|
|
|
Wanafunzi wa Kiislamu tunahaki ya kuikosoa serikali Tulipiga kura kuiweka madarakani Ndugu Mhariri WAKATI wa kampeni za Uchaguzi mkuu (1995) tulishuhudia wagombea madaraka wakija mashuleni kutuomba tuwapigie kura, huku wakituahidi kuwa pamoja na sisi pindi waingiapo madarakani kumbe wametugeuka kwa kutupiga risasi na kutuweka rumande bila ya huduma. Wanafunzi wa Kiislamu tumekuwa tukitumiwa kama ngazi ya kufikia bungeni na waheshimiwa ambao hivi sasa wanakataa kuunda tume kuchunguza madhila yanayowakuta wapiga kura wao. Ni dhahiri kwamba Serikali haifanyi hayo kwa bahati mbaya, kwani inajua na imezoea kuwa, kwa kutumia siasa yao ya premende na kutuimbisha nyimbo za kukisifu chama chao, tutasahau uchungu wa moshi wa sumu ya mabomu wanayoturushia hivi sasa na hatimaye kuwachagua tena. Kutokana na ugeni tulio kuwa nao wanafunzi katika uwanja wa siasa tulikubali kuichagua CCM na kuiweka madarakani kazi hiyo tuliifanya sambamba na maelekezo kutoka kwa walimu wetu juu ya umuhimu wa CCM kuwa madarakani kuwa ni kuendeleza demokrasia na amani ya kweli nchini Tanzania. Sasa wakati umefika kwa wanafunzi kufanya tathmini za kujua namna demokrasia na amani ya kweli inavyodumishwa na serikali ya awamu ya tatu, ni ukweli usiofichika kuwa haki haitendeki katika maisha ya kila siku hapa Tanzania, mfano hai ni ukiukwaji wa makusudi wa katiba ya jamhuri ya muungano kifungu cha19 kinachoeleza wazi juu ya uhuru wa kuabudu kwa kufuata maelekezo ya vitabu vya dini zetu. Cha kushangaza ni pale serikali inapoamuru jeshi la polisi kutufyatulia risasi na mabomu ya moshi wa sumu na kutupa mateso gerezani, eti kwa sababu tumesema Yesu si Mungu wakati kitabu chetu (Qur’an) kinaelekeza hivyo. Je hiyo ndio demokrasia? Amani ya kweli nayo hatuioni kabisa, hivi kama hiyo amani ya kweli ipo vipi baba zetu wanatupwa rumande tena bila dhamana, wakati wanajua kuwa ndio wanaotupatia huduma muhimu zikiwemo za masomo? Vipi mama zetu wadhalilishwe na kuteswa hivi wanadhani hatuna uchungu wa mama zetu? Kwanini mwanafunzi mwenzetu Chuki Athumani apigwe risasi bila kosa? Wanafunzi wa Kiislamu tuna haki ya kuikosoa serikali kwa njia yeyote ile, kwani kwa mwenendo huu wa serikali kuwa na chuki na Waislamu utafika wakati tutasema assa basi! Serikali ya Tanzania ikumbuke yaliyoikuta serikali yaRais Sohato kule Indonesia na hatimaye Ustaadh Yusufu Habibi kuiongoza nchi hiyo hivi sasa. Ni ukweli uliowazi kuwa serikali imekuwa ikiendesha vitendo visivyo vya haki dhidi ya Waislamu tangu iingie madarakani! Wanafunzi wa Kiislamu hatutakaa kimya, kwani tuna haki ya kuikosoa serikali inayotudhulumu. Chilyunga M.H.
Majibu ya tuhuma ya uongozi mbaya wa BAKWATA katika Wilaya ya Misungwi Ndugu Mhariri Katika Gazeti la AN-NUUR toleo Na. 152 la tarehe 5-11 Juni katika nakala yake ya maoni iliandikwa tuhuma hiyo hapo juu na watu wachache wanaojiita Waumini wa Wilaya ya Misungwi. Tunapenda kuijibu kama ifuatavyo:- Uongozi wa BAKWATA katika Wilaya hii ni uongozi wa Waislamu wote na utaendelea kuwashughulikia kikamilifu bila ya kujali fitina zinazofanywa na kikundi kilichojitenga chaWaislamu wachache wanao kataa uongozi wa Baraza. Hivyo kuhama msikiti wa Misingwi (Masjid L-Jamia) kitendo hiki takribani Waislamu wote wa Misungwi kiliwahuzunisha. Dhamira ya Kikundi hiki ni kutaka kuondosha kabisa uongozi wa BAKWATA hapa Wilayani pia kusimika Uongozi wa Taasisi nyingine. Ni wazi juhudi zao za kufanya hivyo zilizoanza muda mrefu zimekwama. Sisi tunadhani shutuma za hivi sasa ni mbinu mpya kulipaka matope BAKWATA na uongozi wa Kiislamu kwa ujumla. Katika shutuma hizo madai yao hayana Msingi kwani yalikwisha tatuliwa na Sheikh wa Mkoa na kumalizika nahususani ni ya Mtaa mmoja tu Wialya nzima yaani Misungwi. Sio kweli kwamba katika msikiti wa Misungwi hutangazwa mambo yasiyo kuwa ya Kiislamu isipokuwa hupewa taarifa Waislamu kupitia kipaza sauti kilichopo hapo Msikitini. Na inapobidi kutangazwa hilo litakiwalo basi hutangazwa kwa kuzingatia heshima ya Msikiti kama waliolibainisha hilo wanawazuoni wenye kutegemewa katika vitabu mbali mbali. Yanayotangazwa ni kama:- Vifo,
Ama kuhusu wahadhiri kuzuiwa kutoa Daawa msikitini, si sahihi na wala hakuna mhadhiri yeyote anayezuiliwa kufanya hivyo hapa Misungwi kwani tunafahamu hiyo ingekuwa kwenda kinyume kabisa na maagizo ya MwenyeziMungu kama alivyobainisha katika Qur’ani tukufu suratil Al-imran aya 104 inasema na wawepo katika nyinyi watu wanaolingania heri (Uislamu) na wanaoamrisha mema na kukataza mabaya na hao ndio watakaotengekewa. Mwongozo wa Baraza kuhusu wahadhiri wote ni kwamba wao au vikundi vyote viwe vya humu nchini au nje ya nchi vinavyojishughulishana Daawa vinapotembelea misikitini vijitambulishe; hiyo ni pamoja na kuonyesha barua kutoka BAKWATA Mkoa inaposhindikana maelelzo binafsi hukubaliwa. Hii husaidia utoaji wa taarifa mkoani. Utaratibu huu waumini hawa wameuelewa vibaya na hii inadhihirisha ‘Attawifatul-karaha waliyokuwa nayo juu ya BAKWATA yaani (Mapenzi ya kukichukia kitu). Muhadhiri aliyetajwa alikemea mambo msikitini akaandikiwa barua nakala ikaenda Kituo chaUsalama, ndiyo aliyechochea mgawanyiko wa Waislamu na kusababisha kuwepo misikiti miwili na bado anaendelea na tabia hiyo. Muhadhiri huyu amewahi kutumia hadhara na msikiti kukashifu viongozi wa Baraza wote akiwemo Sheikh wa Mikoa na wengineo pia kutoa waadhi wa matusi, uongozi ulishindwa kuvumilia na kuchukua hatua dhidi yake. Tungependam kujua kuwa:- Je kuwapiga Waislamu msikitini ilivyowahi kutendeka na baadaye kutangazwa katika vyombo vya habari ni mafundisho ya Qur-ani na Sunna? Kudhalilisha na kukashifu wanazuoni kwama Sheikh wa Mkoa wa Mwanza alivyofanyiwa ni Sunna? Pia kutambika msikitini kwenu hapo mnafanya Sunna za Mtume? Kule kutokubaliana kwenu na wanazuoni kuhusu Ijumaa nyinyi mkafikia kuzua Ijumaa mbili katika Mtaa mdogo kama huu wa Misungwi huu si upotoshaji? Hivi karibuni kundi lenu lilitamka kuwa Waislamu wote wanaoongozwa na BAKWATA ni makafiri huu ni mwongozo gani wa Qur-ani na Sunna? Wageni walioharibikiwa safari wa kweli hupatiwa nafasi kuomba msaada kwa waumini wanaokuwepo msikitini si kweli kuwa huzuiliwa. Tunahitimisha kuwa mara baada ya kundi hili kujitenga halina tena wajibu
kuuliza mambo yanayoendelea katika Uongozi wa BAKWATA Mtaa, Msikiti na
penginepo hawahusiki. Ombi letu ni kulitaka kundi hili kuacha kujaribu
kumvikaSheikh wa Mkoa wa Mwanza kilemba cha ukoka kwa kumpongeza, kwani
yeye hafurahii utengano na kashifa.
Serikali isituzibe macho Waislamu Ndugu Muhariri, NAOMBA kutoa langu dukuduku kuhusu Serikali hii ambayo imekua ikiwafunika macho wananchi wake kijanja janja. Rais amevunja bodi ya misamaha ya wafungwa eti kwa kutokuzingatiauwiano katika jamii. Hivi hili tu ndilo ambalo halikuzingatia uwiano katika jamii? Baraza Kuu lilitoa mifano mingi tu ambayo imeonyesha jinsigani nchihii isivyo wathamini Waislamu katika kuongoza sekta mbali mbali, pia katika kushughulikia matatizo ya Waislamu. Hatujasikia Rais akitoa kauli yake kuhusu Waislamu ambao waliuliwa na polisi katika msikiti wa Mwembechai.Je? Ni malalamiko mangapi ambayo baraza kuu imeyatoa kwa serikali bila ya kushughulikiwa? Tena mambo ya msingi kabisa ikiwa mojawapo ni kuomba iundwe tume kuchunguza mauaji ya Mwembechai kujua chanzo cha mauaji yaliyofanywa na polisi. Mbona Rais amekaa kimya? Au hao waliouliwa si katika wananchi wake? Mussa Absdala
Ndugu Mhariri BAADA ya kulazwa na pingu kwa muda mrefu, asiye na uwezo wa hata kunyanyuka kitandani akiwa amepooza sehemu za chini za mwili wake. Wafunga pingu hao wenye mamlaka ya juu wamebaini ukweli kuwa mwanafunzi Chuki Athumani (17) hakuwa na hatia yoyote. Wenye mamlaka wameonyesha masikitiko yao baada ya kuidhoofisha kiasi kikubwa hali ya mwanafunzi mwenzetu huyo. Pamoja na wenye mamlaka ya juu kujitolea kwa hali na mali kumhudumia mwanafunzi huyo, lakini wangapi ambao wametiwa hatiani pasi na makosa na bado wapo katika adhabu mpaka hivi sasa? Na chakusikitisha zaidi, miongoni mwao kuna wanafunzi , watoto wadogo wa mitaani na wanawake. Wanafunzi ambao hawakuruhusiwa kufanya mitihani yao ya mwisho, wenye mamlaka wanawafikiriaje? Mwanzo wa kusikitika umeanzia kwa Chuki, je, utaisha kwa Chuki tu? Ambaye afya yake imedhoofishwa kwa kiasi kikubwa. Au sikitiko litakuwa tikisiko kwa upande wa pili. Mwisho kabisa, kumsikitikia Chuki tu hautakuwa na maana yeyote yaani si chochote si lolote endapo wapo wengi kama Chuki ambao wanahitaji kusikitikiwa. Je, wenye mamlaka ya juu watachukua hatua gani kwa wazembe waliopelekea hali ya Chuki kuwa mbaya. T. Minje,
Ndugu Mhariri MHESHIMIWA Juma Kapuya, Waziri katika serikali ya awamu ya tatu naomba utufafanulie kwa ukweli na uwazi chuki unayozungumzia ni dhidi ya nani na kwa nini? Haiwezekani chuki iwepo, anayechukiwa asiwepo na kama yupo sababu isiwepo! Angalau ungetutajia anayechukiwa ni nani na kwa nini, au kama sababu haioni basi atutajie anayechukiwa. Kwa mfano, Waislamu leo wakiambiwa wanamchukia yule mtu aliyewaamrisha wale polisi pale Mwembechai Februari 13, 1998 kwa kuwaeleza "piga yule", "ongeza", halitokuwa jambo la ajabu. Ni sahihi kabisa mtu wa aina hii kuchukiwa. Lakini kwa wale wenzetu ambao walikaa kwenye vikao wakapeana taarifa za jinsi walivyotuma majeshi pale Mwembechai kisha wakapongezana kwa mafanikio kutokana na yale waliyoyakusudia inawezekana wasijue wala kuona sababu ya Waislamu kuwa wamechukia. Maana kwao wao kuua Waislamu kwa risasi, kuwatia vilema watoto wadogo kama akina Chuki Athumani, ni sawa tu! Na si ajabu kuwashangaa hata kuwashutumu wanaochukia kuuliwa kwa ndugu zao. Vivyo hivyo, watutajie basi wanaochukiwa na Waislamu kuhusu suala la dhulma katika elimu, maana inawezekana kwa mtazamo wao wasione sababu ya kuchukiwa, lakini tu wawape basi fursa Waislamu wapate kuwaeleza sababu za chuki walizonazo dhidi ya hao wanaoonekana kuchukiwa. Kwa mantiki hiyo, itakuwa jambo la maana endapo serikali itatoa fursa pia kwa Waislamu kusikia hoja zao (serikali) kuhusu lawama au chuki wanazodai kuwanazo Waislamu kwa njia ya mjadala wa kupata ukweli wa mambo na siyo kauli za kebehi, kejeli na lawama peke yake. Hassani Mwami,
Ndugu Mhariri KAULI ya Waziri Kapuya dhidi ya Waislamu aliyoitoa Bagamoyo katika sherehe za Maulid haiwezi kuachiwa isije ikaleta madhara kwa jamii iliyojaa watu wema kama Waislamu. Mara nyingi Waislamu wanapoalikwa katika hafla za dini yao huzungumza mambo kwa munasaba wa imani yao. Nafikiri Juma Kapuya nae ni Muislamu. Kama alikuwa hana uwezo wa kuisoma Barzanji japo mlango mmoja, basi angalau angeishia kumtukuza Mtume (s.a.w) na Allah (s.w) aliyemtuma kuwa mfano kwetu wa kutekeleza mwongozo wake wa Qur’an hapa duniani. Kama hili pia lilimshinda, basi angekaa kimya tu kama waalikwa wengine wasiokuwa Waislamu ambao huwa si lazima kwao kujishughulisha na mabo yasiyo wahusu. S.S. Seif,
Wazazi na walimu wawajibike katika malezi Ndugu Mhariri Ni jambo la kusikitisha sana kuona mwanafunzi wa shule ya Kiislamu Alharamayn Islamic College ametolewa kwenye magazeti ya kashfa na matusi kama Sanifu kwa kichwa cha habari, "Mwanafunzi aliyezaa na Naibu Waziri apewa 15,000". Je, kashfa kama hizi nani abebe lawama? Mwanafunzi, mzazi au mwalimu wa huyo mwanafunzi? Kwa hakika wote watatu wanastahiki lawama. Kwa saabu hawakushirikiana kuhakikisha kijana wao wa Kiislamu anapata mafunzo ya Kiislamu, vile vile na kuyafuatilia ipasavyo. Kwa upande wa wazazi, kwanini mzazi anamgharamia mwanawe kumpeleka shule ya Kiislamu, bila ya kufuatilia maendeleo ya kijana wake? Anasahau Hadithi ya Mtume Muhammad (s.a.w) inayosema kila mtu ni mchunga na ataulizwa juu ya alichokichunga. Wewe mzazi kwa nini uone raha kijana wako wa Kiislamu hafuati mafunzo ya pale ulipompeleka ajifunze? Kijana wa Kiislamu kupata mimba akiwa mwanafunzi kuna faida gani ya kusoma shule ya Kiislamu! Wazazi waelewe kwamba, lazima siku ya kiama mtaulizwa juu ya mlivyovichunga. Mwanafunzi wa Kiislamu atakuwa mnafiki kama hutofuatilia mafundisho ya Mwenyezi Mungu ipasavyo kama Mungu anavyosema katika sura 95 aya ya 4-5. Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu katika umbo lililobora kabisa, kisha kutokana na matendo yake maovu amemrudisha mwanadamu huyo chini kuliko walio chini. Hii ni dhahiri kwamba tukifanya matendo maovu tunakuwa na hadhi ya chini kuliko mnyama, kwa sababu sisi tumepewa akili. Ewe mwanafunzi wa Kiislamu ni jambo gani linalokufanya umuasi Mungu. Mungu aumbae amekujaalia wewe usome elimu iliyo sahihi kama mtihani kwako. Kutofuata maadili mazuri ya Kiislamu wakati wewe ni mwanafunzi wa Kiislamu ni kujipalia makaa ya moto jahanam ambao kuni zake ni watu na majabali. Wewe kama mwanafunzi wa Kiislamu kwa nini usukumwe sukumwe kufuata sheria? Kufanya mambo ya ajabu ukiwa mwanafunzi wa Kiislamu ni kuushushia hadhi Uislamu. Ni bora ujulikane. Jamii ya Kiislamu inakutegemea. Kwa upande wa walimu pia wataulizwa juu ya wanavyuvichunga. Mwanafunzi anasoma shule kuanzia kidato cha kwanza anamuasi Mwenyezi Mungu mpaka anapata mimba akiwa kidato cha tatu. Miaka yote hiyo wewe mwalimu umechukua hatua gani. Mwanafunzi huyo ni wazi hafuati maadili ya Kiislamu kwa nini asubiriwe mpaka aipake matope shule? Walimu pia kumbukeni kwamba, ni lazima mtaulizwa juu ya mlivyovichunga. Mariam Ussi,
Ndugu Mhariri Naomba nafasi hii ili nitoe yale machungu yanayonisibu moyoni kuhusu malezi. Kwa kweli kuna vitengo vingine vya malezi ya watoto vinachangia mmomonyoko wa maadili katika jamii kwa mfano mtoto wa shule ya chekechea baada ya kufundishwa masomo ya kukabiliana nayo pindi atakapoanza shule darasa la kwanza yeye anafundishwa kunengua hadharani, hii ni dalili mbaya kabisa ya malezi. Ombi kwa wazazi na walezi kwa ujumla iili kukabiliana na tatizo la ufuska na matukio mengine machafu ni kusisitiza mavazi ya heshima yavaliwe ili kujihifadhi miili ili watu wasitembee wala kukaa uchi ili tabia ijengeke mapema tangu chekechea ili kulinda heshima ya watoto na wazazi kwa ujumla. Sukuzi S.M.
|
Maoni yetu: Prof. Juma Kapuya, vipi Muislamu usijue agenda za Waislamu? Hatimaye Mzee Katambo, Chata waachiwa
Sheikh Bafadhil aitaka Bakwata iwe
mtetezi wa Waislamu
Makala: Uinjilisti wa Mbuni haufai
Mussa Katambo: Mzee aliyewekwa rumande kwa kuandaa mihadhara Makala: Elimu ya ngono yapenyezwa
tena Zanzibar
Arusha wasema: Hongera Mhe. KK kwa
kuwa mfano mwema
Wanawake Songea kuandaa maonesho
Kesi ya mgogoro wa Ardhi
AN-NUUR marufuku
gerezani?
Waislamu Karagwe wadai kusalishwa
na imamu asiyejua kutawadha
Ofisi mpya za Rabita
|