AN-NUUR
Na.158 Rabi' Awal 1419, Julai 17 - 23, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Wanawake wameamua kuwa wazi kweli kweli

Na Bi. Fatma Musa 

KWA kawaida katika nchi yoyote ile kila awamu ya uongozi inakuwa na sera zake, ambazo zinaiongoza awamu hiyo. 

Katika nchi yetu ya Tanzania ambayo siasa yake ni ya ujamaa na kujitegemea tokea nchi yetu ipate uhuru mnamo mwaka 1961, mpaka sasa zimefika awamu tatu za uongozi na kila awamu imekuwa na sera zake. 

Katika awamu ya kwanza ya uongozi, sera yake ilikuwa ya uhuru wa kila mtu kutoa mawazo yake. Kwa bahati mbaya, kila aliyejaribu kutoa mawazo yake kama yalipingana na Rais (Mwalimu Nyerere) basi mtu huyo aliishia kizuizini. Kwa maana hiyo uhuru huo ulikuwa ni kiini macho. 

Katika awamu ya pili, uhuru wa kutoa mawazo uliendelezwa na ulikuwa uhuru wa kweli kila mtu alikuwa huru kabisa, watu walitoa mawazo yao, hata yaliyomkosoa Rais. 

Na uhuru huo uliheshimiwa sana. Napenda kumpongeza kiongozi wa wamu hii kwa hilo. 

Katika awamu ya tatu, hii tuliyonayo, sera yake kubwa ni uwazi na ukweli. Lakini kwa kweli sera hii haitekelezwi hata na viongozi wa nchi wenyewe. Mambo mengi yamekuwa yakitokea na kunyamaziwa kimya au kuelezewa visivyo. Je, huu ndio uwazi wenyewe? 

Katika siku za karibuni limetokea suala la Mwembechai, Waislamu wameuawa na wengine wametiwa vilema. Pamoja na wananchi kutaka kujua kulikoni (nini sababu hasa ya tatizo hilo) serikali hadi leo hii imenyamaza kimya. 

Tume ya uchunguzi haijaundwa na hakuna lolote linaloendelea. Hii ina maana kuwa uwazi umewashinda na sera hii imeshindwa kufanya kazi. 

Kwa habati mbaya wanawake wa Tanzania wameielewa vibaya sera hii na wameamua kuitekeleza ipasavyo, hivyo wameamua kuwa wazi kabisa, kwa kuiacha miili yao wazi na hata kuuza miili yao wenyewe. 

Katika historia ya nchi yetu, tukirejea nyuma tunaona wanawake katika zama hizo ilikuwa ni jambo la ajabu kumuona mwanamke sehemu zake za mwili, kama mapaja yake, sehemu za tumbo n.k.. 

Lakini hivi leo, hasa katika awamu hii ya tatu, si jambo la ajabu kumuona mwanamke akiwa nusu na robo uchi, hii inaonyesha kuwa wanawake wameamua kuwa wazi na wawazi kweli kweli hata wa miili yao. 

Na hii ndio inayosababisha matatizo katika jamii yetu kama ya uzinifu, ubakaji n.k. Na kama hili halitaangaliwa na kutafutiwa ufumbuzi, hali itakuwa mbaya zaidi. 

Linalosikitisha zaidi ni kuwa, hata wanawake wa Kiislamu wameingia katika mkumbo huo na wao wameacha mafundisho ya dini yetu tukufu (24:31), (33:59) na kuifuata sera hii ya uwazi. 

Na hali hii kama haitabadilika hali itakuwa mbaya zaidi kwa kuwa wanawake wa Kiislamu wameacha mwongozo wao waliopewa na Mola wao. 

Mwisho napenda kuwakumbusha wanawake wenzangu wa Kiislamu, wasidanganywe na propaganda za makafiri za kuwa ukivaa hijjab unakuwa nyuma ya wakati . Na wafahamu kuwa, Uislamu ndio dini pekee inayokwenda sambamba na wakati. 

Tushikamane na Qur’an na mafundisho ya Mtume (s.a.w) ili tuweze kuokoa jamii yetu na maangamizi yanayoielekea. 

Juu
  

Kimya kingi kina mshindo mkuu

Vipi Mhe. Rais wale walioua? 

Na Mussa Ally 

"TIME has come to separate the men from the boys". Men go to war, boys go to school. Hiyo ni kauli ya shujaa katika ukweli marehemu Kighoma Malima akiuarifu umma kuwa wakati umefika wa kuwajua wanaume na watoto. Wanaume waende vitani, watoto waende shuleni. 

"Freedom is coming tomorrow", naye Leleti Khumalo maarufu "Sarafina" anasisitiza katika "The sound of freedom" akitupa moyo kwamba uhuru wa kweli hauko mbali kinachosubiriwa ni wakati kutoa majibu. 

Kabla sijaenda mbali ningependa kuyarejea matukio ya hivi karibuni ya mauaji ya kutisha na ya kinyama ya Mwembechai ambapo baadhi ya Waislamu walionusurika wamebakiwa na ulemavu wa kudumu. 

Kisha cha raia hao mahashumu kulemazwa kuuawa kikatili na hata kuning’inizwa jela ni kukataa Uungu wa Yesu! 

Wakati huo huo muuaji (serikali ya CCM) anadai kuwa eti hana dini! 

Sehemu ya mauaji ni katika nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu (Msikiti)! 

Mara baada ya kadhia hiyo chafu kabisa kuwahi kutokea nchini katika miaka hivi karibuni, viongozi waliibuka na hotuba za kejeli, dhihaka, matusi na vitisho dhidi ya Uislamu na Waislamu. 

Miongoni mwao ni Makamu wa Rais, Dk. Omar Ali Juma, Waziri Mkuu Mhe. Frederick Sumaye, Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Ali Ameir Mohamed, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Yusuph Makamba na wengineo ambao walidiriki kuwafananisha Waislamu na Uislamu wao na uhuni, wizi wa bia, vichwa ngumu, utukanaji na matusi mengine makubwa kuliko ya nguoni. 

Walitumia ndimi zao kudhalilisha kundi moja katika jamii. 

Nikiachana na waheshimiwa bosi Mhe. Rais Benjamin William Mkapa. Je, amechukua hatua zozote za msingi kuwashughulikia wauaji? Jibu liko wazi, hapana. 

Na kwa nini hajafanya hivyo hadi sasa? Au machoni pake Waislamu si chochote? Au ni sawa na swala, kongoni, pofu, mbogo au pundamilia porini? 

Na kama sivyo ninalo swali la kuuliza, iweje asiunde tume ya uchunguzi hadi sasa, anasubiri nini? 

La mgambo limelia, ukombozi utakuja kesho kama si jioni ya leo. 
Juu
  

Mtazamo wa madhalimu wa Tanzania kwa Waislamu

Na Rajab Isa 

Katika gazeti moja toleo litolewalo kila Julai 4, 1998, lilichapisha habari inayoongoza mbele kwa kichwa kikubwa kisemacho, "Baada ya Msikiti wa Mwembechai kuwa shwari…. Vurugu za Waislamu zaibuka Kigoma." 

Kwa kuwa tumeona na tumejifunza kwa ushahidi wa kutosha kuwa katika mapambano yaliyopo nchini kati ya Serikali na Waislamu, vyombo vya habari hutoa mchango wake mkubwa dhidi ya Waislamu na hivyo kwenda sambamba katika kufaulisha mipango ya kudhoofisha Waislamu kwa kupakazia,kuchochea, kuzushia, na kukuza jambo ili kutoa picha mbaya ni vizuri nidokeze kidogo hilo kwa kigezo cha tukio la Kigoma. 

Gazeti linatuambia "Baada ya Msikiti wa Mwembechai kuwa shwari… vurugu za Waislamu zaibuka Kigoma." 

Ni jambo maarufu kwa Watanzania wote kuwa yaliyotokea Mwembechai na Waislamu kuuwawa ni baina ya serikali na Waislamu. 

Aidha, mvutano uliotokea Msikiti wa Kitongoni Ujiji ni baina ya waumini kwa waumini. 

Kwa chombo kinachotoa habari kwa nia njema uhusiano wa kitukio, Kigoma na Mwembechai uko wapi hapa? 

Katika gazeti hilo hilo toleo Na. 1647 la Julai 7, 1998, makala inayoongoza ukurasa wa mbele mwandishi anatoa fatwa kwa kuwaandikia wasomaji kuwa Mtume Muhammad (ambae ni kiongozi wa Waislamu) ndie muasisi wa dini hiyo ya Kiislamu. 

Hakika muasisi wa dini yaKiislamu ni Mwenyezi Mungu na Muhammad (s.a.w.) ni mjumbe alieletwa kuhuisha imani hiyo ya kale. Dini ya Uislamu imetoka kwa Mwenyezi Mungu na Mitume kama Isa (Yesu), Ibrahim, Musa, Daudi, Suleman na wengine ni Mitume waliofundisha na kutangaza imani hiyo kabla ya kuja Muhammad. 

Imani hii inayoitakidiwa na mamilioni ya Waislamu ni maarufu kote duniani na ndivyo ilivyo katika Qur-ani Tukufu. 

Hivi Mhariri wa gazeti hilo analifahamu bali kwa nia ile ile ya kupakazia, kudhoofisha, kutengeneza uwanja wa mapambano na Waislamu huku akiamini analo gazeti atakaloandika vichwa vikubwa "vurugu za Waislamu sasa zahamia katika vyombo vya habari" ndio maana anaandika bila ya woga kuwa Uislamu ni dini iliyoanzishwa na binadamu. 

Ama nikiwakumbusha Waislamu wenzangu juu ya Serikali ya Tanzania inavyotuangalia Waislamu kama maadui na mahasimu wake wakuu, ni jinsi serikali hii ilivyoazimia kutumia kila mwanya kuwaangamiza Waislamu. 

Katika tukio hili la Kigoma, mwandishi wa gazeti la "Majira" toleo Na. 1645 la Julai 5, 1998 anasema, walipomuhoji kamanda wa Polisi wa Mkoa, Bw. Pius Chaka jinsi alivyofahamu tukio hilo aliwaambia. "….baadhi ya Waumini wa dini hiyo (Waislamu) walitangaza hadharani kumzuia Sheikh wa Mkoa wa Kigoma Tofiki Malilo kuhutubia sala ya Ijumaa." 

Alipohojiwa kuhusu jinsi ya kulishughulikia, aliwaambia waandishi, "….matamshi ya waumini hao yalisababisha Polisi kuandaa kikosi chakutuliza ghasia (FFU) ili ruvugu zikitokea zidhibitiwe." 

Hivi ndivyo Serikali ya Tanzania huyakabili mambo ya Waislamu. Yaani kamanda wa Polisi wa Mkoa kusikia tu watu mitaani wakisema "Tutamzuia Sheikh wa mkoa kuhutubu" yeye tayari alikwishaandaa magari, mabomu ya gesi, virungu na paredi zito kwa vijana wa FFU watakao kwenda Msikitini kuwakabili Waislamu. 

Gazeti hilo toleo Na. 1644 na toleo Na.1647 linatwambia, kamanda Pius alifanikisha maandalizi na FFU wamekuwa wakitembeza mikong’oto Msikitini Kigoma na kuwafyatulia mabomu Waislamu. Hatua hizi za polisi hapa nchini huzikuta kwa watu wa imani nyingine ispokuwa kwa Waislamu tu. 

Hivi karibuni Wamasai Arumeru walipinga hadharani ongezeko la kodi na kuashiria mapambano ya umwagaji damu. Wakazusha vurugu kubwa kwa kuwapiga wenziwao waliokiri kulipa kodi hiyo na hatimaye kuchoma moto nyumba ya mwenyekiti wao na kuharibu mali nyingi. 

Zaidi na hayo wakiwa na silaha huko Arusha walitanda mitaani wakiwapekua na kuwaweka makumi ya wananchi chini ya ulinzi mkali 

Polisi walitumiwa salamu za vifo endapo watathubutu kuwakabili kwa kile walichodai wana haki ya kuwapiga na kuwatesa wale waliowatuhumu na kuwakamata. 

Pamoja na kuwa yote haya yalitendwa hadharani hapakuwa na mabomu yaliyolipuliwa, virungu wala vijana wa FFU waliotoa mkong’oto kama inavyokuwa halali kwao kwa fursa zinazotokea misikitini kupewa kozi ya matumizi ya silaha kwa kuwadungua risasi Waislamu. 

"Ukweli na uwazi" ukajitokeza hapa. Serikali ikamng’oa Waziri tena waziri mkubwa toka Dar es Saaam mpaka Arusha aende akawabembeleze Wamasai na kuwapa semina. 

Bila shaka semina hiyo ilikuwa ni kuwaelimisha kuwa risasi zilizopo ni chache zinawatosha wale wa Misikitini tu. 

Hapa utaona picha ya wazi ya matabaka na hakuna tabu kujua tabaka ambalo serikali imelifanya kuwa hasimu wake mkubwa. 

Ni kwa sababu ya uhasimu huo ambao chanzo chake ni Waislamu kudai usawa na haki ndio maana leo hii majeshi ya Tanzania yamekuwa yakiwapiga risasi na kuwaua Waislamu na kisha viongozi wakuu wa Serikali kutoa motisha wa pongezi kwa vijana waliofuzu shabaha. Na kuwaongezea muda kina Gewe walipaswa kustaafu. 

Waislamu kama raia wengine, tulikuwa na kila sababu ya kutegemea Serikali itusikilize, itulinde sisi, Maimamu, Masheikh, Bibi zetu, Mama zetu, Babu zetu, Baba zetu, Dada zetu, watoto wetu, ibada zetu na misikiti yetu. Lakini vyote hivi tulivyovitaja leo hii ndio sehemu ya majaribio kwa askari wa Tanzania. 

Lazima tufahamu suala la kuwanyamazisha Waislamu kwa kumwaga damu yao ni agenda kubwa ya wababe wa dunia na serikali ya Mkapa bila shaka inaowajibika katika hilo. 

Katika hali ya "uwazi na ukweli" wanaotendewa Waislamu Tanzania sidhani kama kuna kijiji, Tarafa, Wilaya au Mkoa ambako Waislamu bado hawajaweka mikakati madhubuti ya kujilinda na kujihami. 

Hivi karibuni huko Bosnia, Waislamu wenzetu yalipoanza kama haya ya Mwembechai, walizubaa kama sisi tunavyojipa matumaini ya uongo wakidhani polisi wa makafiri wanafanya masikhara. 

Matokeo wakawa wakivamiwa majumbani, misikitini wakiwaua kama kuku. 

Lakini walipotanabahi na kutumbua nyongo, Mwenyezi Mungu aliwapa mgao wa silaha kutoka katika zile walizobeba majeshi ya "Uwazi na Ukweli"ya Bosnia na akawapa ushindi uliowashangaza wenyewe na mataifa ya nje. 

Ni vizuri tujikumbushe baadhi ya aya za Qur-an tukufu tupate yaqini na hatua anazotuelekeza Mola wetu kukabilianana dhulma. 

"Basi vyote mlivyopewa ni starehe ya maisha ya dunia tu, lakini kilichoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora na cha kudumu (milele). Watakistahiki wale walioamini…. Ambao jeuri inapowafika huzitetea nafsi zao." (42:36/42:39.) 

"Na malipo ya ubaya ni ubaya ulio sawa na (ubaya) huo,….. Na wale wanaolipiza kisasi baada ya kudhulumiwa hao hakuna njia ya kulaumiwa. Bali lawama iko juu ya wale wanaodhulumu watu na wakawafanyia jeuri katika ardhi pasipo haki; hao ndio watakaopata adhabu iumizayo." (42:40-42.) 

"Popote mlipo mauti yatakufikieni na hata mkiwa katika ngome madhubuti… Basi msirejee na kutaka suluhu (piganeni na maadui zenu) maana nyinyi ndio mtakaoshinda; na Mwenyezi Mungu yu pamoja nanyi; wala hatakunyimeni (matokeo) ya vitendo vyenu. 4"78/47:35. 

Hapa Mwenyezi Mungu anapinga watu kuwakalia kichwani watu wengine. Anaagiza watu wajikinge na dhulma kwa kutetea nafasi zao kadiri ya nguvu walizopewa. 

Anasisitiza kwa wale wanaodhulumiwa kuwa hakuna njia ya amani na utulivu kwa dhalimu dawa ya moto ni moto walipize kisasi. Anawashangaa waoga wanaopigwa shavu la kulia wanageuza kushoto kwa kuwaambia mauti hayaji kwa kujitetea tu bali hata wakiwa katika ngome madhubuti roho zitang’o’a nauchungu ni ule ule au zaidi. 

Mwisho anawaambia Waislamu kuwa, madhalimu wakishaonja damu yao hawataacha wataendelea basi Waislamu waondoe dhana ya suluhu, amani na utulivu, wapigane, Mwenyezi Mungu atakuwa pamoja nao katika midani ya kutetea haki na uhuru wao. 

Kwa mantiki ya ujumbe wa aya hizi za Mwenyezi Mungu utaona "Intifada" pekee ndio dawa ya kukomesha dhulma na si vinginevyo. Tusipojenga ufa kwa malighafi ya "Intifada" anayotupa Mwenyezi Mungu, basi kingine cha kujengea ukuta hatutakipata. Nchini hapa hakuna haki wala sheria. "Sheria" ziko kwa ajili ya kulinda wakubwa na raia vipenzi wao. Muislamu huna chako. 
 

Juu 
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI 

Maoni yetu: Wananchi kataeni kupotoshwa

SUALA LA MWEMBECHAI: Wabunge wataka kujua nani aliamrisha kuua
Na Mwandishi wetu 

Katiba ya nchi yapuuzwa: Waislamu wapigwa marufuku kuhubiri 

Mtihani darasa la saba 1998: Manispaa Moro yaagiza ipewe majina ya wanafunzi Wakatoliki
Na Rajab Rajab, Morogoro

 “Wushu”ya Waislamu wa China na jinsi ilivyowasaidia kupambana na dhulma dhidi yao
Na MUSSA ALLY 

Yesu wa kwenye Mathayo siyo Yesu wa kwenye Luka
Na. Masoud Mohammed

Ni nani hawa Waislamu wa Siasa Kali ?
Na USTADH  A.S. FUNDI 

Waislamu tuondokane na unyonge
Na Abubakar Marwilo

Maisha ya ndoa kwa Mwislamu

Waislamu wana mwelekeo wao
Na Sheikh Pandukizi Dilunga

Ni mwaka gani Yesu alianza kuitwa Mungu
Na MCHUNGAJI A.T. MANONI 

Wanawake wameamua kuwa wazi kweli kweli
Na Bi. Fatma Musa

Kimya kingi kina mshindo mkuu: Vipi Mhe. Rais wale walioua?
Na Mussa Ally

Mtazamo wa madhalimu wa Tanzania kwa Waislamu
Na Rajab Isa

Aliyoyasema KK bungeni

Waislamu mkoa wa Morogoro wampinga Yahya
Na. Abu Adli 

Polisi wachafua mazingira ya msikiti wa Mwembechai
Na Badru Kimwaga

Wanawake wa Kiislamu Ubungo darajani wamuunga mkono Sheikh Bafadhil
Na Kassim Juma

Barua za wasomaji 

Mashairi 

Mafundisho ya Qur'an: Kanuni za kumkumbuka Allah na kutumia katika njia yake

Masomo 

Chakula na lishe: Lishe ya mtoto aliyekuwa mgonjwa
Na Mujahiid Mwinyimvua
 

 

 

 

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita