|
|
|
Waheshimiwa toeni kauli zenye mashiko Lakini hata katika sayansi za jamii suala la utafiti ni nyeti na muhimu sana. Kwa mfano hatutarajii msomi aibuke na kauli kusema kwamba Waislamu wanalalamika bure kwamba wanaonewa wakati si kweli. Au aibuke na kauli zinazodai kwamba serikali inatoa haki kwa wote bila ya kuwa na ushahidi madhubuti. Anachotarajiwa na jamii ambayo inalalamika ni kufanya mambo mawili. Kwanza yeye binafsi afanye utafiti juu ya yale yanayolalamikwa.. Lakini pili, na ambalo ni muhimu zaidi asaidie kuielimisha mamlaka inayohusika iunde tume kuyachunguza madai yanayotolewa. Na hivi ndivyo walivyofanya na wanavyoendelea kufanya Waislamu. Wanayo madai, wamefanya utafiti, data wanazo na wanaielimisha serikali yao iyaundie tume madai haya. Waislamu wanasema kwamba serikali inawaonea na wanatoa ushahidi, wamewaua bila ya kosa, wamevunja na kuingia msikitini kwao na viatu, wamewatesa na kuwadhalilisha akina mama, wamewatesa wazee wa miaka 83 wasio na hatia, wamewanyima dhamana na matibabu kinyume cha sheria na katiba! Tulichotegemea ni mtu kusimama na hili halihitaji mtu awe Profesa, aseme haya si kweli, hayakutokea au yametokea lakini si kuonewa kwasababu mlistahiki kufanyiwa hivyo na atoe hoja zake za kisomi. Katika sayansi, kila kipengele kinachochangia matokeo ya jambo ni lazima kizingatiwe. Mfano, katika elimu mimea (Botany) tunafahamu kwamba ili mbegu iote na ikue inahitaji maji, hewa, chakula na mwanga. Sasa huwezi ukayapa uzito maji pekee ukaacha hewa kwasababu vyote vinasaidiana na kupeana nguvu. Na zaidi kukosekana kwa kimojawapo huharibu mfumo wote. Kwa mantiki hiyo hiyo, mtu huwezi leo kusimama kusifia mahospitali bila kueleza awali zilijengwa kwa fedha gani. Sote tunajua kwamba kodi za wazee wetu zilichotwa na serikali ya kikoloni na kupewa mashirika ya Kikristo kujenga na kuendesha mashule na mahospitali wakati Waislamu wakinyimwa. Hili mbona wasomi wetu wanakosa ufundi na umahiri wa kulieleza hadharani. Lakini vile vile, unapozungumzia mafanikio ya mashule na mahospitali ya Wakristo huwezi kuacha kuzungumzia "Memorandum of understanding" kati ya serikali na makanisa, au ni mabilioni mangapi ya shilingi serikali yetu inatoa kila mwaka ili kuendesha mahospitali ya Bugando na KCMC. Aidha, huwezi kuzungumzia mafanikio ya Wakristo na kufeli kwa Waislamu katika nyanja mbalimbali leo, bila kuzungumzia pia hatua ya serikali yetu kuyafungulia milango mashirika ya kidini ya Kikristo na nchi za Ulaya katika miaka ya 1960, huku ikipiga marufuku jumuiya za Kiislamu na kukata mawasiliano na wenzao wa nje. Tungependa tusisitize kwamba namna pekee ya kushughulikia malalamiko haya ya Waislamu ni kuunda tume huru ya uchunguzi na utafiti Jambo la kusikitisha ni kwamba, wakati hatua za kupata ukweli wa mambo hazijachukuliwa, baadhi ya viongozi wa serikali wamejipa haki ya "kujibu" malalamiko ya Waislamu kwa namna ambayo haipi serikali hadhi inayostahiki mbele ya macho ya wananchi. Mfano wa hivi karibuni ni kauli ya Waziri wa Elimu, Prof. Kapuya aliyoitoa Bagamoyo katika Baraza la Maulid yaliyoandaliwa na Bakwata Julai 7, 1998. Prof. Kapuya katumia nafasi ile kuwashutumu Waislamu kuhusu kuwa nyuma kielimu kwa kuwashushia lawama zisizokuwa na msingi kwa maana ya kutotokana na utafiti wowote wa kisayansi bali hisia na kauli za namna ya watu wanaopenda kusema lolote kila wanapohisi kufanya hivyo. Baya zaidi ni kwamba, Prof. Kapuya ameamua kutumia jamii ya Wakristo kama kigezo chake cha kuwatathmini Waislamu katika maendeleo ya elimu. Hatujui kwa nini kafanya hivyo kwa sababu yeye kama kiongozi wa serikali tulimtegemea kutoa kauli zake kwa mujibu wa sera, mipango na maandalizi ya serikali waliyowafanyia wananchi kisha ayatolee ushahidi kuonyesha kuwa hapakuwa na kizingiti chochote katika utekelezaji au usimamizi wa utekelezaji wa sera hizo kama ambavyo Waislamu wamekuwa wakilalamika miaka nenda miaka rudi! Bila shaka, serikali kwa kupitia kwa viongozi wake kama Prof. Kapuya wanataka kuona Waislamu wanapambana na Wakristo katika malumbano ya nani mwenye mwelekeo, sera na dira ya maendeleo nchini. Hakika katika hili serikali imedhihirisha kuwa ama haina jibu sahihi kwa lawama za Waislamu au wana ajenda ya kutaka kuwapambanisha Waislamu na Wakristo nchini kwa kisingizio chochote kile! Waislamu wamesalimika na fitna za kutaka kuwapambanisha na Wakristo katika suala la mahubiri ya dini. Ni hivi karibuni tu viongozi wa makanisa wamekana madai ya serikali kuwa Waislamu wamekuwa wakikashifu Ukristo katika imani yao kuwa Yesu si Mungu. Na hivyo Waislamu wasingependa serikali katika suala hili la maendeleo kuwasakizia Wakristo. Kama kuna upendeleo kwa Wakristo dhidi ya Waislamu unaofanywa na serikali, basi ijulikane kuwa si jukumu la Kanisa kuongoza serikali na kama hili lipo, ni kosa linalofanywa na serikali kuwapa Kanisa mamlaka ya kuweka mwelekeo, sera na dira ya nchi badala ya serikali kufanya hivyo. Na katika hilo, serikali labda vile vile kupitia Waziri wake, Prof. Juma Kapuya itueleze lini itawaambia Waislamu nao waandae mwelekeo, sera na dira ya maendeleo ili serikali ipate kuitumia na kuwafanya wasifike na kupatiwa fursa za kuingia katika mikataba ya memorandum of Understanding na mataifa ya nje kama vile ambavyo Wakristo walivyoruhusiwa kuingia na serikali ya Ujerumani. Serikali itoe fursa hiyo ili Waislamu wapewe mamilioni ya pesa za kodi ya wananchi kama vile ambavyo inaruhusu ujenzi wa Hospitali za Wakristo, kisha zikageuzwa kigezo cha kuwasimangia Waislamu! Serikali ieleze lini Waislamu wapeleke sera zao ili nao wapate upendeleo wa kuchaguliwa peke yao katika nafasi za Ukatibu Tawala wa mikoa na kwenye Mabaraza ya Parole! Serikali ni vyema sasa ikatuambia vile vile ni sera gani iliyoipendeza na hata kuanzisha uhusiano na Makao Makuu ya Kanisa Katoliki (Vatican) kwa hadhi za kibalozi na sera zipi zilizowachukiza na kuizuia kuikubali OIC? Tunaomba majibu yatakayotuonyesha kuwa serikali yetu haiendeshwi kwa mwelekeo, sera na dira ya Kanisa tena Kanisa lenyewe Katoliki kama ilivyoonyeshwa kwenye kitabu cha Dr. Sivalon. |
Maoni yetu: Prof. Juma Kapuya, vipi Muislamu usijue agenda za Waislamu? Hatimaye Mzee Katambo, Chata waachiwa
Sheikh Bafadhil aitaka Bakwata iwe
mtetezi wa Waislamu
Makala: Uinjilisti wa Mbuni haufai
Mussa Katambo: Mzee aliyewekwa rumande kwa kuandaa mihadhara Makala: Elimu ya ngono yapenyezwa
tena Zanzibar
Arusha wasema: Hongera Mhe. KK kwa
kuwa mfano mwema
Wanawake Songea kuandaa maonesho
Kesi ya mgogoro wa Ardhi
AN-NUUR marufuku
gerezani?
Waislamu Karagwe wadai kusalishwa
na imamu asiyejua kutawadha
Ofisi mpya za Rabita
|