AN-NUUR 
Na.183 Ramadhan 1419, Januari 8 - 14, 1998 
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita
 
Marekani si rafiki mwema 
 

Hata Iran nayo iliwashawahi kuwa kipenzi cha Marekani wakati wa utawala wa Shah. Wananchi wa Iran walipoung’oa utawala kibaraka wa Shah na kusimamisha utawala unaokubaliwa na walio wengi, wakawa mahasimu wa Marekani. Wakatengenezewa adui wa kuwapiga vita (Iraq). Kumbe urafiki wa Marekani unanoga pale tu taifa lingine likakapofuata muongozo na maelekezo kutoka "White House". Yaani uwe kikaragosi cha Marekani. 

Bila shaka somo hili limeeleweka vyema kwa viongozi wa Iraq na wananchi wake kwa ujumla. Wameshagundua kujipendekeza kwa Marekani ni kukalia kuti kavu. Marekani haijali marafiki bali maslahi yake tu. Iraq inafanya kila namna kuupa mgogoro huu sura ya vita dhidi ya Uislamu ili kupata huruma ya Waislamu ulimwenguni, lakini inakuwa vigumu. 

Ukweli ni kwamba vita hii haina uhusiano wowote na Uislamu bali ni Waislamu. Waislamu ndio wanaoteswa bila ya kosa (victims of circumstances). Hicho ndicho kinachotuuma na kutufanya tuichukie Marekani na washirika wake. 

Ajabu iliyopo mataifa ya Waarabu kama Saudia Arabia, Kuwait na mengineyo ya UAE yanalaani mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iraq wakati wao wenyewe ndiyo wanaotoa "base" ya mashambulizi hayo. Wanadiplomasia wa Marekani wanapotaka kuungwa mkono na mataifa ya Kiarabu katika hujuma zake za kijeshi dhidi ya Iraq, Saudi Arabia, Kuwaiti na UAE ndizo za mwanzo kufuatwa na zinatoa ushirikiano unaohitajika. Wanawaona Wamarekani ni watu wema sana na wenye uwezo wa kuwalindia ufalme wao. 

Kama Waislamu wa Iraq wanaangamizwa na majeshi ya kigaidi ya Marekani, hao wanaohifadhi majeshi haya katika Ghuba ya Uajemi tuwaitaje? Wana haki ya kuilaani Marekani? Hapana! Wao na Marekani wote wanastahiki kulaaniwa! Anayeshirikiana na jambazi ni jambazi vile vile! 

Watawala wa Iraq wameshaona umuhimu wa umoja wa Kiislamu duniani. Umoja wao wa Kiarabu (Arab-League) umeshindwa kuzuia dhoruba iliyowakumba kutokana na udhaifu wa umoja huo. Kimbilio pekee la wa Iraq kwa Waislamu wenzao na wala si Waarabu wenzao. Kwa sababu madhalimu hawana uwezo wa kupambana na Waislamu wa dunia nzima. 

Wananchi wa Iraq wanahitaji msaada kutoka kwa Waislamu wenzao na jumuiya ya kimataifa kwa ujumla. Hawahitaji laana wala shutuma dhidi ya Marekani ili wanusurike na maangamizo ya Marekani. Kwa sababu imeshindikana kuzuia mashambulizi dhidi ya Iraq, basi klichobaki sasa ni kukomesha mashambulizi hayo na viwango vya uchumi ili kuinusuru Iraq na vizazi vyake. 

Iraq haihitaji laana za Arab-League dhidi ya Marekani wala Jumuiya nyingine yoyote ya Kiarabu. Mpango wa kuishambulia Iraq ulikuwepo miaka minane iliyopita nao hawakuchukua hatua zozote za maana kuzuia hali hiyo. Kwani hawakujuwa kwamba mkusanyiko wa majeshi ya Marekani katika eneo la Ghuba ni jambo la hatari na linalotishia maisha ya watu wa eneo hilo? 

Marekani inang’ang’ania eneo la Ghuba ya Uajemi kwa sababu ya maslahi yao ya kisiasa na kiuchumi. Kisiasa, eneo hili ni himaya ya Waislamu. Marekani inafanya kila hila itikadi ya Kiislamu isitawale eneo hili. 

Uislamu unatishia mpango wa Marekani wa kutawala ulimwengu. Kwa hiyo, agenda mojawapo ya Marekani kuweka vituo vya kijeshi nchini Saudia Arabia, Uturuki na maeneo mengine ya UAE ni mkakati dhidi ya Uislamu. Watapambana na yeyote atakayeanzisha cheche za harakati za Kiislamu katika eneo hilo. 

Kiuchumi, Wamarekani wamewekeza sana vitega uchumi vyao katika eneo la Ghuba. Wana malengo ya kutumia maliasili ya eneo hilo (mafuta) kwa manufaa yao. Ndiyo maana wameweka viongozi vibaraka (wafalme) watakaowaunga mkono kwa kila wanalotaka. Atakayepinga ataitwa mkorofi na lazima ang’olewe madarakani. 

Inadhaniwa wanachotafuta Marekani nchini Iraq ni kuuangusha utawala wa Rais Saddam Hussein ambaye si mtiifu tena kwa "White House". Na hivyo husemwa kwamba Marekani imefanya kila jitihada kumng’oa Saddam madarakani bila mafanikio. Imetumia vita vya Ghuba imeshindwa! Imewachochea Wakurd imeshindikana! 

Wametumia vikwazo vya uchumi na "USCOM" bado hawajafanikiwa! Na sasa wanafanya mashambulizi ya kijeshi kwa lengo la kuwafanya wananchi wa Iraq waichukie serikali yao kwa kushindwa kuwalinda. Kwa rehema zake Allah, mashambulizi hayo yamewaunganisha zaidi wa Iraq kama taifa na wote wanaiangalia Marekani na Uingereza kama maadui zao. 

Hivi sasa Marekani imetangaza mpango wake mpya wa kuwasaidia wapinzani wa serikali ya Iraq kumuondoa Saddam Hussein madarakani. Ule mpango wa kuteketeza silaha za maangamizo sasa umekufa imebaki "agenda" yao ya muda mrefu ya kumuangusha Saddam Hussein na kupachika "kikaragosi" chao katika Ikulu ya Iraq kitakachoifanya "White House" kuwa Qibla chake kama ilivyo kwa mataifa mengine ya Kiarabu yanayolizunguka eneo la Ghuba. 

Ukweli wa mambo ni kuwa angalau kwa sasa Marekani haina agenda ya kumng’oa Saddam. Swali lao kubwa ni je; aking’oka Saddam akae nani? Hawataki iwe kama Somalia. Anaondoka Siad Bareh, kila mtu anakuwa Rais. Saddam bado anawafaa Wamarekani kwa kuwadhibiti wananchi wa Iraq. 

Labda onyo kwa mataifa ya Kiarabu yanayoikumbatia Marekani ni kwamba yasidhani majeshi ya Marekani yako Ghuba kwa ajili ya kuwalinda wao wala kuimarisha ujirani mwema. Wanalinda maslahi yao. Mahitaji ya kisiasa na kiuchumi ya Marekani yanaongezeka kila kukicha. Itafikia wakati kidogo kilichopo katika Ghuba ya Uajemi kitagombewa na wenyeji na mabeberu wa Marekani na hapo ndipo balaa litakapoanza. 

Marekani kama mbabe wa dunia itatumia majeshi hayo hayo yanayohifadhiwa na wenyeji kuwatwanga wenyeji na kufaidi kilichobaki. Marekani haina mchezo wala urafiki kwa maslahi yake. Itapambana na yeyote yule bila kujali lolote ili mradi wapate wanachotaka. 
 

Juu 
 

YALIYOMO 
 
 
Tahariri 
Onyesheni ushujaa wa Badri 

Daniel kuwatimua waumini Msikitini 

Waislamu Moshi: Wadai kulishwa nguruwe, vibudu 

Dondoo za Kisakolojia 
Na. Abu Halima Sachangwa 

Kona ya WachaMungu  

Jicho la Uzalendo 

Maulana Sayyid Jamal-Din Afghan 1214 - 1254 (1838-1897) - 2 

Vipi umoja wetu uwe hatari ? 

MASHAMBULIZI YA MAREKANI NCHINI IRAQ  

Marekani si rafiki mwema  

Tunahitaji UN ya Waislamu - 2  

Njia bora zitakazotusaidia kuwalea watoto 
Na Ust. Hashim Rusaganya, Mombasa 

Ijue Madrasatul-Qaadiriya Sokoni I Arusha. 
Na Habiba Swedi, Arusha 

Tutafute kwanza ufalme wa Allah (s.w.) 
Na Mwapwani Mohammed 

Sheikh Kisiwa atunuku zawadi 

Chuo cha Kilimo Ukiriguru kupata Msikiti mpya  
Na Mwandishi Wetu, Mwanza  

Huduma za maji Kondoa haziridhishi 
Na Abu Zuberi, Kondoa  

Mnyororo wa imani 
Na Sheikh Bernard P. Nyangasa 

Je, Yesu alibatizwa? 
Na Muhibu Said  

Kufuatia Waislamu kuritadishwa Merela Morogoro: Masheikh wa mjini watupiwa lawama  

Abiria walaani kumwagiwa pombe Kondoa 

Sheikh Bafadhil ateuliwa kudhamini waandishi wa habari Morogoro 
Na Mussa Ally, Morogoro 

Sayansi na Teknolojia 
[Tatizo la mwaka 2000] 

Masomo ya Dini ya Kiislamu 

Barua za Wasomaji 

Chakula na lishe 
[Mlo wa siku ya Idd] 


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtanzania.org
 
Home Links Islam Tanzania Matoleo yaliyopita