AN-NUUR 
Na.176 Shaaban  1419, Novemba 20 - 26, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Umuhimu wa Elimu ya Awali kwa watoto wadogo - 2
Na Ustaadh Kupa Pazi Said
 

WAPO watu wengi wanaohoji hatua za utoaji wa elimu ya awali kwa watoto wadogo hasa katika hatua ya kwanza ambayo ni kabla ya kutungwa mimba. Wanachohoji ile athari inayopatikana kutokana na dua ya jimai. Kinachowashangaza ni vile dua inaposomwa kabla ya jimai kuwa kinga ya shari za shetani kwa mtoto na inapoachwa hukosa kinga hiyo! 

Ndugu wasomaji, lazima tufahamu daraja ya msemaji wa maneno hayo kwanza, kisha daraja zetu. Yeye kwetu ni mfano ulio bora (Qur. 33:21). Pia yale anayotamka ni sehemu ya ufunuo toka kwa Allah (s.w.) (Qur. 53:3)Vile vile tumekatazwa kutanguliza maneno yetu mbele ya neno lake (Qur. 49:1) na kunyanyua sauti zetu mbele yake (Qur. 49:2). Tunachotakiwa nikutii amri yake na tusiwe na khiyari kwa alichotuamuru (Qur. 33:36). 

Jambo lolote likiamrishwa na Mtume (s.a.w.) jua ndani yake kuna faida kubwa, na jambo lolote lililokatazwa na Mtume (s.a.w.) hata kama ni dogo, basi athari yake ni kubwa zaidi kuliko udogo wa jambo hilo. 

Kwa mfano, Mtume (s.a.w.) amekataza watu waliokula vitunguu thaum na vitunguu maji wasiingie Msikitini kwa sababu watawaudhi malaika na waumini wenzao. Kwa kuwa tumeliona dogo jambo hilo, tumeamua kula ndani ya Msikiti hivyo vitunguu kwa kuvitengeneza kachumbari pamoja na pilau. Matokeo yake ni kukosa mapenzi na msaada wa malaika katika matatizo yetu mengi yanayotufika Msikitini, majeshi ya Ibilisi yanaingia Misikitini yatakavyo nasi hatuna uwezo wa kupambana nayo kama tulivyoamriwa na Allah (s.w.). 

Tumekatazwa kupandanisha vidole vya mikono tukiwa Msikitini kwa sababu tendo hilo ni katika matendo ya shetani. Sisi tumedharau, na athari yake ni huku kuchezewa na Ibilisi tuwapo Msikitini hata tunashindwa kufanya adabu mbalimbali za Msikiti. 

Mtume (s.a.w.) amefundisha kuwa moyo ni kipande cha nyama ambacho kinausalimisha mwili kinaposalimika au kinaudhuru mwili kinapodhurika. Pia viungo vitatu (ulimi, tumbo na tupu) ni sababu kubwa ya kuingia kiwiliwili motoni kwa kusema mabaya, kula haramu na kutohifadhika na uchafu. Na hivyo hivyo ni sababu kubwa ya kiwiliwili kuingia peponi kwa kusema mema, kula halali na kuhifadhika na uchafu. Ikiwa yote hayo twayakubali kuwa yana athari kubwa ingawa ni madogo, basi tukubali pia kuwa dua ya jimai inamuathiri mtoto awe mwema au muovu kabla ya mimba. 

Msingi mkubwa wa elimu ya awali kwa watoto 

Lazima tukubali kuwa John na mama Maria, Joseph na Khadija, Khamis na Eva, wanapooana hawawezi kuleta dua kabla ya jimai. Pia hawawezi kuleta dua hiyo Bakari na Sofia ambao kwao ibada ni uchuro! Si dua tu, bali hatuwezi kutegemea kutoka kwao kuwa wataweza kusaidiana na mwalimu/mlezi wa watoto wadogo kutoa mafunzo ya awali kwa watoto kama alivyofundisha Mtume (s.a.w.). 

Ndoa njema chini ya misingi ya sheria, ndiyo msingi mkubwa wa kuta elimu ya awali kwa watoto. Mume mwema mfano wa mzee Imran, na mke mwema ni mfano wa mama Maryam, ndiyo kichocheo cha malezi mema ya watoto. Allah amesema: 

"...Na wanawake wema ni wa wanaume wema, na wanaume wema ni wa wanawake wema. Hao wameepushwa na hayo wanayosema; watapata wao msamaha na riziki iliyo tukufu". (24:26). 

Na Mtume (s.a.w.) amesema: 

"Mwanamke huolewa kwa mambo (sifa) manne: Kwa ajili ya mali yake, na kwa ajili ya koo lake, na kwa ajili ya uzuri wake, na kwa ajili ya dini yake. Shikamaneni na mwenye dini utabarikiwa". (Muttafaqun’alayh) 

Mtume (s.a.w.) amechagua sifa hiyo ya dini kutokana na ukweli kuwa mara nyingi wanawake wenye mali au walio wazuri kupindukia au wale wanatoka kwenye koo kubwa kubwa huwa na kibri, majivuno na tabia za kutamani maisha ya hali ya juu. Hali hiyo inapokosekana, huwa hamna masikilizano nyumbani, na huwa ndio mwisho wa ndoa. Mtume amesema: 

"Mwenye kuoa mwanamke kwa ajili ya mali yake, Allah hatomzidishia ila ufaqiri. Na mwenye kuoa mwanamke kwa ajili ya koo lake, Allah hatomzidishia ila hali duni (maangamio). Na mwenye kuoa mwanamke ili atulize jicho lake, Allah atambariki kwa mwanamke huyo, na atambariki mwanamke huyo kwa mwanaume huyo". (Ibn Hiban) 

Kama ilivyo kwa wanaume, wanawake nao wametakiwa kuchagua wachumba walio bora ili wasaidiane katika suala zima la maelzi, Mtume (s.a.w.) amesema: 

"Akichumbia kwenu yule mliyeiridhia dini yake na tabia yake, muozeni. Na kama hamkumuozesha, itakuwa fitna katika ardhi, na uharibifu mkubwa". (Tirmidhy) 

Baada ya kila mmoja kuchagua mchumba mwema na kuoana, lnafuata suala zima la malezi ya watoto. Uislamu umewabebesha jukumu hilo wazazi wawili, na umewaamrisha watilie umuhimu jambo hilo la malezi mema ya watoto. Allah (s.w.) amesema: 

"Enyi mlioamini! Ziokoeni nafsi zenu na (nafsi za) jamaa zenu na mtoto ambao kuni zake ni watu na mawe. Juu yake ni malaika wenye nguvu, wakali, hawamuasi Mwenyezi Mungu aliyowaamuru, na wanafanya waliyoamrishwa". (66:6) 

Tamko la Allah (s.w.) "Ziokoeni nafsi zenu na (nafsi za) jamaa zenu na moto", limetafsiriwa na Salaf salih kama ifuatavyo: 

Aliy (r.a.) amesema: "Waadabisheni na wafunzeni. 

Dhwihak (r.a.) na Muqaatil (r.a.) wamesema: "Ni haki juu ya kila Muislamu aifunze familia (jamaa) yake, ambao ni katika ndugu zake wa karibu na wafanyakazi wake na watumwa wake yale aliyowaamrisha Allah (s.w.) na waliyowakataza". 

Mtume (s.a.w.) amesema: "Waamrisheni watoto wenu kuswali watimizapo umri wa miaka saba. Na wapigeni juu ya (kuwasisitiza jambo) hilo watimizapo miaka kumi. Na watenganisheni kwenye malazi (wa kiume na wa kike)" (Abu Daud) 

Tunachojifunza hapa ni kuwa watoto huamrishwa kuswali na kufanya Ibada nyingine katika umri wa miaka saba. Hii inamaanisha kwamba huanza kufunzwa wakiwa chini ya umri huo. Lakushangaza ni kuwa baba aenda Msikitini, lakini mwanawe wa kiume amwacha nyumbani eti atafanya fujo Msikitini! 

Na kuna wazee Misikitini kazi yao kufukuza watoto tu basi katika Misikiti eti kwa sababu hawajatimiza umri wa miaka saba! Mmeelewa vibaya mafunzo ya Rasuli (s.a.w). Tulisema huko nyuma kwamba watoto husoma kwa kuona, kusikia na kucheza. Kwa hiyo inambidi mtoto wa kiume aende na baba Msikitini ili akaone watu wanavyoswali ili aigize. Na mama aigwe na mwanawe wa kike nyumbani. Pia aisikie Qur’an ikisomwa katika swala naye aigize. Na alifanye hilo tendo zima la kuswali kuwa ni mchezo kwake ndiyo awe na hamu ya kujifunza kuswali, vinginevyo haswali ng’o! 

Kwa hiyo ukimsubiri mpaka afikie umri wa miaka saba ndiyo umfunze siyo umuamrishe, mtagombana kila siku. Alijifunza kwanza ndiyo akawa Imamu katika umri huo mdogo. 

Baba na mama fahamuni kuwa nyie ni sababu kubwa ya watoto kuwa wema au waovu. Mtume (s.a.w.) amesema: 

"Kila mtoto anayezaliwa huzaliwa hali ya kuwa ni Muislamu. Basi wazazi wake ndiyo watakaombatiza wamfanye Myahudi au Mnaswara au Mamajusi" (Bukhari) 

Sio kumtoa katika dini kwa kumbatiza tu, bali waweza kumbakiza akaitwa Aisha, lakini asifanane kitabia na kiitikadi na huyo Aisha aliyekuwa mkewe Mtume (s.a.w.). Pengine kwa makusudi umempeleka mtoto wako akaimbe wimbo "Yesu ndiye Mungu Mkuu na kila goti lnapaswa lipigwe kwa jina lake" kwenye kituo cha malezi ya watoto kilichopo Kanisani. Na ukadharau kituo kilichopo Msikitini au madrasani kwenye wimbo huu: " Allah ndiye Mungu Mkuu; hana Mshirika; Yesu ni Nabii wake, Muhammad ni Nabii wake, ndiye wa mwisho aliye Bora". 

Wazazi jihadharini kwani nyie nyote ni wachungaji na mtaulizwa. Na hasa nyie wanawake ndiyo mtaulizwa zaidi kwani katika malezi ya watoto nyie mna sehemu kubwa. Mtume (s.a.w.) amesema katika Hadith iliyopokelewa na Ibn Umar (r.a.): 

"Kila mmoja wenu ni mchungaaji, na kila mmoja wenu ni mwenye kuulizwa kutokana na alichokichunga. Kiongozi ni mchungaji. Na mwanamume ni mchungaji juu ya watu wa nyumbani kwake. Na mwanamke ni mchungaji juu ya mumewe na watoto wake. Basi kila mmoja wenu ni mchungaji, na kila mmoja wenu ni mwenye kuulizwa kutokana na kile alichokichunga". (Bukhar na Muslim) 

Wazazi jihadharini na watoto wenu, kwani kuwapa malezi mema yanayoridhiwa na Allah (s.w.) ni sababu ya nyie kusalimika na adhabu ya Allah (s.a.), vinginevyo mtaangamia. Allah (s.w) amesema: 

"Enyi mlioamini! Kwa hakika baadhi ya wake zenu na watoto wenu ni maadui zenu, basi jihadharini nao. Na kama mkisamehe, na kuvumilia, na kughofiria, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu, Mwingi wa rehema. Bila shaka mali zenu na watoto wenu ni mtihani. Na kwa Mwenyezi Mungu kuna ujira mkubwa". (64:14-15) 

Tunapoangalia mwongozo wa Mtume (s.a.w.), tunapata mifano mingi katika kuwalea waoto. Kwa sababu yeye alikuwa mwalimu bora, na mlezi bora wa watoto, na alikuwa ndiye kiigizo chema. Kwa hakika Mtume (s.a.w.) alikuwa akitilia umuhimu rika la utoto katika kuzifunza nyoyo zao itikadi sahihi ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu (s.w) na alikuwa akiwafunza tabia njema, na akiwaongoza katika adabu zote kwa ujumla. 

Mmoja wa waliopata malezi ya Mtume (s.a.w) utotoni mwake ni Ibn Abbas (r.a.). Yeye anasimulia kuwa Mtume (s.a.w.) alimwambia yafuatayo: 

"Ewe kijana! Je, nikufundishe maneno atakayokunufaisha kwa maneno hayo Mwenyezi Mungu? Nikasema: Nifundishe. Akasema: Muhifadhi Mwenyezi Mungu, ataakuhifadhi. Muhifadhi Mwenyezi Mungu utamkuta mbele zako. Mjue wakati wa raha yako, atakujua wakati wa shida yako. Na unapoomba, Muombe Mwenyezi Mungu. Na unapotaka msaada, taka msaada kwa Mwenyezi Mungu. Kwa hakika imekauka kalamu kwa yale yaliyokuwa.  

Basi viumbe wote wangetaka wakunufaishe kwa jambo ambalo hakukuandikia Mwenyezi Mungu, hawataweza juu ya hilo. Na wakitaka wakudhuru kwa jambo ambalo hakukuandikia Mwenyezi Mungu, hawataweza juu ya hilo. Na jua kwamba katika kusubiri, juu ya yale yanayokuchukiza, mna kheri nyingi. Na kwa hakika nusra iko pamoja na kusubiri. Na kwa hakika faraja iko pamoja na matatizo. Na kwa hakika penye uzito kuna wepesi" (Ahmad) 

Inasimuliwa pia toka kwa Umar bin Abiy Salamah (r.a.) amesema: "Nilipokuwa (mtoto) katika nyumba za Mtume (s.a.w.) na ukawa mkono wangu unatembea pembe zote za shani, akaniambia: "Ewe mtoto! Mtaje Mwenyezi Mungu ( mwanzo wa kula) na ule kwa mkono wako wa kulia, na ule katika sehemu inayokuelekea" (Bukhari) 

Nasaha kwa wenye kumiliki Misikiti 

Enyi mliochukua jukumu la kumiliki (kuongoza) nyumba za Allah (s.w.) - Misikiti. Jihurumieni nafsi zenu kwa kitendo chenu cha kumnyang’anya mwenye nyumba hizo - Allah (s.w) "Hati miliki ya nyumba hizo", mkazifanya ni zenu eti kwa sababu mmetoa viwanja vyenu na sehemu ya mali zenu katika ujenzi wa Misikiti hiyo. Au nyie mkajifanya ndio warithi kwa kuwa walijenga wazee wenu hata kama nyie ni waovu! Au kwa kuwa mnaishi eneo lililokaribu na Misikiti hiyo kwa muda mrefu. Kumbukeni yafuatayo: 

Msikiti katika enzi za Mtume (s.a.w.) ulikuwa ni kituo cha harakati zote za kuueneza Uislamu. Tangu ustawi wa jamii - wanawake, vijana, watoto, mayatima, mafukara, masikini, wajane n.k. kwa hiyo iwacheni huru Misikiti itoe huduma za elimu, afya, lishe n.k. 

Msiwe ni chanzo cha kuzuia kheri ikiwa ni pamoja na kujengwa shule/madrasa, kufukuza watoto, kula zaka na sadaka isivyo halali n.k. 

Misikiti ni nyumba za Allah (s.w.) kwa hiyo haabudiwi ila Yeye Peke Yake. Kwa hiyo kuweni tayari kukiri makosa pale mnapokosea na kama mmeharibu, basi wajibikeni. 

Nasaha kwa wazazi 

Chungeni ndoa zenu kwani ni msingi mkubwa malezi. Pelekeni watoto wenu kwenye vituo vyenye kufunza itikadi sahihi. Wasimamieni watoto wenu watekeleze kwa vitendo vyote wanayofundishwa madrasa/shuleni. 

Nasaha kwa walimu 

Ili kulinda tabia njema iliyopo kwenye madrasa/shule zenu, ni bora msiwapokee watoto wanaotoka madrasa/shule nyingine mpaka mmepata maelezo kamili toka kwa walimu wao wa zamani. Mkigundua kuwa wana tabia ya kuhama hama bila sababu za msingi msiwapokee. 

Msiwe watumwa wa wazazi kwa kufundisha watakavyo wao, badala ya kufundisha atakavyo Allah (s.a.w). Timizeni malengo yenu mliyojiwekea kabla hamjafariki ili iwe ni sababu ya kuendelea kupata thawabu kaburini. 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
Maoni 
Kuwa na mawazo ya kufugwa tunajidharaulisha 

Sakata la mabucha  ya Nguruwe kuibuka upya 
Na Mwandishi Wetu  

Kondom sio kinga ya Ukimwi 

Bakwata yairushia polisi makombora Ngaramtoni 

MACHO YA SHUTUMA 
Na Abu Halima Sa Changwa 

Serikali yatakiwa iwachukulie hatua wauaji 
Na Mwandishi Wetu 

Historia ya Msikiti wa Ngaramtoni 

Silaha yetu ni kura ya pamoja 
Na Alhaj Yusuf Kalala, Washington DC  U.S.A 

Anuani ya fikra 
Na Abu Halima Sa Changwa 

Kuukaribisha mwezi mtukufu 

Tunahitaji "UN' ya Waislamu! 
Na Said  Rajab 

Kongamano la wanawake wa Kiislamu Newala lafana 

Umuhimu wa Elimu ya Awali kwa watoto wadogo - 2 
Na Ustaadh Kupa Pazi Said 

Kesi mojawapo ya mihadhara yafutwa 

Wasaidieni watoto wenye vipaji - Prof. Kilonzo 

Mahafali ya kidato cha nne Thaqafa: Wazazi wakumbushwa wajibu wao 

Wanafunzi Mwanza wadai haki za kuabudu mashuleni kwa usawa 
Na Iddi M. Katiba, Mwanza 

Saidianeni katika shida - Sheikh Abdallah 

Waislamu, Wakristo Rufiji watakiwa kuunda umoja 

Someni  muiokoe jamii kimaadili 

Acheni Shirki 

Kesi nyingine ya Waislamu Mwembechai yaahirishwa 
Na Muhibu Said 

Kusilimu kwa Wakristo kwaleta kero Mwanza 

Nzasa waomba msaada wa chakula, madawa 

Katibu wa Bakwata Moro ang'olewa Msikitini 

Masomo ya Dini ya Kiislamu  

Barua za Wasomaji 

Mashairi 

Chakula na lishe 
[Umuhimu wa chakula katika shule za awali]  

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita