|
MASHAIRI
Hawa walio wagumu!
Hodi hodi Mhariri, NASAHANI nakujia,
Nipate kuwa habari, umma wa Watanzania,
Wapate zangu habari, gazetini kupitia,
Hawa walio wagumu, watupeleka pabaya.
Hasa hawa wanawake, wallahi ninaapia,
Ni wagumu wanawake, upinzani kuingia,
Wana nini wanawake, dhuluma kukumbatia,
Hawa walio wagumu, watupeleka pabaya.
Ni waoga wanawake, CUF kuweza ingia,
Ni kidumu peke yake, ndiko wengi waingia,
Kumbe msingi wake, ni amani wahofia,
Hawa walio wagumu, watupeleka pabaya.
Wamekuwa ni daraja, kidumu kujipitia,
Amani watajataja, eti ndio wahofia,
Upinzani ukitaja, hata haki wasusia,
Hawa walio wagumu, watupeleka pabaya.
Wengine ni kina babu, kero kwa wetu umoja,
Ni watu watabutabu, kuunda wetu umoja,
Upinzani kwa tabu, nao AMANI ni hoja,
Hawa walio wagumu, watupeleka pabaya.
Kama ni hiyo amani, wao wanao hofia,
Ataevuruga nani? kama si kusingizia,
Mpenda vitu ni nani? Wallahi wamesinzia,
Hawa walio wagumu,watupeleka pabaya.
Kilicho wasibu nini?, Kwa Mungu nawaombea,
Wanakorogwa na nini?, Mbona jama wapotea,
Hawaitaki kwa nini?, “Haki” iliyopotea,
Hawawalio wagumu, watupeleka pabaya.
Au kukosa Elimu?, ndiko kuna wasumbua,
Sasa kwa nini wagumu?, ni kikwazo wamekua,
Mbona maisha magumu, kila mtu anajua,
Hawa walio wagumu, watupeleka pabaya.
Hivi dhiki hawaoni? kwa nini wang’ang’ania,
Wajifanya kisirani, kutuzuilia njia,
Watajibu kwa manani, Wallahi nawaapia,
Hawa walio wagumu, watupeleka pabaya.
Haya ni maisha gani, ya nyinyi kung’ang’ania,
Watu wengi wako ndani, kisa haki wahusia,
Watu wadini fulani, rumande wanaumia,
Hawa walio wagumu, watupeleka pabaya.
Mtu usemapo kweli, utatiwa kifungoni,
Nchi yenye chuki kali, ubaguzi chini chini,
Wawakataa wakweli, kisa eti wapizani,
Hawa walio wagumu, watupeleka pabaya.
Kaditama ni mwishoni, nawaomba wapinzani,
Kikwazo sasa AMANI, mkifuzu mtawini,
Sasa na dini AMANI, watu wawe na imani,
Hawa walio wagumu, watupeleka pabaya.
Almasi H. Shemdoe, “Tunda laMatumaini”,
Dar es Salaam.
Ulevi ni ule ule
Naamka kitandani, usingizi meniruka,
Ni usiku wa manani, kalamu nitaishika,
Nikakaa kwa makini, tungo nikaziandika,
Nnainuka kitini, asubuhi imefika.
Naanza kuziandika, tungo zangu gazetini,
Ukweli mnawahaka, kuwaeleza jamani,
Msije mkadhurika, lazima muwe makini,
Wamebadilisha chupa, ulevi ni ule ule.
Wamebadilisha jina, la mgombea kitini,
Aliyekuwapo jana, anaitwa Salmini,
Uchaguzi ukafana, kisha kumweka amani,
Wamebadilisha chup, ulevi ni ule ule.
Kuchaguliwa Amani, wengi walifurahia,
Kwenu nyingi mtihani, ni wazi hilo kujua,
Hili msipoamini, Wallahi mtaumia,
Wamebadilisha chupa, ulevi ni ule ule.
Hata wakifanya nini, chama chao ni kibovu,
Msije mkaamini, mkaacha kula mbivu,
Kwa kumuweka amani, mwaja kula vibovu,
Wamebadilisha chupa, ulevi ni ule ule.
Kura msije zitupa, hao ndio wale wale,
Mwishowe watakutupa, Pemba kurudie kale,
Wanaendesha kwa pupa, hawana ila kelele,
Wamebadilisha chupa, ulevi ni ule ule.
Amani hata akija, huko Ikulu sikia,
Tanufaisha Unguja, Pemba ataiachia,
Hiyo ndiyo yao haja, ni sera yao tambua,
Wamebadilisha chupa, ulevi ni ule ule.
Amani yeye mwenyewe, sio mbaya tambua,
Kosa lake muelewe, ni chama alochagua,
Kitamfanya alewe, bila yeye kujijua,
Wamebadilisha chupa, ulevi ni ule ule.
Sera zao kwa hakika, ni zile zile sikia,
Wananchi kuwaweka, hapa walipofikia,
Maradhi yamefurika, ujinga umeenea,
Wamebadilisha chupa, ulevi ni ule ule.
Nimefika kituoni, hapa nnaishilia,
Tutaonana jioni, kazini nakimbilia,
Likitoka Nasahani, upesi mje nambia,
Msije mkanihini, nakala kunitumia.
Ummul Jamilah,
Dar es Saaam.
Kasuku (Swali)
Kasuku ndege mwituni, wa asilia zamani,
Kasuku yu mtatani, hasa kapatwa na nini,
Kasuku namtamani, anajifia jamani,
Kasuku huyu ni nani, nauliza gazetini.
Kasuku wangu jamani, tuni zake burudani,
Kasuku wangu nyumbani, aliimba si uani,
Kasuku si Myunani, watu walimtamani,
Kasuku huyu ni nani, nauliza gazetini.
Kasuku huyu tunduni, hakuwa na mpinzani,
Kasuku si mpagani, huyu wangu ana dini,
Kasuku wangu makini, watu walitoka pwani,
Kasuku huyu ni nani, nauliza gazetini.
Kasuku aumwa nini, nambieni gazetini,
Kasuku si mwanandani, hili ndugu fahamuni,
Kasuku si mpinzani, si siasa abadani,
Kasuku huyu ni nani, nauliza gazetini.
Kasuku ni wamanani, alitoa vya moyoni,
Kasuku harakatini, malipo hakuthamini,
Kasuku yu ukingoni, alingoja ya peponi,
Kasuku huyu ni nani, nauliza azetini.
Kasuku maji shingoni, watu tena hafanani,
Kasuku pake tunduni, sio bara asilani,
Kasuku si wazamani, wamiaka karibuni,
Kasuku huyu ni nani, nauliza gazetini.
Kasuku si ungujani, sio nje bali ndani,
Kasuku si wamarekani, bali wa hapa jijini,
Kasuku yu taabani, watuwenda upenuni,
Kasukuhuyu ninani, nauliza gazetini.
Kasuku si hayawani, kazi kwenu gazetini,
Kasuku huyu ni nani, hebu nisaidieni,
Kasuku yupo gizani, ameshikwa wahisani,
Kasuku huyu ni nani, nauliza gazetini.
Kasuku si masikini, kinamkondesha nini,
Kasuku muokoeni, nifanye nini jamani,
Kasuku wangu tunduni, ananitoka machoni,
Kasuku huyu ni nani, nauliza gazetini.
Kasuku hajifichani, Nganenga na Jushakani,
Kasuku ni wa manani, Kijukuu na Mbotoni,
Kasuku saidieni, mnijibu gazetini,
Kasuku huyu ni nani, nauliza gazetini.
Kalamu naweka chini, Kasuku huyu ni nani,
Na pia nishaurini, yamfaa tiba gani,
Undani niambieni, asumbuliwa na nini,
Kasuku huyu ni nani, nauliza gazetini.
King Leopard (I),
S.L.P. 12478,
Dare s Salaam.
|
YALIYOMO
TAHARIRI
Kama hamtaki demokrasia,
mnataka nini basi?
Prof.
Lipumba ana uwezo wa kuongoza nchi - CCM
Kampeni
za uchaguzi 2000, CCM yamalizia muda wake na kusema:
Imefanya
kazi ya ‘kuipendeza’ Marekani
Vita
dhidi ya rushwa ianzie kwa vigogo -Lipumba
Wakati
umefika wanawake kushiriki siasa - Mugissa
TLP
yadaiwa kuukejeri Uislamu
CUF
Kigamboni kuzindua kampeni leo
USHAURI NASAHA
Nimechoka
kuwa mtangazaji wa redio
MAKALA
Mungu
na mataifa ya dunia
MAELEZO BINAFSI
Mjue
mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Prof. Lipumba
MIPASHO NASAHA
Krosi
matiplikesheni!
MAKALA
Wananchi
kajiandikisheni kupiga kura ili kuleta mabadiliko ya serikali kwa njia
ya amani
KALAMU YA MWANDISHI
Mkijirekebisha
mtakaribishwa
Habari
za Kimataifa
LISHE
Unakula
au unaliwa?
MASHAIRI
MICHEZO
Yanga, Mtibwa nani bingwa leo?
Ugomvi mkubwa baina ya Simba
na Yanga waibuka
Arsenal yaitandika Liverpool
Ngorongoro Heroes yaenda Msumbiji
|