AN-NUUR
Na.158 Rabi' Awal 1419, Julai 17 - 23, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Ni nani hawa Waislamu wa Siasa Kali ?
 

Ni ukweli usiopingika kwamba Uislamu ulianza kupata nguvu mpya mara baada ya mapinduzi yaliyofanywa na watu wa Iran kumng’oa madarakani Shah-in Saha wa nchi ya Iran na kuleta serikali yenye mwelekeo wa maadili ya Kiislamu. USTADH A.S. FUNDI anaelezea zaidi katika makala hii. 

KWA zaidi ya mwongo mmoja sasa (1980-1998); Uislamu umejiimarisha zaidi sehemu mbalimbali duniani kote. Mageuzi hayo yameonekana kutokea Mashariki ya Kati, Majimbo makuu ya Kusini ya Urusi, Afrika ya Mgharibi, na hivi karibuni ndani ya moyo wa Ulaya Mashariki. 

Kujizatiti huku kupya kwa Uislamu kumeonekana na maadui wake kama tishio la usalama wa ubepari (Capitalism) na Ukomunisti (Communism) ulimwenguni. 

Na ni hakika kuwa Uislamu una maadui wengi sana. Washirikina wote ni adui wa Uislamu, makafiri ni maadui wa Uislamu, mafasiki ni maadui wa Uislamu, na madhalimu wote adui yao mkubwa ni Uislamu. 

Kila kukicha propaganda hizi na zile, programu hizi na zile, mikakati hii na ile kuundwa na maadui kama kwa lengo la kuusambaritisha Uislamu usisimame popote duniani. 

Katika makala hii nitajaribu kuonyesha mbinu moja kuu inayotumiwa na kambi hii ya maadui wa Tawhiid (Upweke wa Allah (s.w.) katika kuupiga vita Uislamu, na hasa harakati za kuulingania Uislamu. 

Kabla ya kuchambua kwa undani hiyo mbinu kuu ya kusitisha harakati za Kiislamu duniani, hebu kwanza tuangalie baadhi ya virumbajengo vinavyotumika pia katika kuitayarisha akili ya mwanadamu kuja kuunga mkono mbinu hiyo bila ya kujitambua. 

Kwanza ni lazima kuwapumbaza watu makini na wasio makini kwa kuwaundia michezo itakayowashughulisha wasahau lengo la kuja kwao duniani. Pumbazo kuu linalowachukua watu wote, wake kwa waume watoto na watu wazima ni mchezo wa mpira. Pesa, juhudi, wakati, akili, wataalamu kutumika kuhakikisha kuwa mchezo huu unawashughulisha wanadamu wote duniani, usiku na mchana na wasijielewe kuwa wanaathirika na wanaathri jukumu lao la kushindana na shetani ili Tawhiid itawale maisha yote ya mwanadamu. 

Fikiria jinsi "WORLD CUP" ilivyoathiri akili za watu na kwa lengo gani? Faida gani imepatikana, ila ni pumbao tu la akili. Sikiliza jinsi Qur-an inavyosema juu ya hilo". 

"Kwa hakika watu hawa wanayafadhilisha (wanayapenda) maisha ya kidunia na wanaacha nyuma yao (hawashughulikii) siku nzito (ya Akhera inayowangojea)" – Surah Addahir (76:27) 

Na Allah anamkumbusha mtu makini kwamba dunia hii haikuumbwa kwa mchezo tu, bali kwa lengo maalum. Qur’an inasema: 

"Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake kwa mchezo. (Na) kama tungalitaka kufanya mchezo, tungejifanyia sisi wenyewe. (Tusingekutieni humo) kama tungekuwa wafanyao mchezo" – Surah al-Anbiyaa (21:16-17). 

Mchezo huu wa mpira si haramu katika sharia, lakini itafikia hadi yakuwa makuruhu na haramu hasa endapo mtu atapoteza wakati wake wote kwa kushughulikia mpira peke yake na kuacha yaliyo muhimu na ya lazima kuliko huo mpira. 

Pumbao jingine ambalo maadui wa Twhiid wangependa watu makini wapumbae na kujipumbaza ili wasifikiria yaliyo muhimu maishani; ni nyimbo za aina zote, hasa zile zinazotumia mazumari, magitaa,matarumbeta, makengele na vyuma vya namna mbalimbali. 

Nyimbo za taarabu, nyimbo za regae, ambazo tayari zimeregeza miili na akili za watu wengi, watoto kwa watu wazima; nyimbo za dansa, nyimbo za aina aina katika madisco, mchiriku, lelemama, msondo, mdundiko na magoma mengine yasiyokuwa haya. Lakini nyimbo hizi zinazozalishwa huko Ulaya zina msukumo mkubwa kwa vile zimetengenezewa viambajengo vyake vinazozifanya ziwe maalum (special). Hizo ndizo zinazotukiwa katika "fashion shows" (maonyesho ya mitindo ya mavazi), ndizo zinazotumika katika "beauty shows" (maonyesho ya urembo), ndizo zinazotumika kwenye "send off parties" (hafla za kuagana) na ndizo zenye kutumika katika sherehe nyingi nyingine. Na aghalabu huambatana na vinywaji vikali vya pombe mvinyo, bangi na kadhalika. Hizi ndizo zinazotengenezewa video za kujifunzia mitindo mbalimbali ya rumba, samba, ragae, calypso, soal, ndombolo, na mingineyo mingi. 

Akili za vijana wasichana akina baba, akina mama zimezubaishwa, zimepumbazwa na kuzembea kwa mvuto wa ajabu wa nyimbo na ngoma hizo za Shamkwa re, Ikibinda,kiasi ambacho hakuna arusi au sherehe au hafla ya Waislamu na hata "Masheikh" itafanyika ikose mitimbwiliko hiyo. Ni ajabu ya kusimulia! 

Karibu kabisa na pumbazo la akili za Waislamu na hili la nyimbo na magoma ni "makasino" (casino) ambayo ni "night clubs" (majumba ya starehe ya usiku). Ndani ya majumba haya huwekwa ulevi wa kila aina katika vinywaji, michezo ya kamari iliyotengenezewa mashine maalum za kisasa zenye rangi aina-aina zivutiazo macho, na michezo ya "strip-tease" (wanawake/wanaume kuvua nguo moja, baada ya nyingine hadi kubakia utupu kabisa), inayoambatana na muziki mbele ya watazamaji. Humo pia kuna makatalogi (vitabu vya bidhaa) ya sura za wanawake toka pande zote za dunia walioajiriwa spesheli na wamiliki wa "casino" hiyo ambao mwanaume huchagua na kulipa pesa ili akutananishwe na mwana-mama huyo katika vyumba ambavyo vimetengwa spesheli. 

Huu ndio unaoitwa ustaarabu na utamaduni wa kisasa. Hizi ndizo starehe za ‘‘wakubwa’’ Starehe za wenye pesa, starehe za kuondoa uchovu na kuburudisha akili! Ni ajabu ya kusimulia. 

Ni Mwislamu gani aliye makini atakayepitisha usiku wake katika starehe hizi abaki na fikra za kujikomboa kutoka utumwa wa kifikra kutoka kwa maadui wa Tawhiid? 

Mambo yote yaliyotajwa hapo juu ni kinyume kabisa na maisha safi ya utulivu na amani ya kiuch-Mungu ya Kiislamu. Angalia jinsi Qur-an inavyosema: 

"Na katika watu wako wanaokhitari (chagua) (kutunga) maneno ya upuuzi (nyimbo) ili wawapoteze (wawapumbaze) watu (wengine) njia ya Allah (s.w.); pasipo wao kujua lolote, na wanaicheza sherehe (wanaipuuza) hiyo njia ya Allah (s.w.). Basi hao (ndio) watakaopata adhabu ifedheheshayo (hapa duniani na Akhera.).Surat Luqman (31:6). 

Pia katika aya nyingine ya Qur-an anawaeleza na kuwatambulisha ni akina nani watakaofuzu huko Akhera. Qur-an yasema: 

"Hakika wamefuzu Waislamu. Ambao katika swala zao huwa ni wanyenyekevu. Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi (ngonjera za nyimbo). Suratul Muuminun (23:1-3). 

Soma kwa kurejea pia Suratul Qasas (28:55) aya inayobainisha kwa uwazi kuwa walioamini (Waislamu) wanatakiwa kujitenga na maneno ya"Laghwa" (upuuzi wa porojo, nyimbo, vichekesho n.k.), na kwamba wasijibizane na wenye kusema upuuzi huo. 

Baada ya kufanikiwa kuwazuga na kuwatia kwapani Waislamu kwa mapumbazo ya namna hii na mengine ambayo hatuna nafasi ya kuyataja hapa; maadui wa harakati za wanatawhiid sasa wakazua mbinu ya kuwahofisha Waislamu na wasio waisilamu juu ya Zimwi liitwalo "Fundamentalism". 

Kambi hii ya uadui dhidi ya Uislamu wa kimsingi imeandaa na kupika ‘jungu’ la propaganda juu ya kuwako kwa Waislamu wanaoitwa "Fundamentalists".Na wakawapakaza kila aina ya rangi mbaya ili wasipendeze machoni wala masikioni mwa watu. 

Ni nani hawa "Fundamentalists?" Hawa ni wanatawhiid katika tafsiri sahihi ya Kiislamu. Ni wacha-Mungu wanaoamini kuwa Allah (s.w.) ameleta Qur-an Takatifu kuwa ni mwongozo uliokamilika wa maisha ya mwanadamu. Na wanaamini kuwa Muhammad (s.a.w.) ndiye Mtume wa kweli, ni kigezo na mfano wa kweli na ni wa mwisho kuja kukamilisha ujumbe wa Allah (s.w.) kwa walimwengu wote. 

Na Wanatawhiid hawa wamechagua kuwa wanaharakati ili wailinganie dini ya Allah (s.w.) kwa walimwengu wote. Na endapo Da’wah yao itafanikiwa, wasimamishe Ufalme wa Allah duniani kama ulivyo huko Mbinguni. Nao wanafanya hivyo kwa kuitikia mwito wa Allah (s.w.) alioutoa katika Qur’an Takatifu aliposema: 

"Enyi mlioamini rukuuni (swalini) na sujuduni na mwabuduni Mola wenu na fanyeni mema, ili mpate kufaulu. Na piganieni dini ya Allah (s.w.) kama inavyostahiki (kupiganiwa). Yeye (Allah) amekuchagueni (muwe umma ulio bora) wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika dini (ambayo) ni mila ya baba yenu (Nabii) Ibrahim; yeye (Allah) alikwisha kuiteni: Waislamu, tangu (katika vitabu vya zamani) huko. Na katika hii (Qur-ani) pia (mumeitwa hivyo). Ili mtume awe sahidi juu yenu na ninyi muwe mashahidi juu ya watu waliotangulia. Basi simamisheni swala na toeni zake na shikamaneni pamoja (ulimwengu mzima) kwa ajili ya Allah. Yeye ndiye Mola wenu. Mola mwema alioje, na msaidizi mwema alioje!" Saratul Haj (22:77-78) 

Waislamu wacha-Mungu hawa wanaamini kuwa huu ndio ujumbe wa msingi wa kushika na wa kufanyia kazi kwa vitendo. 

Maneno haya yanatakiwa yafasiriwe kwa vitendo ndipo yatakapozaa faida zilizokusudiwa na ujumbe wenyewe. Istoshe Wanatawhiid hawa wanajua kwa yakini kuwa mwongozo wa Quran Takatifu hauna shaka yoyote. Ni ukweli na hakuna ukweli mwingine wowote zaidi yake. Mwongozo huu wa Quran Takatifu ukifuatwa kikamilifu kwa kuzingatia mafunzo ya Sunnah sahihi za Mtume Wake Muhammad (s.a.w.), basi Waislamu wanayodira ya maisha. 

Misingi thabiti ya utatuzi wa matatizo ya mwanadamu katika maisha yake ya kiroho, kimwili, kiuchumi, kisiasa, kijamii, kiutamaduni, kielimu, kisaikolojia, kimaendeleo yote yamo ndani ya mwongozo huu thabiti. 

Sambamba na kutambua hilo; Waislamu wacha-Mungu ambao ndio wanatawhiid na wanaharakati halisi; hufanya juhudi kujenga mazingira ambayo yatawezesha kuenea kwa mfumo sahihi wa maisha ulimwenguni kote, bila kujali mipaka ya kijiografia, mabara (continents), rangi za ngozi za watu, lugha zao au tamaduni zao. 

Waislamu wanaruhusiwa kufanya hivyo kwa kauli ya Allah (s.w.) katika Quran Takatifu isemayo:- 

:Basi pigana katika njia ya Allah. Hukalifishwi ila nafsi yako (uwezo wako). Na wahimize Waislamu (waende) huneda Allah akauia mashamulio ya waliokufuru. Na Mwenyezi Mungu ndiye mkali wa kushambulia na mkali wa kuadhibu". Suratun Nisaa (4:84). 

Inaendeleao toleo lijalo. 

  
Juu 
 

YALIYOMO
 
TAHARIRI  

Maoni yetu: Wananchi kataeni kupotoshwa 

SUALA LA MWEMBECHAI: Wabunge wataka kujua nani aliamrisha kuua 
Na Mwandishi wetu  

Katiba ya nchi yapuuzwa: Waislamu wapigwa marufuku kuhubiri  

Mtihani darasa la saba 1998: Manispaa Moro yaagiza ipewe majina ya wanafunzi Wakatoliki 
Na Rajab Rajab, Morogoro 

 “Wushu”ya Waislamu wa China na jinsi ilivyowasaidia kupambana na dhulma dhidi yao 
Na MUSSA ALLY  

Yesu wa kwenye Mathayo siyo Yesu wa kwenye Luka 
Na. Masoud Mohammed 

Ni nani hawa Waislamu wa Siasa Kali ? 
Na USTADH  A.S. FUNDI  

Waislamu tuondokane na unyonge 
Na Abubakar Marwilo 

Maisha ya ndoa kwa Mwislamu 

Waislamu wana mwelekeo wao 
Na Sheikh Pandukizi Dilunga 

Ni mwaka gani Yesu alianza kuitwa Mungu 
Na MCHUNGAJI A.T. MANONI  

Wanawake wameamua kuwa wazi kweli kweli 
Na Bi. Fatma Musa 

Kimya kingi kina mshindo mkuu: Vipi Mhe. Rais wale walioua? 
Na Mussa Ally 

Mtazamo wa madhalimu wa Tanzania kwa Waislamu 
Na Rajab Isa 

Aliyoyasema KK bungeni 

Waislamu mkoa wa Morogoro wampinga Yahya 
Na. Abu Adli  

Polisi wachafua mazingira ya msikiti wa Mwembechai 
Na Badru Kimwaga 

Wanawake wa Kiislamu Ubungo darajani wamuunga mkono Sheikh Bafadhil 
Na Kassim Juma 

Barua za wasomaji  

Mashairi  

Mafundisho ya Qur'an: Kanuni za kumkumbuka Allah na kutumia katika njia yake 

Masomo  

Chakula na lishe: Lishe ya mtoto aliyekuwa mgonjwa 
Na Mujahiid Mwinyimvua 
  

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita