|
|
|
Na Mujahid Mwinyimvua. KATIKA makala hii neno shule ya awali linamaanisha kituo cha kuwalelea/kuwasomesha watoto wadogo ambao hawajaanza elimu ya msingi (darasa la kwanza mpaka la saba kwa Tanzania). Katika vituo vya shule ya awali, mara nyingi watoto huwa na umri kati ya miaka 2 mpaka 6 au zaidi kidogo. Umri huo ni muhimu sana kwa maendeleo ya mtoto, kimwili na kiroho. Chakula kina nafasi kubwa ya kumjenga mtoto kimwili, na wengine wanasema hata kiroho. Kwa hiyo, umuhimu wa chakula katika vituo hivyo ni jambo lililowazi. Hata hivyo, kwa vile bado kuna baadhi ya shule za awali hasa madrasa na wazazi ambao wanaona kuwa swala la chakula katika vituo vyao si muhimu na litaongeza gharama, makala hii imelenga kuwazindua watu wa aina hiyo ( wanaosita kuwapa watoto chakula) na kuielimisha jamii kwa ujumla juu ya dhana ya chakula katika shule ya awali. Chakula tunacho kula kina faida kubwa moja, nayo ni kutupatia virutubisho (nutrients). Hivyo virutubisho vina kazi kubwa tatu. Kazi ya kwanza ni kujenga mwili. Kwa mfano, sote tuna jua kuwa binadamu kwa hali ya kawaida huzaliwa na baba na mama. Anapozaliwa huwa mdogo na hapo tunamwita mtoto mchanga. Baada ya miaka kadhaa huwa mkubwa na kuweza kufanya mambo yake mwenyewe. Mwanaadamu kama huyo anaweza kuongezeka umbo, kutoka mtoto na kuwa mkubwa kwa sababu ya virutubisho vinavyotokana na vyakula tunavyokula. Kazi ya pili ya virutubisho ni kuupa mwili nguvu na joto. Mambo au kazi mbalimbali zinazofanywa na binaadamu zinawezeshwa na nguvu (energy) inayotokana na virutubisho. Kutembea, kuongea, kulia, kubeba mizigo, kusoma, n.k. ni baadhi tu ya kazi hizo. Kazi ya tatu ya virutubisho ni kulinda mwili usipate magonjwa. Ulaji duni na magonjwa ni sababu kubwa zinazosababisha vifo vingi kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano katika nchi hasa za ulimwengu wa tatu ikiwemo Tanzania. Kwa mfano, taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha na mambo ya watoto (UNICEF) ya mwaka 1990 inaonyesha kuwa watoto 176 kati ya watoto 1000 wanaozaliwa Tanzania hufa kila mwaka kabla ya kutimiza umri wa miaka mitano. Ni muhimu watoto katika shule ya awali (madrasa, chekechea, n.k.) wapatiwe chakula cha kutosha, safi na salama na kilicho mlo kamili (balanced diet). Hii ni kwa sababu baadhi yao wanatoka nyumbani bila kula chakula chochote na wengine wanakaa mbali, wanapoteza muda mwingi njiani kabla ya kufika nyumbani. Katika kutayarisha chakula cha watoto wa shule ya awali, mwalimu au mlezi lazima azingatie mafungu makuu ya chakula yafuatayo: Chakula cha kujenga mwili Chakula cha aina hii ni muhimu sana kwa watoto wa shule ya awali. Hii ni kwa sababu mwili wake (pamoja na akili) unahitaji kujengeka na kukua. Mfano wa vyakula vinavyojenga mwili ni kama vile maziwa, nyama, samaki, mayai, senene, ndege, maharage, choroko, soya, njegere, karanga n.k. Chakula chenye kuupa mwili nguvu na joto Watoto hufanya shughuli mbalimbali kama vile kucheza, kusoma, kukimbia, n.k. ili mwili uweze kumudu kazi hizo na zile za kujenga mwili, lazima mwili upate vyakula vyenye kutoa nguvu, mfano wa vyakula hivyo ni mchele, viazi, mahindi, mtama, ndizi, karanga, alizeti, samli, siagi, asali, mihogo, kweme, n.k. Chakula cha kulinda mwili Chakula hiki husaidia kulinda mwili wa mtoto asipatwe na magonjwa mbalimbali. Mfano wa vyakula hivyo ni kama vile mbogaa mboga (mboga za majani, nyanya, karoti, n.k.) na matunda mbalimbali, embe, machungwa, mananasi, papai, ubuyu, ukwaju n.k.) Zaidi ya makundi hayo ya vyakula, watoto wa shule za awali lazima wapatiwe maji safi na salama kwa mfano yaliyochemshwa na kuchunjwa na kuhifadhiwa katika chombo safi. Ni matarajio yangu kuwa makala hii imekidhi haja iliyokusudiwa. Hivyo
basi wenye shule za awali na wazazi na jamii kwa ujumla tuendelee kutoa
chakula bora na maji safi na salama kwa watoto wetu na wale ambao bado
hawajaanza kutoa huduma hiyo waanze sasa, la sivyo tuaathiri
ukuaji na elimu ya watoto wetu
|
YALIYOMO
Maoni Kuwa na mawazo ya kufugwa tunajidharaulisha Sakata la
mabucha ya Nguruwe kuibuka upya
Bakwata yairushia polisi makombora Ngaramtoni MACHO YA
SHUTUMA
Serikali
yatakiwa iwachukulie hatua wauaji
Historia ya Msikiti wa Ngaramtoni Silaha yetu
ni kura ya pamoja
Anuani
ya fikra
Tunahitaji
"UN' ya Waislamu!
Kongamano la wanawake wa Kiislamu Newala lafana Umuhimu
wa Elimu ya Awali kwa watoto wadogo - 2
Kesi mojawapo ya mihadhara yafutwa Wasaidieni watoto wenye vipaji - Prof. Kilonzo Mahafali ya kidato cha nne Thaqafa: Wazazi wakumbushwa wajibu wao Wanafunzi
Mwanza wadai haki za kuabudu mashuleni kwa usawa
Saidianeni katika shida - Sheikh Abdallah Waislamu, Wakristo Rufiji watakiwa kuunda umoja Someni muiokoe jamii kimaadili Kesi
nyingine ya Waislamu Mwembechai yaahirishwa
Kusilimu kwa Wakristo kwaleta kero Mwanza Nzasa waomba msaada wa chakula, madawa Katibu wa Bakwata Moro ang'olewa Msikitini Chakula
na lishe
|