|
|
|
Na Hassan Omar Kuongeza RAM kwenye kompyuta ni jambo rahisi sana na kwa bahati nzuri bei ya RAM kila siku inashuka kwa kasi kubwa sana. Na jambo zuri zaidi ni kuwa kila kompyuta ikiwa na RAM nyingi zaidi basi ndipo inapofanya mambo kwa kasi kubwa zaidi. Mambo hayo matatu: urahisi wa kuongeza RAM; bei nafuu; na uongezekaji mkubwa wa kasi ya kompyuta, ndiyo yanayowafanya watu wengi wakawa wanaongeza RAM kwenye kompyuta zao mara kwa mara. Nimepata kuona kompyuta zenye RAM ya mpaka 1 GB, jambo ambalo siku za nyuma kidogo tu, mtu alikuwa hawezi hata kuliwaza! Unapotaka kuongeza RAM kwenye kompyuta, hata hivyo, kuna mambo kadhaa ya kuyazingatia. Kwa mfano:
Ukiifungua kompyuta yako na kuweza kuona sehemu inayowekwa RAM unaweza kirahisi kuona kama zipo soketi za ziada ambazo bado hazijachomekwa RAM zozote. Angalia ujue kama soketi hizo zinahitaji SIMMs zenye pini 30 au pini 72, au DIMMs. RAM za miaka ya karibuni zinakuja kwenye muundo wa SIMM (Single Inline Memory Module). SIMM ni kibao kidogo kilichowekewa chip kadhaa juu yake. Kwenye upande mmoja wa SIMM kuna pini kadhaa. SIMMs (Single Inline Memory Modules) za zamani kidogo zina jumla ya pini 30, wakati SIMMs za siku hizi zina jumla ya pini 72. SIMMs za pini 30 ni za urefu wa inchi tatu, wakati SIMMs za pini 72 ni kubwa zaidi ya SIMMs za pini 30 kwa aislimia ishirini na tano. Kompyuta zote za 386 zinazotumia SIMMs, basi hutumia SIMMs za pini 30. Kompyuta za zamani zaidi za 386 zilikuwa zinatumia RAM za muundo wa SIP (Single Inline Package) au pia zinaitwa SIPP (Single Inline Pin Package), ambazo hivi sasa ni shida sana kuzipata, na kwa kweli ni kupoteza wakati kuongeza RAM kwenye kompyuta ya 386 inayotumia SIPs. Kompyuta za 486 za zamani pia nazo hutumia SIMMs za pini 30. Lakini katika kipindi cha mpito cha kati ya mwaka 1994 na mwaka 1995, baadhi ya makampuni yanayotengeneza motherboard, yalikuwa yanatengeneza motherboard zenye soketi za SIMMs za pini 30 na pia pini 72. Kwenye motherboard, SIMMs zinapangwa kwa "benki" (banks) maalum. Kompyuta za zamani kama 286 na 386SX zilikuwa zinatumia benki zenye jumla ya SIMMs za pini 30 mbili kwa kila benki moja. Kwa nini ikawa hivyo? Kwa sababu, kila SIMM moja ya pini 30 ina uwezo wa kutoa bit 8 za data ilizozihifadhi kwa wakati mmoja. CPU za ukoo wa 286 na 386SX zilikuwa zinatumia basi la data (data bus) la ukubwa wa bit 16; yaani zilikuwa na uwezo wa kuzichukua bit 16 kwa mpigo kutoka kwenye RAM na kuzishughulikia. Ndio maana zikahitaji SIMM mbili za pini 30 ili kwa pamoja ziweze kuipatia CPU bit 16 inazozitaka. Kompyuta za 386DX na 486 zinatumia basi la data la bit 32. Ndio maana kwenye kompyuta hizo, benki za SIMMs za pini 30 zinakuwa za SIMMs nne kwa kila benki. Kila SIMM inatoa bit 8 – SIMMs nne zinatoa jumla ya bit 32 zinazohitajika. SIMMs za pini 72 zina uwezo wa kutoa jumla ya bit 32 kila moja. Ndio maana benki za SIMMs za pini 72 kwenye 486 zina SIMM moja tu kwa kila benki moja. Umuhimu wa kujua idadi ya SIMMs zinazohitajika kwenye benki ya SIMMs za aina fulani kwenye kompyuta ya aina fulani, ni kwa vile huwezi kuwa na benki ya SIMMs iliyo pungufu. Kwa mfano, kwenye kompyuta ya 486, huwezi kutumia SIMMs mbili tu za pini 30 – ni lazima ziwe nne, au nane, au kumi na mbili, n.k. – yaani idadi inayogawika kwa nne. Kwa mfano huwezi ukawa na SIMMs sita tu za pini 30 kwenye kompyuta ya 486 – hazitafanyakazi! Kompyuta za Pentium zinatumia basi la data la bit 64 na takriban kompyuta zote za Pentium zinatumia SIMMs za pini 72. Haya, niambie! Kwenye kompyuta ya Pentium kila benki ya SIMMs za pini 72 inahitaji SIMMs ngapi? Kama umesema SIMMs mbili, basi umepatia. Lakini siku hizi RAM zinakuja kwa muundo mpya unaoitwa
DIMM (Dual Inline Memory Module). DIMMs ni rahisi kuzitambua kwa
vile zenyewe ni ndefu zaidi na zina jumla ya pini 168. DIMM ina uwezo wa
kutoa bit 64 za data kwa mpigo. Kwa hivyo, suali jengine: benki
ya DIMMs za pini 168 kwenye kompyuta ya Pentium inahitaji DIMMs ngapi?
Umesema DIMM moja? Umepata! Soketi za DIMMs zilizo kwenye kompyuta ya Pentium
ziko kama zinavyoonekana kwenye Picha 1. ![]() SIMMs za pini 30 zilikuwa zinakuja kwa ukubwa wa 256 KB, 1 MB, 4 MB na 16 MB. SIMMs hizo siku hizi ni adimu sana na ni za bei mbaya. SIMMs za pini 72 zinakuja kwa ukubwa wa 1 MB, 2 MB, 4 MB, 8 MB, 16 MB, 32 MB, na hata 64 MB. DIMMs zinakuja kwa ukubwa wa 8 MB, 16 MB, 32 MB, 64 MB, 128 MB, na 256 MB. Soketi za SIMMs za pini 30, sio zote zinazoweza kuhimili SIMMs za ukubwa wa 4MB na kuzidi hapo; na soketi za SIMMs za pini 72, sio zote zinazoweza kuchomekwa SIMMs za ukubwa wa 8 MB na zaidi. Ni lazima usome manual ya motherboard uone ni ukubwa gani wa SIMMs unaoweza kuhimiliwa na soketi za SIMMs zilizo kwenye motherboard hiyo. SIMMs zenye "parity" ni tafauti kidogo na SIMMs zisizokuwa na "parity" (non-parity). Idadi ya chip zinazokuwa kwenye SIMMs zenye parity huwa ni nambari isiyogawika kwa mbili (yaani "odd"). Kwa mfano, SIMMs nyingi za non-parity huwa na chip 8, wakati zenye parity huwa na chip 9. Chip ya ziada inaitwa kuwa ni "chip ya parity", na kazi yake ni kuipelekea CPU bit moja ya parity. Bit ya parity huingizwa kila SIMM inapotuma data kwenda kwenye CPU ili kuzifanya idadi ya "1" zilizotumwa ziwe "odd" (nambari isiyogawika kwa mbili). Kwa mfano kama idadi ya "0" kwenye data ni sita, na idadi ya "1" kwenye data hiyo ni kumi, chip ya parity itaongeza "1" moja ili idadi ya "1" iwe kumi na moja, nambari isiyogawika kwa mbili. Kama idadi ya "1" tayari ni nambari isiyogawika kwa mbili, chip ya parity itaongeza bit "0". Kwa namna hiyo, data zikifika kwenye CPU idadi ya "1" inaangaliwa – kama sio "odd" basi huonesha kuwa data hizo zina makosa na hatua nyengine hufuatia kusahihisha makosa hayo. SIMMs za aina ya "non-parity" hazifanyi kitu kama hicho ingawa pia hazileti matatizo kwenye kompyuta kwani hutumika njia nyengine kadhaa kuhakikisha kuwa data zinafika kwenye CPU bila ya makosa yoyote. Haipendekezwi kuchanganya SIMMs za parity na za non-parity. Ukilazimika kufanya hivyo basi kwenye CMOS Setup itabidi useme kuwa hutumii SIMMs za parity, bila ya hivyo kompyuta haitafanyakazi. Kwenye kila benki ya SIMMs ni lazima uchomeke SIMMs zilizo sawa kwa kila hali. Yaani ziwe sawa kwa ukubwa – kwa mfano zote ni za 256 KB, au zote ni za 1 MB, n.k; ziwe sawa kwa kasi – kwa mfano zote ni za 60 nanoseconds, au 70 ns, au 35 ns, n.k. Kasi ya SIMM ni kipimo cha muda unaohitajika kwa SIMM hiyo kuipatia data CPU. Kasi ya SIMM unaiona kwenye maandishi yaliyo juu ya SIMM. Maandishi yanayomalizia na –80 huonesha kuwa kasi ya SIMM hiyo ni 80 ns; yanayomalizia –70 ni kwa SIMMs za kasi ya 70 ns, yanayomalizia na –60 ni za kasi ya 60 ns, n.k. Kila nambari ikiwa ndogo ndio kasi ya SIMM inakuwa kubwa. Sasa tuangalie mifano mbali mbali ya kuongeza RAM kwenye kompyuta.
Kama kompyuta hiyo tayari ina RAM ya ukubwa wa 1 MB, basi bila shaka ina SIMMs nne za pini 30 na ukubwa wa 256 KB kila moja. Kama kompyuta hiyo ina benki nne za SIMMs, kila benki inahitaji SIMMs mbili, kwa hivyo itaweza kuchukua SIMMs zisizozidi nane. Kwa kuwa SIMMs nne za 256 KB tayari zimeshachomekwa, nafasi iliyobaki ni ya SIMMs nne tu – yaani benki mbili. Unaweza kuongeza kwenye benki moja SIMMs mbili za ukubwa wa 1 MB kila moja, ili kufanya RAM ya jumla ya 3 MB (4 x 256KB + 2 x 1MB). Au unaweza kuongeza SIMMs nne za 1 MB kufanya jumla ya 5 MB (4 x 256KB + 4 x 1MB). Au unaweza kuchomoa SIMMs mbili za 256 KB na ukaongeza SIMMs sita za 1 MB kufanya jumla ya 6.5 MB (2 x 256KB + 6 x 1MB). Au unaweza kuzichomoa SIMMs zote za 256 KB na ukaweka SIMMs nane za 1 MB kufanya jumla ya 8 MB. Michanganyiko ya namna hiyo yapo mingi. Lakini kwa ujumla kama unataka kompyuta yako iwe na RAM ya ukubwa wa 16 MB, basi kama motherboard inaruhusu, ni gharama ndogo zaidi kuzichomoa SIMMs zote nne za 256 KB na nafasi yake ukachomeka SIMMs nne za 4 MB kila moja. Kompyuta za 286 na 386SX haziwezi kuhimili RAM ya ukubwa wa zaidi ya 16 MB. Kwa hivyo usije ukachomeka SIMMs nane za 4 MB kwa kutaka kuwa na RAM ya 32 MB – hiyo haitafanyakazi! Ukiamua kuchanganya SIMMs za ukubwa tafauti (kwa mfano 256 KB na 1 MB), zitangulize kuzichomeka SIMMs kubwa kwenye benki ya mwanzo, yaani "benki 0." Kama umechanganya SIMMs za kasi tafauti kwenye benki mbali mbali, basi tanguliza za kasi kubwa zaidi kwenye benki 0. Jadueli 1 inaonyesha michanganyiko mbali mbali
ya SIMMs inayowezekana (kinadharia) kwenye kompyuta ya 286 au 386SX yenye
soketi 4 za SIMMs za pini 30. Kwa taarifa zaidi ya michanganyiko hasa inayoruhusiwa
kwenye motherboard yako, itakupasa kusoma manual ya matherboard
hiyo.
Jadueli 1
Kuongeza RAM kwenye kompyuta ya 486 kwa kutumia SIMMs za pini 30 Kumbuka kuwa benki za SIMMs za pini 30 kwenye 486 zinahitaji SIMMs nne kwa kila benki. Kama kompyuta yako ya 486 ina jumla ya RAM ya 4 MB, basi kama ina soketi nane za SIMMs za pini 30, inawezekana tayari imewekewa SIMMs nne za 1MB kila moja. Kuna namna mbili nzuri za kuongeza RAM kwenye kompyuta hiyo, nazo ni kuongeza SIMMs nne za 4 MB ili kupata jumla ya RAM ya 20 MB (4 x 1MB + 4 x 4MB), au kuongeza SIMMs nne za 1 MB kufanya jumla ya RAM ya 8 MB. Kama kompyuta ya 486 ina jumla ya RAM ya 6 MB, basi bila shaka ina soketi kumi na mbili za SIMMs za pini 30, ambazo zimechomekwa SIMMs nne za 1 MB, na SIMMs nane za 256 KB. Kwa namna hiyo, unaweza kuzichomoa SIMMs nne za 256 KB na badala yake ukachomeka SIMMs nne za 4 MB kufanya jumla ya RAM ya ukubwa wa 21 MB (4 x 4MB + 4 x 1MB + 4 x 256KB), au SIMMs nne za 1 MB kufanya jumla ya 9 MB. Kama kompyuta ya 486 tayari ina RAM ya ukubwa wa 8 MB,
basi kama ina soketi nane za SIMMs za pini 30, itakuwa ina SIMMs nane za
1 MB. Njia pekee ya kuongeza RAM kwenye kompyuta hiyo ni kuzichomoa SIMMs
nne za 1 MB na badala yake ukachomeka SIMMs nne za 4 MB kufanya jumla ya
RAM ya ukubwa wa 24 MB.
Kuongeza RAM kwenye kompyuta ya 486 yenye soketi za SIMMs za pini 30 na pini 72 Kikawaida, motherboard za 486 zenye mchanganyiko wa soketi za SIMMs za pini 30 na pini 72, huwa na soketi nne za SIMMs za pini 30 na soketi mbili za SIMMs za pini 72. Utakumbuka kuwa kwenye kompyuta ya 486, benki ya SIMMs za pini 30 inahitaji SIMMs nne, wakati benki ya SIMMs za pini 72 inahitaji SIMM moja tu. Kama kompyuta ya namna hiyo tayari ina RAM ya ukubwa wa 4 MB, basi inawezekana ina SIMMs nne za pini 30 za ukubwa wa 1 MB kila moja, au SIMM moja tu ya pini 72 ya ukubwa wa 4 MB. Kama utaweza kupata kwa bei rahisi SIMMs nne za pini 30 na ukubwa wa 4 MB, basi unaweza kuzichomeka hizo baada ya kuzichomoa SIMMs nne za pini 30 za ukubwa wa 1 MB, na kupata RAM ya ukubwa wa 16 MB. Lakini SIMMs za pini 30 za 4 MB ni ghali sana na pia ni adimu kupatikana. Kwa hivyo, mpango mzuri wa kuongeza RAM kwenye kompyuta hiyo, kama tayari inazo SIMMs nne za 1MB, unaweza kuongeza SIMM moja ya pini 72 ya ukubwa wa 4 MB kufanya RAM ya ukubwa wa 8MB; au unaweza kuongeza SIMM moja ya pini 72 ya ukubwa wa 8 MB kufanya jumla ya RAM ya ukubwa wa 12 MB; au unaweza kuongeza SIMM moja ya pini 72 ya ukubwa wa 16 MB kufanya RAM ya ukubwa wa 20 MB, n.k. Jambo la kuangalia hapo ni kuwa sio motherboard zote za 486 zinazoweza kuhimili RAM za 8 MB. Unaweza kutumia mfano huo kujua jinsi ya kuongeza RAM
kwenye kompyuta ya 486 yenye mchanganyiko wa soketi za SIMMs za pini 30
na pini 72, kwa viwango mbali mbali vya RAM ambayo tayari imo kwenye kompyuta.
Kitu cha muhimu ni kuelewa kuwa SIMMs za pini 72 ni za bei nafuu zaidi
kuliko za pini 30, na kila SIMM ikiwa kubwa basi huwa ni ya bei nafuu zaidi
kwa kila MB. Kwa mfano, SIMM moja ya 16 MB ni ya bei nafuu zaidi kuliko
SIMMs nne za 4 MB.
Kuongeza RAM kwenye kompyuta ya 486 yenye soketi za SIMMs za pini 72 Motherboard za kompyuta za 486 zenye soketi za SIMMs za pini 72 huwa na soketi nne za SIMMs hizo. Kwa kuwa benki ya SIMMs za namna hiyo inahitaji SIMM moja tu, unaweza kuongeza SIMM moja moja. Hiyo ni rahisi sana kwa hivyo hatuna haja ya kuelezea sana namna ya kuongeza RAM kwenye kompyuta hizo. Labda tuchukue mfano wa kompyuta ya namna hiyo yenye RAM ya ukubwa wa 8 MB na unataka kuifanya iwe na RAM ya ukubwa wa 16 MB. Kama inazo tayari SIMMs mbili za 4MB, unaweza kuichomeka ama SIMMs neyngine mbili za 4 MB, au SIMM moja ya 8 MB, kufanya jumla ya RAM ya ukubwa wa 16 MB. Kama ina SIMM moja tu ya 8 MB, basi unaweza kuongeza SIMM nyengine moja ya 8 MB kufanya jumla ya 16 MB.
Tunapozungumzia Pentium tunajua kuwa ama inatumia soketi za SIMMs za pini 72 au DIMMs za pini 168. Benki za SIMMs zinahitaji SIMMs mbili, wakati benki za DIMMs zinahitaji DIMM moja moja tu. Kwa hivyo ukiongeza SIMMs itabidi uongeze mbili mbili, wakati ukiongeza DIMMs unaweza kuongeza moja moja tu. Kwa vile DIMMs zipo mpaka za ukubwa wa 256 MB, kazi ya kuongeza RAM kwenye Pentium kwa kweli ni rahisi sana mradi tu unaingiza SIMM au DIMM kufuatana na aina ya soketi zilizopo. Kwa kutumia maelezo yaliyotangulia, hapana shaka utaweza kirahisi sana kuongeza RAM kwenye kompyuta za Pentium, na hata za Pentium MMX, Pentium Pro, na Pentium II.
Kwenye sehemu hii tumejifunza jinsi ya kuongeza RAM kwenye kompyuta. Tumegundua kuwa kumbe hatuwezi tu kupachika SIMMs idadi yoyote kwenye kila kompyuta. SIMMs zinapangika kwa benki maalum, na benki hizo zinahitaji idadi tafauti ya SIMMs kwenye kompyuta mbali mbali. Kwa mfano benki ya SIMMs za pini 30 kwenye kompyuta ya 486 inahitaji SIMMs nne wakati SIMMs za pini 72 kwenye kompyuta hizo zinakuwa kwenye benki za SIMM moja moja tu. Hiyo ni kutokana na idadi ya bit zinazotakikana kutumwa kwa mpigo kutoka kwenye RAM kuingia kwenye CPU. Kwa kompyuta ya 486 CPU inahitaji bit 32 ambazo inazipata kutoka kwenye SIMMs nne za pini 30, kila moja ikitoa bit 8. SIMM ya pini 72 inaweza kuzitema bit zote 32 kwa mpigo ndio maana ikahitajika moja tu. Tumejifunza pia kuwa ni gharama ndogo kutumia SIMMs kubwa kuliko mchanganyiko wa SIMMs ndogo. Kwa hivyo, kwa mfano ukitaka kuwa na RAM ya ukubwa wa 16 MB, ni bei nafuu zaidi kutumia SIMM moja tu ya 16 MB kuliko SIMM nne za 4 MB. Na pia tumejifunza kuwa haipendelewi kuchanganya SIMMs za parity na za non-parity. Lakini tukilazimika kufanya hivyo hatuna budi kuweka kwenye CMOS Setup kuwa SIMMs zote hazitumii parity. Kwa kumalizia, tungependa kukumbusha mambo mawili. Kwanza, SIMMs, na DIMMs ni rahisi sana kuathiriwa na "electrostatic charge", yaani chaji ya umeme wa asili unaotokana na michuano ya vitu mbali mbali. Chaji za aina hiyo zinaweza kukuganda kwenye nguo zako na hata kwenye viganja vyako. Ili kuepusha kuziharibu SIMMs hakikisha kuwa huzigusi ovyo ovyo tu. Ni vyema kugusa kitu cha bati au chuma, kama sanduku la kompyuta, kabla ya kuigusa SIMM au DIMM. Au vizuri zaidi ni kuvaa kitu kinachoitwa static band, hasa kama unafanyakazi ya kubadilisha RAM mara kwa mara. Kwa vyovyote vile, jiepushe kugusa sehemu za SIMMs na DIMMs zilizo wazi. Jambo la pili ni kukumbushia tu, ukishaongeza RAM kwenye kompyuta utahitaji kuhifadhi kwenye CMOS ukubwa mpya wa RAM ulio kwenye kompyuta yako. Ingia kwenye CMOS Setup kama kawaida kwa kubonyeza Delete au F1. Ukishaingia kwenye CMOS Setup huna haja ya kufanya chochote, chagua Save and Exit na kompyuta yako itaendelea kufanyakazi kama kawaida. Tunatumai kuwa maelezo na mifano iliyotolewa itakusaidia
kukabiliana na haja mbali mbali za kuongeza RAM kwenye kompyuta mbali mbali.
|
YALIYOMO
'White Paper ni ulaghai wa Serikali ya CCM' Na Mwandishi wetu Sheikh Omar Bashir awekwa rumande
Mpango wa 'Kupindua' uongozi
wa Bakwata: Masheikh Dar waitwa polisi kuhojiwa
Zahrau Day yatikisa Tanga
MAKALA: Hatuna haja ya maelekezo ya
yule aliyetufikisha hapa
Huduma za afya Kondoa haziridhishi
Tunahitaji 'UN' ya Waislamu!
Hoja binafsi: Wawekezaji watuondokesha makwetu Jamii inapokuwa soko huria...
Someni kwa ajili ya Allah - Sheikh
Baruti
Madrasa Al-Ii'Tiswamu
Al-Umaahaati Fiisabiililillah - Moro
Madrasat Hidayat Mbagala
Hali ya Uislamu Moro
Vijijini yazidi kuwa mbaya
Sheikh Masoud Mwinyi awaonya
Waislamu kuacha migogoro Babati
Tusikaribishe mfungo wa Ramadhani
kwa Vunja Jungu
'Acheni zinaa muepukane
na ukimwi'
Wavunja jungu watahadharishwa
Hoja/Uchambuzi:
Njia ya uzimani ni nyembamba,
waionao ni wachache
Habari:
Kesi ya Waislamu Mwembechai
yaahirishwa kwa mara nyingine
Kongomano la wanawake wa
Kiislamu Bagamoyo
Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|