|
|
|
Dhana ya Umoja wa Mataifa iliibuka na kutiwa zege katika karne hii ya 20. Ilijaribiwa mara mbili; zote katika jitihada ya kuepusha vita vya dunia. Ujerumani (Super Power) wakati ule ndiyo sababu hasa ya kuibuka fikra za kuundwa Umoja wa Mataifa. "League of Nations" ilianzishwa baada ya Vita Kuu ya Kwanza mwaka 1919 mjini Geneva. ‘League of Nations’ ilishindwa kabisa kuzuia kuibuka kwa vita kuu ya pili (1939-1945) na hivyo kusababisha kuundwa kwa "UNITED NATIONS’ (Umoja wa Mataifa) tulionao sasa. Umoja huu (UN) uliundwa kwanza na washirika wa maadui wa Ujerumani na Japan. Misingi, nia na madhumuni ya ‘UN’ ilitokana na malengo ya wanachama waanzilishi kwamba wasiruhusu historia mbaya ya Taifa moja lenye nguvu kunyanyasa mengine ijirudie. Hoja nyingine ya msingi ilikuwa kuyarejesha mataifa yaliyoshindwa vita katika ulimwengu mpya; na hii ingewezekana kwa ushirikiano wa mataifa yaliyoshinda na yaliyoshindwa. Jukumu kubwa la baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni kudumisha amani ya ulimwengu na usalama wa kimataifa. Lakini jambo la ajabu, baraza hili limedhibitiwa na mataifa matano tu yenye nguvu yanayoitwa (wanachama wa kudumu wa baraza la usalama). Nchi nyingine zote zinaburuzwa tu katika baraza la uslama kwa hiyo hazina sauti wala uwezo wa kuchangia katika maamuzi yanayohusu amani ya ulimwengu na usalama wa kimataifa. Si kwamba kasoro hii haionekani au nchi wanachama wa ‘UN’ hazitaki kulipanua zaidi baraza la usalama, bali ni ukiritimba na mikakati ya Mataifa Makubwa yanayotaka kulitumia baraza hili kwa manufaa yao. Baraza la Usalama lingekuwa na maana zaidi na linalokidhi haja kama lingehusisha nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa. Amani ya dunia na usalama wa kimataifa hauwezi kuachiwa mataifa matano tu, halafu tutegemee mafanikio. Mfumo huu wa kidhalimu na kikabaila ndiyo sababu kuu ya ‘UN’ kushindwa kudumisha amani na usalama wa ulimwenguni na hivyo kuiweka dunia katika hatari ya kuzuka kwa vita kuu nyingine.Umoja wa Mataifa umekuwa hodari sana wa kutoa visingizio na viini macho kwa ulimwengu kila migogoro isiyokuwa na maslahi kwa mataifa makubwa inapoibuka. Ulimwengu mzima umeshuhudia jinsi umoja wa mataifa ulivyolishughulikia suala la Bosnia. Waislamu walipokuwa wanaangamizwa na Waserbia, Umoja wa Mataifa haukuchukua hatua za haraka kusimamisha maangamizo kwa Waislam. Badala yake tulikuwa tukionyeshwa picha kuu za maiti, majeruhi, wakimbizi na majanga mengine yaliyotokana na vita hivyo; huku Bi SADAKO OGATA (Kamishna na UNHCR) akitoa misaada ya nguo, vyakula na madawa kwa wakimbizi. Jitihada hasa za kusimamisha maangamizo yale kwa kweli hazikuwepo. Umoja wa Mataifa ulishindwa hata kuutangazia ulimwengu kwamba wanaoangamizwa ni Waislam. Kilichofanywa ni kuwawekea Waislamu vikwazo vya silaha ili washindwe kujihami na hivyo ‘operation’ ya kuwamaliza ifikie lengo. Waislamu walikuwa wanahitaji msaada wa kuokoa maisha yao na ya vizazi vyao, Umoja wa Mataifa unawapelekea mablanketi na mapajama bila ya kuzingatia tatizo lao la msingi! Hiyo ndiyo zawadi ya michango yao katika ‘UN’. Mwenyezi Mungu alipoleta nusra na Waislamu walipopata nguvu ya kupambana na Waserbia (Wakristo) ndipo Umoja wa Mataifa ukaingilia kati kuwanusuru Waserbia na vita ikaisha. Kumbe wakati wote ule Umoja wa Mataifa ulikuwa upande wa Waserbia ndiyo maana hawakuvumilia walipoona kibao kimegeuka. Tuangalie tena Umoja wa Mataifa jinsi ulivyowadhulumu na kuwasaliti Waislam wa Kosovo. Waislamu wa Kosovo wameuwawa kwa halaiki na kuchomewa vijiji vyao pamoja na makazi yao na askari wa Kiserbia. Askari wa Slobadan Milosovich waliendesha ‘operation’ maalumu ya kuwaangamiza Waislamu wa Kosovo. Kama ilivyo kawaida ya Umoja wa Mataifa, umeshindwa hata kuutambulisha ulimwengu tu kwamba wanaochinjwa Kosovo ni Waislam. Wamewabatiza jina la ‘Ethnic Albanians’ ili ulimwengu usitambue ni nani anayeangamizwa Kosovo. Walipoona malengo yao yanakaribia kutimia, wanajidai kukusanya askari wa NATO na kutishia kuivamia kijeshi Yugoslavia iwapo haitoondoa majeshi yake Kosovo. Wakampa Milosovich siku 14 za kuondoa majeshi yake Kosovo; muda ambao aliutumia vyema kukamilisha malengo yao. Umoja wa mataifa uliingilia kati mgogoro wa Somalia si kwa lengo la kuutatua wala kuleta amani nchini humo. Walikuwa na ‘agenda’ mbaya dhidi ya Wasomali ambao ni Waislam watupu. Walitaka kupanda mbegu mbaya ya kusambaratisha mila na desturi za Kiislamu nchini Somalia kwa kutumia tofauti za Kisiasa na za kiukoo za Wasomali. Lakini kwa rehma zake Allah, mambo yakawawia vigumu wakavunja kambi Somalia na kutimua mbio. Kama nia ilikuwa kuleta sulhu na amani nchini Somalia ‘UN’ isingekimbia mpaka sulhu ipatikane. Hiyo ni mifano michache tu kati ya mingi inayothibitisha jinsi Umoja wa Mataifa usivyokuwa na manufaa kwa Waislamu. Jambo la kushangaza ni kwanini Waislamu hawatanabahi na kujiepusha na umoja wa kidhalimu kama huu? Sudan na Afghaninstan zimeshambuliwa na Marekani kwa uonevu tu! Serikali ya Sudan imeitaka dunia ishuhudie uonevu wa Marekani; na kuomba Umoja wa Mataifa upeleke wachunguzi kuhakikisha kama kweli kiwanda kilichopigwa kilikuwa kinazalisha kemikali za silaha za sumu kama Marekani inavyodai. Mpaka leo’ UN’ kimyaa! Inashindwa kabisa kujibu changamoto ya Sudan. Itajibuje wakati wao na Marekani lao moja (mahasimu wa Uislamu!). Kama malengo ya kuundwa Umoja wa Mataifa yalikuwa kudhibiti mataifa makubwa yenye nguvu (Ujerumani) yasiyaonee mataifa dhaifu, mbona Marekani inanyanyasa mataifa dhaifu ya Waislamu kwa kutumia umoja huo huo wa mataifa? Marekani ina haki gani ya kuitishia kijeshi Iraq? Umoja wa Mataifa kwa maana ya mataifa hauna mgogoro wowote na Iraq. Mgororo uliopo ni kati ya Marekani na Iraq. Marekani inatumia kivuli cha Umoja wa Mataifa kutimiza azma yake mbaya dhidi ya Taifa la Iraq. Propaganda imetengenezwa katika namna ambayo Iraq inaonekana kukaidi maazimio ya kimataifa wakati ukweli ni kwamba maazimio hayo ni ya Marekani. Labda dunia ijiulize Marekani ina kitu gani dhidi ya Taifa la Iraq? Wakaguzi wa silaha kali wa Umoja wa Mataifa (UNSCOM) ni kiumbe cha Marekani na wanafanya kazi kwa ‘agenda’ za Marekani na wala siyo Umoja wa Mataifa.Mataifa hayana ugomvi na Iraq. Iraq inadai imeshatoa ushirikiano wa kutosha kwa "UNSCOM’ na inachohitaji sasa ni kwa ‘UN’ kutimiza ahadi yake ya kuiondolea vikwazo vya uchumi. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Anan, anasema hana mpango wa kwenda Baghdad kuitikia wito wa Iraq mpaka atakapoambiwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Amemuonya Rais Saddam Hussein achukue uamuzi wa busara wa kuendelea kushirikiana na majasusi hao wa Marekani (UNSCOM) hata kama ‘UN’ haitimizi ahadi zake za kuiondolea vikwazo Iraq. Rais wa Marekani, Bill Clinton akaitangazia dunia kupitia CNN kwanza kushindwa kwa Iraq kushirikiana na ‘UNSCOM’ kutaifanya Marekani ifanye shambulio la kijeshi dhidi ya Iraq, na Saddam Hussein ndiye atakayebeba lawama. Kwanini Marekani ndiyo iwe ya kuishambulia kijeshi Iraq na siyo Umoja wa Mataifa? Kwani Bill Clinton ni jemedari wa majeshi ya Umoja wa Mataifa? Dunia inapaswa ifahamu Marekani ina nia gani na taifa la Iraq, na Iraq inapigana dhidi ya nini, na Umoja wa Mataifa ni maficho ya nani! Wananchi wengi wa Iraq ni Waislam. Vikwazo vya uchumi vilivyowekwa na
‘UN’ vinaua na kuangamiza Waislamu wa Iraq. Mashambulizi ya kijeshi yanayoandaliwa
na Marekani dhidi ya Iraq yataua na kutia vilema Waislam. Umoja wa Mataifa
wenye majukumu ya kudumisha amani na usalama wa ulimwengu uko dhidi ya
Waislamu. Je? Waislamu wa dunia nzima, wakati haujafika tu wa kuwa na’
UN’ ya Waislam itakayoundwa kwa misingi na malengo yale yale yaliyoundiwa
Umoja kwa Mataifa.
|
YALIYOMO
Maoni Kuwa na mawazo ya kufugwa tunajidharaulisha Sakata la
mabucha ya Nguruwe kuibuka upya
Bakwata yairushia polisi makombora Ngaramtoni MACHO YA
SHUTUMA
Serikali
yatakiwa iwachukulie hatua wauaji
Historia ya Msikiti wa Ngaramtoni Silaha yetu
ni kura ya pamoja
Anuani
ya fikra
Tunahitaji
"UN' ya Waislamu!
Kongamano la wanawake wa Kiislamu Newala lafana Umuhimu
wa Elimu ya Awali kwa watoto wadogo - 2
Kesi mojawapo ya mihadhara yafutwa Wasaidieni watoto wenye vipaji - Prof. Kilonzo Mahafali ya kidato cha nne Thaqafa: Wazazi wakumbushwa wajibu wao Wanafunzi
Mwanza wadai haki za kuabudu mashuleni kwa usawa
Saidianeni katika shida - Sheikh Abdallah Waislamu, Wakristo Rufiji watakiwa kuunda umoja Someni muiokoe jamii kimaadili Kesi
nyingine ya Waislamu Mwembechai yaahirishwa
Kusilimu kwa Wakristo kwaleta kero Mwanza Nzasa waomba msaada wa chakula, madawa Katibu wa Bakwata Moro ang'olewa Msikitini Chakula
na lishe
|