|
|
| Profesa
amekosea kusema kwamba...
Na A.M. Hamza KWENYE mahojiano yao walioyafanya kati ya Mhariri wa Msemakweli na Profesa Kaisi; katika gazeti la Msemakweli – Agosti 16-22, 1998 Mhariri alimuuliza Profesa, na akamjibu maswali kadhaa. Swali moja, lile linalohusu kama "Waislamu na Wakristo wanaamini na kumwabudu Mungu yule yule mmoja?" Majibu yake Profesa ameyakosea mno, kwa mujibu wa Biblia yenyewe kiasi kwamba nimeona kuwa ni lazima makosa haya yawekwe sawa. Kwenye sehemu ya kwanza ya jibu lake, lazima nikiri kuwa "Mungu" wa Ukristo, "Mungu mwenye Roho Mtakatifu na Mwana nafsini mwake". Siye Mungu tunayemwabudu Waislamu. Mungu tunayemuamini na kumuabudu ana nafsi moja tu (Isaya 45:23, Qur’an 2:163), hana mwana, hakuzaa wala hakuzaliwa (Isaya 43:10, Qur’an 112:3). Nimeweka nukuu za Biblia makusudi ili kumthibitishia Profesa kuwa kauli yake ya pili kwenye jibu lake ni kosa kubwa katika masuala ya dini ya Mwenyezi Mungu. Ni kosa kubwa kudai, kama alivyodai kuwa "Allah" wanayemuabudu Waislamu siye Mungu ajiitaye katika kitabu cha Biblia (Kutoka 3:15) "Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo", na kusisitiza jina hilo kuwa ndilo kumbukumbu kwa vizazi vyote milele na milele". Ni kweli kabisa kuwa jina hili la Mungu ndilo kumbukumbu kwa vizazi vyote milele na milele, Manabii wa kweli wa Mwenyezi Mungu wameleta dini ya Mungu huyu. Hawakutuletea jina hili tu; yaani Yehova (Kiebrania) ya Allah (Kiarabu), bali wametuletea na sifa zake pia. Nabii Musa (as) aliyepewa maneno hayo ya Kutoka 3:15 aliamrishwa atangaze: Sikiza, Eh Israeli, BWANA, Mungu wetu, BWANA ndiye mmoja (Kumb. 6:4). Nabii Daudi (as) naye alipokuja alitumwa asisitize hilo hilo: Hizi zitaharibika, bali Wewe utadumu; Nazo hizi zitachakaa kama nguo, na kama mavazi utazibadilisha, nazo zitabadilika. Lakini wewe U yeye yule; na miaka yote haitakoma. (Zaburi 102:26-27). Nabii Malaki naye alipokuja aliagizwa anadi: Je! Sisi sote hatuna Baba mmoja? Mungu aliyetuumba siye mmoja tu? (Malaki 2:10). Bwana Yesu (as) naye alipoletwa alimtukuza na kumhubiri Mungu Mwenyezi huyu huyu: …Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja. (Marko 12:29) Na uzima wa milele ndio huu, wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma (Yohana 17:3). Wala usimwite mtu baba duniani, maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni. Wala wasiitwe viongozi, maana kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo. (Mathayo 23:9-10) Yesu akamwambia, mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, naye ndiye Mungu. (Luka 18:19) Hatukuletewa jina la Mungu Mwenyezi, bali tumeletewa sifa zake tumjue ili wajapo "Manabii" "waotaji ndoto" na "Miungu yao mingine" tusihadaike (Kumb. 13:1-5). Baadhi ya sifa hizo ni hizi: Tunaweka nukuu za Biblia sambamba na zile za Qur’an Tukufu ili kumuonyesha Profesa kuwa Waislamu tunamuamini na kumuabudu Mwenyezi Mungu yule yule wa Ibrahim, wa Ismail, wa Ishaka, wa Yakobo, wa Musa, wa Issa (Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yao wote) na wa Muhammad (saw). Yu hai daima, yeye peke yake hapatikani na mauti. (Isaya 57:17, Timotheo 6:16, Qur’an 2:255, Qur’an 28:88) Hakuzaa wala hakuzaliwa. (Isaya 43:10, Qur’an 112:3) Hafanani, wala hafananishwi na chochote. (Isaya 40:18, Qur’an 112:4) Haonekani. (1 Timotheo 6:16, Qur’an 6:103) Akili zake hazichunguziki. (Isaya 40:28, Qur’an 6:103) Kwake hakuna kubadilika-badilika. (Zaburi 102:26 –27, Yakobo 1:17, Qur’an 33:62) Hachangii Uungu wake, wala sifa zake na chochote au yeyote. (Isaya 42:8, Qur’an 2:255, 6:163). Hana mshirika. (Isaya 40:13 –14, 44:6-8, Qur’an 6:163). Lakini nasisitiza tena, lazima nikubaliane na Profesa, na kumjulisha mengine zaidi, kuwa Mungu wa Ukristo siye Mungu tunayemuamini na kumuabudu Waislamu. Sisi tunamuamini, kama machache hayo hapo juu yanavyoonyesha, na kumuabudu Mungu wa Ibrahimu, Ishaka, Yakobo, Musa, Daudi, Yesu na Muhammad. Mungu wa Manabii wote. Kwa manufaa ya Profesa, na wasomaji wako wote wanaofuatilia masuala haya, itakuwa vizuri sana kama tutazisoma nukuu zifuatazo kwa makini sana na kuzingatia maudhui yake. Maana huko ndiko kwenye asili halisi ya "Mungu" wa Ukristo; na kwa sababu hii ni kosa kubwa sana kumnasibisha "Mungu" huyu wa Ukristo na Mungu wa Ibrahimu, na Ishaka na Yakobo. (Kutoka 3:15). "Na makutano walipoona aliyoyafanya Paulo wakapaza sauti zao, wakisema kwa Kilikaonia, Miungu wametushukia kwa mifano ya wanadamu. Wakamwita Barnaba, Zeu na Paulo, Herme, kwa sababu ndiye aliyekuwa mnenaji. Kuhani wa Zeu ambaye hekalu lake lilikuwa mbele ya mji, akalete ng’ombe na taji la maua hata mlangoni, akitaka kutoa dhabihu pamoja na makutano. (Matendo 14:11-13). Sasa namuomba Profesa afikiri; anadhani kuna tofauti, ukiondoa ya majina, baina ya Miungu hii ya Kipagani, "inayojibadilisha maumbo na kuwa wanadamu". Na Mungu yule aliyemuhubiri Paulo? "Iwe na nia hiyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwa pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuko namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu. (Wafilipi 2:5-7) Je? Ipo tofauti ya maana hasa? Hawa sio jamii moja ya Miungu?
|
TAHARIRI HAKI YA KUABUDU MASHULENI: Hoja ya uwingi isizuie haki ya wachache Aliyeandika Yesu si Mungu bado akabiliwa
na kesi
Wazazi walia na Mkuu wa shule
Mkwawa
Serikali iache kudhulumu
Waislamu - Bakwata
KESI YA MIRATHI: Hukumu ya
Jaji Agostino yatupwa
Sumaye sasa atoa ‘waadhi’ Msikitini
Sekondari ya Kiislamu Sumbawanga,
mtihani kwenu – Sheikh Akilimali
37 wasilimu Mwanza
Akamatwa kwa kusoma gazeti la ANNUUR ! MGOGORO WA CHWAKA NA MARUMBI: Serikali
ya Dk. Salmin itafute ufumbuzi
MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA - 4 Kwa nini walengwa wa mabomu wawe ni
Marekani?
Profesa amekosea kusema kwamba...
Ugaidi ni ugaidi, hata wa Marekani
ni ugaidi
UGAIDI: Chanzo si magaidi, ni dhuluma
ya Marekani
Jengeni familia bora
Tuwasaidie Waislamu kielimu
na kiuchumi - Bi Zuhura
Tumieni uhuru wenu vyema
Hoja za kutofautisha Yesu na Issa
ni udhaifu, ni uzushi mtupu! - 4
Mihadhara ya Wakristo yatawala Handeni
Ziara ya Kadinali Pengo Moro
Aonyesha ujuzi wa kutengeneza
Trekta
Waislamu wasizifanye sharia
za dini kuwa nzito – Sheikh Mzonge
Sengerema waomba msaada
Chakula na Lishe
|