NASAHA
Na. 062 Jumatano  Agosti 23 - 29, 2000
Ukurasa wa mwanzo
Islam Tanzania
Matoleo yaliyopita
TAHARIRI 
S.L.P. 72045, Dar es Salaam

Kama hamtaki demokrasia, mnataka nini basi?

Mfumo wa siasa wa vyama vingi uliporudishwa nchini mwaka 1992, chama tawala kilidai kutaka kusifiwa kwa kurudisha mfumo huo kwa hisani yake kutokana na kupenda demokrasia, maana ilidaiwa kuwa wananchi waliukataa mfumo huo kwa asilimia 80 (80%) ya maoni yao.

Hiki ni kitendawili cha kushangaza: Ni vipi yule anayejigamba kupenda demokrasia abatilishe maoni na uamuzi wa walio wengi?

Ufumbuzi wa kitendawili hiki ni kwamba ubatilishaji huo haukulalamikiwa na yeyote kati ya wale wenye asilimia 80, badala yake ulishangiliwa na wote!.

Hata hivyo, ukweli wa maoni yale hatimaye ulijulikana. Ni 80% ya wananchi ndio waliotaka vyama vingi na iliyobaki (20%) ndiyo iliyokuwa ikitaka kung'ang'ania mfumo wa chama kimoja.

Ukweli wa maoni yale pia ulionesha kuwa wananchi wale wenye 80% walitoa hoja zao kwa kitendawili. Sababu ya kufanya hivyo ilielezwa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa kwamba ilitokana na dhana ya kuwepo kwa mtego. Ilielezwa kwamba hawakuamini kama wale walioufuta mfumo wa vyama vingi baada ya Uhuru wa Tanganyika, 1961, kisha wakawataka wananchi kudumisha fikra na hatamu za chama kimoja kwa zaidi ya miaka 30, wangelikuwa tayari kukubali mfumo wa vyama vingi.

Hivyo, wananchi wale 80% wakatoa maoni yao kwa namna ambayo ukiyachambua kwa dhati utaupatau kweli, maana na kusudio la maoni hayo. Na ndivyo ilivyokuwa maoni yale yalipofichuliwa yalimaanisha kutakiwa vyama vingi, na endapo itang'ang'aniwa kuwepo chama kimoja, maoni yale yalisema: 'basi na kiwepo, lakini kisiwe na ukiritimba wala hatamu yoyote ya kisiasa ya kumkaba mwananchi kama farasi.'

Wachambuzi wa maoni yale waliyaelewa vizuri sana. Yalikuwa yamejaa salamu za nyakati; kwamba wakati ni ukuta, na ukiamua kupigana nao utaumia, na pengine kusababisha maumivu kwa wengine, na si ajabu hatimaye ukaleta maafa mabaya zaidi.

Tanzania kuna amani. Amani hii haikutengenezwa na yeyote kutokea kwenye jukwaa la siasa. Wala haitokani na mikopo ya IMF au ruzuku ya 'akina Clinton'. Ni amani ya asili iliyojengwa na kudumishwa na mabibi na mababu wa nchi hii. Kama ulikuwepo uhasama baina ya wananchi wa makabila mbalimbali, mabibi na mababu hao walikwisha umaliza na kuwapatanisha wahusika ambao leo ni watani tu; wakutaniana katika misiba na sherehe.

Juhudi na mbinu za wakoloni za kutaka kutumia dini na makabila ili waendelee kutawala nazo zilishindikana. Wananchi waliungana kwa dini na makabila yao, wakawang'oa wakoloni.

Tunayasema hayo kwasababu hivi sasa nchi yetu imo katika mfumo wa siasa za kidemokrasia, mfumo unaotoa haki kwa kila mwananchi kuamua kujiunga na kupigia kura chama akitakacho.

Ingawa mfumo huu unakubalika na wengi katika nchi mbalimbali, kwa habati mbaya, mfumo huu pia ulijengewa hoja na vyombo vya fedha duniani pamoja na mataifa makubwa ya nchi za Magharibi kama moja ya masharti ya nchi kukubalika kupata mikopo toka kwenye vyombo hivyo na misaada kutoka nchi za Magharibi.

Hatudhani kuwa vigezo vya vyombo hivyo vya fedha pamoja na vile vya 'akina Clinton' vyenye kushurutisha kuwepo demokrasia, haki na uhuru kwa wananchi ni vigezo sahihi, vya kututhibitishia kuwepo kwa hali nzuri katika nchi. Sote tunakumbuka kwamab hakuna chombo hata kimoja katika hivyo wala akina walioweza kusitisha uhusiano wao na Afrika Kusini ya makaburu iliyokuwa ikiwatesa wananchi kwa kupinga ubaguzi na kudai haki sawa kwa wote.

Hao ndio waliokuwa wakimuunga mkono aliyekuwa Rais wa iliyokuwa Zaire Mobutu Sseseko, wakati wananchi wa Zaire wakiteseka kwa umasikini, maradhi na ujinga katika nchi yao yenye utajiri mkubwa wa maliasili za madini na kadhalika.

Hao hao ndio waliokuwa wakimuunga mkono Gaidi Jonas Savimbi kuendeleza vita iliyoua na kutesa wananchi wa Angola kwa zaidi ya miaka 20 ya uhuru wao. Wala haitokuwa ajabu tukisikia kuwa wanamuunga mkono gaidi mwingine, John Garang na vikundi vya waasi nchini Sudan vinavyopigana na kusababisha mauaji ya mamia ya wananchi Sudan.

Wala hatudhani kwamba nchi kuwa na vyama au kutokuwa na mfumo wa vyama vingi ni tatizo kwa 'akina Clinton'. Uganda hawana vyama vingi wala hata mfumo wa chama japo kimoja, lakini ni miongoni mwa wenye kusifiwa na 'akina Clinton'. Wanasamehewa madeni na IMF na kuongezewa mengine mengi.

Hatukutoa mifano hiyo kwa maana ya kutaka kuingilia mambo ya nchi zingine, bali ni kutaka kusisitiza tu kwamba kama tumekubaliana kujiwekea mfumo wa vyama vingi vya siasa katika nchi yetu, na kama tunatambua kuwa wananchi wa nchi hii wako huru na wana haki ya kuutumia uhuru wao kujiamulia mambo yao wenyewe, basi vigezo vya ubora wetu wa jinsi tunavyoendesha au tutakavyoendesha nchi yetu, vitoke kwa wananchi wenyewe ambao ndio wenye nchi yao.

Tunachosema ni kuwa ikiwa kama tumekubaliana kuwa na demokrasia ya mfumo wa vyama vingi basi, demokrasia hiyo iachiwe ifanye kazi yake. 

Vyama na wananchi ambao ni wanachama wa vama hivyo pia wapewe haki yao ya kidemokrasia ya kushiriki katika shughuli zote zikiwemo hizi zilizopo sasa za wananchi kujiandikisha na kukipigia kura chama wakitakacho. 

Kadhalika, vyama hivyo vipewe uhuru wa kufanya mikutano ya hadhara ili kunadi mipango ya sera zao, mipango yao, kuwatangaza wagombea wao na kushawishi kura toka kwa wananchi ili, katika Uchaguzi Mkuu ujao, wapate kuwapigia kwa ridhaa yao wenyewe.

Misingi ya uhuru na demokrasia inakataza wananchi kunyimwa haki hiyo. Misingi hiyo inataka mamlaka zote na vyombo vyote vikiwemo vyombo vya dola, kutambua na kudumisha demokrasia, uhuru na haki hizo za wananchi. Misingi hiyo inataka mamlaka na vyombo hivyo vitambue kuwa hakuna kikundi chochote cha wananchi kilichosusiwa uongozi wa nchi, ndio maana wananchi wote wameamua kushiriki katika kuomba kura za wananchi.

Tunaamini kuwa mamlaka za nchi na vyombo vya dola vinatambua majukumu yake ya kuwatumikia wananchi katika wakati huu tuliomo tukielekea kwenye Uchaguzi Mkuu. Lakini ni jambo la kusikitisha kuona mambo yaliyo kinyume na mazingira ya maandalizi ya uchaguzi wa kidemokrasia yanavuma kama mambo mazuri na ya kawaida licha ya kulalamikiwa na wananchi.

Kukithiri kwa rushwa kwenye kura za maoni, na pia madai ya kuwemo kwa rushwa hiyo kwenye kushawishi baadhi ya wagombea, si vitu vinavyostahili kuachwa vionekane vya kawaida wakati kuna mamlaka za kuzuia rushwa nchini.

Yapo pia Mamlaka ya kusimamia adabu na taratibu za vyombo vya habari. Vile vile ipo Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo moja ya majukumu yake ni kuona kuwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika 29 Oktoba, mwaka huu unakuwa huru na wa haki. 

Ikiwa ni hivyo basi iweje baadhi ya vyombo vya habari viachiwe kutoa matangazo ya kupotosha ratiba na mipango ya vyama vingine?

Kwanini mamlaka hizo hazionekani kuchukua hatua dhidi ya vyombo hivyo. Ni kitu gani kinachoshawishi upotofu wa kazi za vyombo hivyo; je, ni ukosefu wa maadili, rushwa au chuki?

Je, mambo hayo au chuki hizo zitakapoachiwa zijengeke na kujulikana na wananchi pasipo kuchukuliwa hatua zozote na mamlaka husika, tunataka wananchiwaelewe vipi?!

Ikiwa katika nchi yetu maadili mema hayatakiwi, rushwa 'imeruhusiwa' na chuki imeachwa ijengeke', je, hayo mengine yatakapoachiwa, bado tutakuwa na haki ya kujivunia kuwepo kwa uhuru na demokrasia ya wananchi kuendesha mambo yao kwa haki na usawa?

Viongozi na wafuasi wa vyama vya upinzani wamekuwa wakilalamika kwamba wamekuwa wakizuiliwa kufanya mikutano yao ya hadhara katika baadhi ya mikoa. Huko Zanzibar tunaambiwa kwamba polisi, wakiwemo wale wenye silaha za kuzuia ghasia, wamekuwa wakivinjari maeneo ya wananchi kujiandikisha kupiga kura. Mwishoni mwa wiki iliyopita katika ufunguzi wa kampeni za uchaguzi polisi, wakiwemo wale wakuzuiaghasia, pia waliripotiwa kutanda katika baadhi ya mitaa ya Dar es Salaam, ambao walionekana kuvinjari zaidi karibuna mikutano ya vyama vya upinzani na kwenye njia zinazoelekea kwenye mikutano hiyo.

Kwa vyovyote vile, hali hii haitoi wala kujenga mazingira ya kuwepo kwa uchaguzi wa kidemokrasia ulio huru na wa haki.

Ndio maana tunauliza, endapo mamlaka na vyombo husika haviruhusu mazingira ya kujenga demokrasia, vinataka nini badili yake?

Juu
 

YALIYOMO
 

TAHARIRI
Kama hamtaki demokrasia, mnataka nini basi?

Prof. Lipumba ana uwezo wa kuongoza nchi - CCM

Kampeni za uchaguzi 2000, CCM yamalizia muda wake na kusema:
Imefanya kazi ya ‘kuipendeza’ Marekani

Vita dhidi ya rushwa ianzie kwa vigogo -Lipumba

Wakati umefika wanawake kushiriki siasa - Mugissa

TLP yadaiwa kuukejeri Uislamu

CUF Kigamboni kuzindua kampeni leo

USHAURI NASAHA
Nimechoka kuwa mtangazaji wa redio

MAKALA
Mungu na mataifa ya dunia

MAELEZO BINAFSI
Mjue mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Prof. Lipumba

MIPASHO NASAHA
Krosi matiplikesheni!

MAKALA
Wananchi kajiandikisheni kupiga kura ili kuleta mabadiliko ya serikali kwa njia ya amani

KALAMU YA MWANDISHI
Mkijirekebisha mtakaribishwa

Habari za Kimataifa

LISHE
Unakula au unaliwa?

MASHAIRI

MICHEZO

  • Yanga, Mtibwa nani bingwa leo?
  • Ugomvi mkubwa baina ya Simba na Yanga waibuka 
  • Arsenal yaitandika Liverpool
  • Ngorongoro Heroes yaenda Msumbiji

  •  


    Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu:Bonyeza hapa
    Au
    Andika barua  kwa: nasaha1420@yahoo.com

    Ukurasa wa mwanzo
    Islam Tanzania
    Matoleo yaliyopita