AN-NUUR 
Na.176 Shaaban  1419, Novemba 20 - 26, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Mashairi
 
 

Wababe wakitawala 

Kinyume kamwe hawezi, dhalimu kitawalia, 
Kufanya mambo azizi, yenye kuwafiki njia, 
Mwendo wao tangu enzi, si "huyu" kajianzia, 
 Ndiyo shukurani yao, "wababe" wakitawala. 

Hujivalisha murua, mbele wakawaijia, 
Mpate kuwachagua, kwa kura kuwapigia, 
"Thumma" utu hujivua, viti wakishakalia, 
 Ndiyo shukurani yao, "wababe" wakitawala. 

Si wema wa kutawala, japo wametangulia, 
Kutenda mambo jamala, hilo tawasingizia, 
Walipo wakisha "kula", lengo limetimilia, 
Ndiyo shukurani yao, "wababe" wakitawala. 

Ndugu zetu mlo Nzasa, si peke mnaolia, 
Ni sote yametugusa, pamoja twaugulia, 
Halipo mlilokosa, hayo kuwaangukia, 
Ndiyo shukuruani yao, "wababe" wakitawala. 

Kuchomewa maskani, bila kuwahurumia, 
Wana na wenu wandani, peupe mkabakia, 
Mmefanyiwa uhuni, Mola atawalipia, 
 Ndiyo shukurani yao, "wababe" wakitawala. 

Tadhani nyie si watu, tena si wao raia, 
Hamna thamani katu, wala kitu kuchangia, 
Yamewafika wenzetu, na sisi yanatujia, 
Ndiyo shukurani yao, "wababe" wakitawala. 

Haya hayatakuwako, macho kuyaangalia, 
Watu kupeana heko, kwa kuwadhuru raia, 
Kweli "wachamungu" wako, viongozi Tanzania! 
 Ndiyo shukurani yao, "wababe" wakitawala. 

Tunapata taawili, maana inatimia, 
Uliowazi ukweli, utawala wa sheria, 
Hizi ndo zake dalili, cheche zinaturukia, 
 Ndiyo shukurani yao, "wababe" wakitawala. 

Nchi mejaa amani, ndo wimbo twausikia, 
Utulivu mesheheni, hawana khofu raia, 
"Wakubwa" oneni soni, kuongopa si murua, 
 Ndiyo shukurani yao, "wababe" wakitawala. 

Nzasa wa kwenu mkasa, wahika umetwingia, 
Twajua hiyo ni posa, harusi inafatia, 
Baada ya ninyi hasa, wapi wataelekea! 
 Ndiyo shukurani yao, "wababe" wakitawala. 

Chonde tusikanganyike, kuubaini udhia, 
Ndiyo staili yake, serikali ya sheria, 
"Ucha Mungu" dira yake, vile walivyotwambia, 
 Ndiyo shukurani yao, "wababe" wakitawala. 

Mwinyi tunamkumbuka, kusema alipatia, 
Si punde yameshafika, mboni zayashuhudia, 
Yanatupata mashaka, kwa dhuluma kuzidia, 
 Ndiyo shukurani yao, "wababe" wakitawala. 

Alikuwa wa huruma, utu alizingatia, 
Kwa pupa "hakutarama", ni mwenda wa kurudia, 
Kimya chake cha hekima, "ruhusa" akipimia, 
 Ndiyo shukurani yao, "wababe" wakitawala. 

Thibitini msilie, nyoyo zisije kuvia, 
Hadhari mshikilie, na Mola kumlilia, 
Rais si wenu nyie, ndo shari kuwafikia, 
 Ndiyo shukurani yao, "wababe" wakitawala. 

Muwe na subira njema, wa Nzasa twawausia, 
Msijione yatima, Mola atawakidhia, 
Wababe wana khatima, kufuzu si yao njia, 
 Ndiyo shukurani yao, "wababe"wakitawala. 

Wako wapi madhalimu, uungu walojitia, 
Nao waliishi humu, wakawatesa raia, 
Siku zao zilitimu, seuze hawa "mikia", 
 Ndiyo shukurani yao, "wababe" wakitawala. 

Mola mpenda witiri, Muumba hii dunia, 
Twakuomba ya Qahhari, waja kuwaangalia, 
Pitisha yako qadari, yote umeshuhudia, 
 Ndiyo shukurani yao, "wababe" wakitawala. 

Jihad R. Saballa, S.L.P.47, SHINYANGA. 


Mauaji Mwembechai 
 

Msalikheri salamu, nazituma gazetini 
Ugweno Raa Simbomu, Shime yangu pokeeni 
Imenisibu hatamu, AN-NUUR fikisheni 
 Waloua Mwembechai, wahusika tokezeni. 

Sio nakumbusha donda, bali damu yavuvia, 
Wametwacha vidonda, damu tumezifukia, 
Waliotaka kushinda, harufu wametwachia, 
 Waloua Mwembechai wahusika tokezeni. 

Waumini twakumbusha, wajibu ukumbukeni 
Duniani wanakesha, raha yetu vilioni, 
Wanaua na kutisha, Mwembechai kumbukeni, 
 Waloua Mwembechai, wahusika tokezeni, 

Ukasuku uacheni, waandishi wambieni, 
Wahariri hakikini, maovu yafichueni, 
AN-NUUR  gazetini, jamii iambieni, 
 Waloua Mwembechai, wahusika tokezeni. 

Iogopeni shilingi, inapoteza amani, 
Tutaviruka vigingi; Mwembechai unganeni, 
Tumewapoteza wengi, kwa risasi motochini, 
 Waloua Mwembechai, wahusika tokezeni. 

Wawapi kina Malima; Af'stani na Sudani, 
Kwa machungu mnasema, tunateswa dunaini, 
Wamagharibi twasema, dawa yetu ijikoni, 
 Waloua Mwembechai, wahusika tokezeni. 

Bendera zenu za vuma, dunia shuhudieni, 
Ya Marekani mwasema, ya nyumbani hamneni, 
Kuimbe UKWELI wauma, "(unaumiza moyoni)", 
 Waloua Mwembechai, wahusika tokezeni. 

Piga huyu piga yule, sote tulishuhudia, 
Ngumi zikiwa kelele, wakubwa chanzo mwajua, 
Msiipishe simile, u-ngwana kujisemea, 
 Waloua Mwembechai, wahusika tokezeni. 

Mwembechai na Manyema, wazee tuwe pamoja, 
Ubungo, Mwenge, Musoma, Mtambani Mtakuja, 
Shinyanga Moshi twasema, wito wa Ponda twangoja, 
 Waloua Mwembechai, wahusika tokezeni. 

Yasini S. Mussa, 
UGWENO, 
KILIMANJARO. 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
Maoni 
Kuwa na mawazo ya kufugwa tunajidharaulisha 

Sakata la mabucha  ya Nguruwe kuibuka upya 
Na Mwandishi Wetu  

Kondom sio kinga ya Ukimwi 

Bakwata yairushia polisi makombora Ngaramtoni 

MACHO YA SHUTUMA 
Na Abu Halima Sa Changwa 

Serikali yatakiwa iwachukulie hatua wauaji 
Na Mwandishi Wetu 

Historia ya Msikiti wa Ngaramtoni 

Silaha yetu ni kura ya pamoja 
Na Alhaj Yusuf Kalala, Washington DC  U.S.A 

Anuani ya fikra 
Na Abu Halima Sa Changwa 

Kuukaribisha mwezi mtukufu 

Tunahitaji "UN' ya Waislamu! 
Na Said  Rajab 

Kongamano la wanawake wa Kiislamu Newala lafana 

Umuhimu wa Elimu ya Awali kwa watoto wadogo - 2 
Na Ustaadh Kupa Pazi Said 

Kesi mojawapo ya mihadhara yafutwa 

Wasaidieni watoto wenye vipaji - Prof. Kilonzo 

Mahafali ya kidato cha nne Thaqafa: Wazazi wakumbushwa wajibu wao 

Wanafunzi Mwanza wadai haki za kuabudu mashuleni kwa usawa 
Na Iddi M. Katiba, Mwanza 

Saidianeni katika shida - Sheikh Abdallah 

Waislamu, Wakristo Rufiji watakiwa kuunda umoja 

Someni  muiokoe jamii kimaadili 

Acheni Shirki 

Kesi nyingine ya Waislamu Mwembechai yaahirishwa 
Na Muhibu Said 

Kusilimu kwa Wakristo kwaleta kero Mwanza 

Nzasa waomba msaada wa chakula, madawa 

Katibu wa Bakwata Moro ang'olewa Msikitini 

Masomo ya Dini ya Kiislamu  

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Umuhimu wa chakula katika shule za awali]  

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita