|
|
| Ugaidi
ni ugaidi, hata wa Marekani ni ugaidi
Na Maalim Ali Bassaleh KAMA tunakubali kuwa kuzipiga mabomu Balozi za Marekani, hapa Dar es Salaam na kule Nairobi, yaliyoua pamoja na kujeruhi watu wasio na hatia, ni kitendo cha ugaidi na kinachostahili kulaaniwa; basi hatuna budi kukiri pia kuwa kuzishambulia Sudan na Afghanistan, na kuua pamoja na kujeruhi raia wa nchi mbili hizo wasio na hatia, nacho ni kitendo cha kiharamia, kinachopasa kulaaniwa na kila yule anayejali utu na kuheshimu misingi ya haki za binadamu. Marekani inadai kuwa kikundi cha kigaidi kinachoongozwa na tajiri mmoja aitwaye Usama bin Laden, aliye mafichoni nchini Afghanistan, ndicho kinachohusika na ulipuaji wa balozi zake. Lakini inafaa tujiulize swali moja. Kuna tofauti gani baina ya kitendo hiki kilichofanywa na Marekani na kile kinachodaiwa kufanywa na bin Laden? Kama kuna tofauti yo yote ile, baina ya vitendo hivyo viwili, basi labda iwe ni kwamba ule ugaidi wa mwanzo ulifanywa na kikundi cha watu wasiokuwa na huruma na maisha ya wanadamu wenzao; na huu ugaidi wa pili umefanywa na serikali ya nchi isiyojali kabisa uhai wa binadamu wengine wasio Wamarekani. Inavyoonekana ni kuwa Marekani inajali zaidi uhuru wa watu wake. Katika kulinda maisha ya Wamarekani, Marekani ipo tayari kuhatarisha uhuru wa maisha ya watu wengine. Potelea mbali wengine wateketee lakini Wamarekani wapone. Huenda hii ikawa ndiyo sababu iliyowapelekea wananchi wa Kenya kulalamika kuwa wakati wa zoezi la kuokoa waliojeruhiwa na lile bomu lililolipuliwa kule Nairobi, vikosi mbalimbali vya uokoaji vilikuwa vimeshughulika kuokoa watu wa jinsi zote; lakini waokoaji wa Kimarekani waliwaokoa wenzao tu. Na wala hawakuwa tayari kutoa msaada kwa watu wa jinsi nyingine yo yote. Hakuna mwanadamu aliyemstaarabu, na anayethamini roho za wengine awezaye kufurahia ulipuaji mabomu unaoangamiza roho za watu wasio na hatia. Aidha, hakuna anayeshabikia kuuliwa Wamarekani, Wazungu, Waafrika au Waarabu; kwani wote hao ni wanadamu. Roho ya mwanadamu ni yenye thamani kubwa, inataka ithaminiwe na ilindwe kwa hali yoyote. Kitendo cha kuua binadamu, wasio na hatia, ovyo, kwa kisingizio cho chote, hakikubaliki. Qur’an Tukufu inasema: "…atakayemwua mtu bila ya yeye kuua mtu, au bila ya kufanya ufisadi katika nchi, basi ni kama amewaua watu wote …" (Al Maidah 5:32). Kwanini Qur’an Tukufu iseme hivyo? Naam, ni kwa sababu Uislamu unawaona wanadamu wote ni kama ndugu wa familia moja. Kwa hivyo kumfanyia ukatili mmoja wao ni sawa na kuwafanyia ukatili wote. Zilipolipuliwa balozi za Marekani na kusababisha vifo vya watu 257 na kujeruhi wengine zaidi ya 5000, sote, kwa umoja wetu, tulilaani vikali kitendo hicho cha kikatili. Serikali zetu za Tanzania na Kenya, zimekuwa zikitoa ushirikiano mkubwa kwa wapelelezi wa Kimarekani, wa FBI, katika jitihada za kuwasaka wale wote wanaohusika na uharamia huo. Tulidhani Marekani itaonyesha ustaarabu; itasubiri mpaka uchunguzi umalizike, iwajue waliohusika, iwatie mkononi, kisha iwakabidhi kwa vyombo vya sheria vinavyohusika; ili sheria ichukue mkondo wake. Lakini wapi! Wakati uchunguzi unaendelea, tayari Marekani inazishambulia Sudan na Afghanistan kwa makombora na kuua raia wasiohusika. Tendo hili ni la uonevu na ni la aibu kubwa sana; hasa linapofanywa na nchi kama Marekani. Tusijidanganye, ugaidi ni ugaidi, ufanywe na Ireland au ufanywe na Marekani! Marekani ni taifa kubwa, lenye nguvu nyingi. Ni taifa lenye kuogopewa na kuheshimiwa. Na serikali ya nchi hiyo ndiyo iliyo mstari wa mbele kuona demokrasia inatekelezwa duniani kote na kwamba haki za binadamu zinaheshimiwa. Iweje basi nchi kama hiyo ivuke mipaka ya nchi yake na itumie nguvu zake za ziada kwa kuzishambulia nchi nyonge na dhaifu, zisizoweza hata kujilinda wenyewe? Tuseme huku ndiko kuheshimu haki za binadamu? Au hii ndiyo demokrasia anayoisimamia Marekani ulimwenguni? Mwenye nguvu mpishe! Bila ya shaka hii ndiyo ile demokrasia ya wanyama mwitu; mkubwa kumrarua mdogo! Bwana Kofi Annan, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameipinga hatua hiyo iliyochukuliwa na Marekani. Kwa sababu imekwenda kinyume kabisa na sheria za kimataifa. Kama Marekani ilikuwa ina ushahidi wa madai yake ilikuwa iwasilishe swali hilo mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo Marekani ni mjumbe wa kudumu na ina kura ya Veto humo, ili lijadiliwe na kutolewa maamuzi ya pamoja. Na hata kama itataka kuyapinga maamuzi yatayotolewa itaweza kufanya hivyo kwa kutumia ile kura yake ya turufu. Mbona Marekani ilipotaka kuiadhibu Iraq, kwa kuivamia Kuwait, ililipeleka swala hilo Umoja wa Mataifa na ikapata kibali cha kuitekeleza azma yake hiyo? Je! Leo imekwisha sahau kuwa kuna Umoja wa Mataifa, na hali Makao Makuu ya Umoja huo yapo katika ardhi yake nayo ndiyo inayogharimia fedha nyingi zaidi katika bajeti ya kuendesha taasisi hiyo? Senetor Don Coasts wa Indiana, kutoka chama cha Republican, amesema Rais Bill Clinton kwa wakati huu, aliokumbwa na kashfa za ufuska hakuwa na hadhi ya kuamrisha shambulio kama hilo alilolifanya. Maneno haya yanaonekana kutilia uzito madai ya nchi nyingi za Kiislamu kuwa Rais Clinton aliamrisha kushambuliwa Sudan na Afghanistan ili kujaribu kuzima ile kashfa inayomkabili nyumbani, ambayo ilikuwa imemwangushia hadhi yake. Kwa vyovyote vile hapakuwa na sababu sahihi ya kujichukulia sheria mkononi mwake wakati vyombo vya kisheria vya kimataifa vipo na vinaweza kushughulikia jambo hilo. Kwa nini kuamrisha wakombora yasiyo na macho kwenda kuua vikongwe, wanawake na watoto wadogo? Tunaambiwa kombora moja, bila ya kukusudiwa, limedondokea Pakistan, katika jimbo la Baluchistan na kuua wanavijji watano na kujeruhi wengine. Tunaiambia Marekani, kama kweli inapinga ugaidi wa mtu au kwa vikundi
vya watu basi, pia, apinge na ugaidi unaosimamiwa na nguvu za dola (State
terrorism)! Isije ikawa kama walivyosema Waswahili: "Mkuki kwa nguruwe,
kwa binadamu unaua!"
|
TAHARIRI HAKI YA KUABUDU MASHULENI: Hoja ya uwingi isizuie haki ya wachache Aliyeandika Yesu si Mungu bado akabiliwa
na kesi
Wazazi walia na Mkuu wa shule
Mkwawa
Serikali iache kudhulumu
Waislamu - Bakwata
KESI YA MIRATHI: Hukumu ya
Jaji Agostino yatupwa
Sumaye sasa atoa ‘waadhi’ Msikitini
Sekondari ya Kiislamu Sumbawanga,
mtihani kwenu – Sheikh Akilimali
37 wasilimu Mwanza
Akamatwa kwa kusoma gazeti la ANNUUR ! MGOGORO WA CHWAKA NA MARUMBI: Serikali
ya Dk. Salmin itafute ufumbuzi
MAPENDEKEZO YA KATIBA YA SHIRIKISHO LA TANZANIA - 4 Kwa nini walengwa wa mabomu wawe ni
Marekani?
Profesa amekosea kusema kwamba...
Ugaidi ni ugaidi, hata wa Marekani
ni ugaidi
UGAIDI: Chanzo si magaidi, ni dhuluma
ya Marekani
Jengeni familia bora
Tuwasaidie Waislamu kielimu
na kiuchumi - Bi Zuhura
Tumieni uhuru wenu vyema
Hoja za kutofautisha Yesu na Issa
ni udhaifu, ni uzushi mtupu! - 4
Mihadhara ya Wakristo yatawala Handeni
Ziara ya Kadinali Pengo Moro
Aonyesha ujuzi wa kutengeneza
Trekta
Waislamu wasizifanye sharia
za dini kuwa nzito – Sheikh Mzonge
Sengerema waomba msaada
Chakula na Lishe
|