AN-NUUR
Na.165 Jamadul Awwal 1419, Septembe 4 - 10, 1998
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA - 4 

Inatoka toleo lililopita 
 

Sura ya Nne 

Bunge la Shirikisho 

Sehemu ya kwanza 
 

BUNGE 

62 (1) Kutakuwa na Bunge la Shirikisho ambalo litakuwa na sehemu mbili, yaani Rais na Wabunge. 

2. Bunge litakuwa na Wajumbe wa aina moja ilizotajwa katika ibara ya Katiba hii ambao wote wataitwa Senators. 

3. Iwapo jambo lolote lahitaji kuamuliwa au kutekelezwa na sehemu zote mbili za Bunge kwa mujibu wa masharti ya katiba hii, basi jambo hilo halitahesabiwa kuwa limeamuliwa au limetekelezwa ipasavyo ila mpaka liwe limeamuliwa au limetekelezwa na Wabunge na vile vile na Rais, kwa mujibu wa madaraka yao kuhusu jambo hilo. 
 

Madaraka ya Bunge 

63. (1) Rais kama sehemu moja ya Bunge atatekeleza madaraka yote aliyokabidhiwa na Katiba hii kwa ajili hiyo. 

(2) Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Shirikisho ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi kusimamia na kuishauri Serikali ya Shirikisho na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba hii. 

(3) Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya Katiba hii Rais atawajibika kufuata na kutekeleza maamuzi yote ya Bunge. 

(4) Kwa madhumuni ya utekelezaji wa madaraka yake Bunge laweza- 

(a) kumuuliza Waziri yeyote swali lolote kuhusu mambo ya Umma katika Shirikisho ambayo yako katika wajibu wake; 

(b) kujadili utekelezaji wa kila Wizara wakati wa Mkutano wa Bunge kila mwaka wa bajeti; 

(c)kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Shirikisho, na kutunga sheria ya kusimamia ;utekelezaji wa mpango huo; 

(d) kutunga sheria pale ambapo utekelezaji unahitaji kuwapo sheria; 

(e) kujadili na kuridhia mikataba yote inayohusu Shirikisho na ambayo kwa masharti yake inahitaji kuridhiwa. 

(f) Kujadili na kuridhia uteuzi wa Rais wa viongozi wa Shirikisho waliotajwa katika Katiba hii. 
 

Madaraka ya kutunga sheria 

64. (1) Mamlaka yote ya kutunga sheria juu ya mambo yote ya Shirikisho yatakuwa mikononi mwa Bunge. 

(2) Mamlaka yote ya kutunga sheria katika Tanganyika juu ya mambo yote yasiyo ya Shirikisho kwa upande wa Tanganyika yatakuwa mikononi mwa Bunge la Tanganyika. 

(3) Mamlaka yote ya kutunga sheria katika Zanzibar juu ya mambo yote yasiyo ya Shirikisho yatakuwa mikononi mwa Bunge la Zanzibar. 

(4) Endapo sheria yoyote iliyotungwa na Bunge la Tanganyika au Zanzibar inahusu jambo lolote katika Tanganyika au Zanzibar ambalo liko chini ya mamlaka ya Bunge, la Shirikisho sheria hiyo itakuwa batili ;na itatenguka. 

(5) Sheria yoyote iliyotungwa na Bunge la shirikisho kuhusu jambo lolote haitatumika Tanganyika au Zanzibar ila kwa mujibu wa masharti yafuatayo- 

(a) Sheria hiyo iwe imetamka wazi kwamba itatumika Tanganyika na vile vile Zanzibar au iwe inabadilisha, kurekebisha au kufuta sheria inayotumika Tanganyika au Zanzibar, au 

(b) Sheria hiyo iwe inahusu mambo ya shirikisho, na kila inapotajwa Tanzania katika sheria yoyote ifahamike kuwa Sheria hiyo itatumika katika shirikisho kwa mujibu wa ufafanuzi uliotolewa na masharti ya ibara hii.. 

65. Kwa mujibu wa Katiba hii kuhusu mambo yote ya Tanganyika au Zanzibar yasiyo mambo ya Shirikisho, Katiba hii itakuwa na nguvu katika Shirikisho zima na endapo sheria nyingine yoyote itakiuka masharti yaliyomo katika Katiba hii, Katiba hii ndiyo itakuwa na nguvu, na Katiba au sheria hiyo nyingine, kwa kiasi inachokiuka Katiba hii itakuwa batili. 
 

Muda wa Bunge 

66.(1) Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya Katiba hii, maisha ya kila Bunge yatakuwa ni muda wa miaka mitano. 

(2) Kwa madhumuni ya Katiba hii maneno "maisha ya Bunge" maana yake ni ule muda wote unaoanzia tarehe ambapo Bunge jipya limeitishwa kukutana kwa mara ya kwanza baada ya uchaguzi mkuu wa kuishia tarehe ya kuvunjwa kwa Bunge kwa ajili ya kuwezesha uchaguzi Mkuu mwingine wa kawaida kufanyika. 
 

Sehemu ya Pili 

Wabunge, na uchaguzi wa Wabunge 

Wajumbe wa Bunge 
 

Wabunge 

67. (1) Bila ya kuathiri masharti mengine ya ibara hii, kutakuwa na aina zifuatazo za Wabunge, yaani 

(a) Wabunge waliochaguliwa kuwakilisha majimbo ya uchaguzi katika Shirikisho 

(b) Wabunge wa kuchaguliwa kuwakilisha majimbo ya uchaguzi katika Tanganyika na Zanzibar 

(2) Rais na Makamu wa Rais kila mmoja wao anaweza kuwa Mbunge. 

Sifa za mtu kuwa Mbunge 

68.(1) Bila ya kuathiri masharti yaliyomo katika ibara hii, mtu yeyota atakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa kuwa Mbunge endapo- 

(a) ni raia wa Shirikisho aliyetimiza umri wa miaka ishirini na moja, na ambaye ana elimu ya kutosha. 

(b) ni mwanachama na ni mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa; au ni mgombea binafsi aliyetimiza masharti yaliyotajwa katika Katiba hii. 

(2) Mtu hatakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa kuwa Mbunge- 

(a) ikiwa mtu huyo anao au kwa hiari yake amejipatia uraia wa nchi nyingine yoyote; au 

(b) ikiwa ni mujibu wa Sheria inayotumika katika Shirikisho imethibitishwa rasmi kwamba mtu huyo ana ugonjwa wa akili, au 

(c) ikiwa mtu huyo amehukumiwa na mahakama yoyote katika Shirikisho na kupewa adhabu ya kifo au ya kufungwa gerezani kwa muda unaozidi miezi sita kwa kukutwa na hatia ya kosa lolote, vyovyote linavyoitwa, linaloambatana na utovu wa uaminifu; au 

(d) ikiwa katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya Uchaguzi Mkuu amepata kuhukumiwa na kupewa adhabu ya kifungo kwa kosa linaloambatana na utovu wa uaminifu au kwa kuvunja sheria ya Maadili ya viongozi wa Umma. 

(e) ikiwa mtu huyo ameshika madaraka ya afisa mwandamizi katika utumishi wa Serikali ya Shirikisho 

(f) ikiwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge inayoshughulikia makosa yanayohusika na uchaguzi wa aina yoyote mtu huyo amezuiliwa kujiandikisha kama mpiga kura au kupiga kura katika uchaguzi wa Wabunge. 

(3) Ifahamike kuwa mtu aweza kugombea uchaguzi kuwa Mbunge wa kuwakilisha jimbo la uchaguzi katika uchaguzi Mkuu wowote ikiwa wakati huo yeye amesimama katika uchaguzi kugombea kiti cha Rais. 

(4) Bunge lawezi kutunga sheria kwa ajili ya kuweka masharti yatakayomzuia mtu asichaguliwe kuwa Mbunge wa kuwakilisha jimbo la uchaguzi ikiwa mtu huyo ni menye madaraka ya nayohusika na shughuli za kuongoza au kusimamia uchaguzi wa Wabunge au shughuli za uandikishaji wa wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Wabunge; isipokuwa kwamba Sheria kama hiyo haiwezi kuweka masharti yatakayomzuia Spika wa Bunge asichaguliwe kuwa Mbunge wa kuwakilisha Wilaya au Mkoa wa uchaguzi, wala masharti yatakayosababisha mtu aliyechaguliwa kuwa Spika kupoteza kiti hicho cha Spika au kiti chake cha kawaida katika Bunge. 

(5) Bunge laweza kutunga sheria kwa ajili ya kuweka masharti yatakayomzuia mtu asichaguliwe kuwa Mbunge wa kuwakilisha jimbo la uchaguzi kwa muda wowote utakaotajwa na Bunge (ili mradi muda huo usizidi miaka mitano) ikiwa mtu huyo atapatikana na hatia mbele ya mahakama kwa ajili ya aina yoyote ya makosa yatakayotajwa katika Sheria hiyo yanayohusika na uchaguzi wa Wabunge. 

(6) Kanuni zifuatazo zitatumika kwa ajili ya ufafanuzi wa aya ya (c) , na ya (d) (e) za ibara ndogo ya (2) ya ibara hii, yaani- 

ikiwa mtu atapewa adhabu ya kufungwa gerezani ikifahamika kuwa adhabu hiyo ya kifungo imetolewa badala ya adhabu ya kutozwa faini au imetolewa kwa sababu mtu huyo ameshindwa kulipa faini aliyaomriwa kulipa, basi muda wa kifungo cha namna hiyo hautahesabiwa. 

(7) Kwa ajili ya ufafanuzi wa maelezo kuhusu sifa za uchaguzi yaliyomo katika ibara zifuatazo, kila atakapotajwa katika Katiba hii kwamba utekelezaji wa jambo lolote wahitaji mtu mwenye sifa au uchaguzi au mtu ambaye hakupokeza sifa za uchaguzi, basi isipokuwa kama maelezo yahitajika vinginevyo, ifahamike kuwa sifa zinazohusika ni zile zinazomwezesha mtu kuchaguliwa kuwa Mbunge wa kuwakilisha jimbo la uchaguzi kama ilivyoelezwa katika ibara ndogo ya (1) ya ibara hii. 
 

Kiapo cha Wabunge 

69 .Kila mbunge atatakiwa kuapishwa katika Bunge kiapo cha uaminifu kabla hajaanza kushiriki katika shughuli za Bunge; lakini Mbunge aweza kushiriki katika uchaguzi wa Spika hata kabla hajaapishwa. 

Tamko rasmi la Wabunge kuhusu maadili ya viongozi 

70. (1) Kila Mbunge atatakiwa, kabla ya kumalizika siku thelathini tangu aapishwe kushika madaraka yake kama Mbunge kuwasilisha kwa Spika nakala mbili za tamko rasmi kwamba hajapoteza sifa za uchaguzi kwa mujibu wa masharti ya aya ya 

(d) ya ibara ndogo ya (2) ya ibara ya 67 

(2) Tamko rasmi linalotakiwa kuwasilishwa kwa Spika kwa mujibu wa masharti ya ibara hii litatolewa kwa kutumia fomu maalum itakayowekwa kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge. 
 

Muda wa Wabunge kushika madaraka 

71, (1) Mbunge atakoma kuwa Mbunge na ataacha kiti chake katika Bunge litokeapo lolote kati ya mambo yafuatayo- 

(a) ikiwa litatokea jambo lolote ambalo kama asingekuwa Mbunge lingemfanya asiwe na sifa za uchaguzi au apoteze sifa za uchaguzi au asiweze kuchaguliwa au kuteuliwa kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii; 

(b) ikiwa jimbo analoliwakilisha limepiga kura ya kutokuwa na imani na Mbunge wake na kutamka asiendelee kuwa Mbunge wa jimbo hilo na kwamba uamuzi huo umeshawakilishwa kwa Spika wa Bunge; 

(c) ikiwa itathibitishwa kwamba amevunja masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma; 

(d) iwapo Mbunge anachaguliwa au anateuliwa kuwa makamu wa Rais; 

(f) kwa Mbunge ambaye anatakiwa kutoa taarifa rasmi ya mali kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 73, ikiwa atashindwa kutoa hilo tamko rasmi kwa mujibu wa masharti ya hiyo ibara ya 73 katika muda uliowekwa mahususi kwa ajili hiyo kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge, 

Lakini iwapo Mbunge hatakoma kuwa Mbunge kwa mujibu wa jambo lolote kati ya mambo hayo yaliyotajwa na kama hatajiuzulu au kufariki mapema zaidi basi Mbunge ataendelea kushika madaraka yake kama tu Mbunge mpaka wakati wa Uchaguzi Mkuu utakaofuata. 

(2) Kwa mujibu wa katiba hii Mbunge hatahesabika kupoteza kiti chake cha ubunge endapo atajiuzulu uanachama wa chama chake cha siasa au hufukuzwa uanachama na chama chake cha siasa mbunge huyo atahesabika kuwa mbunge wa kujitegemea mpaka kipindi cha ubunge wake kisha katika kipindi hicho chote haruhusiwi kujiunga na chama chochote cha siasa 

(3) Bunge laweza kutunga Sheria kwa ajili ya kuweka masharti yatakayomwezesha Mbunge kukata rufaa, kwa mujibu wa Sheria kupinga hukumu ya kuthibitishwa kwake kuwa ni mtu mwenye ugonjwa wa akili au kupinga kupatikana kwake na hatia kwa kosa la aina iliyotajwa kwa mujibu wa masharti ya ibara ya (5) ya ibara ya 68 ya Katiba hii na sheria hiyo yaweza kueleza kwamba hiyo hukumu iliyopingwa na huyo Mbunge haitatiliwa nguvu kisheria mpaka umalizike kwanza muda utakaotajwa katika Sheria hiyo. 
 

Watu wenye madaraka Serikalini kukoma utumishi wanapochaguliwa 

72. Iwapo mtu yeyote mwenye madaraka katika utumishi wa Serikali, madaraka aina iliyotajwa katika ibara ya 68 (2) (e) ataamua:- 

(a) kuwa mgombea uchaguzi wa Rais au Makamu wa Rais au Mbunge, 

(b) kugombea uongozi wa ngazi yoyote katika chama cha siasa kinyume na masharti ya ajira, 

Mtu huyo atahesabiwa kuwa utumishi wake umekoma tangu tarehe yake ya kuwa mgombea uchaguzi au ya kugombea uongozi katika chama cha siasa. 
 

Masharti ya kazi ya Wabunge 

73. Wabunge wote wa aina zote watalipwa mshahara, posho na malipo mengineyo kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge. 
 

Tume ya Uchaguzi 

74. (1) Kutakuwa na Tume ya Uchaguzi ya Shirikisho ambayo itakuwa na wajumbe wafuatao watakaoteuliwa na Rais kutokana na majina yatakayopendekezwa kwake na vyama vya siasa vilivyoandikishwa pamoja na jumuia au Taasisi binafsi za umma. 

(2) Tume ya uchaguzi itakuwa ni idadi ya wajumbe wasiopungua watano na wasiozidi kumi na tano. 

(3) Majina yatakayopendekezwa kwa Rais kama ilivyoelezwa katika ibara ndogo ya (1) yatatokana na watu ambao siyo wanachama wa chama chochote cha siasa ambacho kimeandikishwa. 

(4) Kila uteuzi utakaofanywa na Rais kwa mujibu wa ibara ndogo ya 1 sharti ithibitishwe na Bunge. 

(5) Wajumbe wa Tume watawachagua Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi kwa kufuata kanuni kwamba endapo Mwenyekiti ni mtu anayetoka sehemu moja ya Shirikisho, Makamu wake atakuwa ni mtu anayetoka sehemu ya pili ya Shirikisho na uchaguzi huo uwe umefanyika katika Mkutano wa kwanza wa Tume ya Uchaguzi. 

(6) Watuw afuatao hawataweza kuteuliwa kwa wajumbe wa Tume ya Uchaguzi yaani- 

(a) Waziri au Naibu Waziri, Jaji wa Mahakama Kuu au ya Rufaa au afisa mwandamizi kwenye utumishi wa Serikali. 

(b) Mbunge, au Diwani. 

(c) Mwanachama wa chama chochote cha siasa. 

(7) Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya ibar ahii, Mjumbe wa Tume ya uchaguzi atakoma kuwa Mjumbe litokeapo lolote kati ya mambo yafuatayo- 

(a) ukimalizika muda wa miaka mitano tangu alipoteuliwa; na ieleweke kwamba mjumbe anaweza kuteuliwa tena kwa kipindi kimoja kingine, au;\(b) ikiwa litatokea jambo lolote ambalo, kama asingekuwa Mjumbe wa Tume, lingemfanya asiweze kuteuliwa kuwa Muumbe wa Tume ya Uchaguzi. 

(8) Rais aweza tu kumwondoa katika madaraka Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi kwa sababu ya kushindwa kutekeleza kazi zake, ama kutokana na maradhi, au kwa sababu ya tabia mbaya au kupoteza sifa za kuwa mjumbe na kwamba uamuzi huo utathibitishwa na Bunge. 

(9) Majukumu ya Tume ya Uchaguzi yatakuwa ni- 

(a) kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura katika uchaguzi wa Rais na Wabunge katika Shirikisho; 

(b) kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa Rais na Wabunge; na 

(c) kuchunguza mipaka na kuigawa shirikisho katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi wa Wabunge; 

(d) kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura na uendeshaji wa uchaguzi wa madiwani. 

(e) kutekeleza majukumu mengine yoyote kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge. 

(10) Kwa madhumuni ya utekelezaji bora wa majukumu yake, Tume ya Uchaguzi itakuwa ni idara inayojitegemea na mtendaji mkuu wake atakuwa ni Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye atateuliwa na kufanya kazi kwa mujibu wa masharti ya Sheria iliyotungwa na Bunge. 

(11) Bunge laweza kutunga sheria kwa ajili ya kuweka masharti ya kuweka utaratibu wa kusimamia uchaguzi wa Wabunge wanaowakilisha majimbo ya uchaguzi. 

(12) Tume ya uchaguzi yaweza kutekeleza shughuli zake bila ya kujali kwamba kuna nafasi miongoni mwa viti vya Wajumbe au kwamba Mjumbe mmoja wapo hayupo , lakini kila uamuzi wa Tume ni lazima uungwe mkono na wajumbe walio wengi kati ya wajumbe wote wa Tume. 

(13) Bunge laweza kutunga sheria kwa ajili ya kuweka masharti ya kuweka utaratibu wa kuwateua Wajumbe wa kusimamia uchaguzi wa Wabunge wanaowakilisha majimbo ya uchaguzi na , bila ya kuathiri masharti ya Sheria kama hiyo au maagizo ya Tume ya Uchaguzi, madaraka ya tume ya uchaguzi ya kusimamia uchaguzi yaweza kutekelezwa na wajumbe hao. 

(14) Katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii, Tume ya uchaguzi haitalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu yeyote au idara yoyote ya Serikali, au maoni ya chama chochote cha siasa. 

(15) Katika utekelezaji wa madaraka yake kwa mujibu wa Katiba hii, Tume ya Uchaguzi ya Shirikisho itashauriana mara kwa mara na Tume ya uchaguzi ya Tanganyika na Tume ya uchaguzi ya Zanzibar. 

(16) Itakuwa ni marufuku kwa watu wanaohusika na uchaguzi kujiunga na chama chochote cha siasa, isipokuwa tu kwamba kila mmoja wao atakuwa na haki ya kupiga kura iliyotajwa katika ibara ya 17 ya Katiba hii. 

(17) kwa madhumuni ya ibara ndogo ya (16) watu wanaohusika na uchaguzi ni- 

(a) Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, 

(b) Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, 

(c) Wajumbe wote wa Tume ya Uchaguzi, 

(d) Mkurugenzi wa uchaguzi pamoja na watumishi wote wa Tume ya Uchaguzi. 

(e) Wasimamizi wote wa Uchaguzi katika majimbo ya uchaguzi. 

(18) 

Baada ya kumaliza muda wao katika Tume ya Uchaguzi itakuwa ni marufuku kwa mjumbe yeyote kujihusisha na siasa mpaka muda wa miaka mitatu uwe umepita tangu kuacha kuwa mjumbe wa Tume ya uchaguzi. 

(19) Wajumbe wa Tume ya uchaguzi hawatafanya kazi siku hadi siku (part timers). 
 

Majimbo ya Uchaguzi 

75. (1) Bila ya kuathiri masharti mengineyo yaliyo katika ibara hii kila mkoa katika shirikisho litakuwa jimbo la uchaguzi kwa wabunge wa bung ela shirikisho ikumbukwe pia kila wilaya katika shirikisho litakuwa jimbo la uchaguzi kwa wabunge wa mabunge ya Tanganyika na Zanzibar. 

(2) Tume ya uchaguzi, itakuwa na mamlaka ya kuweka mpaka ya majimbo ya uchaguzi. Na baada ya kufanya hivyo itawakilisha maamuzi yake Bungeni kwa uthibitisho. 

(3) Bila ya kuathirika masharti ya Katiba hii, Tume ya Uchaguzi yaweza mara kwa mara, na angalao kila baada ya miaka kumi, kuchunguza mgawanyo wa Shirikisho katika majimbo ya uchaguzi, na yaweza kubadilisha majimbo ya uchaguzi kama matokeo ya uchaguzi huo au kutokana na matokeo ya hesabu ya watu wote katika Shirikisho. 

(4) Endapo baada ya uchaguzi kufanywa kuhusu mgawanyo wa Shirikisho katika majimbo ya uchaguzi kunafanyika mabadiliko katika majimbo ya uchaguzi, au katika idadi ya Wabunge wanaowakilisha majimbo ya uchaguzi au mabadiliko kwa idadi ya majimbo ya uchaguzi au idadi ya Wabunge, basi mabadiliko yatakayotokea katika idadi ya Wabunge wanaowakilisha majimbo ya uchaguzi yataanza kutumika wakati Bunge litakapovunjwa tena baada ya kutokea mabadiliko hayo ya idadi ya majimbo au idadi ya Wabunge katika majimbo ya uchaguzi. 
 

Uchaguzi na Uteuzi wa Wabunge 

Uchaguzi katika majimbo ya uchaguzi 

76. (1) Kila mara baada ya Bunge kuvunjwa, kutakuwa na uchaguzi wa Wabunge katika majimbo yote ya uchaguzi. 

(2) Ikiwa kiti cha Mbunge yeyote aliyechaguliwa kuwakilisha jimbo la uchaguzi, kitakuwa wazi kwa sababu nyingine yoyote isiyohusika na kuvunjwa kwa Bunge basi mshindi wa pili katika matokeo ya uchaguzi wa Mbunge wa jimbo hilo atatangazwa na Tume ya Uchaguzi kuwa Mbunge wa jimbo hilo. 

(3)Bila ya kujali masharti ya ibara hii yaliyotangulia, ifahamike kwamba ikiwa tarehe ya kuvunja Bunge imetangazwa au inafahamika kutokana na matukio yaliyoelezwa katika ibara ndogo ya (3) ya ibara ya 90, basi uchaguzi wa namna hiyo hautafanywa katika kipindi chote cha miezi sita ya nyuma ikihesabiwa tangu tarehe hiyo. 
 

Utaratibu wa uchaguzi wa wabunge wa majimbo ya uchaguzi 

77. (1) Wabunge wanaowakilisha majimbo ya uchaguzi watachaguliwa na wananchi kwa kufuata masharti ya Katiba hii na vile vile masharti ya Sheria iliyotungwa na Bunge kwa mujibu wa Katiba hii inayoweka utaratibu kuhusu uchaguzi wa Wabunge wanaowakilisha majimbo ya uchaguzi. 

(2) Kutachaguliwa Mbunge mmoja tu katika jimbo la uchaguzi. 

(3) Wagombea uchaguzi katika jimbo la uchaguzi watatakiwa watimize masharti yafuatayo- 

(a) wawe wamependekezwa mmoja mmoja, na vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi katika jimbo hilo; 

(b) wamewasilisha majina yao kwa Tume ya Uchaguzi kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na Sheria iliyotungwa na Bunge; 

(c) na kama ni wagombea binafsi wawe wamewasilisha majina yao na sera zao kwa Tume ya Uchaguzi kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na Sheria ya Bunge. 
 

Uamuzi wa suala kama mtu ni Mbunge 

78. (1) Kila shauri kwa ajili ya kupata uamuzi juu ya suala- 

(a) Kama uchaguzi au uteuzi wa mtu yeyote kuwa Rais au Makamu wa Rais ulikuwa halali au sivyo, au 

(b) kama uchaguzi au uteuzi wa mtu yeyote kuwa mbunge ulikuwa halali au sivyo; au 

(c) Kama Rais au Makamu wa Rais amekoma kuwa Rais au Makamu wa Rais na kiti chake ki - wazi au, 

(d) kama Mbunge amekoma kuwa Mbunge na kiti chake katika Bunge ki wazi au hapana litafunguliwa na kusikilizwa kwanza katika Mahakama ya Shirikisho. 

(2)Bunge laweza kutunga sheria kwa ajili ya kuweka masharti kuhusu mambo yafuatayo- 

(a) watu wanaoweza kufungua shauri katika mahakama ya Shirikisho kwa ajili ya kupata uamuzi juu ya suala lolote kwa mujibu wa masharti ya ibara hii; 

(b) sababu na nyakati za kufungua shauri la namna hiyo, utaratibu wa kufungua shauri na masharti yanayotakiwa yatimizwe kwa kila shauri kama hilo; na 

(c) kutaja mamlaka ya Mahakama Shirikisho juu ya shauri kama hilo na kueleza utaratibu wa kusikiliza shauri lenyewe. 

(3) Kutakuwa na haki ya kukata rufaa mbele ya Mahakama ya Rufani ya Shirikisho kupinga uamuzi wa Mahakama Shirikisho juu ya shauri lolote lililosikilizwa kwa mujibu wa masharti ya ibara hii. 
 

Sehemu ya tatu 

Utaratibu, madaraka na haki za Bunge 

Spika na Naibu wa Spika 

Spika na mamlaka yake 

79. (1) Kutakuwa na Spika wa Bunge ambaye atachaguliwa na Wabunge kutoka miongoni mwa watu ambao ni Wabunge au wenye sifa za kuwa Wabunge; atakuwa ndiye kiongozi wa Bunge na atawakilisha Bunge katika vyombo na vikao vingine vyote nje ya Bunge. 

(2) Waziri, Naibu Waziri au mtu mwenye madaraka ya aina nyingine yoyote itakayotajwa na sheria iliyotungwa na Bunge kwa madhumuni ya ibara hii, hataweza kuchaguliwa kuwa Spika. 

(3) Mtu yeyote atakayechaguliwa kuwa Spika atatakiwa, kabla ya kumaliza siku kumi na tano tangu kuchaguliwa kwake, kuwasilisha kwa Rais tamko rasmi kwamba hajapoteza sifa za uchaguzi kwa mujibu wa masharti ya aya ya (d) ya ibara ndogo ya (2) ya ibara ya 69. Tamko hilo litatolewa kwa kutumia fomu maalum itakayowekwa kwa kutumia fomu maalum itakayowekwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge. 

(4) Rais atawasilisha kwa Kamishana wa Maadili nakala moja ya kila tamko rasmi lililowasilishwa kwake kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (3) ya ibara hii. 

(5) Spika atatakiwa kuwasilisha kwa Rais nakala mbili za taarifa rasmi ya maelezo ya mali ya huyo Spika na, kadri itakavyokuwa, mali ya mke au mume wake. Spika atatoa taarifa hiyo kwa kutumia fomu maalum iliyowekwa kwa ajili hiyo kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge na atatoa taarifa ya namna hiyo mara kwa mara kadri itakavyoagiza sheria hiyo. 

(6) Masharti ya ibara ya 72 yatatumika pia, kwa kadri itakavyowezekana , kwa taarifa ya mali yoyote itakayotolewa na Spika, kwa mujibu wa masharti ya ibara hii. 

(7) Spika atakoma kuwa Spika na ataacha kiti cha Spika litokeapo lolote kati ya mambo yafuatayo- 

(a) Iwapo mtu huyo alichaguliwa kutoka miongoni mwa Wabunge, basi ikiwa atakoma kuwa Mbunge kwa sababu yoyote ambayo haihusiki na kuvunjwa Bunge; au 

(b) ikiwa kutatokea jambo lolote ambalo, kama asingekuwa Spika, lingemfanya mtu huyo asiwe na sifa za uchaguzi au apoteze sifa za uchaguzi wa Spika; au 

(c) ikiwa mtu huyo ataondolewa kwenye madaraka ya Spika kwa azimio la Bunge lililoungwa mkono na Wabunge ambao idadi yao haipungui theluthi mbili ya Wabunge wote; au 

(d) ikiwa mtu huyo atashindwa kuwasilisha kwa Rais tamko rasmi kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (3) ya ibara hii; au 

(e) ikiwa mtu huyo atapatikana na hatia kwa kosa la kutoa habari za uongo, kwa kiapo kinyume cha sheria ya kanuni ya Jinai, kuhusu tamko rasmi lolote lililotolewa kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (3) ya ibara hii; au 

(f)ikiwa mtu huyo atashindwa kuwasilisha kwa Rais taarifa ya mali kwa mujibu wa masharti ya ibara ndogo ya (5) ya ibara hii kabla ya kumalizika muda uliowekwa kwa ajili hiyo kwa mujibu wa Sheria iliotungwa na Bunge; 

(g) ikiwa itathibitika kuwa mtu huyo amevunja masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma; 

(8) Hakuna shughuli yoyote itakayotekelezwa katika Bunge (isipokuwa uchaguzi wa Spika) wakati wowote ambao kiti cha Spika kitakuwa ki wazi. 

(9) Mtu yeyote ambaye si Mbunge atakayechaguliwa kuwa Spika, atatakiwa kabla ya kuanza kutekeleza madaraka yake, kuapishwa katika Bunge kiapo cha uaminifu. 
 

Naibu wa Spika 

80. (1) Kutakuwa na Naibu wa Spika wa Bunge ambaye atachaguliwa na Wajumbe kutoka miongoni mwa Wabunge. 

(2) Waziri, Waziri mdogo au mtu mwenye madaraka ya aina nyingine yoyote itakayotajwa na Sheria iliyotungwa na Bunge kwa madhumuni ya ibara hii, hataweza kuchaguliwa kuwa Naibu wa Spika. 

(3) Wabunge watamchagua Naibu wa Spika nyakati zifuatazo- 

(a) Bunge litakapokutana kwa mara ya kwanza baada ya Uchaguzi Mkuu au mapema iwezekanavyo baada ya wakati huo; na 

(b) katika kikao cha kwanza cha Bunge baada ya kiti cha Naibu wa Spika, kuwa wazi kwa sababu yoyote isiyohusika na Bunge kuvunjwa au mapema iwezekanavyo baada ya kikao hicho. 

(4) Naibu wa Spika, atakoma kuwa Naibu wa Spika na ataacha kiti cha Naibu wa Spika, litokeapo lolote kati ya mambo yafuatayo- 

(a) ikiwa mtu huyo atakoma kuwa Mbunge; au 

(b) ikiwa kutatokea jambo lolote ambalo kama asingekuwa Naibu wa Spika, lingemfanya mtu huyoasiwe na sifa za uchaguzi au apoteze sifa za uchaguzi wa Naibu wa Spika; au 

(c) ikiwa mtu huyo ataondolewa kwenye madaraka ya Naibu wa Spika kwa azimio la Bunge. 

Utaratibu wa kumchagua Spika na Naibu wa Spika 

81. (1) Kutakuwa na uchaguzi wa Spika katika kikao cha kwanza cha Mkutano wa Kwanza wa Bunge jipya, na katika kikao cha kwanza chochote mara baada ya kutokea nafasi katika kiti cha Spika. 

(2) Kutakuwa na uchaguzi wa Naibu wa Spika wakati wowote katika Mkutano wa Kwanza wa Bunge Jipya utakaoteuliwa na Bunge na vile vile katika kikao cha kwanza cha bunge mara baada ya kutokea nafasi katika kiti cha Naibu wa Spika. 

(3) Uchaguzi wa Spika, na vile vile uchaguzi wa Naibu wa Spika, utafanywa kjwa kura ya siri, na utaendeshwa kwa kufuata utaratibu uliowekwa na kanuni za Bunge. 
 

Ofisi ya Bunge 

Katibu wa Bunge 

82. (1) Kutakuwa na Katibu wa Bunge ambaye atateuliwa na Rais kulingana na mapendekezo ya Tume ya Utumishi Serikalini. 

(2) Katibu wa Bunge atakuwa ndiye mtendaji mkuu katika ofisi ya Bunge na atawjaibika kwa utendaji bora wa shughuli za Bunge kwa kuzingatia masharti ya Katiba hii. 

Sekretariati ya Bunge 

83. (1) Kutakuwa na Sekretariati ya Bunge itakayokuwa na nafasi za madaraka katika utumishi wa Serikali kwa idadi atakayoagiza na Tume ya Utumishi Serikalini. 

(2) Sekretariati ya Bunge itakuwa na watumishi kwa idadi na ngazi za utumishi itakavyoamuliwa mara kwa mara na tume ya Utumishi inayohusika baad aya kushauriana na Katibu wa Bunge. 

(3) Sekretariati ya Bunge chini ya uongozi wa Katibu wa Bunge itaendeleza kazi na shughuli zote zilizowekwa au zitakazokuwa ni muhimu kwa ajili ya kuhakikisha utekelezaji bora wa Bunge na wa Wabunge wa madaraka ya Bunge chini ya katiba hii. 

Itaendelea toleo lijalo
 
 

Juu 
 

YALIYOMO
 
 
TAHARIRI 
HAKI YA KUABUDU MASHULENI: Hoja ya uwingi isizuie haki ya wachache 

Aliyeandika Yesu si Mungu bado akabiliwa na kesi 
Na Mwandishi Wetu 

Wazazi walia na Mkuu wa shule Mkwawa 
Na Mwandishi Wetu, Iringa 

Serikali iache kudhulumu  Waislamu - Bakwata  
Na Mwandishi Wetu

KESI YA MIRATHI: Hukumu ya Jaji Agostino yatupwa 
Na Mwandishi Wetu 

Sumaye sasa atoa ‘waadhi’ Msikitini 
Na Mwandishi Wetu, Arusha 

Sekondari ya Kiislamu Sumbawanga, mtihani kwenu – Sheikh Akilimali 
Na Harun Rashid, Sumbawanga 

37 wasilimu  Mwanza 
Na Mwandishi Wetu, Mwanza 

Akamatwa kwa kusoma gazeti la ANNUUR ! 

MGOGORO WA CHWAKA NA MARUMBI: Serikali ya Dk. Salmin itafute ufumbuzi 
Na Mwandishi Wetu, Pemba 

MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA - 4 

Kwa nini walengwa wa mabomu wawe ni Marekani? 
Na Maalim Ali Bassaleh 

Profesa amekosea kusema kwamba... 
Na A.M. Hamza 

Ugaidi ni ugaidi, hata wa Marekani ni ugaidi 
Na Maalim Ali Bassaleh 

Dhana ya Udugu wa kiislamu 

UGAIDI: Chanzo si magaidi, ni dhuluma ya Marekani 
Na HASSAN KIMANGALE 

Jengeni familia bora 
Na Abuu Said, Iringa 

Tuwasaidie Waislamu kielimu na kiuchumi - Bi Zuhura 
Na SAID RAMADHANI KISSIMBA 

Tumieni uhuru wenu vyema 
Na Abuu Zaina, Iringa 

Hoja za kutofautisha Yesu na Issa ni udhaifu,  ni uzushi mtupu! - 4  
Na Muhibu Said 

Mihadhara ya Wakristo yatawala Handeni 
Na Mwandishi Wetu, Handeni 

Ziara ya Kadinali Pengo Moro  
Na Mussa Ally, Morogoro 

Aonyesha ujuzi wa kutengeneza Trekta 
Na Mwandishi Wetu 

Waislamu wasizifanye sharia za dini kuwa nzito – Sheikh Mzonge 
Na Ashraf  Yusuf, Moshi 

Sengerema waomba msaada 
Na Idd Katimba, Mwanza 
 
Mafundisho ya Quran 

Barua za wasomaji 

Mashairi: 

Masomo ya dini ya Kiislam 

Chakula na Lishe 
Matunzo ya mtoto mwenye lishe duni 

Matangazo 
 
 

 

 

 

 
 Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:
Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita