AN-NUUR 
Na.178 Shaaban  1419, Desemba 4 - 10, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Historia
Upinzani dhidi ya Serikali ya Kiislamu wakati wa Khalifa wa Kwanza 
 

Upinzani dhidi ya Dola ya Kiislamu 

Katika sehemu hii tutatazama upinzani dhidi ya Dola ya Kiislamu tangu wakati wa Abubakr hadi kuuawa kwa Khalifa Ali. Wakati wa ukhalifa wa Abubakr upinzani ulitoka kwa Waislamu (koo, makabila na wengine) waliouhama Uislamu na kuna upinzani uliotoka kwa Warumi na Wapesia (Waajemi). 

Habari za kutawafu kwa Mtume (s.a.w.) zilipelekea makabila mengi kuuhama Uislamu na kutaka kuivamia Madina na kuiteketeza Dola ya Kiislamu. Tukio hili katika vitabu vya Tareikh huitwa Riddah kwa Kiarabu na apostasy kwa Kiingereza. 

Kwa ujumla Dola ya Kiislamu iligawanyika katika makundi sita ya watu. kuna waliobakia na Uislamu wao bila kutetereka hasa watu wa Madina, Taif na Makka. Wanafiki ni kundi lililokuwepo na hila zao za mwisho ziligonga ukuta mwaka mmoja tu kabla ya kifo cha Mtume hivyo walikuwa macho kuvizia fursa yoyote iliyopatikana waitumie. Kulizuka kundi la Waislamu waliobakia Waislamu lakini walikataa kupeleka Zaka Madina kwa hoja kuwa itumike kuwasaidia wasiojiweza katika eneno lao. 

Wapo waliobaki Waislamu lakini walikataa kulipa Zaka kabisa. Kundi lingine ni lile lililoritadi na kurudia dini zao za asili. Kundi lingine ni wale mitume wa uwongo47 walioanza tangu wakati wa Mtume na sasa wakaongezeka kufikia wanne. Ikumbukwe pia wakati wa majilio ya wajumbe mbali mbali kwa Mtume, yapo makabila ambayo hayakusilimu ila yaliitambua Dola ya Kiislamu wakawa wanalipa Jizya. Mfano ni kabila la Hanifa la sehemu ya kati ya Arabia. Wayahudi nao ambao siku zote walikuwa maadui wa Mtume si kuwa tu wametolewa Madina lakini hata huko Khaibar walikohamia walishindwa na kulazimishwa kuutambua utawala wa Kiislamu na kulipa Jizya. 

Sio Wayahudi tu bali Wakristu wa Najran na Urumi waliazimia kuangamiza Dola ya Kiislamu kwa vile wote walikuwa wanalipa Jizya. Hivyo ni dhahiri uasi katika Dola ya Kiislamu ulikuwa mkubwa. Dola yote ya Kiislamu ilisambaratika, maadui walikuwa wengi na waliobakia na utii kwa Dola ni miji baina ya Madina, Makka na Taif.48 kama ilivyokwisha tajwa awali. Kabla ya kutazama hatua alizochukua Abubakr Siddiqi ni vyema kwanza tuchambue sababu zilizopelekea uasi huu. 

Sababu zilizopelekea Uasi 

Kwa wale waliosilimu kisha baada ya kutawafu Mtume walikataa kulipa Zaka na wale waliokubali kulipa Zaka lakini wakajenga hoja kuwa hawatapeleka Madina lakini itumike kwa watu wao; makundi yote haya sababu yao kubwa ya kufanya hivi ni udhaifu wa Imani kama isemavyo Qur’an: 

Walisema wanaokaa jangwani (kumwambia Mtume) "Tumeamini" Sema uwaambie Hamjaamini, Lakini semeni Tumesilimu maana imani haijaingia nyoyoni mwenu bado... (49:14). 

Ama kwa wale waliorudia dini zao za asili walikuwa na sababu mbili moja ya kiuchumi kulinda biashara zao na mali zao kwa kuondokana na kulipa Jizya na pili kulinda hadhi zao na nafasi zao katika koo zao na mila zao. Sababu hizi pia ndizo zilizopelekea uasi kwa wale waliokuwa hawakusilimu lakini walikuwa wanalipa Jizya. Ila kundi hili linasababu nyingine, utukufu wao. Na kwa wale waliodai utume na walioungana nao pamoja na sababu zilizotajwa wakiongezea husda na uroho wa mamlaka. Bado ipo hoja inayowahusu Waarabu wote, wengi wao walizoea maisha yasio na mpangilio maalum, wasio na nidhamu na wasiotambua utii ila kwa koo zao au makabila yao. Mabadiliko yaliyoletwa na Mtume yaliwaweka katika mfumo wa maisha wenye nidhamu wasioitaka. Waliukubali wakati wa Mtume kwa kuwa walikuwa hawana jinsi; kufa kwa Mtume kumetoa nafasi sio ya kujitenga na utawala wa Madina bali walikusudia kuuhilikisha kabisa.49 Kwa upande wa Wayahudi na Wakristu ni kweli waliasikulind tawala zao na utukufu lakini kulinda dini (itikadi) zao pia kulitoa msukumo mkubwa. Sababu hizi na nyinginezo ambao huenda hatukuzitaja zaweza kuwa ndio chimbuko la "Riddah" Uasi. Ni vyema sasa tuone Abubakr alivyoikabili hali hii na kurudisha utulivu ndani ya Dola ya Kiislamu. 

Usama aenda Syria 

Hatua ya kwanza aliyochukua Abubakr ni kukamilisha hatua aliyochukua Mtume (s.a.w.) majuma machache kabla ya kifo chake alipotuma jeshi la Waislamu chini ya uongozi wa Usamah Ibin Zaid kwenda Syria kulipiza kisasi cha vita vya Mutah. Jeshi hili lilipokuwa kambini kujiandaa kwa msafara wa Syria Mtume akatawafu. Kutawafu kwa Mtume (s.a.w.) kulifanya Usamah avunje kambi na aahirishe msafara. Baada ya majuma matatu tangu atawafu Mtume, Khalifa Abubakr aliliamuru jeshi hili likamilishe maandalizi na lianze msafara. Kutokana na hali ya uasi iliyokuwa kubwa ndani ya Dola ya Kiislamu baadhi ya maswahaba walimshauri Abubakr asilipeleke jeshi hilo kwa usalama wa Madina. Abubakar alikataa kwa hoja kuwa hawezi kuacha jambo ambalo Mtume (s.a.w.) ameliamuru. Hivyo hivyo walimtaka abadili mkuu wa msafara asiwe Usamah kwa kuwa ni mdogo na hana uzoefu. Kwa hoja ile ile ya kufuata nyayo za Mtume Abubakr hakukubaliana nao. Huyu ndie Abubakr Siddiqi alivyofuata nyayo za Mtume (s.a.w.) katika hali ya kutisha kama ile na uasi usiokikomo bado kwa imani yake iliyokomaa alitoa jeshi likakamilishe kazi aliyoianza Mtume (s.a.w.). Baada ya siku arobaini Usamah alirudi Madina na Ushindi mkubwa.50 

‘ Siku tatu tangu Usamah alipoondoka na jeshi lake wakazi wa jangwani waliivamia Madina lakini walirudishwa nyuma na maswahaba wachache waliokuwepo wakiongozwa na Khalifa mwenyewe. Hivyo mji wa Madina ukawa katika ulinzi mkali. 

Tumeona kuwa walioasi walikataa kutoa Zaka. Abubakr aliita shura na kuzungumzia hatima ya wanaokataa kulipa Zaka. Maswahaba wengi walishauri kuwa kwa wakati ule na hali ilivyokuwa haikuwa vyema kuwachukuliakwa kuzingatia upinzani mkubwa uliokuwepo na upinzani wa mitume ya uwongo. Kusikia hivi Abubakr alitangaza kuwa; "Naapa kwa jina la Allah, nitapigana peke yangu hata kama wengine hawatanisaidia kwa kila ambae hataki kutoa Zaka hata kama ni kidogo.51 Alitangaza vita dhidi ya uasi wote. Akakusanya majeshi na kuyagawa bataliani kumi na moja; kila bataliani ikatumwa kwa waasi, katika waasi hawa wapo waliopigana na wapo waliosalimu amri. jitihada za kuzima uasi ni kama ifuatavyo: 

Kukomeshwa kwa Uasi 

Miongoni mwa makabila yaliyovamia Madina ni Bani Abbas na Zukian. Makabila haya yalipokuwa yanakimbilia Rabaza baada ya kushindwa kuivamia Madina waliwaua kikatili watu wa makabila yao ambao hawakuasi. Khalifa Abubakr aliongoza msafara wa kuwafukuza, adui alishindwa, wengi waliuliwa na baadhi yao kuchukuliwa mateka. Uasi wa Bahrain nao ulizimwa. Wakazi wa Bahrein walikuwa matawi mbali mbali ya ukoo wa Bani Rabia - kubwa kati yao ni Bani Bakr. Kiongozi wao alikuwa Munzir ambae alisilimu. Munzir alimkubali mkazi aitwae ‘Ala’ kutoka Madina akiwa anafundisha Uislamu. Baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.) Munzir nae akafa, jimbo hili liliasi chini ya uongozi wa Hotem. A’la alifika Madina na akapata jeshi la kutosha kuzima fujo za Bahrein. Katika uwanja wa vita Hotem aliuawa na uasi kukomeshwa na jeshi lililoongozwa na Jarud. Hali ilikuwa hivyo hivyo kwa uasi wa Oman. Malkia wa Oman alikuwa Jeyfar ambae alikubali utukufu wa Uislamu mwaka mmoja au miwili kabla ya kufa Mtume (s.a.w.) Amr alikuwa muwakilishi wa Mtume katika mahakama yake. Mara baada kifo cha Mtume jimbo hili liliasi. Kazi ya kuzima uasi walikabidhiwa Hudhafa na Arfaja wakisaidiwa na Ikrima. 
 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
'White Paper  ni ulaghai wa  Serikali ya CCM' 
Na Mwandishi wetu 

Sheikh Omar Bashir awekwa rumande 
Na Mwandishi Wetu 

Mpango wa 'Kupindua' uongozi wa  Bakwata: Masheikh Dar waitwa polisi kuhojiwa 
Na Mwandishi Wetu 

Zahrau Day yatikisa Tanga 
Na Mwandishi Wetu 

MAKALA: Hatuna haja ya maelekezo ya yule aliyetufikisha hapa  
Na Alhaj Yusuf Kalala, Washington DC USA 

Huduma za afya Kondoa haziridhishi 
Na Abu Zubeir 

Wasemavyo wanaharakati 

Tunahitaji 'UN' ya Waislamu! 
Na Twahir Rashid 

Hoja binafsi: Wawekezaji watuondokesha makwetu 

Jamii inapokuwa soko huria...  
Na Said Rajab 

Someni kwa ajili ya Allah - Sheikh Baruti  
Na Muhibu Said 

Madrasa Al-Ii'Tiswamu Al-Umaahaati Fiisabiililillah - Moro 
Na Rajab Rajab, Morogoro 

Madrasat Hidayat Mbagala 
Na Mussa Salum  

Hali ya Uislamu Moro Vijijini yazidi kuwa mbaya  
Na Rajab Rajab, Morogoro 

Sheikh Masoud Mwinyi awaonya Waislamu kuacha migogoro Babati  
Na Abu Zuberi - Babati 

Tusikaribishe mfungo wa Ramadhani kwa Vunja Jungu  
Na Abeid Poyo 

'Acheni zinaa muepukane na ukimwi'  
Na Mussa Salum 

Wavunja jungu watahadharishwa 
Na Mwandishi Wetu, Morogoro 

Hoja/Uchambuzi: 
Je, hivi tuendelee kushika amri za Mungu tena? 
Na Mwinjilisti Bunga E. Dettu 

Njia ya uzimani ni nyembamba,  waionao ni wachache 
Na Yasin Valerian Massawe 

Habari: 
Semina ya Maimamu Tanga yadai: Maimamu wanapuuzwa  
Na Mwandishi Wetu 

Kesi ya Waislamu Mwembechai yaahirishwa kwa mara nyingine  
Na Muhibu Saidi 

Kongomano la wanawake wa Kiislamu Bagamoyo 
Na Mwandishi Wetu 

Sayansi na Teknolojia 
[Kuongeza RAM kwenye Kompyuta] 
 
Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Madini ya Zinc] 

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita