|
|
|
Prof. Juma Kapuya, vipi Muislamu usijue agenda za Waislamu? KATIKA kusherehekea Maulid N-nabii baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti kwamba Rais ametoa mbuzi wawili na mchele kilo 100 kwa makazi ya Wazee ya Nungwe, Kigamboni Jijini. Rais ametoa mchango huo ili kuwawezesha wazee hao wasiojiweza waweze kupata mlo safi katika siku hii muhimu ya kusherehekea uzawa wa Mtume (s.a.w.) na iwe furaha kwao badala ya kusononeka. Wakati Mheshimiwa Rais Benjamin William Mkapa akitoa sadaka yake hiyo kuwawezesha wazee wa Kiislamu japo wachache washerehekee kwa furaha sherehe za Maulid, Waziri wa Elimu Mhe. Profesa Juma Athuman Kapuya, amewapa Waislamu nasaha ambazo zahitaji tafakuri na uchambuzi kwa kituo. Mr. Juma Athuman akiitumia nafasi yake kama mgeni rasmi katika Baraza la Maulid aliwaelezea Waislamu wa Tanzania kama watu wasio na dira; wasio na malengo ya muda mrefu, wenye uadui miongoni mwao na wasiofanya lolote la maendeleo yao ila kulalamika tu na kusingizia serikali kwamba inawapiga vita wakati inatoa haki kwa wote. Mhe. Profesa Kapuya amedai kwamba Waislamu wamekuwa wakiunda vikundi vingi si kwa lengo la kuleta maendeleo bali kugombea misaada toka kwa wafadhili. Lakini katika mazito aliyoyazungumza Profesa Juma Athumani ni kuwakumbusha Waislamu kwamba Qur’an inasema kwamba Waislamu wote ni ndugu – In-namalmu’minina Ikh’wa. Kisha akasherehesha kwa hadith ya Mtume (s.a.w.) inayosema kwamba, hawi Mu’min mtu mpaka ampendelee Muislamu mwenzake yale anayoyapenda. Baada ya kuyasema hayo akasema kwamba kinyume na mafundisho hayo Waislamu hawana moyo wa kuhurumiana bali hutakiana mabaya kila siku. Ni kweli Innamal’ Mu’minina Ikh’wa. Ndio maana katika hudaibiya Waislamu walikuwa tayari kupigana japo hawakuwa na silaha baada ya kusikia Othman bin Affan (R.A.) kauliwa. Na ndio maana Waislamu duniani kote waliwaunga mkono wenzao wa Bosnia na wanaendelea kuwaunga mkono Waislamu wa Kashmir, Palestina, Kosovo, Sudan, Libya n.k. Ni kweli: Innamal Mu’minina Ikh’wa; ndio maana katika kesi mashuhuri ya Chifu Abdallah Said Fundikira aliyosingiziwa rushwa Waislamu walimuunga mkono wakijazana mahakamani – akina mama na buibui zao kwa maelfu na akina baba na kanzu na kofia zao kwa maelfu. Kesi ikatemwa. Ndio maana vile vile, Waislamu walisimama kidete kumuunga mkono Dk. Salmin Amour dhidi ya wale waliotaka kuwasulubu kuhusiana na suala la OIC huku wakifumbia macho ubalozi wa Vatican nchini. Na ndio maana Waislamu walisimama imara kuwa pamoja na Marehemu Profesa Kigoma Ali Malima,alipokuwa "akisulubiwa" na vikao vya chama, Wabunge, vyombo vya habari n.k. kwa kusimamia kwake uadilifu, ukweli na haki kwa wote, na kuibainisha dhulma wanayofanyiwa Waislamu. Ni kweli kabisa "Inna Malmu’minina Ikh’wa ndio maana Waislamu wote nchi nzima wameungana kulaani mauaji yaliyofanywa napolisi pale Mwembechai. Wanachanga fedha kuendesha kesi; wanawasaidia watoto ambao baba zao wako ndani na wanaendesha mikutano na makongamano kujadili kadhia hii. Katika kuoneana kwao huruma na kupendana Waislamu kama Mhe. Kitwana Kondo,wamewaona viongozi wakuu wa serikali, ameongea na waandishi wa habari na amesimama Bungeni na kuzungumza juu ya dhulma wanayofanyiwa Waislamu. Na matokeo tumeyaona. Wazee. Wanawake, watoto na wengine pia wameachiwa. Mtoto Chuki Athumani amefunguliwa pingu na anapata matibabu pamoja na kuachwa huru. Na la zaidi Waislamu wanataka kumuona Chuki Athumani anatembea kama wao wanavyopenda kutembea. Wapo mbioni, kumpeleka Ulaya kupata matibabu kwa mabingwa wa upasuaji wa mishipa ya fahamu (Neural Surgions). Lakini pamoja na hayo kauli ya Mhe. Profesa Juma Athumani Kapuya kwamba hakuna moyo wa kuhurumiana ila kutakiana mabaya ni sadakta vilevile. Wakristo waliopongezana katika vikao rasmi vya chama baada ya mauaji ya Mwembechai tuliwaelewa. Ambao tulikuwa hatuja waelewa ni hawa akina Juma tena maprofesa na timu yao. Alhamdulillah; Mhe. Waziri katusaidi, kwamba moyo wa kuhurumiana haupo ila kutakiana mabaya. Ndio maana Waislamu waheshimiwa wameshiriki kwenye vikao rasmi kupongeza askari waliowaua Waislamu kwa kuwalenga shabaha – "piga yule" "Mwongeze". Na ndio maana wamempigia makofi Mheshimiwa mwenzao Waziri Mkuu alipotangaza vita dhidi ya Waislamu ndani ya Bunge. Alhamdulillah, Waislamu wote walio mitaani (lower classes) wameuelewa vizuri ujumbe wa Qur’an na Hadithi juu ya Udugu, umoja na kuhurumiana. Tatizo ni vipi na hawa waliopata uwasiri, ubunge na ujumbe wa NEC watayazingatia mafundisho haya wawe tayari kukemea udhalimu na kuwaonea huruma watu kama Chuki Athumani, Mzee Chata n.k. Mheshimiwa Waziri Kingunge Ngombale Mwiru si Waziri wa Afya wala wa Mambo ya Ndani; lakini Waislamu wamemshuhudia akiungana na mamia ya Waislamu wanaofurika Muhimbili kumjulia hali mtoto Chuki Athumani. Inakuwaje Mawaziri na Wabunge Waislamu wasionekane? Kweli kunakutakiana mabaya na kutokuhurumiana kama aliyoyasema Prof. Juma Athumani Kapuya. Waislamu wanayo Agenda yao na mipango pia yanayolingana na dira yao. Wakuu wa Serikali, Mawaziri, maafisa waaandamizi wa serikali katika sehemu mbalimbali na wasomi walio Wakristo ni ama wazee wa kanisa; wajumbe na washiriki madhubuti (committed) wa taasisi na kamati mbali mbali za kupanga, kuratibu, kuendesha na kusimami programu mbalimbali za kuleta maendeleo ya waumin na dini yao hata kama ni kwa kudhulmu haki za wengine. Hawa hawasimami kwenye majukwaa na kuwashutumu waumini wenzao kwamba hawana mipango na mwelekeo kwasababu wako pamoja nao na wao ni sehemu ya waumini na wana wajibu kama watu binafsi na kwa nafasi zao kuipigania dini yao. Wanaoshangaza ni hawa wanaohoji Waislamu Agenda yao nini na kudai kwamba hawana mipango. Mjadala unaoendelea kati ya Bw. Mtaki, Mchungaji Kusupa, waumini wengine na Waislamu bila shaka umeshajibu hoja nyingine za Mheshimiwa Waziri Profesa Kapuya. Ila tu wakati tukimpongeza na kumshukuru Mhe. Rais kwa kuwawezesha japo baadhi ya Wazee wa Kiislamu kusherehekea vizuri sherehe za Maulid Nnabii; tungependa tukumbushie kwamba bado wale wauaji hawajafikishwa mahakamani na kama alivyosisitiza Mhe. Waziri wa Elimu Prof. Kapuya tusingependa tuonekane hatuna moyo wa kuhurumiana. Na kama pia alivyotilia mkazo Mhe. Profesa Juma Athumani Kapuya katika kuingia karne ya 21. Isingekuwa vyema nchi yetu ikaingia karne hiyo na doa la dhulma. Wauaji wafikishwe mahakamani; waliowanyanyasa wanawake na kumtia kilema mtoto Chuki Athumani nao sheria iwahukumu pia. Na kisha ubaguzi na upendeleo kama ilivyojitokeza katika suala la Parole; uteuzi wa makatibu tawala, mikoa, Tume mbalimbali; Wakuu wa Mikoa, Wilaya n.k. ukomeshwe. Tungependa kumalizia kwa kukumbusha kwamba, mwaka 1848 nchini Ufaransa kulitokea machafuko makubwa yaliikumba miji yote ya nchi hiyo. Wananchi wadhulumiwa wa matabaka ya kati (middle classes) na chini (lower classes), baada ya kuchoshwa na mwenendo wa watawala, kwa mamilioni walimiminika mitaani kuonyesha hasira zao. Kiini cha machafuko yale kilikuwa ni uchumi mbovu, siasa mbovu, ukandamizaji,
kupuuzwa na kukejeliwa wananchi hao walio wengi. Hatima ya machafuko yale
wanahistoria wanaijua vyema. Kwahiyo tunawaomba Waheshimiwa wetu pamoja
na kupalilia ulwa lakini tujali pia maslahi ya wengine na hasa maslahi
ya kudumu ya taifa hili. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki nchi yetu.
|
Maoni yetu: Prof. Juma Kapuya, vipi Muislamu usijue agenda za Waislamu? Hatimaye Mzee Katambo, Chata waachiwa
Sheikh Bafadhil aitaka Bakwata iwe
mtetezi wa Waislamu
Makala: Uinjilisti wa Mbuni haufai
Mussa Katambo: Mzee aliyewekwa rumande kwa kuandaa mihadhara Makala: Elimu ya ngono yapenyezwa
tena Zanzibar
Arusha wasema: Hongera Mhe. KK kwa
kuwa mfano mwema
Wanawake Songea kuandaa maonesho
Kesi ya mgogoro wa Ardhi
AN-NUUR marufuku
gerezani?
Waislamu Karagwe wadai kusalishwa
na imamu asiyejua kutawadha
Ofisi mpya za Rabita
|