AN-NUUR
Na.158 Rabi' Awal 1419, Julai 17 - 23, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Waislamu wana mwelekeo wao

Na Sheikh Pandukizi Dilunga 

MHESHIMIWA Kapuya amedai kwamba Waislamu hawana mwelekeo. Ni Waislamu gani wasio na mwelekeo? Ni wale wanaoongozwa na Bakwata na kupendwa na "Waheshimiwa na Maprofesa na Madokta" kwa kuwapa viti vya mbele katika hafla zao, au ni wale wanaoipinga Bakwata na kuchukiwa na Waheshimiwa, Maprofesa na Madokta? 

Kusema Waislamu wamekosa mwelekeo ni makosa, kwa sababu kila binadamu (kiumbe) ana mwelekeo (utaratibu/dini) wake wa maisha. Waislamu mwelekeo wao ni Uislamu ambao umebainishwa ndani ya Qur’an Tukufu na Hadithi za Mtume (s.a.w) – (Qur’an 3:19). 

Katika mwelekeo huo, Waislamu wanatakiwa wamtii Allah (s.w) katika nyanja zote, ikiwa ni pamoja na siasa, uchumi, elimu, afya, ustawi wa jamii n.k. Na wale wasio na mwelekeo huu ni makafiri nao pamoja na mbwembwe zao hawatafanikiwa (Qur. 3:85). 

Ili kuiweka wazi mielekeo hii, tuyachambue makundi haya yafuatayo: 

BAKWATA: Tangu ilipoanzishwa, haijajenga jengo la shule/Msikiti/Madrasa/Hospitali n.k. zaidi ya majengo waliyopora kwa Waislamu. 

1970 Bakwata ilifanya mkutano wa Masheikh wote wa Tanzania. Moja ya maazimio yaliyotolewa, ni kuandaa Muhtasari (syllabus) wa elimu ya msingi ya dini ya Kiislamu. Mpaka sasa hakuna hata kitabu kimoja walichoandika kinachokwenda sawa na Muhtasari huo. 

1990 walitangaza katika gazeti la Muislamu Na. 33 Uk. 8 kuwa pembeni ya shule ya Jumuiya Sec. School – Tanga watajenga Chuo cha elimu ya juu ya Dini ya Kiislamu nchini ambacho kingeitwa Tanga Muslim Academy. Mpaka sasa ni mwaka wa nane hata msingi haujachimbwa! 

Walikuwa na gazeti liitwalo "Muislamu", ambalo baadaye walilibadilisha jina na kuliita "Safina". Hivi sasa hiyo Safina imezama katika "Bahari ya fitna isiyo na mwelekeo". Wasemaji wakuu wa Bakwata hivi sasa wanaropoka kwa "kutoa saa 24 kummaliza KK" katika magazeti ambayo mwelekeo wake ni kuandika kwa kuipamba kila habari inayoudhuru Uislamu, na kupotosha kila habari inayounufaisha Uislamu. 

Katika hafla zao zote, ziwe za Maulid, Baraza la Maulid, swala za Idi, Baraza la Idi, ufunguzi wa Misikiti wanayopora kwa Waislamu n.k. Nafasi ya "mgeni wa heshima" huwapa Maprofesa/Madokta/Waheshimiwa, ambao wengi huwa hawana elimu sahihi inayohusiana na hafla hizo. Kwa hiyo, huwa hawana la kusema zaidi ya kutoa "matamko ya serikali" ambayo mwelekeo wake ni kuwaudhi Waislamu katika siku zao za furaha. Kwanini sherehe za kidini wageni rasmi wawe "kina Min Kum" tu? Je, serikali imeshawahi kutoa nafasi kama hiyo kwa Sheikh, Imamu, Ustadh au kiongozi yeyote wa taasisi ya dini ya Kiislamu katika hafla zao za kitaifa ili nao walihutubie taifa? 

Bakwata haina radio wala TV na zile za watu pia wanabana vipindi vyote vya dini ya Kiislamu visishikwe na Waislamu walio kinyume nao wakawafundisha Waislamu na jamii kwa ujumla usahihi wa dini ya Kiislamu kupitia vipindi hivyo vyenye muda mchache. 

Walifunga shule ya Al-Haramayn (taasisi) kwa muda mrefu, na kuwafanya wanafunzi wakose masomo kwamuda mrefu. Walipoifungua, waliwaruhusu Waalimu wawili tu kufundisha. Hata hivyo, mpaka sasa wameshafanyiwa vituko vya ajabu ikiwa ni pamoja na kuchomewa ofisi, kuwekewa vinyesi ofisini n.k. Haya na mengine mengi wanayofanya Bakwata, tunaomba Mheshimiwa Kapuya utueleze yana mwelekeo upi katika ile miwili. Je, ndiyo kuhurumiana huko? 
 

WAFUASI WA BAKWATA: 

Hawa ni wale Waislamu wa majina au wa ukoo. Na wengi katika hawa hupenda kujiita "waumini" na kama ni viongozi serikalini au katika taasisi, hupenda kujiita "Min Kum". Wanachofahamu wao ni kutia fitna ili mambo yenye maendeleo kwa Waislamu na jamii kwa jumla yasifanyike. Mfano ni ile shule ya msingi Arafat inayomilikiwa na Jumuiya ya Ansaar – Tanga. Waislamu "Min Kum" walitaka shule hiyo isijengwe eti kwa sababu iko karibu na shule ya msingi Msambweni. Lakini walisahau kabisa kwamba zipo shule mbili za serikali zilizokaribiana, shule ya Chuma na shule ya Masiwani. 

Mfano mwingine ni wa shule ya sekondari – Masjid Qubah ambayo ilikaa kipindi kirefu bila kusajiliwa kwa kuwa waasisi wake ni maadui wa Bakwata. 

Waislamu hawa ndio wanaoleta vurugu katika taasisi mbalimbali khususan Misikiti. Hugombania kuwa viongozi wa Misikiti na wanapokufa hurithi watoto wao! Je, hawa mwelekeo wao ni upi? Ndio kuhurumiana huko? 
 

WAHESHIMIWA: 

Mheshimiwa Rais: Amesema kuwa serikali yake ni ya uwazi na ukweli. 

Mpaka sasa hajatoa kauli kuhusu dhulma, mauaji na uvunjaji wa katiba uliofanywa na serikali yake dhidi ya Waislamu pale Mwembechai. Tunasikia katoa agizo kuwa wazee, watoto, wanafunzi, wanawake na wagonjwa waachiwe. Kwanini asitoe agizo hilo hadharani? Kwanini asikemee uzembe uliofanywa na watumishi wake waliosababisha vifo na kupooza kwa Waislamu? 

Kwanini alikataa kukutana na Waislamu kuzungumzia mauaji ya Waislamu Mwembechai, haliyakuwa walimuomba afanye hivyo? Je, Mheshimiwa Rais ana mwelekeo upi? Ndio kuhurumiana huko? Ndio uwazi na ukweli huo? Ndio kuwapenda Waislamu huko kama alivyosema msaidizi wake? 

Mheshimiwa Makamu wa Rais (msaidizi mkuu wa Rais – Taifa) na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa (msaidizi mkuu wa Rais – Mkoa): 

Waheshimiwa hawa wamekuwa wanatoa maneno ya vitisho, kashfa na dharau dhidi ya Waislamu. Wao ndio kikwazo kikubwa cha Waislamu kukutana na Rais. Walikuwa wageni waalikwa katika ufunguzi wa "Muhadhara halali" wa kumtangaza "Mungu wa Tanzania – Yesu" ambapo walishiriki kuruka ruka, kupiga makofi na kuimba pambio! 

Wao ndio kichocheo kikubwa cha magomvi ya Misikitini ambao wamejipachika cheo cha "Min Kum" na kulazimisha waumini wakubali viongozi wanaowataka wao, vinginevyo wanawapiga mabomu na kuwaita "wahuni" au "vibaka". Je, waheshimiwa hawa wana mwelekeo upi? Je, ndio kuhurumiana huko? 
 

MHESHIMIWA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: 

Yeye ndiye anayemiliki jeshi la polisi lililofanya uvamizi Msikitini na kupiga mabomu kisha kuingia na viatu Msikitini. Humo wakawadhalilisha wanawake, wakatesa, wakapiga na hatimaye kuwapeleka polisi. 

Yeye ndiye mwenye mahakama zilizowanyima watuhumiwa haki ya dhamana na kuachiwa watu kabla hawajaletwa mahakamani. 

Yeye ndiye mwenye Magereza mahali ambapo Waislamu waliteswa, kudhalilishwa kwa kuwekwa uchi na kupekuliwa na kutopewa dawa zinazolingana na maradhi yao. Humo ndimo kuna chakula kibovu kuliko kile anachokula bata katika mfereji wa choo. 

Kwa cheo chake hicho, kazuia utekelezaji wa "agizo la Rais" hadi Waislamu wakaathirika vibaya. Na waliotolewa, aliwatoa kwa shinikizo la hoja za Waislamu. Chakushangaza mpaka sasa bado anamshikilia Mzee Abdulrahman Kipochi ambaye pia afya yake siyo nzuri. Au yeye si mzee anayehusika na agizo la Rais la kuachiwa wazee? Mheshimiwa huyu ana mwelekeo upi kwa kuwatesa nduguze? Je, ndio kuhurumiana huko? 
 

MKUU WA JESHI LA POLISI: 

Mpaka sasa hajatoa kauli ya kuadhibiwa wadhalilishaji, watesaji, walionajisi sehemu ya ibada, walioua kama alivyofanya kwa wale askari walioua mzururaji Dar. Je, Mheshimiwa huyu ana mwelekeo gani? Ndiyo kuhurumiana huko? 
 

MHESHIMIWA KAPUYA: 

Ulisema kwamba Waislamu kukosa maendeleo tusimtafute mchawi. Sisi hatuna haja ya kumtafuta mchawi kwa sababu yuko wazi hakujificha, naye anafahamu kuwa tunamjua ndio maana tunapomwambia "wewe mchawi" hajibu kitu. 

Mchawi wetu ni Nyerere, naye amerithi mikoba ya huo uchawi wa kuudhuru Uislamu kwa wakoloni, na nyie Waheshimiwa ndiyo mnasaidia kutuchanja chale! 

Serikali haina dini lakini watu wake wakiwemo waheshimiwa wana dini zao. Kwa kujua hilo, ndio maana waheshimiwa wengi hutoa upendeleo wa pekee kwa watu wa imani zao. Mfano ni hiyo ofisi yako. Kila aliyekalia kiti hicho, alijitahidi kuwaendeleza nduguze kielimu. Hata Mheshimiwa Malima naye alifanya hivyo. Je wewe mwelekeo wako ni upi ili nduguzo wanufaike na nafasi yako? Je, unatuhurumia kwa kutusimanga bila kutupa miongozo ya kutuletea maendeleo? 
 

WAISLAMU: 

Waislamu kwa kufahamu mwelekeo wao, wamefanya mengi, mfano wamepigana vita mbalimbali na wakoloni ili kuwazuia wasiharibu mwelekeo wao. Wamepinga dira ya maendeleo mpaka 2025. Je, watu wasio na mwelekeo wangejua vipi kuwa Dira hiyo haiwafai Waislamu. 

Waislamu wamejenga shule nyingi zipatazo 141 kabla na baada ya uhuru. Nakutajia baadhi ya hizo, hapo ulipotoa kashfa kwa Waislamu katika Chuo cha Sanaa, kuna shule ya Mwanamakula. Zamani shule hii ilikuwa ya H.H. Agha Khan. Jumuiya Sec. School ya Tanga inayomilikiwa na Bakwata ambayo ilikuwa ikiitwa Muslim School. 

Shule ya msingi Lumumba iliyopo Lumumba St. na Aggrey St. zamani ilikuwa ikiitwa Al Jumiyyatul Islamiyaah. Nyumba ya Walimu ndiyo ofisi ya Bakwata Mkoa hivi sasa. Shule hii ilijengwa 1940. 

Mwanza St. kuna shule ya msingi Punja, zamani ilikuwa ikiitwa Punja Muslim School kutokana na heshima ya mfadhili aliyemalizia ujenzi wa shule hiyo aitwaye Habib Punja. 

1966 Waislamu walijenga shule karibu na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakaiita Boma Muslim School. Hivi sasa inaitwa Boma Pr. School. Barabara ya zamani ya Kigogo Waislamu walijenga shule wakaiita Kigogo Muslim, sasa inaitwa Kigogo Primary School (Rutihinda), shule ya msingi Uhuru Morogoro, ni Muislim School ilijengwa na Waislamu. 

Shule ya Kinondoni Muslim ambako kuna ofisi za Bakwata Makao Makuu, ilijengwa na Waislamu kisha ikaporwa na serikali na kuwapa Bakwata. 

Shule zote zilizoporwa, baadhi zinamilikiwa na serikali na baadhi zinamilikiwa na Bakwata. Shule zilizoporwa kwa wenzetu Wakristo, baadhi wamerudishiwa na baadhi zinamilikiwa na serikali lakini bado utaratibu ni wa Kanisa. 

Kwa mfano shule ya St. Joseph ambayo inaitwa Forodhani. Kanisa lipo pale pale, Mkuu wa shule ni Padri ambaye anaishi pale pale, sala zinaendelea kama zamani n.k. Hivi sasa imerejeshwa kwa Kanisa. 

Waislamu walipoona sasa ipo haja ya kuwa na elimu ya juu zaidi, waliitikia wito wa kujenga Chuo Kikuu hapa nchini. Wakatoa michango kama ilivyoonyeshwa katika AN-NUUR Na. 150 ukurasa wa 11 na Chuo kikajengwa. Wengi mnaitwa Maprofesa kwa kusoma chuoni hapo bila kukumbuka kuwa chuo hicho shemu kubwa ya gharama za ujenzi imetolewa na hao hao mnaowatukana kuwa hawana mwelekeo wala dira (Waislamu)! 

Je, tukilalamika kuwa tunaonewa tuna kosa gani? Mtu akilalamikia chake, sio kumwambia "usitafute mchawi" bali mpe haki yake. Kwahiyo, turudishieni shule zetu kama mnavyofanya zoezi hilo kwa Wakristo. 

Kama Wakristo walivyoahidi kuwapigia kura "wacha Mungu" (Wakristo) na Waislamu walifanya hivyo kwa kukuchagueni nyie Waislamu wenzao tena Maprofesa. Badala ya kufanya yale yatakayowainua Waislamu kwa kutumia hizo nyadhifa zenu ili mlipe fadhila ya kupata magari na mishahara minono, nyie mnashangilia yanayofanywa na Wakristo kupitia kwa Waheshimiwa wao wa Kikristo, na mnafanya hayo kuwa ndiyo kigezo chenu cha kuwatukana Waislamu kuwa hawana mwelekeo? Tulidhani Maprofesa na Madokta watu imara na wenye msimamo kumbe wachovu kweli! Mnazuia mihadhara ya dini yenu inayotangaza "umoja wa Mungu" na kuthibitisha "Utume wa Issa (Yesu)" kwa kuwaua, kuwadhalilisha na kuwaweka ndani ndugu zenu, na kuruhusu mihadhara ya Wakristo inayopinga "Umoja wa Mungu" na kuthibitisha "Uungu wa Issa (Yesu) kwa Watanzania" huku mnapiga makofi na kuimba pambio? Ama kweli waheshimiwa mmekosa mwelekeo. Na kama mnao mwelekeo, basi unakuelekezeni motoni! 

  
Juu 
 

YALIYOMO
 
 

TAHARIRI 

Maoni yetu: Wananchi kataeni kupotoshwa

SUALA LA MWEMBECHAI: Wabunge wataka kujua nani aliamrisha kuua
Na Mwandishi wetu 

Katiba ya nchi yapuuzwa: Waislamu wapigwa marufuku kuhubiri 

Mtihani darasa la saba 1998: Manispaa Moro yaagiza ipewe majina ya wanafunzi Wakatoliki
Na Rajab Rajab, Morogoro

 “Wushu”ya Waislamu wa China na jinsi ilivyowasaidia kupambana na dhulma dhidi yao
Na MUSSA ALLY 

Yesu wa kwenye Mathayo siyo Yesu wa kwenye Luka
Na. Masoud Mohammed

Ni nani hawa Waislamu wa Siasa Kali ?
Na USTADH  A.S. FUNDI 

Waislamu tuondokane na unyonge
Na Abubakar Marwilo

Maisha ya ndoa kwa Mwislamu

Waislamu wana mwelekeo wao
Na Sheikh Pandukizi Dilunga

Ni mwaka gani Yesu alianza kuitwa Mungu
Na MCHUNGAJI A.T. MANONI 

Wanawake wameamua kuwa wazi kweli kweli
Na Bi. Fatma Musa

Kimya kingi kina mshindo mkuu: Vipi Mhe. Rais wale walioua?
Na Mussa Ally

Mtazamo wa madhalimu wa Tanzania kwa Waislamu
Na Rajab Isa

Aliyoyasema KK bungeni

Waislamu mkoa wa Morogoro wampinga Yahya
Na. Abu Adli 

Polisi wachafua mazingira ya msikiti wa Mwembechai
Na Badru Kimwaga

Wanawake wa Kiislamu Ubungo darajani wamuunga mkono Sheikh Bafadhil
Na Kassim Juma

Barua za wasomaji 

Mashairi 

Mafundisho ya Qur'an: Kanuni za kumkumbuka Allah na kutumia katika njia yake

Masomo 

Chakula na lishe: Lishe ya mtoto aliyekuwa mgonjwa
Na Mujahiid Mwinyimvua
 
 

 

 

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita