|
|
|
Kuhamishwa mijini KATIKA dunia ya kileo ili uambiwe kweli unaishi mjini na utofautiane na wakazi wa vijijini ni muhimu nyumba unayoishi iwe na umeme na maji kutoka vituo vikuu. Kinyume cha hivyo kwa mtazamo wangu hata kama utakuwa unakaa katikati ya jiji utakuwa umehamia kijijini. Kuna sababu nyingi zinazopelekea watu wa mijini kukosa umeme na maji vya kutiririka, hata hivyo sababu kubwa ni kushindwa kwa watu kulipa "bil" za kuunganishiwa na za matumizi. Kuanzia 1996 idadi ya watu wa mijini wanaokatiwa huduma hizi imekuwa ikiongozeka mwaka hadi mwaka kutokana na kupanda kwa "bili" miezi hadi miezi. Nikifungua jalada (file) langu la TANESCO wanaonipatia umeme, nagundua bili za 1995 zilikuwa za baina ya shilingi 5,000 na 8,000. Kufikia mwishoni mwa 1997 nilikuwa nalipia wastani wa shilingi 12,000. Kuanzia mwezi Aprili 1998 bili zangu na wenzangu wengi zinaonyesha tunatakiwa kulipa baina ya shilingi 25,000 na shilingi 50,000. Baada ya kulalamika sana na malalamiko yangu kuambulia patupu, nimeamua kutokutumia kifaa chochote cha umeme zaidi ya taa ya kuonea ambayo huwa naiwasha pale inapoitumia nikiwepo tu. Sababu ya ongezeko kubwa hili ilhali sina tanuri la mikate nyumbani, nimeambiwa na wahusika ni kutokana na ongezeko la kodi ya thamani (VAT). Kwenye TANESCO najua mkono wa moja kwa moja wa wawekezaji bado uko njiani, hata hivyo VAT ni miongoni mwa athari za masharti yao. Nafungu faili langu la malipo ya maji, nagundua kabla ya kuingia kwa wawekezaji, nilikuwa nalipa shilingi 576 malipo ambayo nayo yameongezeka hatu kwa hatua na sasa natakiwa nilipe shilingi 4,200 kwa mwezi. Kutokana na kipato changu simudu kulipa mabili hayo, na nikaweza kuendesha maisha yangu kikawaida kama zamani kwa kuuza askirimu. Ili kufanikisha mradi huu nahitaji kupata jokofu ambalo litatumia umeme. Kabla sijatumia jokofu malipo yangu yamekuwa hivyo. Washauri wangu wananiambia kwa vile bili za TANESCO mara nyingine hazitegemei matumizi rahisi, ni bora nitafute jokofu lakini nahofia kutafuta kisababu cha kupandishiwa mpaka laki. Nafikiria kununua barafu nimpe kijana wangu akauze "juisi" kituo cha mabasi, lakini juzi moja nilikuta biashara hiyo ikifanywa na kampuni kubwa la wawekezaji la Coca Cola, katika mradi huo wa kuuza soda kwa vikombe maeneo hayo hayo ninayofikiria mimi kumpeleka kijana wangu. Nikaamua na mimi nifanye hivyo hivyo, uwezekano wa kushindwa ni mkubwa, kwanza juisi yangu itasingiziwa mambo chungu nzima, na hatimaye manispaa ili kuwaridhisha wawekezaji watanitimua tu. Kuhamishwa vijijini Maisha ya mji kwa dalili yamenishinda, sasa nafikiria kurudi kijijini kwetu kwa asili, kando kando ya bahari. Kabla ya hata kufungasha, ndugu zangu wanaotoka huko wananihadithia ugumu wa kwenda huko. Wanasema matumaini yangu ya kuishi kwa gharama nafuu ni finyu, kwani sehemu nyingi za kuvulia samaki haziruhusiwi hata kuzikanyaga kwa vile ni maeneo ya wawekezaji wanaotaka kuwekeza kwenye utalii, au ni maeneo ya wapenzi wa mazingira. Sasa nafikiria kwenda popote pale hasa sehemu za misituni, kwa matumaini kwa mara nyingine wasafiri wanaokuja kutoka huko wananikatisha tamaa. Mapendekezo yangu ni kwamba nikienda huko nijenge kibanda changu kandokando ya mto, lakini naambiwa huko nitakutana nao wale wale walionifukuzisha mjini, huko nitawaona kwa sura ya walinzi wa mazingira. Hivyo watanizuia kukata kuni, kulima na hata kuteka maji mtoni ili ati nisiyachafue. Nikiwaza nadharia yao ya kulinda maji yasichafuliwe napata wasiwasi iwapo kweli wanahuruma na watumiaji au ni kulinda biashara yao tu kwa visingizio. Wawekezaji ninaohakikishiwa kukutana nao kwenye msitu nikusudiao kwenda ni wapenzi wa mimea, wapenzi wa konokono, wapenzi wa panzi na kadhalika. Popote nitakapoamua kukaa lazima kutakuwa na mmea fulani ambao uko hatarini kutoweka au mdudu fulani asiyepatikana popote ulimwenguni isipokuwa hapo. Kwa sababu hizo ni lazima nihame hapo kabla ya kujenga, ili nisije nikahamishwa kwa kuchomewa moto. Nimechoka na wawekezaji na wapambe wao, hivi ni nani huyu aliyewakaribisha wawekezaji wanaotuhamisha makwetu. Wawekezaji wanaowafanya wa mijini watake kuhamia vijijini na wa vijijini watake kuhamia mijini. Matokeo yake kweli tunahama lakini hatuhamii, bali tunatatarika njiani. Cha kusikitisha zaidi nimesikia kule
Buliyanhulu kipande cha ardhi ya Tanzania kimenunuliwa na wananchi wa nchi
moja ya Amerika. Hivi sasa wenye kauli na eneo hilo la nchi hii ni wananchi
wa nchi hiyo. Naogopa kusema hivi sasa nchi yetu imeuzwa kwa wawekezaji.
Na Said Rajab Mfumo wa biashara ya soko huria tunaojaribu kuujenga unahitaji uangalifu na umakini wa hali ya juu sana. Uhai wa biashara yoyote inayotegemea nguvu ya soko ni masoko yake (wateja) . Baadhi ya’vigogo’ wanaitumia dhana ya soko huria kucheza rafu. Wanaigeuza jamii yetu kuwa soko la biashara za hovyo wanazobuni. Matokeo yake wanaiangamiza jamii nzima kwa manufaa yao binafsi. Tangu sheria ya vyombo vya habari irekebishwe na watu binafsi waliporuhusiwa kushiriki katika sekta hii muhimu ya habari, tumeshuhudia utitiri wa magazeti, radio binafsi, na vituo vya Televisheni. Vyombo hivyo vya habari viliingizwa kwa kasi nchini kwa malengo ya kibiashara zaidi ya kutoa huduma kwa jamii. Ndiyo maana habari zinazoandikwa au kutangazwa na vyombo hivyo ni zile zenye kusisimua na zinazokidhi haja ya masoko tu jamii itanufaikaje na habari zinazoandikwa au makala siyo jambo muhimu. Kuna baadhi ya magazeti hapa nchini ni maalumu kwa masuala ya ngono na ukahaba. Na jamii yetu imefikishwa mahala kukubali kashfa hii kama jambo la kawaida. Magazeti hayauziki bila ya kuandika kashfa za ngono! Hayapendwi sharti kuwepo mikasa ya machangudoa na wateja wao! Hayafurahishi mpaka kuwe na michoro ya vikatuni vizinifu! Hivi jamii inapolishwa uchafu huu nini matarajio ya baadaye? Tunataka kujenga taifa la wazinzi? Magazeti kama chombo cha habari yanatabia ya kudhibiti fikra za wasomaji. Ukisoma mambo ya kihuni mara kwa mara akili yako nayo inahamia huko huko. Inaogopesha kuona kuwa magazeti yanayoandika habari za uzinzi (sensetional) yanakumba wasomaji wengi. Tafsiri yake jamii inasoma kwa bidii sana mambo ya kihuni na yasiyokuwa na maana. Jamii imegeuzwa soko la habari za kihuni na kijinga bila ya kutambua. Janga la ukimwi linalotishia maisha ya Watanzani walio wengi limetumiwa kama chachu ya biashara haramu ya kondomu. Viongozi wa ngazi ya juu wa taifa wamekuwa wakiwahamasisha wananchi watumie kondomu kujikinga na ukimwi. Jamii ya Watanzania imeingizwa kwenye ‘mkenge’ na viongozi wao wa taifa kuhusu matumizi ya kondomu; na hivi sasa wananchi wako katika hatari ya kuambukizwa. Viongozi wanatamba kwamba kampeni ya kudhibiti ukimwi imefanikiwa kwa sababu mamilioni ya kondomu yameshauzwa nchini! Mauzo ya kondomu ndiyo kipimo cha kudhibiti ukimwi! Jamani tumche Mungu! Hiki ni kigezo biashara ya kondomu ina soko kiasi gani na wala siyo mafanikio ya kudhibiti ukimwi. Watanzania tunageuzwa soko la kondomu wala hatugutuki! Wataalamu wa ukimwi wameshaongea mara nyingi sana kwamba kondomu siyo kinga ya ukimwi. Ukimwi hauna kinga wala tiba. Lakini viongozi wetu, vyombo vya habari, na jamii nzima ya Watanzania hatuna utamaduni wa kuzingatia mambo ya kitaalamu. Tumekuwa hodari wa kusoma ‘songombingo’ tu bila ya kupitia makala zinazoandikwa na wataalamu. ‘Vigogo’ wanaisaliti jamii kwa kutosema kweli kuhusu udhaifu wa kondomu. Wanaogopa kupoteza masoko ya mradi huu wa ZINAA SALAMA.Tusipoachana na uasherati; hata tukivaa ‘tube ya baiskeli’ wachilia mbali kondomu, ukimwi utatumaliza tu! Ulipoanzishwa mradi wa ‘Speed-governor’ hoja ilijengwa kwamba lengo lilikuwa kudhibiti ajali za barabarani. Debe lilipigwa na viongozi wa taifa mpaka wananchi wakakubali kuwa ufumbuzi wa ajali za barabarani umeshapatikana. Wenye mabasi na magari mengine ya abiria walishinikizwa kununua ‘speed-governor’ kwa gharama kubwa la sivyo magari yao hayataruhusiwa kufanya shughuli. Bada ya magari kufungwa ‘Speed-governor’ ajali zimekwisha? Kila siku tunashuhudia ajali mbaya na za kutisha na ‘speed-governor’ zipo. Wenye mabasi na wananchi wamefanywa soko la miradi ya watu! Mbaya zaidi vyombo hivi vinanunuliwa kwa gharama kubwa na nisharti ufunge katika gari lako. Nani anayefaidika? Katika miaka ya nyuma tulikuwa hatujui kama kuna biashara ya madawa ya kulevya ulimwenguni. Kwa kawaida biashara hii hufanywa na watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha na wenye nyadhifa mbalimbali. Tujiulize hawa ‘vigogo’ wanaofanya biashara hii haramu wamepataje soko la biashara hii katika jamii yetu? Wako tayari kuliachia soko lao hili? Soko limebuniwa kwa kumomonyoa maadili mema ya jamii na kuingiza ya kishenzi. Soko lao linapanuka zaidi kadri tunavyoendelea kukumbatia mila na desturi mbovu. Vita dhidi ya madawa ya kulevya haitafanikiwa iwapo maadili mema ya jamii yataachiwa yatoweke. Kuna lingine hili jipya la kuruhusu watu binafsi waendeshe biashara ya silaha nchini. Hoja inayojengwa ni kwamba; "Serikali inajitoa katika biashara na kuiachia sekta binafsi. Hata hivyo wafanyabiashara wa maduka ya silaha wataruhusiwa kuuza silaha chini ya udhibiti mkali wa Serikali." Kuna ukweli hapo kutokana na uzoefu wa huko nyuma? Wakati soko si huria silaha tele zipo mikononi mwa majambazi, vipi zikiuzwa na akina John na Rapesh Patel! Viwanda vya kutengeneza silaha hizi vilivyoko Marekani na nchi nyingine
za magharibi vimepoteza soko katika nchi zao na hivi sasa vinakaribia kufa.
Serikali za Marekani na Uingereza zinadhibiti sana kuzagaa kwa silaha katika
jamii zao kutokana na mauaji ya mfululizo ya kutumia silaha yanayotokea
nchini mwao. Hali hii imesababisha masoko mengi ya silaha katika nchi hizo
yanaharibika na hivyo kutishia uhai wa viwanda vya silaha. Wasiwasi tulionao
ni kwamba tusije kugeuzwa soko la silaha zilizokwama huko Ulaya na Mrekani.
Wafanyabiashara binafsi siku zote wanalenga kupata faida kubwa kwa gharama
ndogo. Na faida kubwa katika biashara ya silaha itapatikana kwa kuwa na
soko kubwa zaidi na la uhakika. Jamii itakuwa katika hali gani? Kila silaha
zitakavyozagaa ndipo mauaji ya kikatili na uhalifu wa kutumia silaha utakavyozidi;
na mahitaji zaidi ya silaha yataongezeka kutokana na usalama kuwa mdogo.
Tutakuwa tumewapa soko la kutumainiwa hasa!
|
YALIYOMO
'White Paper ni ulaghai wa Serikali ya CCM' Na Mwandishi wetu Sheikh Omar Bashir awekwa rumande
Mpango wa 'Kupindua' uongozi
wa Bakwata: Masheikh Dar waitwa polisi kuhojiwa
Zahrau Day yatikisa Tanga
MAKALA: Hatuna haja ya maelekezo ya
yule aliyetufikisha hapa
Huduma za afya Kondoa haziridhishi
Tunahitaji 'UN' ya Waislamu!
Hoja binafsi: Wawekezaji watuondokesha makwetu Jamii inapokuwa soko huria...
Someni kwa ajili ya Allah - Sheikh
Baruti
Madrasa Al-Ii'Tiswamu
Al-Umaahaati Fiisabiililillah - Moro
Madrasat Hidayat Mbagala
Hali ya Uislamu Moro
Vijijini yazidi kuwa mbaya
Sheikh Masoud Mwinyi awaonya
Waislamu kuacha migogoro Babati
Tusikaribishe mfungo wa Ramadhani
kwa Vunja Jungu
'Acheni zinaa muepukane
na ukimwi'
Wavunja jungu watahadharishwa
Hoja/Uchambuzi:
Njia ya uzimani ni nyembamba,
waionao ni wachache
Habari:
Kesi ya Waislamu Mwembechai
yaahirishwa kwa mara nyingine
Kongomano la wanawake wa
Kiislamu Bagamoyo
Sayansi na Teknolojia
Chakula na lishe
|