hatoki (kwenda kusali) siku Idd El-Fitri mpaka ale na alikuwa hali siku ya Idd El-Adh’ haa mpaka achinje. 

5. Kubadilisha njia. Amesema Jabir, Mwenyezi Mungu amuwiye radhi, kwamba: Alikuwa Mtume (S.A.W.) ifikapo siku ya Idd anabadilisha njia (kwa maana kwamba anaporudi kusali hupita njia nyingine na sio ile njia aliyopita wakati wa kwenda)- Ameipokea Hadithi hii Imam Bukhary. 

6. Kuleta Takbira. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na ili mkamilishe hisabu (ya siku mlizoacha kufunga kwa udhuru) na ili mumtukuze Mwenyezi Mungu (kwa Takbira) kwa vile amekuongozeni". Sura Al-Baqara(2), aya 185. Na amesema Mwenyezi Mungu:"Na mtajeni Mwenyezi Mungu katika siku zinazohisabika (siku tatu baada ya Idd El- Haj)". Sura Al-Baqara(2), aya 203 

  

WAKATI WA TAKBIRAH 

a) Katika Idd El-Fitri wakati wa Takbira unaanza tangu kuonekana kwa mwezi wa Mfungo Mosi au kukamilika hisabu ya siku za mwezi wa Ramadhani mpaka kuanza hotuba ya Idd. 

b) Katika Idd El-Adh’ haa wakati wa Takbira unaanza tangu asubuhi ya siku ya Arafah (tarehe 9 mfungo Tatu) mpaka mwisho wa siku za Tashriiq (tarehe 13 mfungo Tatu). Hayo yamesihi kunukuliwa kutoka kwa Aliy bin Abi-Twalib, Ibn-Abbas na Ibn-Masoud Mwenyezi Mungu awawiye radhi wote. 



Michezo isiyoruhusiwa katika Uislamu 

SIFA zote njema anastahiki Mwenyezi Mungu (s.w.) kwa kuendelea kutuwezesha kuandaa matoleo haya yanayohusu mafundisho muhimu kwa Funga ya Ramadhani. Katika toleo letu lililopita tuliangalia kuhusu "Vipi tufunge". Vipi tufunge ilibainisha muongozo wa ibada ya Swaumu ya Ramadhani katika ukamilifu wake. 

Tuliweza kuona kuwa kujizuia na kula, kunywa, kujamii na kadhalika bila ya kufanya jitihada za kutosha katika kuzingatia masharti na kuchunga miiko mingineyo ya Swaumu, ni kazi bure; sawa na kuamua kushinda njaa ama kwa maneno mengine ni kwamba Allah (s.w.) hatazikubali funga zetu. 

Funga iliyokamilika ama funga inayokubaliwa na Allah (s.w.) ni ile inayoambatana na kudhibiti midomo yetu, macho yetu, mikono yetu, miguu yetu, masikio yetu, ghadhabu zetu, nyoyo zetu na pia akili zetu. 

Ukamilifu wa funga ni pamoja na kutekeleza yote katika maamrisho na kuacha yote katika makatazo yake Mwenyezi Mungu (s.w.). Hii ndiyo funga itakayotufikisha katika lengo alilotukusudia Allah (s.w.) pale alipotuamrisha kufunga (Swaumu ya Ramadhani) ili tuweze kuwa wacha - Mungu. (Qur’an 2:183). 

Insha-Allah katika toleo hili tutaangalia kuhusu michezo iliyoharamishwa katika Uislamu. Tutaweza pia kuona michezo iliyo halali kwa Muislamu na madhara yanayotokana na michezo yote iliyoharamishwa. 

Michezo iliyoharamishwa katika Uislamu: 

Michezo iliyoharamishwa katika Uislamu tunaweza kuigawa katika mafungu mawili. 

Fungu la kwanza: Ni ile ambayo uharamu unatokana na kuchupa mipaka ya Allah (s.w.). Hata kama mtu atacheza michezo inayoruhusiwa kwa nia nzuri kwa mfano kuupa mwili mazoezi, kujipa mazoezi ya kujihami n.k. itakuwa ni haramu michezo hiyo endapo atachupa mipaka ya Allah (s.w.) katika uchezaji wake kama vile kucheza bila kuusitiri mwili (kuvaa bukta hadharani), kutumia lugha mbaya, kupitisha wakati wa swala, n.k. 

Fungu la pili: Ni ile ambayo imeharamishwa katika Qur’an na inayofanana na hiyo. Michezo yote iliyoharamishwa katika Qur’an tutaigawanya katika makundi manne ili ifahamike vema. 

Kundi la kwanza: Linahusu michezo yote ya upuuzi (laghwi). Michezo hii ni yenye kuzubaisha ama kupumbaza na kumsahaulisha mtu majukumu yake na lengo lake la kuwepo hapa ulimwenguni. Tunajifunza katika aya zifuatazo: 

"Kila nafsi itafungika (motoni) kwa amali (mbovu) ilizozichuma, Isipokuwa watu wa kuliani, wanaulizana juu ya watu wabaya: Ni kipi kilichokupelekeni motoni? Waseme: Hatukuwa miongoni mwa waliokuwa wakiswali, wala hatukuwa tunalisha Misikitini. Na tulikuwa tukizama (katika upuuzi) pamoja na waliokuwa wakizama". (Qur’an 74:38-45). 

"Hakika wamefuzu Waislamu ambao katika swala zao huwa ni wanyenyekevu. Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi." (Qur’an 23:1-3) 

"Na wale ambao hawashuhudii shahada za uwongo, na wanapopita penye upuuzi, hupita kwa heshima (zao)". (Qur’an 25:72) 

Kundi la pili: Linahusu michezo yote ya kamari au bahati nasibu (pata potea) na inayofanana na hiyo. Michezo yote hii pia imekatazwa katika Qur’an kama aya zifuatazo zinavyobainisha: 

"Enyi mlioamini! Bila shaka ulevi na kamari na kuabudiwa (au kuombwa) asiyekuwa Mwenyezi Mungu, na kutazamia (kupiga ramli, utabiri n.k.) ni uchafu na ni kazi ya shetani. Basi jiepusheni navyo ili mpate kufaulu". (Qur’an 5:90) 

"Wanakuulizeni juu ya ulevi na kamari. Sema; katika hivyo mna madhara makubwa na manufaa kwa watu. Lakini madhara yake ni makubwa zaidi kuliko manufaa yake ... " (Qur’an 2:219) 

"Hakika shetani anataka kukutilieni uadui na bughudha baina yenu kwa ajili ya ulevi na kamari na anataka kukuzulieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na (kukuzuilieni) kuswali. Basi je hamtaacha mabaya hayo? 

Kundi la tatu: Linahusu Ngoma na Disko. Michezo yote ya ngoma na disko kama tuionavyo katika utamaduni wa jamii zetu ni haramu kwa sababu kuu mbili zifuatazo: Kwanza, michezo hii ni laghwi yaani michezo ya upuuzi, huwafanya wahusika wapoteze muda mwingi nje ya kutekeleza mambo yenye manufaa nao au nje ya lengo la kuumbwa kwao. Pili, michezo hii huchezwa katika mchanganyiko wa wanawake na wanaume na huwa ni vichocheo vikubwa sana vya zinaa. Katika Uislamu ni haramu kushiriki katika shughuli yoyote inayochochea zinaa. 

"Wala msikaribie zinaa. Hakika hiyo ni uchafu (mkubwa) na njia mbaya (kabisa)". (Qur’an 17:32) 

Pia ni vema tuweke wazi kuwa vigoma vya daku ni haramu. Ni utaratibu uliowekwa na wanadamu. Si katika mafundisho ya Uislamu. Huwezi kutumia kitu kilichoharamu (ngoma) kwa kutendea kheri, na vyote viwili vikawa ni kheri. 

Kundi la nne: Linahusu nyimbo na mashairi. Nyimbo au mashairi huwa halali au haramu kutegemeana na lengo la nyimbo au mashairi hayo. Ni wazi kuwa nyimbo au mashairi ya kimapenzi ambayo ni vichocheo vya zinaa na upotevu mwingineo ni haramu moja kwa moja. Pia mashairi ama nyimbo ambazo ndani yake kuna lugha mbaya, au kuna kuitukana au kuipinga dini ya Allah (s.w.), basi mashairi hayo au nyimbo hizo zitakuwa ni haramu. Hali kadhalika mashairi na nyimbo ambazo ziko pale kumpotezea mtu muda wake ni laghwi na ni haramu. 

Kwa upande mwingine, nyimbo na mashairi ambayo ndani yake kuna hekima na mafunzo ya aina mbalimbali ambayo hayaambatani na sauti na midundo yenye kuchochea zinaa yanakubalika katika Uislamu. 

Michezo inayoruhusiwa katika Uislamu: 

Michezo yote ile ambayo inampelekea mchezaji kupata uwezo zaidi wa kiafya na kiakili wa kumuabudu Allah (s.w.) imeruhusiwa na kusisitizwa na Uislamu. Suala la afya ya mwili na akili limepewa kipaumbele katika Uislamu. Mtume (s.a.w.) amesema: 

"Afya kwa mtu anayemuogopa Allah (s.w.) ni bora kuliko utajiri". 

Mara kwa mara Mtume (s.a.w.) alikuwa anamuomba Allah (s.w.) ampe afya nzuri. Pia Mtume (s.a.w.) katika kusisitiza afya njema ya kimwili na kiakili amesema: 

"Waumini (wacha Mungu) wote mbele ya Allah ni sawa lakini aliye bora zaidi ni yule mwenye siha nzuri zaidi". 

Hivyo, michezo yote isiyochupa mipaka ya Allah (s.w.) itakayochezwa kwa lengo la kujenga afya ya mwili na akili imeruhusiwa na Uislamu. Vile vile michezo yote itakayochezwa kwa lengo la kujihami na maadui wa Uislamu kwa kufanya mazoezi ya kivita kama vile kulenga shabaha, kutupa mikuki, mieleka, mbio za farasi n.k. imesisitizwa na Uislamu. Mtume (s.a.w.) amebainisha vizuri kuhusu michezo yote iliyo halali na ile iliyo haramu pale: 

Utbah bin Aamir alipoeleza kuwa Mtume wa Allah amesema: "Kila mchezo atakaocheza mtu ni haramu ila kutupa mishale, kumfunza farasi wake nan kucheza na mkewe. Hakika hii ndiyo michezo ya kweli (yenye faida)". 

Madhara ya michezo iliyoharamishwa: 

Michezo ya kikamari husababisha uadui na bughudha kwa pande zinazohusika kutetana, kusengenyana, kutukanana, kubishana na kutaniana. Uadui kati ya timu mbili za mashabiki si jambo geni kwetu. Watu kupigana mpaka kuuana kutokana na kudhulumiana katika michezo ya kamari si jambo geni kwetu. 

Michezo ya kikamari pia huwazuilia watu kumkumbuka Allah (s.w.) kwa kuwapotezea muda na kuwasahaulisha majukumu muhimu ya maisha yao binafsi, familia na jamii kwa ujumla. Aya ifuatayo inathibitisha haya: 

"Hakika shetani anataka kukutieni uadui na bughudha baina yenu kwa ajili ya ulevi na kamari na anataka kukuzuilieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na (kukuzulieni) kuswali. Basi, je, hamtaacha mabaya hayo?" 

Michezo ya upuuzi huwazuilia watu kuswali kwa kuwapumbaza wachezaji na wasikilizaji au watazamaji kiasi cha kujenga tabia ya kupuuza swala. Tumeyashuhudia haya katika magenge ya mabao yaliyo karibu na Misikiti ya mijini. Ni jambo la kushangaza kuwakuta Waislamu wakiendelea na bao kuanzia asubuhi mpaka jioni na kupitwa na swala zote za kutwa kisha huziswali kadha wakati wa Isha au kama watafanikiwa kuziswali watashindwa kabisa kuuhudhurisha moyo katika swala zao kwa sababu mioyoni mwao bado watakuwa wanazingatia michezo yao ya laghwi. Haya yote mawili, kuswali kadha na kutouhudhurisha moyo katika swala ni miongoni mwa matendo ya kupuuza swala yaani kushindwa kusimamisha swala. Kupuuza swala ni jambo ambalo litatuangamiza kwa sababu hatutasalimika na adhabu ya Mwenyezi Mungu (s.w.): 

"...kwa hakika swala kwa Waislamu ni faradhi iliyowekewa nyakati makhsusi". (Qur’an 4:103) 

Bwana Mtume (s.a.w.) amesema: 

"Haiwi swala pasipo kuuhudhurisha moyo ndani ya swala, kwa sababu mwenye kuswali anang’ong’ona na Mola wake, na mahala pa kunong’onea ni moyoni. Pindi moyo unapoghafirika, basi swala yake hubatilika pamoja na swala ya viungo. Kwa sababu moyo ndio msingi wa ibada na sehemu zote za kiwiliwili zlizobaki zinaufuata moyo". 

Michezo ya kipuuzi inaimarishwa zaidi katika mwezi wa Ramadhani kwa lengo la kupoteza muda ili kufikia wakati wa kufuturu ama kula daku. Matokeo yake ni watu kuswali Taraweih mbio mbio ili kuwahi michezo ya kipuuzi ama matokeo yake ni kupoteza muda bure na kushindwa kuchuma neema tele alizotukusudia Allah (s.w.) katika mwezi wa Ramadhani. Yafaa tusisite tena kuwa kuswali mbio mbio ni haramu kwa sababu kuna masharti muhimu ya swala ambayo tutashindwa kuyakamilisha kwa sababu ya haraka tulizonazo na hivyo kuwa tumepuuza swala. Rejea toleo Na. 2 lililopita linalohusu "Adabu katika swala". 

Kwa maoni, maswali au mapendekezo, tafadhali tuandikie, Waandishi (Funga ya Ramadhani), S.L.P. 296, Arusha, Tanzania. 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Tahariri 
Baada ya futari nzuri: Tuwatupie macho wenye njaa 

Rais Mkapa kuwa mgeni rasmi Baraza la Idd 

Ubungo yakumbwa na ukame 

Waumini, Masheikh Arusha wasutana kwa futari ya Mrema 

Dondoo za saikolojia 
Na. Abu Halima Sa Changwa 

Waislamu turejee kwa Allah 

MSADAT yazidi kutia moyo Tanga 

Mjue Usama bin Ladin 

MAFUNZO KUHUSU FUNGA YA RAMADHANI 

Michezo isiyoruhusiwa katika Uislamu 

Ustadh Farid: Kijana aliyejitolea kuwapa Da'awa watalii 

Hakuna Magharibi wala Mashariki: Uislamu ni ubinaadamu 
Na Abubakari S. Marwillo 

Ijue madrasati Mar-wa ya Dodoma mjini 
Na Abu Zuberi, Dodoma 

Ijue Madrasat Jadidul Fiqhyyat - Tabata Kimanga 
Na B. Mwakangwale 

Madrasat Hidayatul Muumini Mwadui 

Washindi wa mashindano ya Hadithi za Mtume (s.a.w.) wapatikana 

Madrasa Shafii Ujiji Kigoma yaonyesha umahiri wake 

Waanzisha mifuko kusaidia wagonjwa Dodoma 

Waislamu Kondoa waomba msaada kumalizia Msikiti 

Mnyororo wa imani-2 
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa 

Kutoka magazeti ya zamani: 
Wanaoshitakiwa kwa uhaini kortini leo 

Jengo la Waislamu Moshi lageuzwa Kanisa la Walokole 
Na Mwandishi Wetu, Moshi 

Masjid Nurania yaswaliwa Ijumaa 
Na Rajab Rajab, Morogoro 

Jabal Hira kutoa mafunzo ya Kompyuta Morogoro 
Rajab Rajab na Mussa Ally, Morogoro 

Sayansi na Teknolojia 
[Internet ni nini?] 

Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Thamani ya mlo wa Uyoga] 
 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita