AN-NUUR 
Na.184 Ramadhan 1419, Januari 15 - 21, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Barua za Wasomaji 
 

Waislamu hawawachinji wananchi Algeria 

Ndugu Mhariri 

NAOMBA nizungumzie kero za magazeti, maredio na TV ya Tanzania. Ni matarajio ya kila muungwana kuwa chombo chochote kitakachojishughulisha na masuala ya jamii kitakuwa na msimamo wa kati na kati bila kulalia upande mmoja au kushiriki katika mashambulizi dhidi ya dini moja. 

Katika hali ambayo ndivyo ilivyo hapa kwetu Tanzania, imetokea asilimia 99 ya vyombo vya habari vinamilikiwa na wasiokuwa Waislamu na hata vile vya vyama na serikali wenye kauli na maamuzi pia sio Waislamu. 

Matokeo ya hali hiyo yamevifanya vyombo hivi vya habari kushiriki moja kwa moja katika vita vya habari dhidi ya Uislamu vinavyoendelea duniani chini ya usimamizi wa mtandao wa nchi za Magharibi. 

Mfano hai wa kushiriki katika vita dhidi ya Uislamu, vyombo hivi vya habari vya Tanzania mara nyingi hutangaza kuwa Waislamu Algeria wamewaua wanawake na watoto kwa kukata shingo zao kwa mapanga na mashoka. 

Lakini wakati huo huo, huwa wanadai mpashaji wao wa habari hizo ni msemaji wa serikali ya Algeria. 

Mapambano yanayoendelea Algeria ni kati ya Waislamu na Serikali. Unapotangaza habari za Waislamu kwa kutegemea taarifa ya serikali una maana gani? 

Siku gani katika historia ya mapambano ya uhuru Afrika Kusini, kaburu alitoa taarifa sahihi kuhusu Mandela? 

Dunia haina utata na hoja kwamba mamilioni ya kura za wananchi wa Algeria (wakiwemo hao wanaodaiwa kuchinjwa) ndio waliyokipa chama cha Kiislamu ushindi mkubwa ulioporwa na serikali (kwa shinikizo la nchi za Magharibi). 

Iweje tena kuwe kuna kuchinjana kati ya waliochaguliwa na waliopiga kura? 

Kwa nini vyombo vya habari vya Tanzania visitegemee vile vile habari kutoka kwa msemaji wa Kiislamu Algeria? 

Rashid Rashid (RR) 
Kigogo, 
Dar es Salaam. 



Uchaguzi wa Sheikh wa Bakwata wa Mtaa 

Ndugu Mhariri 

TAFADHALI naomba nafasi katika gazeti lako tukufu nitoe dukuduku langu kuhusu uchaguzi wa Sheikh wa Bakwata wa mtaa wa Pahi, Kondoa. 

Mnamo Agosti 8, 1998 ulifanyika uchaguzi wa Sheikh wa Kata. Fomu zililetwa mapema za kugombea nafasi hiyo, zikajazwa na wagombea watatu. 

Wagombea hao walikuwa Mwalimu Abubakari Ali Hando, Mwalimu Iddi Ali na Sheikh Athumani Nchula aliyekuwa madarakani tangu mwaka 1982 mpaka mwaka 1998. 

Agosti 8, 1998 ilirudi fomu ya Sheikh aliye madarakani, wajumbe walidai fomu za wagombea wengine wawili. 

Maofisa waliotumwa na Bakwata Wilaya kusimamia uchaguzi walisema "Sheikh Nchula amepitishwa na wilaya maana hana makosa". 

Mimi napinga hoja hiyo, si kweli kabisa, Sheikh huyo anayo makosa chungu mbovu. Amekuwa madarakani miaka 16 hakuleta maendeleo yoyote katika jamii ya Kiislamu. Wilaya ikisema Sheikh hana makosa, inamlinda tu. 

Mpenzi wa Haki, 
Omar Idi Nkusa, 
Pahi, Kondoa. 



Wito kwa Waislamu kufikia lengo la ibada 

Ndugu Mhariri 

IBADA imekuwa ikifahamika kwa mtazamo finyu ambao unasababisha Waislamu wengi wao wasifikie lengo la ibada hizo. Baadhi ya Waislamu wameelewa vibaya maneno ya Mtume Muhammad (s.a.w.) aliposema Uislamu umejengwa kwa nguzo tano. 

Hivyo baadhi ya Waislamu wamezichukulia nguzo tano tu ndio ibada. Nguzo tano zilivyotajwa hapa ni mfano tunapoambiwa jengo au nyumba imejengwa kwa nguzo lakini sio nguzo tu ndio nyumba, vipo vitu vingine zaidi ambavyo vinasababisha nyumba kuwa nyumba. 

Ibada ni pamoja na nguzo tano, lakini vile vile ibada inatokana na neno Abd ambalo lina maana ya mtumwa, kwa hivyo ibada ni utumishi au utumwa. 

Ibada kama lengo letu la maisha ni pamoja na kukubali sheria za Mwenyezi Mungu katika kila hali. Vile vile kujitoa katika sheria zote ambazo zitaenda kinyume na Mwenyezi Mungu, matendo yetu yote yafuate sheria za Allah (s.w.). 

Tunatakiwa tuishi ndani ya mipaka ya Allah (s.w.) katika kila jambo tunalolifanya. Hivyo maisha yetu yote ni ibada, kula kwetu, kuchuma kwetu, kulala kwetu, kusema kwetu, kutembea kwetu, kusoma kwetu n.k. yote haya ni ibada tunayotakiwa tuyatende haya tukiwa tunafuata sheria za Allah (s.w.) tukiwa ndani ya mipaka ya Allah (s.w.). 

Hivyo, tunaposema ibada ni kusali, kufunga, kuhiji, kutoa zaka na kutoa sadaka tu tutakuwa bado hatujaelewa vizuri maana halisi ya ibada tutakapoyagawanya matendo katika sehemu mbili. 

Yaani baadhi tukayafanya ndio ibada kama swala, funga na baadhi kama mfumo mzima wa maisha, utamaduni, kisiasa, kijamii na kiuchumi tukajiona hatuhusiki kuingiza dini, basi bado itabidi tukae chini tuchunguze maana halisi ya ibada. 

Nguzo za Uislamu ni njia tu ya kutupelekea kufikia kuwa wacha Mungu, tunatakiwa maisha yetu ya kila siku yanapoyaendesha tuyaendeshe katika njia ambayo Mwenyezi Mungu anairidhia. 

Kama tunaswali, tunafunga n.k., lakini matendo yetu ni kinyume na sheria za Allah (s.w.) yaani tukishiriki kwenye wizi, zinaa, ulevi, kutoa rushwa, kupokea rushwa bado kabisa hatujaielewa ibada. 

Hivyo Waislamu tunatakiwa tuchanganye ibada zetu pamoja na matendo yetu yote ya kila siku yawe ndani ya mipaka ya Allah (s.w.) hapo tutalifikia lengo halisi la ibadani. 

Kwani Mtume (s.a.w.) anasema: "Wale ambao wataswali swala tano, lakini bado matendo yao ni mabaya (yaani watenda dhambi) siku ya kiama watakuwa muflis yaani waliozidhulumu nafsi zao". 

Hivyo, tujitahidini ibada zetu tuzifanye inavyotakiwa pia matendo yetu yasichupe lengo la ibada ni kumpelekea mja awe Khalifa wa Mwenyezi Mungu na lengo halitofikiwa kama tutayagawa mambo. 

Tumeielewa vibaya ibada kwa kuamini kwamba nguzo tano za Uislamu yaani swala, funga, zaka, hija na shahada. Ibada hizi hasa swala, funga, zaka na hijja ni kufutia dhambi. Huku ni kueleweka vibaya kwa ibada kwani Uislamu hauruhusu kufanya dhambi. 

Tukisema ibada ni za kufutia dhambi ni kwamba tumehalalisha dhambi, kusamehewa dhambi au kutokusamehewa dhambi yote hayo anayajua Mwenyezi Mungu. 

Ingawa Mwenyewe Allah (s.w.) ameahidi kusamehe waja wake. Lakini ibada sio za kufutia dhambi. Tunamwabudu Mwenyezi Mungu kwa sababu tu hili ndio lengo letu la kuumbwa. Kwani Mwenyezi Mungu anasema katika (51:56) kwamba hakuwaumba majini na watu isipokuwa wamuabudu. 

Hivyo, tunapofanya ibada tujue kwamba hilo ni lengo letu la maisha ya hapa duniani. 

Maryam Ussi, 
Ubungo Islamic High School, 
Dar es Salaam. 



Mafundi cherehani mjihadhari 

Ndugu Mhariri 

NAPENDA kuwatadharisha mafundi cherehani katika kazi zao za kushona nguo za wanawake. Kwani wewe fundi unapoletewa kitambaa ili ushone nguo na mwanamke huyo anachagua mshono wa ajabu, kinguo kifupi cha kubana mapaja, makwapa yote nje na wewe unakubali kushona nguo na hivyo na wewe unaelewa kuwa vazi hilo linamkasirisha Allah (s.w.) basi dhambi anazopata huyo mwanamke uliye mshonea hiyo nguo mnachangia. 

Kwani nguo wanazoshonesha mama zetu, dada zetu na hata ndugu zetu ni za kutia aibu kabisa kwani kutakuta mtu mzima na familia yake nguo aliyovaa hata akiangusha kitu kuinama kuokota hawezi na wewe mtu unayemwangalia akiwa anapita unaona hata haya. 

Zuhura Abdallah Mbonga, 
S.L.P. 30194, 
Kibaha - Pwani. 



Pongezi Komandoo! 

Ndugu Mhariri 

Naomba nipate nafasi katika gazeti lako tukufu kutoa pongezi zangu kwa Komandoo Salmin kwa kutuletea maendeleo ambayo hayajapata kuletwa katika kipindi cha miaka 30 ya mapinduzi.  

Kipindi chote cha miaka thelathini tumeshuhudia udini wa viongozi wa SMZ, ijapo wao hawakuwa watu wa dini kama Karume na Jumbe. Walitudhihirishiya udini kwa kutuzuiya kujenga makanisa eti mpaka tujaze yaliyopo, tusile hadharani mchana wa Ramadhani, tusiunde vyombo vya kikristo, tusifungue mabaa, tusifuge nguruwe, tusifungue mashule ya kikristo wala zahanati za kikristo, tusisherehekee Krismasi kwa vifijo katika Ramadhani n.k. 

Leo tunashukuru vikwazo vyote vimeondolewa. Matamasha ya Pasaka tunafanya tupendavyo na mwenye nguruwe wake anafuga, halikadhalika wenye vilabu vyao vya pombe. Hawa ndio viongozi wafaao ambao hawana udini. 

Tunakutakia mafanikio ya kugombea tena mwaka 2000. 

Isaac Wakati, 
Unguja. 

 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Tahariri 
Baada ya futari nzuri: Tuwatupie macho wenye njaa 

Rais Mkapa kuwa mgeni rasmi Baraza la Idd 

Ubungo yakumbwa na ukame 

Waumini, Masheikh Arusha wasutana kwa futari ya Mrema 

Dondoo za saikolojia 
Na. Abu Halima Sa Changwa 

Waislamu turejee kwa Allah 

MSADAT yazidi kutia moyo Tanga 

Mjue Usama bin Ladin 

MAFUNZO KUHUSU FUNGA YA RAMADHANI 

Michezo isiyoruhusiwa katika Uislamu 

Ustadh Farid: Kijana aliyejitolea kuwapa Da'awa watalii 

Hakuna Magharibi wala Mashariki: Uislamu ni ubinaadamu 
Na Abubakari S. Marwillo 

Ijue madrasati Mar-wa ya Dodoma mjini 
Na Abu Zuberi, Dodoma 

Ijue Madrasat Jadidul Fiqhyyat - Tabata Kimanga 
Na B. Mwakangwale 

Madrasat Hidayatul Muumini Mwadui 

Washindi wa mashindano ya Hadithi za Mtume (s.a.w.) wapatikana 

Madrasa Shafii Ujiji Kigoma yaonyesha umahiri wake 

Waanzisha mifuko kusaidia wagonjwa Dodoma 

Waislamu Kondoa waomba msaada kumalizia Msikiti 

Mnyororo wa imani-2 
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa 

Kutoka magazeti ya zamani: 
Wanaoshitakiwa kwa uhaini kortini leo 

Jengo la Waislamu Moshi lageuzwa Kanisa la Walokole 
Na Mwandishi Wetu, Moshi 

Masjid Nurania yaswaliwa Ijumaa 
Na Rajab Rajab, Morogoro 

Jabal Hira kutoa mafunzo ya Kompyuta Morogoro 
Rajab Rajab na Mussa Ally, Morogoro 

Sayansi na Teknolojia 
[Internet ni nini?] 

Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Thamani ya mlo wa Uyoga] 
 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita