|
Na. 062 Jumatano Agosti 23 - 29, 2000 |
|
|
|
|
|
Wananchi kajiandikisheni kupiga kura ili kuleta mabadiliko ya serikali kwa njia ya amani Na Rajab Kanyama Mkondo bora wa Kidemokrasia katika jamii maana yake ni wananchi wenye nchi kuwa na uwezo wa kujiamulia wenyewe kuhusu kiongozi wanaemtaka. Njia muafaka ya kutimiza azma hii azizi, ni kwa wananchi wote walio na sifa ya kupiga kura, kutumia fursa hii bila kukosa. Jambo hili ni kwa sababu, katika utawala wa kidemokrasia, jukumu la serikali ni kubuni, na kusimamia mipango ambayo kwa namna moja au nyingine itawanufaisha wananchi kisiasa, kiuchumi na kijamii. Haya ni masuala yanayohitaji ujuzi na elimu ya kutosha, na yatawezekana tu, kama serikali husika itakuwa na tabia ya kuheshimu wananchi kwa kuwasikiliza shida zao, na kujaribu kuzipatia ufumbuzi. Hii,ni pamoja na kufuata ushauri wao pale watakapoutoa, baada ya kuona kwamba mambo hayapelekwi kama inavyostahili. Katika mfumo wa Kidemokrasia tunaoufuata hapa nchini, wenye jukumu la kuwasilisha maoni na matakwa ya wananchi kwa serikali, ni wabunge, wawakilishi, madiwani,na viongozi wa vyama vya siasa mbali mbali. Kwa maana hii, ni lazima vyombo hivi viheshimiwe na kupewa hadhi inayostahili Hata hivyo, ni lazima wananchi wachukue tahadhari ya kutosha ili wasipotoshwe. Utakapoona wabunge,viongozi wa vyama vya siasa, na wawakilishi wanapotosha ukweli na hawazungumzii kero na matatizo ya kweli ya wananchi, fahamu kwamba watu hao wanawatumia wananchi kama ngazi ya kufanikisha mambo yao wenyewe. Njia pekee, madhubuti yakuhakikisha kwamba serikali iliyoko madarakani inatimiza na kukidhi haja za wananchi, ni kwa kuwa na viongozi wenye elimu ya kutosha, bora na waadilifu watakao iongoza serikali husika. Sifa kuu za kiongozi mwenye sifa tulizotaja ni kupenda na kutochoka kukutana na wananchi wengi kadiri inavyowezekana, na sifa ya pili ni ile ya kujiamini, baada ya kumwaga sera,kiongozi bora hukaribisha maswali. Wanasayansi ya jamii wanasema-Jambo hili hufanywa ili kufafanua na kuweka masuala wazi, kwa sababu upeo wa fikra za wananchi hutofautiana. Viongozi wabovu hupenda kinyume chake, wao sifa yao kuu ni, nidhamu za kinafiki, kiburi na majivuno. Kwa kawaida, viongozi wa aina hii hawapendi maswali, na mara zote hutumia vitisho na mbinu nyingine ili kuficha ukweli. Njia ya Kidemokrasia ya kuwaondoa madarakani viongozi wasiofaa,ni kuwanyima kura wakati wa uchaguzi utakapofika, hatua ya kwanza ni kujiandikisha. Yapo mambo kadhaa, ambayo wewe mwenye nchi mpiga kura unapaswa kuyafahamu, ili kufanikisha azma yako ya kumchagua kiongozi unayemtaka. Sheria ya uchaguzi imewaamuru wasimamizi wa uchaguzi,kuweka orodha ya wapiga kura wote waliojiandikisha kama wapiga kura katika kila kitu cha kuandikisha wapiga kura. Haki ya kukagua orodha ya waliojiandikisha kama wapiga kura ni haki ya msingi, ambayo wananchi wote wanayo. Kama msimamizi wa uchaguzi hakuweka orodha ya waliojiandikisha kupiga kura katika kituo husika, mwananchi yoyote anayo haki ya kumuandikia msimamizi wa uchaguzi amruhusu akague orodha ya wapiga kura waliojiandikisha kama wapiga kura katika kituo husika. Jambo hili ni vema likazingatiwa na wananchi wote, maana kwa kukagua orodha ya waliojiandikisha kupiga kura, wananchi wanaweza kugundua njama za watu kujiandikisha zaidi ya mara moja, au kutumia majina ya bandia, au majina ya watu waliofariki, au ya watu walioletwa mahsusi na mgombea anayetumia ujanja kushinda uchaguzi wa jimbo la ubunge. Kwa kawaida, ubora au ubovu wa serikali, hutokana na maamuzi ya wananchi wenyewe. Jambo hili, husababishwa na tabia mbaya ya baadhi ya wananchi kudharau na kuacha kupiga kura -wakati unapowadia, kwa visingizio kuwa kiongozi yeyote atakayechaguliwa kwao ni sawa tu. Hii ni dhana potofu kabisa, ambayo ni mazao ya kudumaa kwa fikra yakinifu. Iweje mtu utegemee kupata kiongozi mzuri,bila yawewe mwenyewe kushiriki kumchagua? Huu ni upande mmoja, upande wa pili wapo wauza shahada na wale wanaodai kwamba nguvu za chama tawala ni kubwa, kiasi ambacho si rahisi kwa chama cha upinzani kuweza kupata ushindi, na kuunda serikali. Hawa nao, ni matunda ya kasumba na propaganda za wahafidhina za muda mrefu,ambazo zimewadhoofisha kifikra na kuwaaminisha kwamba wao hawana uwezo wa kufikiri, wala kuamua wanachokitaka, tofauti na kile kinachotakiwa na watawala. Wananchi wenye fikra potofu kama hizi, wanasahau kwamba serikali huwekwa madarakani ili iwahudumie wao na si vinginevyo bila ya kujali itikadi zao za kisiasa,kidini, kikabila au rangi zao. Ni jukumu la kila mtu binafsi, kupiga kura kwa lengo moja kubwa, nalo ni kumuondoa Diwani, Mbunge, au rais mla rushwa, asiyejali maslahi ya baadhi ya wananchi wake, ili kupeleka ujumbe kwa serikali mpya itakayoingia madarakani kujali zaidi maslahi ya wananchi,badala ya maslahi ya kikundi cha wanaotawala. Hiyo ndiyo njia pekee ya kuwajibisha serikali,maana mkisha kuwang'oa wakuda wanaoendesha serikali kienyeji katika utendaji wake, viongozi wa serikali inayofuata watajiheshimu, kwa vile watakuwa na uhakika kwamba,hata na wao wanaweza wakaondolewa madarakani kwa kura, wakati wa uchaguzi utakapofika. Kura yako itakuwezesha kuchagua serikali unayoitaka au kuiondoa Serikali ambayo unaona haikutendei haki. Wananchi, wanapaswa kupiga kura kwa kuangalia vigezo halisi ambavyo ni matendo na tija iliyoletwa na serikali iliyoko madarakani. Njia rahisi ya kufanya hivyo, ni kulinganisha hali halisi ya maisha yako, wakati wa utawala wa mzee Ruksa Alhaj Ally Hassan Mwinyi na sasa. Hivi ni kweli, maendeleo ni wananchi kutokuwa na pesa? Hivi ni kweli, maendeleo ni wananchi kutokuwa na ajira na vipato visivyo ridhisha? Hivi ni kweli, maendeleo ni mazao ya biashara kukosa soko, na sehemu nyingine kuachwa kuzalishwa kabisa? Hivi ni kweli, maendeleo ni kuuza mali ya umma kwa wageni, tena kwa bei karibu na bure. Je ni kweli, wananchi walishirikishwa na kukubali mali yao iuzwe na wao wabaki kuwa ni vibarua katika nchi yao? Hivi, ndivyo vigezo vya kutumia siku ya kupiga kura. Maoni na ushawishi wa vyombo vya habari, waachieni wenyewe, maoni na ushawishi wa BAKWATA na Baraza la Maaskofu, wachieni wenyewe,maoni na ushawishi wa wapiga bao, sangoma wanaotabiri kwamba tukibadilisha uongozi wa nchi kutatokea vurugu, tunawaambia wao walie tu,kwanza hawana uwezo wa kufahamu matokeo ya siku za usoni, na kama ni vurugu, wataanzisha wao kwa sababu ya uchu wa madaraka. Wakitaka mfano, wakumbusheni zoezi lao la kutafuta wagombea wa udiwani na ubunge kwa tiketi ya chukua chako mapema. Kama wenyewe kwa wenyewe wamefikia hatua ya kupigana mapanga na kutishiana bunduki,wapinzani wao watanusurika? Wananchi kaeni chonjo, saa ya ukombozi ni tarehe 29 Oktoba 2000,siku ya kuchambua mchele na chuya, kama alivyosema Alhaj Ally Hassan Mwinyi, mtanikumbuka. |
YALIYOMO
TAHARIRI
Prof. Lipumba ana uwezo wa kuongoza nchi - CCM Kampeni
za uchaguzi 2000, CCM yamalizia muda wake na kusema:
Vita dhidi ya rushwa ianzie kwa vigogo -Lipumba Wakati umefika wanawake kushiriki siasa - Mugissa CUF Kigamboni kuzindua kampeni leo USHAURI NASAHA
MAKALA
MAELEZO BINAFSI
MIPASHO NASAHA
MAKALA
KALAMU YA MWANDISHI
LISHE
|
|
|
|
|