NASAHA
Na. 060 Jumatano  Agosti 9 - 15, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
CCM yamtuhumu Mwenyekiti wake pandikizi 

Na Mustafa Said 

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kijiji cha Mdaula, Mzee Khalifa amesimamishwa kazi na uongozi wa wilaya wa chama hicho kwa kutuhumiwa kuwa ni pandikizi wa kambi ya upinzani.

Kwa mujibu wa mzee Khalifa, maamuzi hayo yalifikiwa Julai 27,mwaka huu, katika kikao kilichofanyika katika kijiji cha Mdaula kilichopo Chalinze, katika wilaya ya Bagamoyo ambacho kilihudhuriwa na Bw. Mokiwa ambaye ni Katibu wa CCM wa wilaya. 

Katika kikao hicho, Mzee Khalifa alitakiwa ajieleze kutokana na tuhuma hizo, ambapo alikanusha kutumiwa na kambi ya upinzani kuhujumu chama hicho tawala. 

Baadaye Mzee Khalifa alitakiwa atoke nje ya kikao ili wajumbe waweze kumjadili na ndipo kikao hicho kilipokubaliana kuwa Mzee Khalifa anahusika na tuhuma hizo na hivyo kumsimamisha uongozi. 

Wakati huo huo mgombea Udiwani katika kata ya Chalinze kupitia tiketi ya Chama cha upinzani cha CUF, Bw. Mbarouk Tamim, amesema kuwa ameanza kufuatilia kwa undani juu ya habari kwamba trekta la kijiji cha Mdaula limeuzwa na viongozi wa kijiji. 

Uongozi huo wa kijiji ambao ni wa chama tawala (CCM) umesema kuwa trekta hilo la aina ya VALMET limepelekwa gereji kwa ajili ya matengenezo. Lakini wanakijiji wanahisi kuwa trekta hilo limeuzwa na badala yake imenunuliwa mashine ya kusaga ambayo imefungwa katika kijiji hicho. 

Bw. Tamim amesema kuwa ameamua kufuatilia kwa undani suala hilo kwani liko ndani ya kata ambayo yeye anagombea udiwani kwa hiyo ni haki yake. 

Aidha, Bw. Tamim ameahidi kufuatilia aliyoyaita malalamiko ya wananchi wa kijiji hicho kuwa toka uongozi huo wa kijiji uingie madarakani haujawahi kufanya mkutano wowote kuwaeleza wananchi juu ya mapato na matumizi ya kijiji chao. 

Mgombea huyo wa udiwani ameongeza kusema kuwa mapato yanayopatikana katika kata yote ya Chalinze ni makubwa kiasi kwamba anashangaa kwanini viongozi wa kata hiyo wanashindwa kuwasaidia wazee ambao watoto wao wanashindwa kusoma kwa kukosa ada. 


Propaganda ya Udini itaisambaratisha nchi - CHADEMA 

Na Rajab Nkawa 

UDINI unaoimbwa na viongozi wa CCM na wale wasioitakia mema nchi hii dhidi ya kundi mojawapo la jamii hapa nchini unaweza kuhatarisha amani ya nchi iwapo kundi hilo litajiona kuwa halitakiwi kushika madaraka katika nchi kwa sababu ya dini yao.

Hayo yalisemwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Wilbroad Slaa alipokuwa akizungumza na wananchi wa Temeke katika mkutano wa hadhara wa kumtambulisha mgombea Ubunge wa Jimbo hilo kwa tiketi ya CUF Mhe. Richard Tambwe Hiza. Mkutano huo ulifanyika Agosti 3, mwaka huu,katika uwanja wa Temeke Mwisho. 

Dk. Slaa alisema kuwa wananchi walio wengi wamechoshwa na nyimbo hizo za kikasuku zenye kurudiwa rudiwa ambazo zinalikusudia kundi fulani katika jamii na wala si wanajamii wote. 

Akaendelea Dk. Slaa kusema kuwa kauli hizo zisizofaa zinaendelea kuenezwa na vyombo mbalimbali vya habari vikiwemo vya serikali ambavyo vinaendeshwa kwa kodi za wananchi. 

Aidha, alikitaja kipindi cha "MANENO HAYO" kinachorushwa hewani na Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) kuwa ni moja ya vipindi vyenye kuenzi kauli zisizofaa. 

Japokuwa Makamu Mwenyekiti huyo wa CHADEMA hakuelezea zaidi ni wepi wanaokusudiwa na namna gani amani inaweza kuhatarishwa, lakini pamekuwepo na hisia kutoka kwa Waislamu kuwa pale inapotamkwa udini basi kauli hizo moja kwa moja inanasibishwa na Uislamu. 

Mathalan Waislamu wamewahi kuhoji katika nyaraka zao mbalimbali kuwa iweje chama chenye viongozi watatu wa juu Waislamu kionekane kina udini wakati kile chenye msururu mrefu wa viongozi wa juu Wakristo kisionekane hivyo?. 

Mwenyekiti wa CUF taifa ni Prof. Ibrahim Lipumba, Makamu wake ni Shabani Mloo na Katibu Mkuu ni Maalim Seif, wote ni Waislamu. Kwa upande wa CCM Mwenyekiti ni Rais Benjamin Mkapa, Makamu wake (Bara) ni John Malechela, na Katibu Mkuu ni Philip Mangula, wote ni ni Wakristo. 

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Wilaya ya Temeke na mgombea Ubunge wa Jimbo hilo Mhe. Richard Tambwe Hiza, akiongea na mwandishi wa habari hizi, amesema kuwa dhana hiyo ya udini, kwa kuwa inaelekezwa kwa Waislamu, inawaogopesha wengi wao kujiingiza katika siasa. 

Akaongeza kusema inakuwa dhambi kubwa kwa mtu anayeitwa Sheikh kuingia kwenye siasa, lakini inakuwa thawabu kwa Mwinjilisti au mlokole kuingia kwenye siasa huku Waislamu hao hao wakimkumbatia kwa furaha. 

Alisema kuwa wimbo huu wa udini umeifikisha nchi mahala pabaya ambapo mtu mwenye uwezo wa kuongoza anakoseshwa haki yake ya msingi kikatiba kwa sababu ya dini yake kwa hofu tu taasisi au chama hicho kitaonekana kina udini. 

Mhe. Tambwe akaitaka jamii kuelewa kuwa inaishi katika mchanganyiko wa watu wenye dini na imani tofauti hivyo ni wajibu wa jamii kukubali na kuheshimu ukweli huo. 

Juu
 

YALIYOMO
 

KAULI YA WAISLAMU
BAKWATA na Kanisa

Karume adaiwa ‘kutafuta ujiko’ kwa kutofautiana na Mkapa

Mkapa akiuka sera yake-Chuo Kikuu

Uandikishaji wapiga kura waanza

NLD, NRA, PONA vyamruka Mrema

CUF  yataja wagombea wake Temeke

CCM yamtuhumu Mwenyekiti wake pandikizi

Propaganda ya Udini itaisambaratisha nchi - CHADEMA

USHAURI NASAHA
Kumsaidia mtoto aweze kujitegemea

MAKALA
Lengo la propaganda

MIPASHO NASAHA
NJOZI! NJOZI!

MAKALA
Tujihadhari na risasi za sukari

KALAMU YA MWANDISHI
Popo Bawa la kisiasa

Je, unajua haki yako unapokamatwa na polisi?

Habari za Kimataifa

LISHE
Ulaji wa matunda

MASHAIRI

MICHEZO

  • Baada ya kuitumia kuigaragaza Simba: Shungu akiri ‘ngangari' ni kiboko
  • Manga azikwa Moro
  • •••Dewji ahusishwa na kifo cha mnyama Simba
  • Lunyamila, Kayoza waongoza kwa mabao

  •  


    Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita