NASAHA
Na. 060 Jumatano  Agosti 9 - 15, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Uandikishaji wapiga kura waanza 
  • Dosari ndogo zajitokeza 
Na mwandishi wetu 

UANDIKISHAJI wa wapiga kura umeanza jana nchini kote ambapo huko Zanzibar zoezi hilo limeingia dosari.

Taarifa zilizopatikana kutoka Visiwani humo zimedai vituo kadhaa vimechelewa kufunguliwa kinyume na ilivyokuwa imepangwa. Vituo hivyo vilikuwa vifunguliwe saa mbili asubuhi na kufungwa saa kumi na mbili jioni. 

Taarifa hizo zimeeleza kwamba kituo cha Haile Sellasie ambacho kipo mkabala na Ofisi ya Tume ya Uchaguzi kilifunguliwa saa 4:30 asubuhi, wakati kituo cha Mwanyaya kilifunguliwa saa 7:30 mchana. 

Dosari nyingine ilijitokeza katia kituo cha Bububu ambapo baadhi ya wananchi waliofika kujiandikisha walikosa namba za utambulisho, zimeeleza taarifa hizo. Jijini Dar es Salaam, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa pamoja na ukweli kwamba jana ilikuwa ni siku ya mapumziko, idadi ya watu waliojitokeza kujiandikisha haikuwa kubwa. 

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Lewis Makame amewataka wananchi wajiandikishe mapema ili kuondoa msongamano unaoweza kujitokeza katika siku za mwisho. 

Uchunguzi zaidi uliofanywa na gazeti hili katika majimbo ya uchaguzi ya Kigamboni, Temeke, Ilala na Ukonga umeonesha kuwa katika vituo vyote vya jimbo la Kigamboni kulikuwa na mawakala wa vyama vya CUF na CCM tu. 

Katika jimbo la Temeke baadhi ya vituo vilikuwa na mawakala wa TLP ukiacha wale wa CCM na CUF, sawa na vituo vilivyoko katika jimbo la Ukonga. 

Katika jimbo la uchaguzi la Ilala vituo vyote vilivyotembelewa na NASAHA vilikuwa na mawakala wa vyama viwili tu, CUF na CCM. 

Aidha, hali ya uandikishaji iliendelea vizuri katika vituo vingi isipokuwa vichache zilikotokea rabsha za hapana pale kati ya mawakala na waandikishaji, hali iliyosababishwa na kutoelewa vema mipaka ya shughuli zao. 


NLD, NRA, PONA vyamruka Mrema 

Na Hamisi Kasabe 

VIONGOZI wakuu wa vyama vya siasa vya NLD, NRA na PONA wamekanusha vikali habari zilizodai kwamba wamekubaliana na Augustine Mrema wa TLP kumuunga mkono katika kampeni zake za kukimbilia Ikulu.

Gazeti la The Gurdian la Tazania toleo la Agosti 4, lilimnukuu Hamad kuwa tayari msemaji wa TLP akieleza kuwa tayari vyama hivyo vimekubali kumuunga mkono Mrema. 

Akiongea mjini Dar es Salaam jana katika ukumbi wa Habari Maelezo, Mwenyekiti wa NLD Bw. Emmanuel Makaidi alisema kwamba chama chake kinaogopa sana udini, ubinafsi na ukabila kwa hiyo hakitokuwa tayari kumuunga mkono mgombea anayeonekana kuyakumbatia hayo. 

Bw. Makaidi amedai kwamba TLP ni chama cha kidini chenye mrengo wa Kanisa Katoliki na akaongeza kuwa miongoni mwa mambo kadhaa yanayothibitisha hilo ni rangi za bendera ya chama hicho. 

Bendera ya chama cha TLP ambacho Mrema ni mwenyekiti wake inapambwa na rangi ya manjano na nyeupe rangi ambayo Makaidi amesema zinapatikana katika bendera ya Vatican inayomiliki Kanisa Katoliki kitu ambacho amedai kinaashiria uhusiano wa damu kati ya Kanisa hilo na TLP. 

Akiongea katika mkutano huo kumuunga mkono Bw. Makaidi, Katibu Mkuu wa NRA Bw. Abubakar Olotu aliongeza: "Na hata chama chetu cha NRA hakitakuwa tayari kumuunga mkono Mrema wa TLP kwa sababu hizo hizo". 

Naye Omar Juma Shaame ambaye ni Mwenyekiti wa chama cha PONA Taifa alisema kwamba chama chake hakiwezi kumuunga mkono Mrema katika kuwania kwa kuwa si mwanasiasa. 

Shaame ambaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Maelezo jijini jana akiwa pamoja na Makaidi na Olotu alisema kwamba Mrema ni mfanyabiashara wa dhahabu kwa hiyo PONA haitojiunga naye katika masuala ya siasa. 

"Wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri Mkuu, Mrema alikamata dhahabu ya mamilioni pale Airport Dar es Salaam na kuzikalia bila ya kuchukua hatua zozote za maana", alikumbusha. 

"Sasa ndio maana nikasema huyu mtu (Mrema) ni mfanyabiashara na sio mwanasiasa", aliongeza Shaame na kukataa katakata kuishirikisha PONA na TLP kwani kwa kufanya hivyo ni kukiingiza chama katika biashara. 


CUF yataja wagombea wake Temeke 

Na Mwandishi Wetu 

CHAMA cha Wananchi (CUF) wilaya ya Temeke kimetangaza rasmi majina ya wagombea Udiwani waliopitishwa na chama hicho kugombea Udiwani katika kata ishirini na nne zilizomo katika wilaya hiyo yenye majimbo mawili ya uchaguzi ya Temeke na Kigamboni.

Akiongea na gazeti hili, Mkurugenzi wa Oganizesheni na Uenezi wa Chama hicho wilayani humo, Bw. Said Omar Ngubiyagai, alisema kuwa majina hayo ya wagombea yalipitishwa na Baraza Kuu la uongozi la wilaya lililokutana Julai 24, mwaka huu. 

Orodha ya majina hayo na kata zao kwenye mabano ni kama ifuatavyo: 

Yusufu Chande (Pemba mnazi), Omari Mgaza Rajab (Somangira), Ussi Shomari Mbengeli (Kimbiji), Mwingi Mohamed Maya (Mji mwema), Salehe Omar Msoka (Tandika), Said B. Shueda (Kurasini), Masoud J.B. Kipanga (Mtoni), Mustafa I. Salum (Yombo Vituka), Abdul-Satani Seif (Sandari) na Said O. Njechele (Makangarawe). 

Wengine ni Juma M. Mtimbuko (Mbagala), Nassor Bakar (Kibada), Said S.O. Chivi (Charambe), Nusura Shaaban (Kigamboni), Rajab S. Nkawa (Mbagala Kuu), Yusuf Shaaban (Kisarawe II), Mwalimu Kambi Mwalimu (Vijibweni) na Athumani Matola (Chang'ombe). 

Bw. Ngubiyagai aliwataja wengine kuwa ni Haji M. Haji (Temeke), Mohamed Salehe Kinjenge (Miburani), Mbarouk Khalid (Azimio), Twahir Hamidu Koki (Tuangoma) na Salehe Abdallah Abdul-Kadir (Chamazi). 

Mkurugenzi huyo wa CUF alisema kuwa timu yao ya wagombea udiwani ni nzuri na yenye kukubalika na wananchi katika wiyala hiyo ya Temeke. 

Aidha, alisema Bw. Ngubiyagai kuwa wana matumaini makubwa ya ushindi wa viti vingi na hivyo kuweza kuunda Halmashauri ya wilaya. 

Bw. Ngubiyagai pia alisema kuwa katika majimbo mawili ya Ubunge yaliyomo katika wilaya hiyo ni jimbo la Temeke pekee ndilo mgombea wake amefahamika. Alimtaja mgombea huyo kuwa ni Bw. Richard Tambwe Hiza. 

Aidha, alisema kuwa jimbo la Kigamboni lilikuwa na wagombea wawili ambao ni Bw. Frank Magoba na Bw. Peter Simon na kwamba wanasubiri maamuzi ya ngazi za juu kujua nani kati yao atarudishwa au kama jimbo hilo watapewa CHADEMA ambao ni washirika wa CUF katika kile kinachoitwa umoja wa ukombozi 2000. 

Juu
 

YALIYOMO
 

KAULI YA WAISLAMU
BAKWATA na Kanisa

Karume adaiwa ‘kutafuta ujiko’ kwa kutofautiana na Mkapa

Mkapa akiuka sera yake-Chuo Kikuu

Uandikishaji wapiga kura waanza

NLD, NRA, PONA vyamruka Mrema

CUF  yataja wagombea wake Temeke

CCM yamtuhumu Mwenyekiti wake pandikizi

Propaganda ya Udini itaisambaratisha nchi - CHADEMA

USHAURI NASAHA
Kumsaidia mtoto aweze kujitegemea

MAKALA
Lengo la propaganda

MIPASHO NASAHA
NJOZI! NJOZI!

MAKALA
Tujihadhari na risasi za sukari

KALAMU YA MWANDISHI
Popo Bawa la kisiasa

Je, unajua haki yako unapokamatwa na polisi?

Habari za Kimataifa

LISHE
Ulaji wa matunda

MASHAIRI

MICHEZO

  • Baada ya kuitumia kuigaragaza Simba: Shungu akiri ‘ngangari' ni kiboko
  • Manga azikwa Moro
  • •••Dewji ahusishwa na kifo cha mnyama Simba
  • Lunyamila, Kayoza waongoza kwa mabao

  •  


    Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita