|
Na. 062 Jumatano Agosti 23 - 29, 2000 |
|
|
|
|
|
Yanga, Mtibwa nani bingwa leo?
AMA kweli! Leo ni leo, msema kesho muongo, huko Morogoro katika uwanja wa Jamhuri, miamba miwili katika soka, Yanga na Mtibwa ya Turiani zitaumana vilivyo kuusaka ubingwa wa Tanzania Bara. Kulingana na msimamo wa ligi ulivyo mpaka leo hii, timu yoyote katika hizo inaweza kutawazwa ubingwa ikiwa itapata ushindi wa kabila yoyote. Aidha, hata timu ya Kajumulo yenye maskani yake mkoani Dar es Salam kama ilivyo Yanga inaweza kupata bahati ya mtende ya kuwa bingwa endapo Yanga na Mtibwa zitatoka sare au suluhu na Kajumulo ipate ushindi. Kajumulo (babu Kaju) leo inamenyana na timu machachari ya Singida United huko huko Singida ambayo nayo inahitaji ushindi ili icheze Ligi ya Muungano ya Tanzania kwa mara ya kwanza. Watani wakubwa wa Yanga nchini, Simba ambao waliianza ligi hii kwa kishindo lakini mwishoni wakaharibu, wanayo pia nafasi ya kuingia kwenye tatu bora endapo wataizaba Kagera Stars mabao ya kutosha leo hii huko Bukoba na wakati huo huo wafanye sala ili "Babu Kaju" iumizwe na Singida. Hata hivyo, mchezo ambao bila shaka unavuta hisia za 'Wabongo' wengi ni ule kati ya Yanga na Mtibwa ambao umebatizwa jina mpambano wa kifo kutokana na umuhimu wake wa pekee. Chama cha soka nchini FAT kupitia kwa Mwenyekiti wake, Idd Kipingu kimemtaja mwamuzi wa daraja la kwanza, Hussein Kantabula kuwa atachezesha mng'ang'ane huo huku akisaidiwa na Charles Ndagala na Idd Ramadhani kutoka daraja la kwanza la uamuzi hapa nchini. Izingatiwe kuwa tayari Yanga ilikwisha tangaza kutokuwa na imani na Kantabula kwa dhana kuwa huwa hawatendewi haki sawa kwa wote wachezezapo na kupelekea timu yao kutofanya vizuri. Kufuatia madai hayo ya Yanga, Kipingu ametangaza rasmi jana kupeleka kachero wa marefa Mzee Gracian Matovu kushuhudia mechi hiyo ili kuchunguza mwenendo mzima wa Kantabula katika mechi hiyo licha ya kuwepo kamisaa wa mchezo huo Kassim Kashuke. Mpambano mwingine wa kuhitimisha ligi hiyo leo
ni baina ya Prisons na Coastal Union ya Tanga utakaochezwa mjini Mbeya.
Na Mwandishi Wetu WAKATI ligi kuu Tanzania Bara nane bora inahitimishwa leo, kuna habari kuwa tayari watani wa jadi nchini, Simba na Yanga zimeanza kupigana vikumbo katika kugombea wachezaji wapya. Tukio hili linafanana na lile la mwaka jana wakati klabu hizo kubwa nchini zilipojikuta zikuwanyang'anyia wachezaji Steven Mapunda 'Garincha' na Ephraim Makoye ' Dodo'. Mchezji anayetajwa kuwemo katika sakata hilo safari hii ni kiungo maridadi wa Coastal Union ya Tanga, Waziri Omar Mahadhi bin Jabir. Kwa mujibu wa taarifa tulizonazo, tayari viongozi wa klabu ya Simba wamekwishazungumza na Mahadhi na kijana huyo mwenye umri wa miaka 19 ametoa matumaini kwa wana Msimbazi hao. Kitu cha ajabu, hata viongozi wa klabu ya Yanga nao wamelithibitishia gazeti hili kwamba Mahadhi ameonesha nia ya kutua katika makutano ya mitaa Twiga na Jangwani. "Ni kweli Mahadhi nimemuona ni mchezaji mzuri, na kuna kiongozi wetu tayari amezungumza naye na nimeambiwa kwamba hana matatizo na sisi", amedai Shungu. Gazeti hili limethibitishiwa kwamba Juma Selemani Nkamia, Katibu Mwenezi wa Simba amepewa jukumu na klabu yake kuhakikisha Mahadhi kutua Msimbazi. Akizungumza hivi karibuni mjini Dar es Salaam kuhusu suala hilo, Mahadhi alikanusha kuteta na kiongozi yeyote kuhusu usajili ama Simba au Yanga. Hata hivyo, Mahadhi alikiri kupata fununu kwamba viongozi wa klabu ya Simba ambayo aliwahi kuichezea marehemu baba yake Omar Mahadhi bin Jabir wamepania kumsajili kwa ajili ya msimu ujao wa ligi. Alipoulizwa kama ataamua kuichezea klabu ipi kati ya Simba na Yanga, Mahadhi ambaye ni mwanafunzi wa Kidato cha Tano katika shule katika shule ya Jitegemee Sekondari ya jijini alijibu: "Kwa kweli itategemea na ushauri wa mama aliyeko mkoani Tanga, kama unavyojua baba yetu alishafariki kwa hiyo mtu pekee ninayemtegemea kwa ushauri ni mama tu". Hata hivyo, Mahadhi hakusita kuweka bayana kwamba kiwango cha fedha kitakachotolewa na klabu hizo huenda kikaamua hatima yake katika timu hizo mbili. Kwa sasa Mahadhi licha ya kuwa mchezaji wa Coastal
Unioni pia ni kiungo wa timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 20 mwenye
sifa ya kuzimudu namba 4, 6 na 8 vilivyo.
London, Uingereza MIAMBA ya soka ya Uingereza, Arsenal usiku wa kuamkia jana iliweza kuisambaratisha timu ngumu ya Liverpool kwa mabao 2-0 katika mchezo wa pili wa Ligi Kuu ya Uingereza kwa kila timu. Mchezo huo ulifanyika kwenye uwanja wa nyumbani wa Arsenal, ulikuwa umejaa kila aina ya ubeba uliosababisha wachezaji watatu, wawili wa Liverpool na mmoja wa Arsenal kutolewa nje na mwamuzi. Goli la kwanza la Arsenal lilifungwa katika kipindi cha kwanza. Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Arsenal ilikuwa ikiongoza kwa bao hilo moja. Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, huku kila timu ikifanya badiliko kwa kuwaingiza wachezaji wao nyota, Michael Owen kwa upande wa Liverpool na Kanu kwa Arsenal na kuufanya mchezo uzidi kupendeza licha ya hali ya kuoneshana 'undava' kwa wachezaji iliendelea. Bao la pili la Arsenal lilifungwa na mshambuliaji
hatari wa timu hiyo, Thiery Henry baada 'kumpindua' mchezaji wa Liverpool
na kombora kali lililotemwa na mlinda mlango na mpira kumrudia tena na
kuukwamisha wavuni.
Na Mwandishi Wetu NGORONGORO Heroes, timu ya taifa ya vijana wa Tanzania wenye umri usiochupa miaka 20 inaondoka mapema leo kuelekea nchini Msumbiji kupambana na timu ya vijana wa huko. Mpambano huo wa marudiano ni wa kutafuta nafasi ya kushiriki mashindano ya kugombea kombe la Afrika, maalum kwa vijana wa umri huo. Kanali Idd Kipingu ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Soka nchini, FAT, amesema, timu hiyo itaondoka na jumla ya binadamu 25 wakiwemo wachezaji, makocha, tabibu wa timu na viongozi wa FAT. Ikumbukwe kwamba awali kabisa, Kanali Kipingu alinukuliwa akisema kwamba FAT haina fedha za kuisafirisha timu hiyo ambapo gharama zilikadiriwa kufikia shilingi milioni 20 za Kitanzania. Kuhusu hoja kwamba wapi zilikopatikana fedha za kuisafirisha Ngorongoro, Kipingu amesema tayari kuna watu binafsi na taasisi mbalimbali waliojitolea vyao kuhakikisha inasafiri. Amezitaja baadhi ya taasisi hizo kuwa ni Kurugenzi ya Maendeleo ya michezo katika Wizara ya Elimu na Utamaduni, Kampuni ya Muhammed Enterprises na shule ya Sekondari ya St. Mary's. Katika mchezo huo Ngorongoro inahitaji ushindi au sare ya aina yoyote ya mabao ili isonge mbele kwani katika mchezo wa kwanza hapa jijini timu hizo hazikufungana. |
YALIYOMO
TAHARIRI
Prof. Lipumba ana uwezo wa kuongoza nchi - CCM Kampeni
za uchaguzi 2000, CCM yamalizia muda wake na kusema:
Vita dhidi ya rushwa ianzie kwa vigogo -Lipumba Wakati umefika wanawake kushiriki siasa - Mugissa CUF Kigamboni kuzindua kampeni leo USHAURI NASAHA
MAKALA
MAELEZO BINAFSI
MIPASHO NASAHA
MAKALA
KALAMU YA MWANDISHI
LISHE
|
|
|
|
|