NASAHA
Na. 060 Jumatano  Agosti 9 - 15, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
Karume adaiwa 'kutafuta ujiko' kwa kutofautiana na Mkapa 

Na Mwandishi, Zanzibar 

KAULI ya mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Bw. Aman Abeid Karume juu ya Tanzania kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC)imeelezwa kuwa ina tofauti na kauli ya Rais Benjamin Mkapa juu ya suala hilo ambalo mpaka sasa limeiweka serikali upande mmoja na Waislamu nchini upande wa pili, uchunguzi wa gazeti hili umebaini.

Hayo yamesemwa na wananchi mbalimbali Visiwani kufuatia majibu ya Bw. Karume aliyoyatoa katika mdahalo ulioandaliwa na idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) ambapo Bw. Karume alisema Jamhuri ya Muungano imo mbioni kujiunga na jumuiya hiyo baada ya utafiti kufanyika ambapo imeonekana kwamba ni vizuri Tanzania ijiunge kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Akijibu swali lililoulizwa na msikilizaji Khalid Magana iwapo ataweza kuirjesha hadi ya Zanzibar ikiwemo kuirejesha OIC baada ya Zanzibar kulazimishwa kujitoa katika jumuiya hiyo, Bw. Karume alisema; "... Ninapenda kukupa taarifa tu kwamba serikali ya Jamhuri ya Muungano imefanya utafiti na tayari kuna ripoti imeshatayarishwa kwamba ni vizuri tukajiunga kama United Republic of Tanzania". 

Jibu hilo la Bw. Karume imedaiwa ni tofauti na jibu la Rais Mkapa alilowapa Waislamu juu ya msimamo wa serikali kuhusu Tanzania kujinga na OIC. 

Katika barua yake uliyoiandika Halmashauri ya Waislamu nchini, Rais Mkapa alisema serikali haiwezi kupuuza maoni ya watu wa dini zingine juu ya suala la Tanzania kujiunga na OIC. 

Kanisa Katoliki ndilo lililosimama kidete na kupinga kwa nguvu zote swala la Tanzania kujiunga na OIC. 

Kuhusiana na suala hilo, Kiongozi wa Kanisa Katoliki nchini, Polycarp Kadinali Pengo aliwataka wale wote wanaotaka Tanzania ijiunge na OIC wapeleke hoja zao 

Bungeni wakaeleze manufaa yatakayopatikana kwa nchi hii kujiunga na OIC. 

Imedaiwa kuwa Karume kudai Tanzania itajiunga OIC ni kujitafutia umaarufu kwa kutofautiana na kauli ya Rais Benjamin Mkapa ambaye msimamo wa serikali yake ni tofauti. 

Kadhalika, wamesema wamemshangaa Bwana Karume anapata wapi habari za Tanzania kujinga OIC wakati Wizara ya Mambo ya nje yenye kuhusika na suala hilo haina habari na jambo hilo. 

"Hapa ndipo tumezidi kumshangaa Bw. Karume; siku ile katuambia utafiti wa kujiunga OIC umekwishafanywa na taarifa imetolewa kwamba ni vema Tanzania ijiunge, lakini (Wizara ya) Mambo ya Nje wamekanusha.... Sasa hii inamsuta (Bw.) Karume", alilalamika mwananchi mmoja. 

"Karume anatafuta umaarufu asiyoweza kuupata wala asidhani yeye atakuwa bora kuliko (Dk) Salmin au marehemu mzee wetu Abdul-Wakil", alisema Bw. Sulieman Mohamed wa mjini hapa. 

Wananchi hao wameendelea kudai kwamba Karume hawezi kuamua na kutenda tofauti na matakwa ya viongozi wa CCM toka Bara. 

Wamedai kwa mujibu wa 'sera' ya CCM, Zanzibar. 

Wananchi hao ambao wamedai wana uchungu na "Zanzibar yao" wameendelea kudai kinachotakiwa na CCM ni kupatikana Rais ambaye atakuwa tayari kupokea maelekezo toka Bara. 

Wamedai kwa mjuibu wa "imani" ya CCM, Zanzibar ni mkoa tu na kwamba sera ya CCM ni serikali kuelekea serikali moja ili 'kuimeza' Zanzibar. 

Wananchi hao ambao wamedai wana uchungu na "Zanzibar yao" wameendelea kudai kwamba kinachotakiwa na CCM ni kupatikana Rais ambaye atakuwa tayari kupokea maelekezo toka Bara. 

Wamedai ni Aboud Jumbe peke yake aliyewahi kuushitukia mwelekeo huo wa CCM na Tanzania Bara jambo ambalo lilipelekea kung'olewa madarakani baada ya kuhoji. 

"Marehemu Mzee Karume alikuwa shupavu kuilinda Zanzibar, na ni (Aboud) Jumbe pekee aliyejaribu kufuata nyayo zake lakini akapigwa "stop" na Mwalimu Nyerere, akalazimishwa kujiuzulu huko huko Bara", alisema mwananchi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Hamis Uki ingawa alikataa kutaja yeye na mfuasi wa chama gani cha siasa. 

Wameendelea kueleza kuwa ingawa Jumbe alivuliwa madaraka yote aliyokuwa nayo katika serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, serikali ya Muungano na ndani ya chama cha Mapinduzi,Jumbe aliendelea kutetea maslahi ya Zanzibar ambapo aliandika kitabu kuelezea hali hiyo. 

Wakiendelea kuchambua madai yao ni vipi mgombea huyo kwa tiketi ya CCM hataweza "kuinusuru" Zanzibar walisema Karume amerithi tu jina la Baba yake lakini sio ushupavu wake. 

"Karume huyu ni wa jina tu... sio Karume (Marehemu) aliyeuthibishia ulimwengu kuwa Zanzibar sio mkoa wa Bara bali ni nchi kamili. 

"....Marehemu mzee wetu (Karume) hakumchelea (Mwalimu) Nyerere, alimwambia Azimio lake (la Arusha) likomee huku huko Bara.... na ndivyo ilivyokuwa", alieleza mwananchi mwingine ambaye muda wote wa mazungumzo alikuwa akijiita mkereketwa bila kutaja ni mkereketwa wa kitu au chama gani. 

Azimio la Arusha lilipitishwa mwaka 1967 ambapo baadhi ya mali za watu binafsi zilitaifishwa kulingana na thamani zao. Utaifishaji haukuvuka kuingia Zanzibar. 

Wakihitimisha kutoridhishwa kwao na mgombea huyo wa CCM, wananchi hao wamedai kwamba wamesikitishwa na madai ya Bw. Karume kwamba atasimamia vema ukusanyaji wa kodi Visiwani humu ili kuongeza mapato ya serikali. 

Wamesema wanashangaa ni vipi Bw. Karume ataweza kukusanya kodi toka kwa watu wasio na kipato kwa kukosa ajira. 

"Amani (Karume) katushangaza sana, sisi hatuna ajira, hatuna kipato yeye anataka kukusanya kodi toka kwetu....hivi kodi hii itatoka wapi", alihoji Mohammed Salim ambaye amedai kila siku anataabika kutafuta ajira tangu alipohitimu masomo yake. 

Bw.Mohamed, ambaye alidai ana umri wa miaka 30, alisema ahadi ya mgombea Urais wa Zanzibar kwa kiketi ya CUF, Bwana Seif Shariff Hamad kwamba akichaguliwa atajitahidi kuongeza ajira ni jambo la kutia moyo sana hususan kwa vijana ingawa jambo hilo pekee halitoshi kuboresha maisha ya Mzanzibar. 

Aidha, katika kile walichodai ni kutaka kurejesha hadhi ya Zanzibar, wananchi hao wamesema watakuwa makini wasichague Rais atakayekuwa anapokea maelekezo toka 'Chimwaga'. 

Chimwaga ni ukumbi wa mikutano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliopo Dodoma. 

"Zanzibar ni lazima irejeshe hadhi yake, tutamwingiza Ikulu mtu atakayeweza kuifanya kazi hii na huyo atajulikana baada ya Oktoba", alisema Bw.Ali Muhidini.
Juu


Mkapa akiuka sera yake-Chuo Kikuu 

Na Mwandishi Wetu 

JUMUIYA ya Wanafunzi wa Kiislamu wa Chuo Kikuu chaDar es Salaam (MSAUD)wamesema wameipokea kwa masikitiko makubwa kauli ya Mhe. Rais Benjamin William Mkapa ya kukipiga marufuku kitabu kinachosimulia tukio la kihistoria la Mwembechai ambapo wamedai hatua hiyo ni kinyume kabisa na sera yake ya uwazi na ukweli.

Katika waraka wao uliosambazwa jana na kutiwa saini na Amir wa Majlis-MSAUD, Juma Bakari, wanafunzi hao wamehoji ni kitu gani ambacho Rais anachokiogopa ndani ya kitabu hicho. 

Wamehoji iwapo Rais Mkapa ameogopa kauli za kutisha na uuaji za Jeshi la Polisi au picha za Waislamu waliouawa (mashahidi) Mwembechai na akina mama wa Kiislamu waliodhalilishwa. 

Aidha, wamehoji iwapo amri hiyo Rais Mkapa inatokana na hofu ya kukosa kura za Waislamu iwapo wataubaini "ubaya na dhuluma za utawala wake", au kujulikana nafasi ya Kanisa Katoliki katika mauaji hayo. 

Wanafunzi hao wamesema, kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu ambayo Tanzania inaikubali, ni vema kitabu hicho kiruhusiwe kuingia nchini kuwawezesha wananchi kukisoma. 

"Kinyume na hivyo", wamesema wanafunzi hao wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, "tunakichukulia kitendo hiki cha serikali ya CCM na Rais Mkapa, ambaye ni Mkatoliki, kuwa ni kilele cha dhuluma wanayofanyiwa Waislamu Tanzania kwa maslahi ya Kanisa Katoliki." 

Kitabu hicho kinachoitwa The Mwembechai Killings and the Political Future of Tanzania (Mauaji ya Mwembechai na Mustakabali wa kisiasa wa Tanzania kulipigwa marufuku kwa tamko la Rais alilolitoa Agosti Mosi, mwaka huu na kutangazwa katika gazeti la Serikali toleo la Agosti 4, mwaka huu. 

Katika gazeti hilo la serikali ambalo hutolewa kila Ijumaa,hakuna sababu zozote zilizoelezwa kupelekea marufuku hiyo ya Rais Mkapa kwa kitabu hicho kilichoandikwa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Hamza M. Njozi. 

Mwisho wanafunzi hao wametoa tangazo kwa Waislamu wote ndani na nje ya nchi kujitolea mali zao na nafsi zao katika kuihami dini yao na kurejesha heshima yao kama Waislamu na wananchi wa Tanzania. 

Mwanafunzi mmoja aliyeongea na gazeti hili jana usiku alisema kwamba kupiga marufuku kitabu hakufuti wala kubadili ukweli uliopo. 

Akieleza zaidi mwanafunzi huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema, "tangu mauaji yale Waislamu tumekuwa tukiyajadili mahusiano yetu na serikali ya CCM na tayari tumekwishafikia uamuzi".... Tunasubiri Oktoba." 

Juu
 

YALIYOMO
 

KAULI YA WAISLAMU
BAKWATA na Kanisa

Karume adaiwa ‘kutafuta ujiko’ kwa kutofautiana na Mkapa

Mkapa akiuka sera yake-Chuo Kikuu

Uandikishaji wapiga kura waanza

NLD, NRA, PONA vyamruka Mrema

CUF  yataja wagombea wake Temeke

CCM yamtuhumu Mwenyekiti wake pandikizi

Propaganda ya Udini itaisambaratisha nchi - CHADEMA

USHAURI NASAHA
Kumsaidia mtoto aweze kujitegemea

MAKALA
Lengo la propaganda

MIPASHO NASAHA
NJOZI! NJOZI!

MAKALA
Tujihadhari na risasi za sukari

KALAMU YA MWANDISHI
Popo Bawa la kisiasa

Je, unajua haki yako unapokamatwa na polisi?

Habari za Kimataifa

LISHE
Ulaji wa matunda

MASHAIRI

MICHEZO

  • Baada ya kuitumia kuigaragaza Simba: Shungu akiri ‘ngangari' ni kiboko
  • Manga azikwa Moro
  • •••Dewji ahusishwa na kifo cha mnyama Simba
  • Lunyamila, Kayoza waongoza kwa mabao

  •  


    Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita